Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi wa Agosti na September 2001

KUISHI NI KRISTO NA KUFA NI FAIDA

            Salamu,

            Kwa Watakatifu, watu wa Mungu aliye Baba yetu, na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunamshukuru Mungu wetu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu, kwa kuwa mnazidi kudumu katika tumaini la imani iliyo katika Yesu Kristo. Kwa maana Mungu tumwabuduye kwa roho zetu katika Injili ya Mwana wake, ni shahidi wetu jinsi tuwatajavyo katika sala zetu mara kwa mara pasipo kukoma. Amestahili yeye, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza, kwa kuwa yeye ndiye aliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yake vilikuwako, navyo viliumbwa. Tunawasalimu popote mlipo msomapo ujumbe huu ni katika Jina lile lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, Bwana na Mwokozi wetu. Kwa kuwa ujumbe tulionao ni mrefu tumeona tuweke kwa ajili ya miezi miwili – lakini kwa pamoja.

 Kusudi la kuwaandikia

             Usishangae unapoona umeushika ujumbe huu umekufikia hapo ulipo na kuusoma. Si bahati mbaya wala si bahati nzuri, bali ni mpango wa Mungu.

            Wakati fulani kama miaka kadhaa iliyopita tuliamua kuomba, baada ya kuona kwa macho, na kusikia kwa njia ya redio na kwa vinywa vya watu, na pia kwa kusoma katika magazeti jinsi ambavyo wakristo wengi hasa waliozaliwa mara ya pili wanavyokufa. Wakristo wengi wamekuwa wakifa wakiwa bado vijana kwa njia mbalimbali, lakini wengi ni kwa njia ya magonjwa na ajali za barabani

            Wakristo wengi wanaokufa karibu kila siku ni wa umri kati ya miaka ishirini na miaka hamsini. Tukawa tunasikia watu wengi wakisema ni mapenzi ya Mungu vifo hivyo vitokee. Lakini ndani ya mioyo yetu hatukupata amani juu ya vifo hivi.

             Ndipo tulipoamua kuomba kumuuliza Mungu ni sababu gani zinazofanya watu wake wafe wakiwa na umri mdogo namna hii wakati bado wanahitajika katika kazi ya kueneza injili, wanahitajika na taifa, na wanahitajika na ndugu zao pia. Na Bwana Mungu alitujibu .

            Na tangu wakati huo, Bwana ametuwezesha kulihubiri jambo hili mahali mbali mbali. Lakini ndani ya mioyo wetu tunashuhudiwa ya kuwa ujumbe huu unatakiwa uwafikie watu wa Kristo wengi, wausome, wautafakari na kuufanyia kazi.

            Na hilo ndilo kusudi la kuwaandikia, muusome, muutafakari na kuufanyia kazi. Ni maombi yetu kwa Bwana ya kuwa kwa uwezo wa Roho wake aliye Mtakatifu utakayoyasoma humu yatakuwa msaada kwako.

Kushibishwa kwa wingi wa siku

            Tunaamini umewahi kusikia watu wengi wakisema ‘kila mtu ameandikiwa siku yake ya kufa, ikifika siku hiyo hata akiwa wapi atakufa’. Watu wengi wanausema usemi huu, na walio wengi wanaamini ya kuwa ndivyo Mungu alivyopanga.

            Lakini kwetu sisi kama watu wa Kristo ni vigumu kuuamini usemi huu kwa kuwa hauendi sambamba na Neno la Mungu.

            Biblia inasema katika kitabu cha Waebrania 9:27, “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu”. Mstari huu hausemi watu wamewekewa kufa siku moja. Huu mstari unasema watu wamewekewa kufa MARA moja na SIYO kufa siku moja. Mara moja na siku moja ni maneno yanayomaanisha mambo mawili tofauti.

 Imeandikwa;

“ Bwana akasema,Roho yangu   haitashindana na mwanadamu milele,    kwa kuwa yeye ni nyama, basi siku zake    zitakuwa miaka mia na ishirini” (Mwanzo 6:3).

             Ingawa kuna watu wengi ambao hawafiki hata nusu ya miaka mia na ishirini, lakini kuna watu ambao wameishi zaidi ya miaka mia na ishirini.

            Na katika sehemu mbalimbali katika Biblia imeandikwa ya kuwa ukifanya mambo fulani siku zako zitafupishwa; na ukifanya mambo fulani siku zako zitaongezwa. Kwa hiyo kuishi kwako hapa duniani kutategemea sana jinsi unavyotembea katika mapenzi ya Mungu.

            Si mpango wa Mungu katika Yesu Kristo ufe ungali kijana au mtu wa makamo. Hebu  soma maneno haya:-

 “Kwa hiyo Bwana Mungu asema hivi,Tazama watumishi wangu watakula, bali ninyi mtaona njaa;tazama, watumishi wangu watakunywa, bali ninyi mtaona kiu; tazama, watumishi wangu watafurahi, bali ninyi mtatahayarika.  ……Hatakuwepo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa”. (Isaya 65:13,20).

            Unaposoma mistari ya namna hii, mara moja unaanza kujiuliza kwa nini watu wa Kristo hufa kabla ya kufikia miaka mia, wakati imeandikwa ya kuwa watoto watatimiza miaka mia?

