Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi Novemba 2001

UNAWEZA KUJIFUNZA KUOMBA KWA MAFANIKIO ZAIDI KULIKO UOMBAVYO SASA

Mpendwa katika Kristo Yesu,

            Tulipokuwa tukitafakari katika Roho juu ya yale ambayo Mungu anataka tukuandikie mwezi huu tuliona ndani yetu tunasukumwa kukutia moyo kwa kusema ya kuwa, “ Unaweza kujifunza kuomba kwa mafanikio zaidi kuliko uombavyo sasa”

            Tunaamini neema ya Mungu iko juu yako ili kukusaidia uzidi kuwa na kiu ya kufanikiwa katika maeneo na mambo yote katika Bwana. Ni lengo zuri na lenye nia nzuri ya kuona Kristo akijitukuza katika maisha yako.

            Kuna siku wanafunzi waliwahi kumwambia Bwana Yesu maneno haya: “Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake”. Hii inaonyesha jinsi ambavyo walitamani wawe na mafanikio mazuri katika maombi yao ya kila siku.

Kuna aina mbali mbali za maombi

            Kama vile kulivyo na aina mbalimbali za michezo ya mpira na taratibu za kucheza zinazotofautiana, na maombi ni vivyo hivyo. Kuna aina mbalimbali za maombi na taratibu zake za kuomba zinatofautiana.

            Kama vile ambavyo huwezi kutumia taratibu za kucheza mpira wa miguu katika kutaka zikusaidie ushinde unapocheza mpira wa vikapu, vivyo hivyo na maombi. Taratibu za kuomba maombi ya aina fulani zinaweza zikakufanya ushindwe kujibiwa maombi yako utakapozitumia katika maombi ya aina nyingine.

            Waefeso 6:18 inasema, “ Kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote”

            “Kwa sala zote” wakati mwingine ina maana ya “Kwa aina mbalimbali za maombi”. Kwa sababu neno “zote” linatumika kuonyesha ya kuwa kuna aina za sala au maombi zaidi ya moja. Na Mtume Paulo anataka tusali kwa sala zote. Huwezi kuomba sala zote kama huzijui zote! Unaweza ukajikuta unatumia aina moja tu ya sala au maombi katika kuombea shida zote ulizonazo, na unabaki unajiuliza kwa nini maombi mengine umejibiwa na mengine hujajibiwa.

            Kwa mfano, angalia aina zifuatazo za maombi na uzijue zinavyotofautiana:

  1.  Maombi ya kupokea wakati huo huo unapoomba (Marko 11:24)
  2.  Maombi yanayojua mapenzi ya Mungu juu ya jambo unaloliombea (1Yohana 5:14,15)
  3. Maombi unayoomba jambo ambalo huna uhakika kama ni mapenzi ya Mungu kwako au kwa yule unayemuombea. (Mathayo 26:36 – 42, Warumi 8:26, 27)

4.  Kuomba maombi bila kuacha kuomba hadi au mpaka umepata unachoomba. (Luka 18:1 –8, Luka 11:9 – 13, Isaya 62:6,7)

  1. Kuomba maombi ya kudai upewe haki yako. (Isaya 43:26)

Hii ni mifano michache tu ya maombi na matumizi yake na taratibu zake za kuomba vinatofautiana. Tunachoomba kwa Mungu kwa ajili yako unaposoma barua hii, ni ya kuwa “Bwana azidi kukufundisha kuomba kwa mafanikio kuliko uombavyo sasa”. Tunaamini Roho Mtakatifu yuko pamoja nawe katika kujifunza huku.

Tunahitaji maombi yako

            Tarehe 5 – 9 Disemba 2001 tutakuwa na semina ya Neno la Mungu Iringa Mjini itayojumuisha watu wa madhehebu mbalimbali. Tunahitaji maombi yako ili Mungu atumiminie upako wa mafuta ya Roho Mtakatifu katika kufanikisha maandalizi ya semina; na katika kufanikisha semina yenyewe katika kila eneo.

            Jina la Bwana na litukuzwe tunapozidi kukumbukana katika maombi.

Ni sisi watumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.