Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi Aprili 2002

JE! UNAJUA YA KUWA UNAPOTOA SADAKA
MUNGU HATAFUTI MALI YAKO BALI IMANI YAKO?

Mpendwa katika Kristo,

            Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo.

            Tunamshukuru Mungu sana kwa kutupa nafasi nyingine ya kuwasiliana na wewe kwa njia ya waraka huu. Tena mwezi huu tumepewa neno ambalo tunaamini litakusogeza karibu zaidi na Mungu kama vile lilivyotusogeza sisi. Roho Mtakatifu ameweka swali hili ndani yetu kwa ajili yako linalosema hivi: “Je! unajua ya kuwa unapotoa sadaka,-Mungu hatafuti mali yako bali imani yako?

            Inawezekana unajua au hujui au huna uhakika. Kwa vyo vyote vile na katika hali yo yote ya uelewa uliyonayo, tufuatane pamoja katika kupitia na kutafakari neno la Mungu kwa nia ya kupata jibu la swali hili.

Kwa nini Mungu hatafuti mali yako?

            Watu wengi wanapotoa sadaka ndani yao huwa wana mawazo yanayodhani Mungu ni maskini ambaye anahitaji mali za wanadamu ili zimsaidie katika kazi yake. Kwa mantiki hii wanajenga mawazo yanayowafanya wao wawe ndio watoaji na Mungu kuwa mpokeaji! Lakini biblia ina maneno yanayotuma usahihi zaidi juu ya jambo hili. Imeandikwa hivi:

“Mungu aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa  kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote  uzima na pumzi na vitu vyote”(Matendo ya Mitume  17:24,25).

            Angalia tena maneno haya: “….wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na pumzi na vitu vyote”. Kama Mungu ndiye anayewapa wanadamu wote uzima na pumzi na vitu vyote, hii inaonyesha ya kuwa Yeye ndiye chanzo cha kila kitu tulichonacho.

            Wazo hili tunaliona tena likijitokeza katika Zaburi 24:1 ilipoandikwa ya kuwa: “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake”.

            Ikiwa kila kitu kinatoka kwa Mungu ina maana basi Mungu anapowataka wanadamu wamtolee sadaka ana kitu cha zaidi anachotafuta kutoka kwao! Na si mali zao! Baada ya kulitakari jambo hili kwa muda mrefu sasa tunaona yakuwa sadaka imewekwa na Mungu ili kusaidia kuimarisha uhusiano wake na wanadamu. Kwa msingi huu tunaweza kusema ya kuwa Mungu hatafuti wala kufuata mali zetu anapotutaka tutoe sadaka bali imani tuliyonayo kwake. Hebu tuangalia mifano michache:

Mfano wa 1: Habili na Kaini

            Je! unaelewa ni kwa nini Mungu alikubali sadaka ya Kaini lakini akaikataa sadaka ya Habili nduguye? Katika habari za hawa ndugu wawili tunasoma ya kuwa:

“Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi. Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi sadaka kwa Bwana. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana” (Mwanzo 4:2-5).

            Kama tunavyoona Kaini alikasirika sana kwa sadaka yake kutokubalika na Mungu. Mungu akashangaa kwa nini Kaini amekasirika na akamuuliza: “Kama ukitenda vyema, hutapata kibali….” Kwa tafsiri nyingine anamwambia ya kwamba “hakutenda vyema”. Kama angekuwa ametenda vyema sadaka yake ingekubalika, lakini kwa sababu hakutenda vyema sadaka yake ilikataliwa!

            Ni jambo gani la zaidi ambalo Habili alilifanya hata sadaka yake ikakubalika na Mungu? Ni jambo gani lililopungua katika utoaji sadaka wa Kaini hata kusababisha sadaka yake isikubalike? Maana wote walitoa kwa kadri walivyokuwa navyo. Kwa kuwa imeandikwa hivi: “….kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadri ya alivyonavyo mtu, si kwa kadri ya asivyo navyo” (2Wakorintho 8:12). Kama nia ya kumtolea Mungu sadaka wote (Habili na Kaini) walikuwa nayo, na kila mtu alitoa kwa kadri alivyokuwa navyo, ni kitu gani kilisababisha sadaka ya mmoja wao ikubalike na ya mwingine ikataliwe?