Pia imeandikwa;

“Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyenzi  ……………….Kwa siku NYINGI nitamshibisha, nami nitamwonyesha wokovu wangu” (Zaburi 91:16)“Ili wafarijiwe mioyo yao, wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo’ (Wakolosai 2:2).

            Aliyeahidiwa kushibishwa kwa wingi wa siku ni yule ambaye anakaa ndani ya Kristo aliye siri ya Mungu. Kama umezaliwa mara ya pili na Kristo anakaa ndani yako, na wewe ndani yake ahadi hii ya yako.

            Je! unaelewa maana ya kushibishwa kwa wingi wa siku?

            Ngoja tukupe mfano.

            Mtu anapoweka chakula kingi mezani; Ni yule anayekula anaye mwambia NIMESHIBA. Yeye awekae chakula hapimi kushiba kwa yule anayekula. Anayekula ndiye asemaye ameshiba, na kama hajashiba anaweza kuongezewa chakula.

            Na hivi ndivyo Mungu anavyofanya. Ametuwekea siku nyingi za kuishi juu ya nchi, ziko mbele yetu. Tunatakiwa tukae hapa duniani hadi tushibe! SISI ndio tunaotakiwa kumwambia Mungu ya kuwa tumeshiba!Tutashibishwa kwa wingi wa siku.

            ‘Kushiba’ hapa inamaana siku ya kumaliza kazi tuliyopewa na BWANA tuifanye; au siku ya Yesu Kristo kurudi kutuchukua mara ya pili. Ndiyo maana Yesu Kristo akasema, “Mimi nimekutukuza duniani, hali NIMEIMALIZA KAZI ILE ULIYONIPA NIIFANYE” (Yohana 17:4).

Kwa nini tupo duniani sasa

            Ukiangalia kwa makini hali ya watu wa Mungu; wale waliozaliwa mara ya pili kwa Neno la Kristo; wale walioupokea wokovu kwa njia ya Injili, unashindwa kusoma katika maisha yao sababu hasa ya Mungu kumwokoa mtu, na bado amwache hapa duniani.

            Tulikuwa hatuoni sababu kwa nini Mungu amwokoe mtu, amfanye kuwa Mwana kwake na yeye kuwa Baba, na bado amwache katika dunia iliyojaa majaribu, mahangaiko, dhambi na magonjwa.

            Hebu jiulize hata wewe, kwa nini Mungu alikuokoa kwa muda na mazingira tofauti na mwingine? Na baada ya kukuokoa akakuacha uendelee kuishi hapa duniani? Lazima kuwe na sababu!

            Mungu wetu ni Mungu aliye na mipango na makusudi kamili juu ya kila neno analolisema na kila jambo analolifanya.

Tafakari maneno haya:

            “Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida "(Wafilipi 1:21).

            Ikiwa kufa kwa watu wa Mungu, kufa ni faida kwa nini  wanaomba walindwe wakiwa hapa duniani?

            Kufa na kuondoka hapa ulimwenguni ni faida kwa mtu wa Mungu, kwa kuwa anayaacha matatizo ya dunia hii na anakwenda kuishi pamoja na Kristo katika raha na utulivu milele.

            Lakini jibu swali hili; kwa nini unaomba ulinzi wa Mungu usife, usipatwe na ajali yoyote itakayokatisha maisha hapa duniani?

            Na wakati mwingine kukiwa na hatari mbele yako usiyoifahamu, Roho wa Mungu anakuhimiza kuomba? Na mara nyingine pia huinua watu wengine waombe kwa ajili yako usidhurike, kwa nini iwe hivyo?

            Hii inatupa picha tu ya kuwa kuna sababu kubwa sana ambayo Mungu anayo ya kutuacha hapa duniani, na kutulinda, na kutulisha badala yakutuchukua mara tu baada ya kuokoka.

            Kuna kitu ambacho Mungu anatarajia tukifanye hapa duniani, ambacho ni muhimu sana kwake, kiasi kwamba inabidi atulinde ili tukifanye!

            Kuna kusudi kamili la wewe kuwapo hapa duniani wakati huu. Neno la Mungu linatuambia kuwa kukaa kwako katika mwili huu, kuna faida kubwa kwa watu wengine.

“Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu  mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua  silitambui. Ninasongwa katikati ya mambo  mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na   Kristo; maana ni vizuri zaidi sana; bali kudumu   katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu” (Wafilipi 1:22-24)           

            Tulipokuwa tunaendelea kutafakari sababu za sisi kuwepo hapa duniani baada ya kuokoka, Roho wa Mungu alituongoza kusoma mstari huu:

“Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo” (2Wakorintho 5:20)

            Kuwa mjumbe kwa ajili ya Kristo maana yake nini? Tunatakiwa tuwe wajumbe kwa ajili ya Kristo juu ya nini? Na kwa namna gani? Na kwa nani? Na kwa wakati gani? Neno la Kiingereza lililotafsiriwa kuwa mjumbe ni ‘Ambassador” Na neno zuri linalotoa picha nzuri ya maana ya ‘Ambassador’ ni neno Balozi. Balozi ni mjumbe na mjumbe ni balozi

            Neno balozi na neno mjumbe lina maana sawa lakini kwa jinsi tunavyoyatumia maneno haya, utafikiria neno balozi lina uzito zaidi kuliko neno mjumbe.

