Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi Desemba 2002 

NI TABIA YA MUNGU KUJIBU MAOMBI – USIKATE TAMAA

Salamu katika Jina la Yesu,

Katika mafundisho mengi ambayo Bwana Yesu Kristo aliyafundisha akiwa mlimani na wanafunzi wake, alifundisha pia juu ya maombi.

Yesu Kristo alisema,

“Ombeni, nanyi mtapewa, tafuteni, nanyi mtaona, bisheni, nanyi mtafungulikwa,kwa maana kila aombaye hupokea, naye atafutaye huona, naye abishaye atafunguliwa” (Mathayo 7:7,8).

Kwa maneno haya, na mengine mengi yaliyoandikwa katika biblia juu ya maombi, yanatufunulia, na kutuonyesha wazi juu ya tabia ya Mungu Baba, Mwenyezi juu ya maombi.

Tumewahi kusoma mahali fulani, mtu aliandika juu ya umuhimu wa mkristo kufahamu namna ya kuomba kunakoleta majibu.

Alisema hivi, “Ni muhimu zaidi kwa watu kujifunza kuomba kuliko kupata vyeti vya elimu ya kawaida”.

Hakuwa anamaaanisha kuwa elimu ya kawaida haina maana. La hasha! Lakini tulivyomwelewa ni kwamba alitaka watu waone umuhimu wa kujifunza kuomba. Na kwamba wayaweke maombi katika umuhimu unaostahili katika maisha yao ya kila siku.

Watu wanatumia muda mwingi, na fedha nyingi ili wapate kujifunza elimu hii ya kawaida. Hili ni zuri na linakubalika mbele za Mungu. Lakini inasikitisha kuona kwamba, watu wanatumia muda kidogo, ili kujifunza juu ya maombi.

Hii inatokana na watu kutojua maana ya maombi na umuhimu wake. Na pia huwa inatokana na watu kutopata majibu ya maombi yao kwa Mungu. Na wakati mwingine majibu hayo huwa yanachelewa.

Tatizo la kukata tamaa

Rafiki yetu mmoja alituambia maneno ambayo tunaona yanaelezea sababu ya sehemu kubwa ya watu kurudi nyuma kiroho.

Alisema hivi,

“Nimegundua siku hizi ya kwamba wakristo wengi wamerudi nyuma kiroho, kwa kuwa hawajapata majibu ya maombi yao!”

Tukamwambia, “Hiyo ni kweli kabisa!”

Akaendelea kusema, “Kuna mtu mmoja, ambaye alikuwa ameokoka siku nyingi, na ni mhubiri wa injili, ambaye ameamua kuacha wokovu, kwa kuwa alimwomba Mungu apate mtoto kwenye ndoa  yake, lakini alikuwa bado hajapata, wakati umekwisha kupita miaka kumi.

“Pia aliomba kwa Mungu ajazwe Roho Mtakatifu ili anene kwa lugha mpya, lakini miaka mingi imepita bado hajanena kwa Lugha Mpya. Kwa ajili hiyo siku hizi ni mpinzani mkubwa wa wokovu. Na anaona hata kunena kwa Lugha Mpya si jambo la kweli”.

Tulitafakari habari hii, na tuliona ya kuwa ndugu yetu huyu alikuwa amepatwa na tatizo la kukata tamaa.

Na wakati mwingine tulikutana na Mzee mmoja ambaye alitueleza matatizo ya magonjwa yaliyoikumba nyumba yake. Akatuambia mke na watoto wake wawili wana ugonjwa ambao hospitali zimeshindwa kuutibu.

Tukamwuliza, “Wewe ni Mkristo”?

Akajibu, “ndiyo”

Tukasema, “Unafahamu ya kuwa ukiomba lolote kwa Mungu utapewa, kama yasemavyo maandiko?”

Akasema “Niliwapeleka wagonjwa hawa kwa kiongozi wetu wa kanisa, na aliwaombea mara nyingi lakini hawakupona!”

Tukamwuliza tena, “Ulipoona hawajapona ulichukua hatua gani?”