            Katika kitabu cha Waebrania 11:4 inatupa jibu la swali hili inaposema; “Kwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu iliyo bora kuliko Kaini; kwa hiyo alishuhudiwa kuwa ana haki; Mungu akazishuhudia sadaka zake, na kwa hiyo, ijapokuwa amekufa, angali akinena”. Siri iko hapa! Sadaka ya Kaini haikuwa mbaya, inawezekana ilikuwa ni nzuri, maana imeandikwa ya kuwa Habili alitoa “iliyo bora”. ‘Bora’ ni sifa ya ngazi ya juu zaidi ya ‘nzuri’. Kwa hiyo inawezekana sadaka ya Kaini ilikuwa ‘nzuri’, lakini ya Habili ilikuwa ‘bora’ na ikakubalika na Mungu kwa kuwa aliitoa kwa imani!

            Kwa hiyo tunaweza kusema katika utoaji wa hawa ndugu wawili Mungu alikuwa anatafuta kwanza imani zao kabla ya vitu walivyomtolea! Jifunze katika hili unapotoa sadaka, Mungu anatafuta kwanza imani yako kabla ya kupokea sadaka yako. Ukikosea kwenye eneo la imani, sadaka yako haikubaliki mbele za Mungu hata kama ni nzuri au kubwa kwa kiasi gani. Fikiria mwenyewe ikiwa umewahi kutoa sadaka yoyote ‘kubwa’ na ‘nzuri’ katika maisha yako, - ikiwa hukuitoa kwa imani hakupokelewa na Mungu, na hii inaweza ikawa ni sababu mojawapo ilioyofanya ‘kutokuvuna’ toka kwenye sadaka hiyo.

            Mfano wa 2: Mjane na Matajiri

            Tunasoma katika kitabu cha Marko 12:41,42 ya kuwa: “Naye (Yesu) akaketi kulielekea sanduku la Hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa”. Unadhani Yesu alikuwa anatafuta nini katika kuangalia sadaka zilivyokuwa zinatolewa? Unadhani ni uwingi na udogo wa sadaka za watoaji? La hasha! Bali alikuwa anataka kujua imani zao wameziweka wapi wanapotoa sadaka, kwa kuwa imani ndiyo inayoweka na kuamua thamani ya sadaka uliyotoa itakavyokuwa mbele za Mungu.

            Tunapoendelea kuisoma habari hii katika Marko 12:43,44 tunaona Yesu akiwaita wanafunzi wake; “….akawaambia, huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndivyo riziki yake yote pia”. Kwa tafsiri nyingine alikuwa anasema huyu mjane ametoa sadaka yake akiwa ameweka imani yake kwa Mungu na kwa hiyo thamani ya sadaka yake mbele za Mungu ikahesabika kuwa kubwa kuliko ya sadaka za wengine.

            Yesu alijuaje hili? Je! na sisi tunaweza kujua? Ndiyo! Kwa sababu Roho Mtakatifu aliyemfunulia Yesu juu ya hili yuko pamoja nasi kutufunulia ili tujifunze kumtolea Mungu sadaka zinazompendeza.

            Yesu alisema; “Huyu mjane ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina…..” na “….. katika  umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” Tukianza kutafuta imani ya mjane huyu alipoiweka tutagundua ya kuwa, hakuiweka katika sadaka aliyotoa. Maana ameitoa, tena yote na haimo mikononi mwake. Tunaposema imani tunamaana ya uhakika wa kuendelea ‘kula na kunywa’ baada ya kutoa sadaka yako. Tunaona pia ya kuwa imani hii huyu mama mjane hakuiweka katika fedha iliyobaki baada ya kutoa sadaka – kwa kuwa hakuwa amebaki na kitu. Kwa hiyo imani ya kuendelea ‘kula na kunywa’ baada ya kutoa sadaka aliiweka kwa Mungu – ndiye aliyemtegemea kumtunza baada ya kutoa sadaka. Kwa lugha nyingine alimweka Mungu ‘kwanza’ katika kumtemgemea badala ya kutegemea nguzu zake mwenyewe.