            Kwa hiyo tunaweza kusema: “ Basi tu mabalozi (wajumbe) kwa ajili ya Kristo” Katika nchi ya Tanzania tuna mabalozi wa nyumba kumikumi, ambao pia wanajulikana kuwa ni wajumbe wa nyumba kumikumi. Pia tuna mabalozi walioko nchi za nje waliotumwa kuiwakilisha nchi hii katika maswala na majukumu mbalimbali.

            Sasa na tuliangalie katika ngazi ya kitaifa. Balozi ni mjumbe au mwakilishi wa nchi moja katika nchi nyingine. Kwa mfano: Balozi wa Tanzania nchini Kenya; kwanza ni raia wa Tanzania anayefahamu vizuri msimamo wa nchi hii katika maswala mbalimbali. Yuko Kenya kwa ajili ya Serikali ya Tanzania na raia wa Tanzania.

            Yeye ndiye msemaji mkuu wa Serikali ya Tanzania nchini Kenya. Serikali ya Tanzania inapopeleka ujumbe kwa serikali ya Kenya, inapitia kwa balozi wake aliyeko Kenya.

            Balozi huyo ni picha kamili ya Watanzania kwa watu wa Kenya, katika maneno yake na mwenendo wake. Yeye ni mlinzi wa hadhi ya Tanzania nchini Kenya. Na makazi yake ni nchini Kenya.

            Balozi ni mjumbe aliyetumwa na mtu mwingine. Balozi wa Tanzania katika umoja wa Mataifa, ametumwa na nchi yetu, awe msemaji na mtetezi wa mawazo ya Tanzania katika maswala mbalimbali ya kimataifa. Balozi hasemi mawazo yake mwenyewe. Balozi anasema tu kile alichotumwa kusema na anafanya kile tu ambacho ametumwa kufanya.

            Tunasisitiza hivi, BALOZI HASEMI MAWAZO YAKE MWENYEWE: BALOZI ANASEMA TU KILE ALICHOTUMWA KUSEMA, NA ANAFANYA KILE TU AMBACHO AMETUMWA KUFANYA.Na kitu cha kwanza anachofanya anapofika katika nchi aliyotumwa ni kutoa vitambulisho vilivyo na muhuri na sahihi ya kiongozi wa nchi anayotoka.

            Biblia inatuambia kuwa sisi ni mabalozi kwa ajili ya Kristo hapa duniani; sisi ni wajumbe tuliotumwa kwa ajili ya Kristo hapa duniani. Ndiyo maana Paulo alisema kuishi kwake ni Kristo. Wewe ni mjumbe wa Kristo na kwa ajili ya Kristo hapa duniani. Ikiwa wewe ni Mjumbe, basi wewe ni balozi wa Kristo na kwa ajili ya Kristo.

            Kumbuka kuwa balozi hasemi mawazo yake mwenyewe. Wewe ni balozi wa Kristo hapa duniani kwa hiyo kutokana na wadhifa huo uliopewa unatakiwa usiseme mawazo yako, wala kufanya mambo yako hapa duniani; bali USEME MAWAZO YA KRISTO NA MANENO YAKE; NA UFANYE YAKE TU ALIYOKUTUMA KUFANYA.

            Lakini ni wazi kwamba huwezi kusema mawazo na maneno ya Kristo wakati huyafahamu. Na ikiwa hapa duniani wewe ni balozi basi, inamaanisha hapa duniani si kwako. Na ikiwa hapa duniani si kwako, na wala wewe si mwenyeji wa hapa duniani; basi unatokea wapi na uenyeji (uraia) wako ni wa wapi? Wewe ni mwenyeji wa wapi? Hili swali ni muhimu sana ambalo ni budi ufahamu jibu lake katika roho yako. Bila kufahamu ulikotoka utaifanye kazi ya ubalozi au ya kuwa mjumbe wa Kristo. Balozi (Mjumbe) yeyote anajua alikotoka; anafahamu uraia wake ni wa wapi. Je wewe unafahamu kuwa wewe ni balozi wa nchi gani ukiwa hapa duniani?

            Tunakazia swali hili kwa sababu ujumbe utakokuwa unatoa; au mahubiri unayofanya mbele za watu; na matendo yako yanategemea sasa mahali gani umetoka kiroho na kimazingira.

            Kuna wengine ni mabalozi wa miili yao wenywe. Wanahubiri kwa sababu ya mwili ili wapate mishahara yao na kuvaa. Wao wanaona kuwa kuhubiri ni kama kazi nyingine ya kuajiriwa.

            Lakini  la kushangaza ni kwamba wote wanasema ni mabalozi wa Kristo, wajumbe wa neno la Injili. Na hii si kweli. Muda umefika ambapo Roho wa Mungu amekududia kuliweka wazi hili. Mabalozi wa Kristo wawe wazi; mabalozi wa madhehebu wawe wazi, na mabalozi wa miili yao wawe wazi.

