Barua ya Mwezi Desemba 2001
“….NA
JINA LAKE UTAMWITA YESU”
Mpendwa
katika Kristo Yesu,
Tunakusalimu
kwa Jina la Yesu Kristo Jina hili lipitalo kila jina! Tuna uhakika Mungu
anazidi kukutunza na ndiyo maana hata umepata nguvu na nafasi ya kuisoma
barua hii tunayokuandikia ya mwisho wa mwaka 2001.
Sisi
tunamshukuru Mungu sana kwa jinsi ambavyo anazidi kututunza na
kutusaidia katika maeneo yote ya maisha yetu. Huu ni mwezi wa Disemba na
tangu tuanze Januari – huduma aliyotupa imeendelea vizuri sana.
Tunashukuru sana kwa maombi yako kwa wale waliotuombea; na pia,
tunashukuru kwa ajili ya michango ya fedha kwa wale waliotutumia ili
kugharamia huduma. Mungu azidi kuwabariki kila siku sawa na Neno lake.
… na jina lake utamwita Yesu!
Katika kukumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo
hapa duniani kwa bikira Mariamu, ni jambo gani au ni kitu gani ambacho
unakikumbuka zaidi? Kwetu sisi tuna vitu vingi tunavyokumbuka, lakini
kimoja ambacho kinajitokeza zaidi ni hili Jina la Yesu!
Malaika Gabrieli alipokwenda kwa Mariamu
ili kumjulisha juu ya kuchukua mimba kwa uwezo wa Roho
Mtakatifu-alimwambia ya kuwa,
“utachukuwa mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake
utamwita Yesu”(Luka 1:31).Yusufu ambaye alikuwa amemposa Mariamu pia
alipelekewa habari na malaika Gabrieli juu ya ujauzito wa Mariamu.Akaambiwa,
“Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu…” (Mathayo 1:21).
Uamuzi wa ajabu!
Ukisoma Biblia vizuri na kuitafakari
utagundua ya kuwa hili jina la Yesu ndilo jina la Mungu Baba ambalo pia
amempa mtoto wake!Kwa nini tunasema hivi? Ni kwasababu katika kitabu cha
Waebrania 11:4 tunasoma habari za Yesu ya kuwa, “amefanyika
bora kupita malaika,kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko
lao”Kama jina la Yesu ni urithi au amerithi basi ina maana Yuko
aliyemrithisha! Naye ni Mungu Baba!
Pia, Yesu mwenyewe anasema hivi katika
Yohana 5:43 ya kuwa;
“Mimi nimekuja kwa jina la Baba
yangu,wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe,
mtampokea huyo”
Kwa maneno mengine anatuambia ya kuwa hili
jina la Yesu si lake “mwenyewe” bali la Baba yake ila amepewa ili
aje nalo na kujulikana kwa hili hapa duniani!
Wafilipi 2:9 inatuambia ya kuwa jina hili la Yesu ni “Jina
lile lipitalo kila jina”. Kwa hiyo ni rahisi kuwaza ya kuwa ikiwa jina
la Yesu ni Jina lipitalo kila jina – basi Mungu Baba hana jina jingine
ila hili jina la Yesu! Maana kama angekuwa na jina jingine – basi hilo
ndilo lingekuwa kuu kuliko jina la Yesu. Lakini kwa kuwa biblia
inatuambia jina la Yesu ni Jina lipitalo kila jina, ina maana Mungu Baba
anatumia Jina hili hili!
Huu ni uamuzi wa ajabu sana toka kwa Mungu Baba aliye
Mwenyezi! Kwa kulifunua Jina hili la Yesu, heshima ya pekee itokee
kutoka kwa vitu vyote “vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya
nchi” (Wafilipi 2:10). Kila mara Jina hili linapotajwa katika Roho na
kweli – vitu hivi vyote vinatega sikio na kuwa tayari kutii amri au
agizo litakalofuata na kulitekeleza “kwa utukufu wa Mungu Baba” (Wafilipi
2:11).
Hakuna maisha ya kikristo bila Jina
la Yesu!
Tunatamani sana upate nafasi ya kulitafakari sana Jina hili
la Yesu ili uweze kupata siri nzito zilizo ndani yake. Siri mojawapo ni
hii ya kwamba hakuna maisha ya kikristo bila Jina la Yesu! Labda tuseme
hivi huwezi kutenganisha Jina la Yesu na ukristo na maisha yako ya kila
siku! Ukristo bila Jina la Yesu si ukristo! Kwa nini tunasema hivi? Kwa
sababu:
1. Ikiwa
Umezaliwa mara ya pili au umeokoka basi ni kwa sababu pia unaliamini
Jina la Yesu!
Imeandikwa hivi juu ya wote waliompokea Yesu mioyoni na maishani mwao ya
kuwa:
“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa
kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa,
si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu,
bali kwa Mungu” (Yohana 1:12,13).
2. Jina la Yesu
linapaswa kuhusishwa na kila kitu unachofanya!
Imeandikwa hivi:
“Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo,
fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”. (Wakolosai 3:17)
Tena imeandikwa
hivi:
“….na kumshukuru Mungu Baba sikuzote
kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo” (Waefeso 5:20).
Tena imeandikwa
hivi:
“Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu
dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake” (Waebrania 13:14)
3. Kuna ishara
zitakazofuata kila utakapotumia Jina la Yesu!
Yesu mwenyewe alisema hivi:
“Na ishara hizi zitafuatana na hao
waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;
watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya” (Marko 16:17,18)
Tenga muda wa kulitafakari Jina
hili!
Kwa yule anayesoma Zaburi mara kwa mara hatakosa kuona ya
kuwa Mfalme Daudi alitumia muda mwingi kulitafakari Jina la Bwana hata
akaandika mengi juu ya jina la Bwana linavyohusika na maisha yake.
Tunataka tukutie moyo zaidi kwa barua hii ya kuwa mwezi huu
wa Disemba unapokumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo, kumbuka pia na
kutafakari pia ujio wa Jina hili la Yesu na sehemu yake katika maisha
yako.
Mwisho
Mungu wetu azidi
kukutia nguvu na tunaamini utasimama pamoja nasi katika kuifanikisha
kazi ya Mungu katika mwaka wa 2002. Watoto wetu na Timu nzima ya Huduma
ya Mana inawasalimu.
Ni sisi katika
utumishi wa Kristo,
Christopher na Diana
Mwakasege