            Kwa wale matajiri, Yesu alisema; “….hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi…? Tukitafuta imani ya matajiri hawa tunaona ya kuwa imewekwa katika ‘fedha zilizobaki’ baada ya kutoa sadaka! Hawa walitoa katika sadaka baadhi ya fedha iliyowazidi. Kumbuka ‘sadaka’ inakuwa ‘sadaka’ inayokubalika inapotokea ya kwamba mahali ulipoitoa pameacha pengo ambalo unatarajia Mungu mwenyewe alizibe! Hawa matajiri hawakuwa wametoa sadaka ya namna hii – walitoa baadhi ya mali iliyowazidi, kwa hiyo hakukuwa na sababu ya kumtegemea Mungu – maana hawakuwa na pengo lolote! Baada ya kutoa sadaka, imani ya ‘kula na kunywa’ waliiweka kwenye mali iliyobaki na siyo kwa Mungu wala kwenye baadhi ya mali iliyowazidi waliyoitoa.

            Sasa tukuulize swali, je, unapotoa sadaka imani ya ‘kula na kunywa’ baada ya kuitoa hiyo sadaka huwa unaiweka wapi? Wengi huwa wanaiweka katika mali iliyobaki baada ya kutoa sadaka; ndiyo wanayoitegemea katika kuwalisha! Wengine wameweka katika ‘sadaka’  waliyoitoa, na kutegemea ijizalishe, lakini wamesahau ya kuwa hakuna mbegu au sadaka inayojikuza kwa sababu “mwenye kukuza ni Mungu” (1Wakorintho 3: 6,7). Sadaka ya namna hii isipozaa na kumletea matunda anakata tamaa na kuona utoaji haumsaidii kitu chochote. Lakini kosa lake ni mahali imani yake alipoiweka! Unapotoa sadaka, imani yako ya kuendelea kula na kunywa au kutunzwa baada ya kuitoa hiyo sadaka iweke kwa Mungu na siyo kwenye sadaka uliyoitoa au kwenye mali/fedha zilizobaki baada ya kutoa sadaka.

            Kabla ya kukueleza namna utakavyoweza kuipata imani ya namna hii tunataka tukupe mfano mwingine mmoja.

Mfano wa 3: Mtu Tajiri na Mali yake

            Katika kitabu cha Marko 10:17-30 tunasoma tena mfano mwingine unaotuonyesha ya kuwa katika kutoa sadaka Mungu anatafuta kwanza imani ya mtu aliyonayo kwake na si mali yake. Tunapoisoma habari hii tunaona ya kuwa mtu mmoja tajiri alikwenda kumuuliza Yesu namna atakavyoweza kuurithi uzima wa milele. Yesu akamwambia ikiwa amezishika amri za Mungu. Yule tajiri akasema “yote nimeyashika tangu utoto wangu”

            Yesu akamwambia “umepungukiwa na neno moja”. Yesu alikuwa ana maana gani? Yesu alikuwa anataka yule tajiri ajue ya kuwa katika ‘kushika amri’ Mungu alikuwa anatafuta ‘imani yake’ – lakini neno moja limepungua linalosababisha imani hiyo isionekane. Yesu akamwaambia; “Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate”. Yule tajiri hakufurahi na akaondoka kwa huzuni.

            Kwa nini Yesu alimwambia auze vyote na si vichache au vile vilivyomzidi? Kwa sababu moyo wake ulikuwa unategemea mali yake na siyo kumtegemea Mungu. Ndiyo maana alipoondoka Yesu alisema; “…..jinsi ilivyoshida wenye kutegemea mali (au walioweka imani zao katika mali) kuingia katika ufalme wa Mungu!” (Marko 10:24) “ Kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako” (Mathayo 6:21)

            Yesu alikuwa hatafuti mali au utajiri wa huyo mtu. Wala hakuwa anataka kumfilisi! Yesu alitaka kumsaidia ili aweke imani kwa Mungu na si kwenye mali zake. Lakini kwa sababu moyo wake uliambatana sana na mali zake kuliko kuambatana na Mungu alishindwa kutii agizo la Yesu.

            Hata wanafunzi wake walishindwa kumwelewa haraka katika hili kiasi kwamba Petro akauliza wao watapata nini, kwa sababu wameacha vyote na kumfuata. Yesu akasema; cho chote kile ambacho mtu atatoa kwa ajili yake na kwa ajili ya injili “atapewa mara mia sasa wakati huu…. na katika ulimwengu ujao uzima wa milele” (Marko 10:30).

            Kwa hiyo ukitoa sadaka na  imani yako ikawa kwa Mungu juu ya tegemeo lako baada ya kutoa sadaka, kile ulichotoa Mungu atakurudishia ‘mara mia’ wakati huu.