            Muda umefika wa kufichuliwa watu wote wanaojiita mabalozi wa Kristo, wameokoka, na ni wakristo, watumishi wa Kanisa kumbe ni mbwa mwitu wakali wanaowaendea watu wakiwa wamevaa mavazi ya Kondoo (Mathayo 7:15).

            Muda umefika ambao watu wote wanokaa karibu na wewe, vitu vyote vinavyokuzunguka, mahali unapopita, watu wote hao wanaokuzunguka wajue, kwamba wanajua KUWA WEWE NI BALOZI WA KRISTO MJUMBE KWA AJILI YA KRISTO!

            UTASEMA MAWAZO NA MANENO YA KRISTO. NA UTAFANYA MATENDO YA KRISTO KWA AJILI YA KRISTO MAHALI POPOTE ULIPO NA UTAKAPOKUWA DUNIANI:

            Kuishi kwako hapa duniani ni Kristo na kufa kwako ni faida! Mtume Paulo alipoandika kuwa “Basi tu wajumbe (Mabalozi) kwa ajili ya Kristo,” alikuwa anamhusisha kila mtu ambaye amefanyika kuwa kiumbe kipya ndani ya Kristo. Ikiwa wewe ni kiumbe kipya ndani ya Kristo, basi wewe ni mjumbe(balozi) kwa ajili ya Kristo.

            Ikiwa basi wote waliozaliwa mara ya pili, walio viumbe vipya ndani ya Kristo (waliookoka) wanatakiwa kuwa mabalozi wa Kristo; mbona basi ubalozi wao hauonekani ukifanya kazi? Ubalozi hauonekani katika maisha yako, kwa sababu hujafuatilia katika Biblia kujua neno linasemaje juu ya hili. Laiti basi Kanisa lingefahamu uzito wa wadhifa huu wa kuwa mjumbe wa Kristo hapa duniani, hali ya mambo isingekuwa kama ilivyo sasa ya kukata tamaa – iliyojaa katika mioyo ya watu.

            Laiti basi wewe ungejua uzito wa wadhifa huu wa kuwa mjumbe wa Kristo mahali ulipo ikiwa in nyumbani, kazini, safarini, kanisani, sokoni, hali ya mambo isingekuwa kama unavyoiona sasa.

Wewe mkristo ni raia wa mbinguni.

“Basi tangu sasa ninyi si wageni wala Wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu” (Waefeso 2:19).

Yesu Kristo alipokuwa akituombea alisema:

“Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa WAO SI WA ULIMWENGU, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule muovu. Wao SI WA   ULIMWENGU KAMA MIMI NISIVYO WA   ULIMWENGU. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo NILIWATUMA HAO ULIMWENGUNI (Yohana 17:4-18)

            Weka jambo ili katika moyo wako. Watu wa Kristo si wa ulimwengu huu, bali ni wenyeji wa mbinguni. Watu wa Kristo wako hapa ulimwenguni kwa sababu Kristo amewatuma kufanya kazi muhimu. Kumbuka upo hapa duniani kwa kuwa kuna KAZI ambayo KRISTO amekupa uifanye kabla ya kurudi nyumbani kwetu MBINGINU.

Kwa nini Wakristo wanakufa kabla ya kukamilisha kazi walizopewa:

            Tulipokuwa tunaomba kwa ajili ya Watakatifu wa Mungu, popote walipo hapa nchini, Bwana akatujibu na kutuambia maneno yafuatayo ndani ya mioyo yetu. “Watu wangu wengi wamefunikwa na roho ya mauti bila ya wao kufahamu. Na wengi wanaangamia.”

            Utajuaje ya kuwa umefunikwa na roho ya mauti? Watu wengi huwa wakifunikwa na roho ya mauti kwanza huwa wanaingiwa na hofu ya kufa, na pili huwa wanaona wanaweza kufa wakati wowote, na tatu huwa wanajiandaa kufa kwa kutubu, kulipa madeni au kwa kuandika wosia, na wakati mwingine hata kuanza kugawa mali zao.

            Ukiona una hali ya namna hii ujue umefunikwa na roho ya mauti!

            Tunamkumbuka mama mmoja aliyeokoka aliyetuambia; “Ndugu, kwa muda sasa nimekuwa nikiona moyoni mwangu ya kuwa nitakufa karibuni. Nimepambana na wazo hili kwa muda mrefu naona wala haliondoki. Kwa hiyo nimetubu na kutengeneza mambo yangu kwa sababu naona nitakufa karibuni”

            Mimi nikamwambia; “ Kweli kufa kwa mkristo ni faida kwa kuwa atakwenda kukaa na Yesu Kristo milele. Lakini kumbuka Yesu Kristo alisema ametutuma ulimwenguni kama yeye alivyotumwa. Je! unaposema uko tayari kufa, umekwisha maliza kuifanya kazi aliyokuagiza uifanye? Je! utakuwa na matunda gani ya kazi mikononi mwako utakapokwenda kuonana na Bwana Yesu Kristo baada ya kufa?

            Yule mama akatujibu akasema; “Mmeniambia jambo muhimu ambalo sikulifikiria, kwani ingawa nafanya kazi ya Mungu lakini sina uhakika kama ndiyo kazi niliyoitiwa niifanye. Sasa mnanishauri nifanye nini?