Akajibu akasema, “Niliamua kuwapeleka kwa waganga wa kienyeji, na hadi sasa nimekwisha zunguka kwa waganga wasiopungua arobaini”

Tukamwuliza “Na je! Hali ya wagonjwa ikoje sasa?

Akasema, “Bado hawajapona, ingawa nimekwisha tumia fedha nyingi sana, bila mafanikio …..!!

Kwa kukosa majibu ya uponyaji wa familia yake, ndugu huyu aliamua kuvuka mipaka ya ukristo wake, na kutafuta njia nyingine ili apate msaada.

Pia, huyo alikuwa amekata tamaa, na kuona ya kuwa Mungu hatajibu maombi yake.

Hali ya namna hii imewasonga wakristo wengi sana, ambao kwa kutopata majibu yao kwa muda wanaotaka na kwa njia wanazotaka, wanaamua kutumia njia nyingine, ambazo ni kinyume na ukristo wao, ili wapate mahitaji yao.

Je! Sikio la Mungu ni zito kiasi cha kwamba hawezi kusikia maombi ya watu wake?

Lakini Biblia inasema,

“Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka hata usiweze kuokoa, wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia” (Isaya 59:1).

Na, vile vile kwa kujua hali ya wakristo ya kutokuwa na uvumilivu, imeandikwa ya kuwa

“Imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa” (Luka 18:1)

Inawezekana ya kuwa hata wewe unayesoma haya umo katika hali ya kukata tamaa-au unamfahamu mtu ambaye yumo katika hali kama hii ya kukata tamaa. Inawezekana  umemwomba Mungu juu ya hitaji lako, lakini hujapokea majibu. Na kwa sababu hiyo umeamua, au unajitayarisha kutumia njia nyingine iliyo kinyume na maadili ya Kikristo, ili kupata hitaji lako.

Sasa! Kabla ya kuchukua hatua hiyo, tulia kwanza na usome ujumbe huu, na uyatafakari yaliyomo, na uyatendee kazi; Kwa kuwa Roho wa Mungu, ameuweka ujumbe huu mikononi mwako, kwa makusudi kamili ya kuinua maisha yako ya maombi.

Na utakapozidi kuyatafakari yaliyomo utaona ya kuwa ni tabia ya Mungu kujibu maombi ya watu wake. Na ukijua hili, utaona ya kuwa si busara mtu kukata tamaa ya kujibiwa, unapomwomba Mungu kitu.

Maana ya Maombi

Maombi ni neno ambalo watu wengi ambao wanalitumia hulitumia tofauti na maana yake halisi ilivyo.

Maombi si kukariri maneno fulani na kuyasema huku umefumba macho au umepiga magoti. Maombi ni zaidi ya kufanya haya!

Kuna maombi ya namna mbali mbali, ambayo yanaombwa kwa jinsi tofauti, kwa kufuatana na imani ya mtu. Lakini yote yanaitwa maombi.

Maombi ni mazungumzo kati ya mwombaji na yule anayeombwa, awe ni Mungu, shetani, au mtu yeyote yule.

Na kwa sisi wakristo, maombi ni mazungumzo kati ya mkristo na Mungu wetu, kwa njia ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, Bwana na Mwokozi wetu.

Mungu yule ambaye Wana wa Israeli, waliogopa hata kusogea mahali alipo, sisi tumepewa nafasi ya kumsogelea Mungu kwa damu ya Yesu Kristo (Waebrania 10:19,20)

Ni tabia ya Mungu kujibu maombi ya wateule wake, kama ahadi zake zinavyotueleza.

Watu wengi wanaongea na Mungu kwa njia ya maombi, lakini huwa hawako tayari kusikiliza Mungu anawaambia nini. Wengine wanazungumza na Mungu bila ya kuwa na uhakika ya kuwa watajibiwa.