Imani hii unaipataje?

            Imani ya namna hii unaipata kwa kutii agizo au ahadi ya Mungu inayoambatana na utoaji huo ambao Mungu anataka utoe. Kwa sababu; “Imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo” (Warumi 10:17)

            Kwa hiyo lazima usikie neno la Kristo au ahadi ya Kristo inayohusiana na huo utoaji. Hii inakusaidia kuweka tegemeo lako kwa Mungu aliyekupa ahadi juu ya jinsi utakavyoishi baada ya kutoa sadaka hiyo. Imani ikiisha ingia ndani yako huwa ina tabia ya kutaka au kudai utekeleze agizo lililomo katika ahadi iliyoleta hiyo imani ndani yako. Hebu tuangalie mifano hii:

Ibrahim na Isaka

            Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Ibrahimu alipoambiwa amtoe Isaka kuwa sadaka ya kuteketezwa. Mungu alikuwa hatafuti kumuua Isaka au haja yake katika sadaka ya Isaka haikuwa ni Isaka bali alikuwa anatafuta imani ya Ibrahimu. Katika mazungumzo ya Mungu na Ibrahimu iliwekwa wazi ya kuwa imani ya Ibrahimu ya kuwa “ baba wa mataifa mengi” ilitakiwa iwe kwa Mungu na siyo mahali po pote.   Hii imani ya Ibrahimu isingeweza kuwa katika uwezo wao kwa sababu umri wao ulikuwa mkubwa kwa hiyo wasingeweza kuzaa mtoto ki-kawaida (Warumi 4:17-19). Ilimbidi Ibrahimu aweke imani hiyo kwenye ahadi ya Mungu kwa sababu ndicho chanzo cha imani aliyotakiwa kuwa nayo. Ndiyo maana imeandikwa hivi juu ya Ibrahimu; “Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutoamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu; huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi” (Warumi 10:20,21). Mungu anataka imani zetu zisiwe katika uwezo tulionao wa kuzalisha tunachotaka kizaliwe, bali ziwe katika ahadi za Mungu juu ya maisha yetu ya kila siku na ya baadaye.

            Imani ya Ibrahimu ya kuwa “baba wa Mataifa mengi” haikutakiwa iwe kwa Ishmaeli aliyemzaa na msichana wao wa kazi – Hajiri – bali iwe katika ahadi ya Mungu. Kwa hiyo Mungu alimwambia Ibrahimu akubaliane na wazo la mke wake la kuwafukuza Hajiri na mtoto Ishmaeli watoke katika nyumba yao ili wawe mbali nao (Mwanzo 21:8-21). Mungu anataka imani zetu zisiwe katika uwezo wa wengine kutuzalia au kutuzalishia kile tunachoona kitatusaidia kupata baraka alizotuahidi, bali imani zetu ziwe katika ahadi za Mungu alizosema nasi juu ya maisha ya kila siku na ya baadaye.

            Imani ya Ibrahimu ya kuwa “baba wa mataifa mengi” haikutakiwa iwe kwa Isaka hata kama ni njia ambayo Mungu anataka kuitumia kumbariki – bali imani iwe katika ahadi ya Mungu. Kwa hiyo Mungu alimwambia Ibrahimu amtoe Isaka awe sadaka ya kuteketezwa. Na Ibrahimu alipokubali kumtoa Isaka sadaka alikuwa anaonyesha imani yake kwa Mungu ya kuwa hajaiweka  katika Isaka( ambaye ni njia tu ya kupatia  baraka  Mungu akitaka kuitumia), lakini ameiweka katika Mungu  na ahadi yake.

            Ndiyo maana imeandikwa hivi: “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa ,akamtoa  Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee;naam , yeye aliyeambiwa,katika Isaka uzao wako utaitwa,akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu ;akampata tena toka huko kwa mfano”(Waebrania 11:17-19)

Mungu alitaka aweke imani yake kwake ili Mungu ndiye aamue ni kwa namna gani  atalitimiza neno alilo muahidi Ibrahimu. Ndiyo maana  Ibrahimu alipokuwa tayari  kumchinja Isaka kama sadaka- alimwambia asimchinje! Kwa nini? Kwa sababu  Mungu alikuwa hamtafuti Isaka ili amuue bali Imani ya Ibrahimu ili Isaka aendelee kukaa na Ibrahimu bila kuyumbisha imani ya Ibrahimu!