            Wakristo wengi wako katika hali ya namna hii. Na tulipokuwa tunaendelea kuomba kwa ajili ya tatizo la roho ya mauti juu ya watu wa Kristo, Bwana alitupa sababu tano ambazo zinawafanya wakristo wafe kabla ya kumaliza kazi aliyowapa.

            Kumbuka tunaposema juu ya kifo, hatuna maana kufa kiroho, bali kufa kimwili yaani roho ya mtu kutoka katika mwili. Kuna sababu nyingi hata zaidi ya tano ambazo zinawafanya watu wa Kristo wafe kabla ya kushiba wingi wa siku. Lakini katika barua hii huu tutakushirikisha tano tu ambazo Bwana alitupa ili watu wake wazitafakari.

1.      Kutokuwaheshimu wazazi

“Enyi watoto, watiini wazazi wenu  katika Bwana, maana hii ndiyo haki.  Waheshimu baba yako na mama yakoamri hii ndiyo amri ya kwanza yenye  ahadi, upate heri, ukae SIKU NYINGI   KATIKA DUNIA” (Waefeso 6:1-3)

 “Waheshimu baba yako na mama yako,  kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru,  SIKU ZAKO ZIPATE KUZIDI, nawe upate  kufanikiwa katika nchi upewayo na  Bwana, Mungu wako” (Kutoka 5:16).“Na alaaniwe amdharauye baba yake  au mama yake. Na watu wote waseme,   Amina” (Kumb. 27:16).

            Tatizo la kutowaheshimu wazazi linazidi kuwa kubwa sana siku hizi na hasa katika jamii ya Kikristo. Kama vile tunavyomheshimu Mungu kwa vitu na mali tulizonazo, inatupasa kuwaheshimu wazazi wetu kwa vitu na mali tulizonazo. Inabidi ukumbuke yakuwa walijinyima vingi kukutunza ulipokuwa mdogo ili usome na uwe na maisha mazuri baadaye. Lakini hata kama wazazi wako hawakukusomesha, wewe kama mkristo ni muhimu uonyeshe upendo kwao kwa kuwagawia ulicho nacho. Iko faida gani wewe kuishi maisha mazuri na kula na kusaza, wakati wazazi wako wanateseka na maisha magumu na kukosa chakula na huku wana mtoto waliyemzaa kama wewe?

            Vijana wengi waliookoka wakitaka kuoa au kuolewa huwa wanawapuuza sana wazazi wao. Utawasikia wakisema, “Wazazi wangu hawajaokoka kwa hiyo hata nikiwashirikisha jambo hawawezi kuelewa.”

            Lakini tunataka ukumbuke ya kuwa Biblia haisemi uwaheshimu wazazi waliookoka na uwadharau wazazi wako wasiookoka. Imeandikwa, “Enyi watoto, watiini Wazazi wenu KATIKA BWANA………. Waheshimu baba yako na mama yako ………….. ukae SIKU NYINGI KATIKA DUNIA”.

            Kutokuwatii na kutokuwaheshimu wazazi wako kunafanya SIKU ZAKO ZA KUISHI ZIWE FUPI – UNAKUFA MAPEMA. Na kuwadharau wazazi kunakuletea laana. Usije ukasema wazazi wako wamekulaani, bali kumbuka imeandikwa alaaniwe amdharauye baba yake au mama yake.

            Ikiwa wazazi wako wanakuambia ufanye mambo yaliyo kinyume na neno la Mungu, si hekima kugombana nao na kuwadharau. Kumbuka vita vyetu si vya mwili, wala si juu ya nyama na damu. Wewe wapende wazazi wako, waombee na ombea jambo ambalo hamwelewani nao, na Bwana atakujibu; kwa kuwa ameahidi kujibu. Uwe mvumilivu, usifanye maamuzi ya haraka, kwani yote yawezekana kwake aaminiye. “Tazama, mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili. Je! KUNA NENO GUMU LOLOTE NISILOLIWEZA?” (Yeremia 32:27)

            Ole, ni kwa wale ambao hawapatani na WAKWE ZAO! Mkwe  wako ni mzazi wako ukimdharau unapokea laana; na usipomheshimu siku zako za kuishi duniani zinafupishwa!

            Watu wa Kristo wengi wamenaswa na kutokutii andiko hili. Wengi wao ingawa si wote wamekufa na wake zao wamekuwa wajane na kubaki na watoto wadogo. Na wengine wamekufa na kuwaachia waume zao watoto walio wadogo. Ukifuatilia ndoa za marehemu hao wengine wao (si wote) utakuta walifunga ndoa bila kuelewana na wazazi wao; au wengine walikuwa hawapatani na wakwe zao.

2.      Kuchukia maonyo

            Wakristo wengi huwa wanachukia wanapoonywa juu ya mienendo yao mibaya isiyompendeza Mungu. Na wengine hata hudiriki kuwanunia wale waliowaletea maonyo hayo. Lakini kuna hatari kubwa kuchukia maonyo.