Lakini ukisoma maandiko matakatifu, na ahadi za Mungu utaona mahali pote alipowaambia watu waombe ameahidi kujibu. Kwa mfano amesema hivi:

“Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.” (2Mambo ya Nyakati 1:14,15)

“Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua”  (Yeremia 33:3)

“Ombeni, nanyi mtapewa, ……. kwa maana kila aombaye hupokea” (Mathayo 7:7,)

“Tena siku ile hamtaniuliza neno lolote, Amin, amin, nawaambia, mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu, ombeni, nanyi mtapata, furaha yenu iwe timilifu”. (Yohana 16:23,24) 

Wengi hawana furaha ya kweli katika maisha yao kwa kuwa wameomba, lakini hawajapata walichokiomba. Kwa kuwa bado hujapata ulichokiomba, haimaanishi ya kwamba Mungu hajibu maombi. Mistari hiyo tuliyosoma ni baadhi tu ya ile inayotuonyesha tabia ya Mungu ya kujibu maombi.

Maombi ni kuzungumza na Mungu, na Mungu aseme na wewe, Watu wengi wameifahamu siri hii kwa muda mrefu, kama tunavyosoma katika agano la kale.

Unapoomba uwe na utayari wa kupokea na siyo utayari wa kutokupokea. Ni tabia yake Mungu kukujibu maombi yako.

Usikate Tamaa

Kukata tamaa ni kutokuamini. Kutokuamini ni kutokuwa na uhakika. Kutokuwa na uhakika kunazaa hofu na wasiwasi. Hofu na wasiwasi vinazaa kusita sita. Kusita sita ni jamii ya mashaka. Mwenye hali ya namna hii asitegemee kupokea kitu toka kwa Bwana (Yakobo 1:6-8).

Ukiomba utapewa, uwe na uhakika na jambo hili, kwa kuwa ndivyo Baba alivyotuahidi.

Ibrahimu aliomba kwa ajili ya watakatifu wa Sodoma na Gomora, Mungu alimjibu (Mwanzo 18:16-33)

Musa aliwaombea msamaha wana wa Israeli, Mungu akamjibu na akawasamehe (Kutoka 32:9-14).

Eliya aliomba Mungu ajidhihirishe kwa wapinzani wake, akasikiwa na moto ukashuka toka mbinguni (1Wafalme 18:30-40)

Eliya aliomba mvua isinyeshe juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na nusu, akasikiwa na Mungu, na mbingu zikafungwa (Yakobo 5:17). Pia, baada ya miaka hiyo mitatu na nusu aliomba kwa bidii mvua inyeshe, - na Mungu akajibu na mvua ikanyesha.

Yesu Kristo alituombea msamaha Mungu akatusamehe, na hadi leo bado tunaendelea kuupokea msamaha huo, kwa njia ya msalaba – kila tunapotubu dhambi zetu.

Kanisa liliomba kwa juhudi, wakati wa Mtume Petro, alipokabiliwa na hukumu ya kifo, na Mungu akajibu kwa kumtuma malaika kumfungua (Matendo ya Mitume 12:5-19).

Elizabeth na Zakaria waliomba wapewe mtoto katika ndoa yao, Mungu akawajibu kwa kuwapa Yohana (Luka 1:5-48).

Omba, nawe utapewa. Usiwe mwepesi kukata tamaa. Mungu si mwanadamu hata aseme uongo. Ni tabia yake kujibu maombi ya watu wake.

Tunamwabudu Mungu yule yule wa Ibrahimu, wa Musa, wa Eliya, wa Yoshua, wa Yesu, wa Mitume. Wala hana kigeu-geu. Aliloahidi analifanya. Ameahidi kujibu maombi, kwa hiyo uwe na utayari wa kupokea.

Si tabia ya Mungu kutokujibu maombi ya watoto wake.“Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema , je! si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?” (Mathayo 7:9-11).

Ni furaha ilioje kwa mtoto kujua kuwa atapewa na Baba yake kile alichomwomba? Je! si zaidi sana sisi tulio wana wa Mungu katika Kristo, kwa kuwa Baba ameahidi kutufurahisha kwa kutupa tuombayo?

Kama ulikuwa umefika hali ya kukata tamaa, na kuona Mungu hajasikia kilio chako, tunakuambia ujipe moyo mkuu, kwa kuwa Mungu ameahidi kukupa ulichoomba sawa sawa na mapenzi yake juu yako.

Je! unaweza kwenda kuomba kitu kwa mtu ambaye unajua ni mnyimi ambaye hatakupa kile utakachomwomba hata kama anacho?

