Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi Oktoba 2001

OMBA MUNGU AFUNDISHE KINYWA CHAKO KUTUMIA MANENO VIZURI.

Mpendwa katika Kristo,

            Tunakusalimu ni katika lile Jina lipitalo kila jina – Jina la Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, ambaye pia ni Bwana na Mwokozi wetu.

            Ni furaha yetu kukuandikia tena barua hii tukiamini ya kuwa ulikuwa unaingojea kwa hamu, hasa kwako wewe ambaye umekuwa ukisoma barua hizi kila mwezi. Pia, kwako wewe ambaye ni mara yako ya kwanza kusoma barua yetu hii tunayoiandika kila mwezi, tunasema Mungu wetu tunayemtumikia, na aliyetuongoza kuandika tunachoandika akupe neema ya kuelewa maneno yaliyomo katika barua hii.

Je! umewahi kuombea jambo hili?

            Je! umewahi katika maombi yako kwa Mungu kuomba kinywa chako kifundishwe kutumia maneno vizuri? – au kutumia maneno ipasavyo? Si rahisi kuona umuhimu wa kuomba maombi ya namna hii isipokuwa:

Kwanza:       Unajua umuhimu wa maneno katika maisha yako;

Pili:                 Unajua ya kuwa bila msaada wa Mungu kinywa chako hakiwezi kusema jinsi ikupasavyo kusema

                        Wengine wanajikuta wanaomba maombi ya namna hii hasa wanapoona wanahitaji maneno  yao yakubalike na wale wanaosema nao! Hili ni sawa lakini tunalotaka uone katika barua hii ni ule umuhimu wa kuongozwa na Mungu katika Roho Mtakatifu kusema maneno ikupasavyo kusema, kila wakati na kila mahali.

                        Tunasoma katika kitabu cha Kutoka 4:12 ya kuwa Mungu alimwambia Musa wakati akimtuma kwa Farao ya kwamba “nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalosema”. Ndivyo ilivyokuwa pia wakati Yeremia alipokuwa anaitwa kumtumikia Mungu na akajitetea ya kuwa yeye hawezi kusema kwa kuwa alikuwa mtoto bado. Mungu akamwambia, “Usiseme, mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema neno nitakalo kuamuru”. Halafu Mungu akagusa kinywa cha Yeremia na kumwambia; “ Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako” (Yeremia 1:6-9)

                        Ukifuatilia maisha ya Yesu alipokuwa hapa duniani alisema mara kwa mara ya kuwa Baba yake ndiye aliyekuwa anampa maneno ya kusema na jinsi ya kuyasema. Kwa mfano aliwahi kusema hivi:

 “Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, Yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo” (Yohana 12:49,50)

Utaona ya kuwa maneno kama haya Yesu pia aliyasema katika Yohana 8:26,38 na Yohana 14:24. Kama ilikuwa muhimu kwa Yesu kuongozwa maneno ya kusema na jinsi ya kuyasema na Mungu Baba yake na aliye Baba yetu pia, si zaidi sana sisi ambao ni wafuasi na wanafunzi wake? Ndiyo maana Mtume Paulo katika kitabu cha Waefeso 6:20 anawaomba watakatifu waliokuwa Efeso wakati ule wamuombee kwa Mungu ili apate ujasiri wa kunena jinsi impasavyo kunena!

Lazima kuna umuhimu wake!

Yes! Lazima kuna umuhimu wa kuongozwa na Mungu kusema maneno na jinsi unavyoyasema. La sivyo asingewasaidia wakina Musa, Haruni, Yeremia, Yesu, Paulo na wengine wengi ambao hatujawataja lakini biblia inasema walisaidiwa na Mungu kusema maneno waliyosema na walivyoyasema.

Zipo sababu nyingi zinazoonyesha umuhimu wa jambo hili, lakini katika barua hii tutakuwekea sababu hizi chache zifuatazo:

Sababu ya Kwanza: Maneno yana uwezo wa kubeba  na kuwapa wanaokusikiliza kitu ulichonacho ndani yako. Kwa mfano: Neema uliyonayo katika Kristo inawafikia wengine kwa njia ya maneno unayosema (Waefeso 4:29-31). Kumbuka neema inaokoa na pia inafundisha na kukuwezesha mahali ambapo hukustahili (Tito 2:11-13). Kama vile maneno yanavyoweza kumchafua mtu machoni pa watu wengine, vile vile kuna maneno yanayoweza kumsafisha au kumtakasa (Yohana 17:17). Kama vile ambavyo kuna maneno ambayo yakisemwa yanamfanya ayasikiye ahuzunike, vile vile kuna maneno yanayoweza kusemwa na kumpa mtu ayasikiaye furaha (Yohana 15:11). Pia kuna maneno ukisema yanabeba hekima ambayo hakuna asikiaye atakayeweza kushindana nayo (Luka 21:14,15)

Sababu ya Pili: Maneno yasiyokuwa na maana yana uwezo wa kudanganya wanaoyasikia, kuharibu tabia yao, na pia kuvuta hasira ya Mungu kwa wanaoyasema (Waefeso 5:6; Wakolosai 2:8; 1Wakorintho 15:33). Ndiyo maana tunashauriwa na Zaburi 1:1 kutokuketi barazani pa wenye mizaha. Maneno yasiyokuwa na maana ni maneno ambayo hayakutakiwa kusemwa na hayana faida katika Mungu kwa yule anayeyasikia (Mithali 15:23)