“Adhabu kali ina yeye aiachaye  njia; Naye achukiaye kukemewa   ATAKUFA” (Mithali 15:10)

            Adhabu kali ina yeye amwachaye Yesu Kristo kwa kuwa yeye ndiye NJIA. Na unaelewa kwa nini wakristo hawapendi kukemewa wanapoambiwa ya kuwa wanaenenda kinyume cha ushuhuda wa Yesu Kristo? Wanachukia kukemewa kwa kuwa wamejaa mzaha.

 “Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa  Wala yeye hawaendei wenye hekima”  (Mithali 15:12)

 “Heri mtu yule asiye kwenda katika  shauri la wasio haki; wala hakusimama   katika njia ya wakosaji; wala hakuketi  barazani pa wenye MIZAHA” (Zaburi 1:1) 

“Mwanangu, usidharau kuadhibiwa   na Bwana, Wala usione ni taabu kurudiwa  naye. Kwa kuwa Bwana ampendaye  humrudia, kama vile baba mwanae   ampendezaye. Heri mtu yule aonaye   hekima, na mtu yule apataye ufahamu… ……… ana wingi wa siku katika mkono   wake wa kiume, utajiri na heshima katika  mkono wake wa kushoto” (Mithali 3:11-13, 1,)

            Kumcha Bwana ni kukataa uovu. Roho ya uchaji inakuongoza katika njia za haki na siyo za uovu. Akukemeae uache maovu anakupenda kwani hapendi uangamie. “Kumcha Bwana kwaongeza SIKU ZA MTU; bali miaka yao wasio haki itapunguzwa” (Mithali 10:27). “Usiwe mwovu kupita kiasi; wala usiwe mpumbavu; kwani ufe kabla ya wakati wako?” (Mhubiri 7:17)

3.      Kutumia ulimi vibaya

        Ungefahamu mambo gani ambayo ulimi wako unaweza kufanya ungekuwa mwangalifu katika yote uyasemayo. Hebu soma kwanza maneno yafuatayo:

 “Tumbo la mtu litajazwa matunda   ya kinywa chake; atashiba mazao ya  midomo yake. Mauti na uzima huwa  katika uwezo wa ulimi, na wao   waupendao watakula matunda yake” (Mithali 18:20,21)

 “Enye wazao wa nyoka, mwawezaje  kunena mema mkiwa wabaya? Maana,   kinywa cha mtu huyanena yaujazayo  moyo wake. Mtu mwema katika akiba  njema hutoa mema; na mtu mbaya katika   akiba mbaya hutoa mabaya. Basi, nawaambia,  kila neno lisilo maana, watakalo linena   wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo   siku ya hukumu. Kwa kuwa kwa maneno   yako utahesabiwa haki, na kwa maneno   yako utahukumiwa” (Mathayo 12:34-37)

            Sheria ya ulimi ni hii, anachokiamini ndicho unachokisema; unachokisema ndicho kinachotokea.

 “Basi ulimi hakuna awezaye kuufunga;  ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo   mauti. Kwa huo twamhimidi Mungu Baba   yetu, na kwa huo   twawalaani wanadamu   waliofanywa kwa mfano wa Mungu.   Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu HAIFAI MAMBO   HAYA KUWA HIVYO” (Yakobo 3:8-10)

            Siku hizi limekuwa jambo la kawaida kwa mkristo kusema maneno ya baraka akiwa kanisani au ‘fellowship’, lakini kwa kinywa hicho hicho kusema matusi nyumbani, na masengenyo kwa jirani zake.

            Ndugu yetu, haifai mambo hayo kuwa hivyo! Kumbuka vinywa vyetu ni mitego. Tunayoyasema yanatufunga. Soma Mithali 6:2. Tunayosema yanaweza kuongeza siku za kuishi hapa duniani au kuzifupisha. Kwa hiyo chunga unachokisema.

 4.      Kuingilia wito wa mwenzako

            Katika kanisa, Bwana ameweka huduma na karama mbalimbali. Na kazi ya huduma na karama hizi ni kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya Kristo itendeke; na kwa ajili ya kuujenga mwili wa Kristo.

            Bwana ameita na kuwaweka wengine wawe mitume, wengine manabii, wengine Wainjilisti, wengine Wachungaji na Waalimu. Wengine wamegawiwa karama na vipawa mbalimbali. Na kila siku tunatakiwa tuenende kama uustahilivyo wito wetu tulioitiwa. Mchungaji aenende kama mchungaji. Nabii aenende kama nabii. Mtume aenende kama mtume. Mwinjilisti aenende kama Mwinjilisti.

            Jambo la kushangaza ni kuona mtu aliyeitwa kuwa mwinjilisti anang’ang’ania kufanya kazi ya uchungaji. Na utakuta pia mtu ameitwa kuwa mtume au/na nabii anang’ang’ania kufanya kazi ya mwinjilisti au mchungaji au mwalimu. Kuingiliana kwa wito namna hii kumeleta madhara na magomvi mengi kati ya wakristo. Kwa nini uingilie ofisi na kazi ya mwenzako? Na kazi yako unayoiacha ni nani atakayeifanya? Na mwenzako huyo unayemwingilia unataka aende kufanya kazi wapi?