Ndiyo maana Mungu akasema ; “sasa ninajua ya kuwa  unamcha Mungu , iwapo hukunizuilia mwanao , mwanao wa pekee”(Mwanzo22:12). Mungu  akamrudishia Ibrahimu Isaka  wake, na badala yake akampa kondoo mume  amtoe sadaka  badala ya Isaka. Kwa lugha nyingine Mungu alitaka Ibrahimu ajue ya kwamba kuwa baba wa mataifa mengi  haitatimizwa kwa kupitia  kwa Isaka bali kwa Mungu ambaye ameandaa “kondoo mume” au Yesu Kristo awe chanzo cha kubariki mataifa mengi yawe uzao wa Ibrahimu(Wagalatia 3:13,14)

Mungu anataka imani zetu zisiwe katika njia alizotupa kutubariki au alizotupa ili tumtumikie bali imani zetu ziwe katika ahadi anazotupa kwa ajili ya maisha ya kila siku na ya baadaye. Mungu anataka njia alizotupa au mali  alizotupa ziwe kama ‘hazipo’ au ‘zimekufa’mbele yetu ili imani zetu zibaki  kwa Mungu ambaye “ndani yake yeye tunaishi;  tunakwenda , na kuwa na uhai wetu”(Matendo ya Mitume 17:28). Tukiviweka vitu hivyo au njia hizo katika ‘madhabahu’ na kuzitoa sadaka ili tusizitegemee – Mungu ataturudishia ili tuendelee kukaa navyo lakini pia atatupa na kondoo mume.

Nabii Eliya  na Mjane wa Serapta

Mungu alipokuwa akimtuma  nabii Eliya ili akalishwe na kutunzwa na mama wa Serapta  alikuwa anatafuta imani za wote wawili (Eliya na yule mjane) zikae katika ahadi zake na siyo katika mali walizonazo.

Mungu alitaka nabii Eliya asiweke imani yake kwenye kile chakula cha yule mjane bali kwa Mungu na ahadi yake aliyosema;”Ondoka, uende Serepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko.Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe” (1Wafalme17:9). Eliya asingeweza kuweka imani ya ‘kula na kunywa’ kwa kunguru na kwenye kijito cha Kerethi  kwa sababu kunguru alikuwa ameacha kuleta chakula  na kijito kimekauka.Tena  Eliya asingeweza kuweka kuweka imani yake  ya “kula na kunywa’ kwenye vyakula vya mama mjane wa Serapta , kwa sababu vilikuwa vichache sana. Kwa hiyo ilibidi aweke imani yake ya ‘kula na kunywa’ kwenye ahadi ya Mungu (1Wafalme17: 10-16)

Pia kwa mama mjane wa Serapta, Mungu alitaka aweke imani yake kwa Mungu na katika ahadi yake,na siyo kwenye vyakula alivyokuwa navyo. Ndiyo maana mara ya kwanza alisita kumtengenezea chakula kama alivyoamriwa kwa sababu alikuwa anaogopa kitatokea nini kwake na mtoto wake baada ya kutoa hiyo sadaka kwa Eliya. Hapa ndipo watu wengi wanakwama.Huwa wanashindwa kumtolea Mungu hasa wanapokuta ya kuwa  walichonacho au wanachotakiwa kukitoa ndicho kilichobaki na wakikitoa hawatabakiwa na kitu. Lakini ikiwa utaiondoa imani yako kwenye mali ulizonazo, au mradi ulionao , au fedha ulizonazo,au huduma uliyonayo, au njia uliyonayo, au kazi uliyonayo-ndipo utakapoiweka kwa Mungu  na ahadi yake aliyokupa katika kutoa huko utakakotoa. Na ndipo Mungu atakapokutimizia ahadi aliyokuahidia.

Mwisho

Tumekuandikia barua ndefu mwezi huu  na tunaamini Mungu amekupa nguvu na nafasi ya kuisoma na utaendelea kuyatafakari yaliyomo na kuyafanyia  kazi

Tuzidi kuombeana. Usiache kusoma masomo tunayoyatoa kila wiki kwa sasa yenye kichwa cha “JIHADHARI NA MAFUNUO”.

ni sisi katika utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.