Sababu ya Tatu: Ulivyo na ulivyonavyo sasa ni matokeo ya maneno ambayo umekuwa ukiyasema na kuamini ya kuwa maneno hayo ni kweli au kuamini ya kuwa ndivyo yalivyo (Marko 11:23; Mithali 18:20)

Sababu ya Nne: Utakavyokuwa na utakavyokuwa navyo kesho ni matokeo ya maneno unayoyasema leo na kuamini ya kuwa maneno hayo ni kweli (Hesabu 14:1-38; Hesabu 13:30-33; Mithali 12:14)

Sababu ya Tano: Maneno yako yanauwezo wa kukutega na kukukamata (Mithali 6:2)

Sababu ya Sita: Unaposema unapanda unachosema (Mithali 13:2; Mithali 6:14,19). Unakula au unavuna matunda ya kile ulichopanda kwa midomo yako. Kumbuka maneno ni mbegu (Luka 8:11). Na apandacho mtu ndicho atakachovuna (Wagalatia 6:7). Ikifika wakati wa kuvuna unavuna kingi kuliko ulichopanda! (Luka 6:38)

Sababu ya Saba: Maneno yanayotoka katika kinywa chako yanawapa wale wanaokusikiliza kujua hali ya moyo wako na kujua kile kilichojaa ndani yake. Hii ni kwa sababu “mtu mwema katika hazina ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake” (Luka 6:45)

Sababu ya Nane: Unachosema kinaweza kuvuta nguvu ya Mungu kutekeleza ulichosema. Kwa mfano Wana wa Israeli waliotoka Misri walishindwa kufika Kaanani isipokuwa Yoshua na Kalabu kwa sababu ya maneno waliyoyasema. Maana walisema; “hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi” (Hesabu 13:31). Na Mungu akawajibu ya kuwa; “hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi” (Hesabu 14:28). Yule mama mwenye ugonjwa wa kutokwa damu aliposema – nguvu za Mungu zilivutwa kuja mwilini mwake kutekeleza alichosema (Marko 5:25-34). Na yule mjakazi wa Akida ndivyo alivyopona (Mathayo 8:5-13). Akida alimwambia Yesu, “sema neno tu, na mtumishi wangu atapona”. Yesu ‘alistaajabu’ kusikia imani kubwa ya namna hiyo, kwa hiyo akamwambia, “nenda zako na iwe kwako kama ulivyoamini”. Na mtumishi wa Akida akapona saa ile ile – kwa nini – kwa sababu nguvu za Mungu zilivutwa na maneno ya Akida kutekeleza alichosema!

Sababu ya Tisa: Unaposema unaandika unayoyasema moyoni au nafsini mwako au mwake yule akusikie. Na matokeo yake ni kusema na kutenda kile kilichoandikwa ndani yako. Au yule aliyekusikiliza atajikuta anasema na  anatenda kile kilichoandikwa ndani yake kwa kutumia vinywa vya watu (2 Wakorintho 3:2,3; Zaburi 45:1; Hesabu 30:1,2)

            Sikiliza! Tunaweza kuendelea kukuorodheshea sababu moja baada ya  nyingine, lakini tunaamini kwa hizi chache tulizokuandikia katika burua hii ni changamoto ya kutosha kukusukuma kuomba Mungu akupe maneno ya kusema na kukuongoza jinsi ya kuyasema,kila wakati na kila mahali. Tumeweka mistari mingi ya biblia katika barua hii tukiwa na lengo la kukupa hazina ya kujisomea mwenyewe zaidi juu ya ujumbe tuliokuandikia.

Habari za Huduma

Mwezi uliopita wa Septemba tulikuwa na semina ya Neno la Mungu Shinyanga Mjini ambayo ilihusisha madhehebu mbalimbali na watu kutoka Wilaya mbalimbali za Shinyanga. Tuliona Mungu akiokoa, akiponya na kujaza Roho Mtakatifu watu wake. Pia, tulipata nafasi ya kutangaza na kurusha mafundisho ya semina hiyo kupitia Radio Faraja inayomilikiwa na Kanisa Katoliki. Na hata baada ya kumaliza semina hiyo tumeingia mkataba na redio hiyo kuendelea kurusha masomo tuliyofundisha sehemu mbalimbali. Kwa hiyo sasa tuko hewani Mkoa wa Shinyanga kila Jumamosi na Jumapili kwa saa moja kuanzia saa tatu hadi saa nne kila wiki. Asomaye na afahamu! Na ukifahamu mshukuru Mungu pamoja nasi.

Mwezi huu wa Oktoba tutakuwa na semina mbili – Kilombero tarehe 17 – 21 Oktoba na Mbeya Mjini tarehe 23 – 29 Oktoba. Tunahitaji maombi yako. Na tarehe 9 – 11 Novemba tutakuwa Mererani.

            Mungu azidi kukubariki kwa kukubali kusimama pamoja nasi katika huduma hii ya kufundisha Neno la Mungu.

Ni sisi katika Utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.