            Hebu fikiria hali ya namna hii itokee katika kiwanda kimoja hapa nchini. Mtu aajiriwe kuwa Meneja Masoko lakini yeye kila siku umkute ameacha ofisi na kazi yake na kung’ang’ania katika ofisi ya Meneja Utawala. Matokeo yake ni ugomvi na kukwama kwa kazi zote mbili na mwisho kuanguka kwa kiwanda, kama huyo anayemwingilia mwenzake asiposhughulikiwa kisheria.

            Au fikiria mahali kama hospitali. Itakuwaje ikiwa daktari wa macho aliyefundishwa na kuajiriwa kutibu wagonjwa wa macho, ukimkuta anang’ang’ania katika wadi ya kuzalisha wakina mama waja wazito? Je! anaweza kuzalisha bila kufundishwa? Na hao walioajiriwa kuzalisha waende wapi? Na wagonjwa wa macho watibiwe na nani wakati daktari wa macho ameihama ofisi yake?

            Vivyo hivyo hata katika kazi ya Mungu. Unapoingilia wito wa mwenzako unaleta madhara si kwa mwenzako yule unayemwingilia tu, bali kwa mwili mzima wa Kristo. Wakristo wote wanadhurika na kazi ya Bwana inasimama kwa sababu ya machafuko hayo.

            Katika agano la kale tunasoma ya kuwa mtu ambaye alikuwa anaingilia Ofisi na na kazi ya kuhani Mkuu alikuwa anakufa hapo hapo. Ofisi ya kuhani Mkuu ilikwa Patakatifu pa Patakatifu. Mtu mwingine ambaye Mungu hakumteua na kumtakasa kuwa Kuhani Mkuu akiingia humo alikuwa anakufa.

            Na Bwana alituambia tuwaambie tuseme hivi; hata hivi leo mkristo anayeacha wito wake na kuingilia wito wa mwenzake anakufa! Siku zake hapa duniani zinafupishwa!

 5.      Kutokutii Maagizo ya Mungu

            Kila kiungo katika mwili wa mwanadamu kina umuhimu wake. Na kila mkristo aliyezaliwa mara ya pili ni kiungo katika mwili wa Kristo; kwa hiyo kila mkristo ana kazi muhimu aliyopewa na Bwana aifanye. Kutokutii maagizo ya Mungu juu ya kazi hiyo aliyopewa kunapunguza ziku zake za kuishi hapa duniani.

            Ndivyo ilivyokuwa katika maisha ya Musa na Haruni. Mpango wa Mungu ulikuwa ni Musa na Haruni wawaongoze wana wa Israeli kutoka Misri hadi Kaanani. Halikuwa kusudi la Mungu ya kuwa Musa na Haruni wafie jangwani kabla ya kufika Kanani. Soma kitabu cha Kutoka sura ya 3 na ya 4.

            Kwanini Musa na Haruni walikufa njiani kabla ya safari kumalizika?

 “Bwana akasema na Musa siku hiyo hiyo,  akamwambia, kwea katika mlima huu   wa Abarimu, mpaka kilima cha Nebo,   kilicho katika nchi ya Kanaani niwapayo  wana wa Israeli kuimiliki; UKAFE katika   kilima, huko ukweako, ukusanywe uwe   pamoja na jamaa zako; kama alivyo kufa   nduguyo Haruni katika mlima wa Hori,  akakusanywa awe pamoja na watu wake;   kwa sababu MLINIKOSA NINYI JUU   YANGU KATIKATI YA WANA WA ISRAELI  KATIKA MAJI YA MERIBA HUKO KADESHI,   katika bara ya Sini; kwa kuwa   HAMKUNITAKASA katikati ya wana wa Israeli”   (Kumbukumbu la Torati 32:48-52).

            Ni wazi hapa ya kwamba Musa na Haruni hawakumalizia huduma waliyopewa, wakafa njiani wote wawili kwa kuwa HAWAKUMTAKASA BWANA mble ya Wana wa Israeli. Kwa maneno mengine HAWAKUTII MAAGIZO YA MUNGU BADALA YAKE WALIASI MBELE YA WANA WA ISRAELI. Soma kitabu cha Hesabu 20:1-12. Hawakumpa Mungu utukufu katikati ya Wana wa Israeli.

            Watumishi wengi wa Mungu wamekufa kabla ya kumaliza huduma walizopewa kwa sababu ya kutokutii maagizo ya Mungu waliyopewa. Mungu anapowagiza jambo; wanashindwa kulitekeleza wala hawampi Utukufu wakiwa mbele za watu. Na wengi wanadhani ya kwamba kwa kuwa miujiza inafanyika katika huduma zao basi Bwana anawakubali. Lakini Yesu Kristo ana mawazo tofauti juu ya jambo hili. Hebu na tumsikie anasemaje;

 “Ndipo kwa matunda yao mtawatambua.  Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana,  atakayeingia katika ufalme wa mbinguni;  bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba   yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia  siku ile, Bwana, Bwana hatukufanya unabii   kwa jina lako  na kwa jina lako kutoa pepo,  na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?   Ndipo nitawaambia dhahiri, sikuwajua ninyi  kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao   maovu” (Mathayo 7:20-23).

            Kumbuka karama bila tunda la Roho haitoshi. Tawi lisilozaa matunda hukatwa.

