Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya mwezi wa Julai, 2001

JE! UMEANGALIA KAMA IMANI YAKO IKO MAHALI INAPOTAKIWA?

Mpendwa katika Kristo,

            Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo. Tunashukuru kwamba umepata nafasi ya kuisoma barua hii na kuutafakari ujumbe tulioongozwa na Roho Mtakatifu kukuandikia.

            Tunajua ya kuwa kiu uliyonayo ya kutaka kujua zaidi juu ya Yesu Kristo ndiyo imekusukuma kusoma barua hii. Na tunaamini ya kuwa Roho Mtakatifu aliye pamoja nasi tunapoandika ujumbe huu, yuko pamoja nawe unapousoma? Je! umeangalia kama imani yako iko mahali inapotakiwa?

Tabia ya imani

            Kwa mtu yeyote aliyefuatilia kwa karibu juu ya somo la imani, atakuwa amegundua ya kuwa imani ina tabia yake. Kama unalijua hili basi ni vizuri sana na upo mahali pazuri. Lakini ikiwa ulikuwa hujui basi ngoja tukupe mifano michache.

  • Imani inaweza kuongezeka. Wanafunzi walimwambia Yesu awaongezee imani (Luka 17:5). Kama imani inaweza kuongezeka, basi inaweza kupungua pia!
  • Imani ina ngazi (levels) mbali mbali. Biblia inasema juu ya “…toka imani hata imani” (Warumi 1:17)
  • Imani inaweza kuwa kubwa. Yesu alisema “sijaona imani kubwa….” (Luka 7:9). Kama imani inaweza kuwa kubwa, basi inaweza kuwa ndogo pia!
  • Imani inaweza kuonekana. Yesu alisema, “Sijaona imani kubwa ….”. Pia imeandikwa katika Marko 2:5 ya kuwa “…. Akiiona imani yao …..” Ikiwa imani inaweza kuonekana, basi inaweza isionekane pia!
  • Imani inaweza kufa. Imeandikwa, “….imani pasipo matendo imekufa”. (Yakobo 2:26). Kama imani inaweza kufa basi inaweza kuishi pia!
  • Imani inaweza kujaribiwa. Imeandikwa, “….kujaribiwa kwa imani ……” (Yakobo 1:3). Ikiwa imani inaweza kujaribiwa au kupewa mtihani, basi, inaweza kushinda hilo jaribu au huo mtihani pia (1Yohana 5:4)!
  • Imani haifanyi kazi peke yake!Utaona ya kuwa imani inafanya kazi na matendo (Yakobo 2:20, 26), na kwa upendo ( Galatia 5:6; 1Wakorintho 13:2), na kwa uvumilivu (Waebrania 6:12) na kwa kinywa chako ( 1Timotheo 4:6; Marko 11:23)

Imani inaweza kuwekwa pasipostahili!

            Jambo hili tunaliona tunaposoma habari za Yesu na wanafunzi wake katika Luka 8:22 –25. Katika mstari wa 25 tunaona akiwauliza “Imani yenu iko wapi?” Ni dhahiri kutoka katika swali hili ya kuwa imani walikuwa nayo lakini waliiweka mahali pasipostahili!

            Kutokana na tatizo la bahari kuchafuka na upepo kuvuma kwa nguvu, wanafunzi walijikuta wanamwacha Yesu akilala na wakaweka imani zao katika uzoefu wao wa kuvua samaki baharini! Ndiyo maana hawakuona sababu ya kumpa Yesu usukani wa boti ili awe kiongozi wao. Uzoefu wao uliwasukuma kuhamisha imani zao toka kwa Yesu na kuweka katika nguvu na maarifa yao!

            Kwa nini hawakumpa Yesu uongozi wa boti lao? Na kwa nini tatizo la bahari lililopoanza hawakumwamsha hadi juhudi za uzoefu wao ziliposhindwa? Jibu tunalipata katika mstari wa 25! Hawakujua ya kuwa Yesu ana uwezo wa kutuliza upepo na bahari! Imeandikwa hivi:

“Akawaambia, Imani yenu iko wapi?   Wakaogopa, wakamaka, wakisema wao  kwa wao, ni nani huyu basi hata anaamuru upepo na maji, navyo vyamtii?”          