Je! unaweza kuomba kwa Mungu ambaye hajali wala hajibu maombi ya watu wake? Iko faida gani ya kumwamini na kumtumikia Mungu wa namna hiyo?

Lakini tunaye Mungu anayejibu kwa jina la Yesu Kristo! Huyu ndiye tunayemwamini. Watu wa kale waliijua siri hii. Hata mfalme Yehoshefati alipokuwa amezungukwa na majeshi ya adui, aliomba kwa Mungu ajibuye, na Mungu akampigania na kuwaangamiza maadui (2 Mambo ya Nyakati 20:1-30) – Ukiwa na matatizo mwombe Mungu naye atakusaidia.

Weka hili katika roho yako. Ni tabia ya Mungu katika Yesu Kristo kujibu maombi ya watu wake.

Na usidhani ya kuwa ahadi za Mungu ni kwa Wakristo fulani tu. La hasha, bali ni kwa kila mkristo. Kwa kuwa imeandikwa ‘kila’ aombaye hupokea (Mathayo 7:8). Neno ‘kila’ lina kujumlisha na wewe! Nafasi yako uliyopewa usimpe mtu mwingine. Simama katika nafasi yako ndani ya Kristo, kwa kuwa ukiomba utapewa!

Kiini cha furaha ya Mkristo, ni mawasiliano yasiyokatika kati yake na Mungu wake. Bila kujibiwa maombi, wokovu unakosa ladha inayotamanika na kutumainisha. Furaha ya wokovu ni pamoja na kujibiwa maombi. Kwa hiyo hakikisha unajifunza na kufahamu kuomba maombi yanayojibiwa.

Hujajibiwa maombi yako bado?

Ukiomba na ukaona maombi yako hayajibiwi jiulize maswali haya yafuatayo halafu jirekebishe ipasavyo:

1.      Je! umewasamehe waliokukosea kabla ya kuomba? (Marko 11:25,26)

2.      Je! una mashaka na maneno uliyoyasema ulipokuwa unaomba? (Marko 11:23)

3.      Je! una hali ya kusita sita moyoni mwako? (Yakobo 1:5-8)

4.      Je! unachokiomba unataka kitumike kwa utukufu wa Mungu au kwa kukidhi tamaa yako tu? (Yakobo 4:3)

5.      Je! maneno ya Kristo yamo ya kutosha ndani yako? (Yohana 15:7)

6.      Je! wewe ni mtendaji wa neno la Kristo? (Yohana 2:17-26)

7.      Je! umeomba kwa Jina la Yesu Kristo? (Yohana 16:23,24)

8.      Je! unajisikia kukata tamaa? (Luka 18:1-8)

9.      Je! umetubu dhambi zako? (Isaya 59:1,2)

10.  Je! moyo wako unakuhukumu? (1Yohana 3: 21-23)

11.  Je! umeomba sawa sawa na mapenzi yake? (1Yohana 5:14,15). Kumbuka Neno lake linafunulia mapenzi yake.

Kumbuka yafuatayo

1.      Kwa kuwa Yesu Kristo hajabadilika, Ni yeye yule, jana, na leo, na hata milele; na ya kuwa hana upendeleo, ukikata tamaa ina maana imani yako kwake imeyumba. Kwa sababu kukata tamaa ni kinyume cha imani. Imani ni kuwa na uhakika (Waebrania 11:1), na kukata tamaa ni kutokuwa na uhakika. Palipo na imani hakuna kukata tamaa. Ukikata tamaa maana yake imani yako imeondoka juu ya kitu hicho ulichokikatia tamaa.

Inawezekana ni jambo ulilokuwa unaliombea au kulitafuta kwa muda sasa. Na kwa sababu hiyo au umeacha kuomba au unakaribia kuacha kuliombea, au tayari umeingiwa na mawazo ya kuwa si mapenzi ya Mungu upate unachokiombea kwa sababu tu hujajibiwa. Je! ni kazini? Ndoa yako? Wazazi wako? Mume wako? Mke wako? Watoto wako? Mwenzi wa maisha? Fedha? Masomo? Madeni? Huduma? Kanisani kwako? Biashara? Nyumba ya kuishi?