 Mshitaki wetu Ibilisi

            Biblia inamwita Ibilisi ya kuwa ni mshitaki wetu. Yeye anatushitaki sisi tulio wa Kristo usiku na mchana mbele za Mungu aliye Baba yetu. Je! unajua anatushitaki kitu gani? Analotushitaki ni hili, ya kwamba watu wa Kristo wengi hawaenendi kama Mungu anavyotaka; na anaona Mungu anapendelea kwa kuwa hasimamii Neno lake sawasawa.

            Ibilisi anauliza; kwa nini wakristo wasio waheshimu wazazi wao wanaachwa wakae siku nyingi juu ya nchi? Na pia anauliza maswali mengi yanayofanana na hayo.

“Yule joka akatupwa, yule mkubwa,   nyoka wa Zamani, aitwaye Ibilisi na   Shetani, audanganyaye ulimwengu wote;  akatupwa hata nchi, na malaika zake  wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti   Kuu mbinguni, ikisema, sasa kumekuwa   wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu  wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa   maana ametupwa chini MSHITAKI wa   ndugu zetu, yeye  awashitakiye mbele za   Mungu wetu, mchana ya usiku. Nao   wakamshinda kwa DAMU YA MWANA   KONDOO, na kwa NENO LA USHUHUDA  WAO; ambao hawakupenda maisha yao  hata kufa” (Ufunuo 12:9-11).

            Je! unadhani Mungu anachukua hatua gani anaposikia mashtaka ya namna hiyo juu ya watu wake wanaokwenda kinyume na Neno lake, na ambao wakionywa hatawaki kutubu wala kutengeneza palipo bomoka?

 OLE Ole!

“Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule  Ibilisi ameshuka     kwenu mwenye ghadhabu   nyingi, akijua yakuwa ana wakati mchache tu”  (Ufunuo 12:12b).

 “Ole wake ashindanaye na Muumba wake!   Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je  udongo umwambie yeye aufinyangae;   Unafanya nini? au kazi yao, hana mikono?   (Isaya 45:9).

“Ole wake amwambiye baba yake, Wazaa  nini? au mwanamke una utungu wa nini?  (Isaya 45:10).

“Ole wenu waandishi na Mafarisayo,   wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika   bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu na akiisha kufanyika,  mnamfanya kuwa mwana wa jehanam   mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe”  (Mathayo 23:15).

“Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki!   Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano,

  na ndani yake vimejaa unyang’anyi na kutokuwa  na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza

  ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi”   (Mathayo 23:25,2b).

“Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki!   Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa  chokaa, nayo kwa nje yanaonekana kuwa   mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na   uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje   mwaonekana na watu wenye haki, bali ndani  mmejaa unafiki na maasi” (Mathayo 23:26,27,28).

             Ole wake asiyewaheshimu baba na mama yake kama yanenavyo maandiko, kwa maana roho ya mauti iko juu yake! Ole kwake achukiaye kukemewa katika Bwana ili aache njia zake mbaya, kwa maana roho ya mauti iko juu yake! Ole kwake aingiliaye wito wa mwenzake na kutokutii maagizo ya Mungu; kwa maana roho ya mauti iko juu yake! Ole kwake autumiaye ulimi wake vibaya; kwa maana roho ya mauti iko juu yake!

 Tubu

            Leo hii ukiisikia sauti ya Roho wa Mungu, usiufanye moyo wako kuwa mgumu Ikiwa kuna sehemu ya ujumbe huu inayokugusa, TUBU NA UTENGENEZE PALIPO BOMOKA kati yako na Mungu, na kati yako na watu wengine. Hili ni muhimu kwa kuwa , “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote” (1Yohana 1:9). “Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu ……………… Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu” (Ufunuo 2:5,7).

Kamilisha huduma yako

            Mtu wa Kristo hajawekwa hapa ulimwenguni ili ale na kushiba na kulala tu! Mtu wa Kristo amewekwa ili afanye kazi kwa kuwa ametumwa na Kristo ulimwenguni kama vile Kristo naye alivyotumwa na Baba ulimwenguni.

            Hebu na tusome maneno haya aliyoambiwa Timotheo maana yanatufaa hata sisi leo:

“Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele   za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio   hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake   na kwa ufalme wake, lihubiri neno, uwe   tayari, wakati wake ukufaao na wakati   usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa   uvumilivu wote na mafundisho. Maana   utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho   yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao   wenyewe watajipatia waalimu makundi   makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti;   na kuzigeukia hadithi za uongo. Bali wewe   uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia  mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili   TIMILIZA HUDUMA YAKO” (2Timotheo 4:1 – 5)

 Tafadhali soma pia Mathayo 24:42-51.

 Mwisho

            Tunamshukuru Mungu kwa kukuwezesha kuusoma ujumbe huu; tafadhali usiache kumshirikisha mwenzako. Tafadhali usisahau kutuombea sisi, watoto wetu na timu nzima ili tuifanye kazi ya Bwana aliyotupa katika uwezo wake na kama apendavyo Yeye.

            Ukiwa na jambo la kutushirikisha juu ya ujumbe huu tuandikie.

            Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na Ushirika wa ‘Roho Mtakatifu ukae nasi sote, sasa na hata milele na milele. Amina.

Ni sisi watumishi wenzenu katika Shamba la Bwana.

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.