            Walikuwa wanajua Yesu anajua kuhubiri, kusamehe, kufundisha, kukemea pepo na kuponya magonjwa. Pia, walimjua Yesu kama Kristo na kama Mwana wa Mungu. Lakini hawakujua ya kuwa ana uwezo pia juu ya bahari na upepo hata kuweza kuvituliza vinapoleta shida kwa wanafunzi wake!

Je! Uko kama wanafunzi hawa?

            Unamfahamu Yesu na uweza wake kwa kiwango gani? Imani yako umeiweka wapi? Mazingira tunayoishi yamekuwa chanzo kikubwa cha imani za wengi kuwekwa mahali pasipostahili.

            Unapokabiliana na maisha ya kila siku au unapokabiliana na matatizo yanayokutokea mara kwa mara, au kama umo katikati ya majaribu au matatizo wakati huu, - imani yako umeiweka wapi? Je, ni kwenye kisomo chako? Je, ni kwenye ujuzi na uzoefu wako? Je, ni katika miaka mingi ndani ya wokovu? Je, ni kwa wanadamu wenye uzoefu katika eneo unalohitaji msaada? Je, ni kwenye fedha zako? Je, ni kwa watumishi wa Mungu unaowajua?

            Je, ni kwa kanisa lako – mahali unaposali? Je, ni kwenye maombi? Imani yako umeiweka wapi? Na hapo ulipoiweka, imekufa au inaishi? – inaongezeka au unapungua?

            Je! mahali ulipoiweka hiyo imani yako imekuzalia kitu gani? Au imekuzalia matunda ya namna gani? Au ulikuwa hujui ya kuwa imani inaweza kuzaa? Soma Yakobo 2:20. Na kama imani yako imezaa, imezaa baraka au laana, ushindi au kushindwa, furaha au huzuni, uvumilivu au kukata tamaa?

Ni kipindi gani hiki?

            Hiki ni kipindi ambacho Yesu anatakiwa kuchukua nafasi anayostahili katika kila eneo la maisha yetu. Kila eneo awe kiongozi! Usingoje hadi ukwame ndipo umtafute na kuumpa uongozi wa eneo lililokwama!

            Ni vizuri ujue ya kuwa Roho Mtakatifu anapoamsha kanisa au anapovuma kwa upya kama wakati huu katika nchi yetu – anatingisha imani yako akiikuta mahali pasipostahili! Nia yake ni kwamba uhamishe imani yako mahali ilipo na kuiweka inapostahili – yaani kwa Yesu Kristo! Ni kweli Yesu anaweza kutumia watu, au kisomo, au watu, au fedha, au kitu chochote anachotaka kukusaidia au kukufanikisha – lakini hataki uweke imani yako katika vitu hivyo! Weka imani kwake, na utukufu umrudishie Yeye peke yake! Yesu hashirikiani utukufu wake na kitu chochote au mtu yeyote!

Jambo la kufanya!

  1. Ikiwa, Imani yako haiko kwa Yesu katika eneo lo lote lile. Basi tubu na mwombe akusaidie kutokuamini kwako!
  2. Amini Neno la Mungu linavyosema juu ya Yesu Kristo na Roho wake Mtakatifu!
  3. Umpe Mungu nafasi ya kufanya katika maisha yako kile ambacho Neno limesema anaweza kufanya!

    Kwa sasa tuishie hapa. Tunaamini umepata jambo la kukusaidia katika ujumbe huu. Mara kwa mara angalia kama imani yako ipo mahali inapostahili. Usingoje hadi umekwama ndipo ugundue ya kuwa Yesu unae lakini umemwacha amelala na hana kazi ya kufanya kwa kuwa tu imani yako inatafuta msaada mahali pengine na si kwa Yesu!

    Sisi tunakupenda katika Kristo Yesu! Ni maombi yetu kwa Mungu ya kuwa imani yako idumu katika Kristo wakati wote, mahali popote na katika hali yo yote. Tuzidi kuombeana!

Ni sisi katika utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.