2.      Kuna vyanzo mbalimbali vinavyoweza kumfanya mtu akate tamaa hata kama anasema ameokoka. Biblia imetupa mifano ya namna ya kukabiliana na hali hizo. Mifano ya vyanzo vinavyoweza kukukatisha tamaa ni hii:

(i)                 Chanzo cha Kwanza ni Mungu kuchelewa kujibu maombi yako. Yesu alisema imetupasa kumwomba Mungu siku zote, wala tusikate tamaa. Habari hii imo katika Luka 18:1-8. Pamoja na kwamba inawezekana Mungu anakuvumilia tu kwa sababu kuna jambo unalofanya ambalo halimfurahishi, hategemei uache kuomba kwa kuwa amechelewa kukujibu katika wakati uliotaka. Endelea kuomba. Kuacha kuomba na kukata tamaa, ni kuonyesha ya kuwa imani yako ina shida.

·        Katika Luka 11:5-13 Yesu Kristo pia ametoa mfano mwingine wa mtu na rafiki yake. Jambo alilokuwa anasisitiza ni lile lile la “kutokuacha kuomba”. Akitaka tuombe hadi tupewe, tubishe au tupige hodi hadi tufunguliwe; na tutafute hadi tuone.

·        Katika Mathayo 15:21-28 tunaona mfano wa mama mkananayo ambavyo imani yake kwa Yesu haikumpa nafasi kukata tamaa au kukatishwa tamaa. Mara ya kwanza Yesu hakumjibu Neno. Ungeweza kutafsiri ya kuwa Mungu alikaa kimya! Je! umewahi kuwa na hali ya namna hii? Kuona kama Mungu amekunyamazia au hakujibu kitu? Je! umeamua nini? Je! hali ya kutojibiwa imekukatisha tamaa? Yule mama Mkananayo hakukata tamaa hata baada ya wanafunzi wa Yesu kutoona uzito wa tatizo lake. Yesu aliendelea kujitetea ili asimsaidie yule mama mara mbili zaidi, kabla ya kumponya binti yake. Huko kung’ang’ania kwa mama huyo katika kumwomba msaada – Yesu aliita hali hiyo “Imani Kubwa”

(ii)               Chanzo cha pili kinachoweza kukukatisha tamaa ni maneno ya wanaomzunguka Yesu

·        Mfano wa kipofu Bartimayo katika Marko 10:46-52 unatupa picha nzuri ya hali hiyo. Usifikiri kila mtu aliye na Yesu au ameokoka atataka upate msaada toka kwa Yesu kabla yake. Wakati huyo kipofu alipopaza sauti yake kumwita Yesu ili amsaidie; Waliomzunguka Yesu walimkemea ili anyamaze! Biblia inasema; “….lakini alizidi kupaza sauti”. Na Yesu akasimama, akasikiliza shida yake na kumponya. Fikiria kama angekatishwa tamaa na kule kukemewa na wale waliokuwa karibu na Yesu – ni wazi kwamba asingepata uponyaji wa macho yake! Je! kuna maneno yaliyosemwa juu yako na wale ‘walio karibu na Yesu’ na yamekukatisha tamaa katika maisha yako ya wokovu na ukristo wako? Je! ni katika huduma yako? Tunataka tukutie moyo ya kwamba endelea kumwita Yesu na kumtumikia. Maana katikati ya maneno mabaya na kukukatisha tamaa namna hiyo, Yesu bado atakusikiliza usipokata tamaa!

(iii)             Chanzo cha tatu kinachoweza kukukatisha tamaa ni mapokeo na mipaka ya dini yako. Tunafundisha hili tukitumia mfano wa mwanamke mwenye kutoka damu katika Marko 5:25-34. Huyu mama hakukubali vizuizi vya dini ya kiyahudi kwa akina mama “wenye kutokwa damu,” vimzuie kutafuta uponyaji kwa Yesu. Na wewe usikubali dini yako na mapokeo yake vikuzuie kutafuta msaada kwa Yesu.

(iv)             Chanzo cha nne kinachoweza kukukatisha tamaa ni mazingira yanayokuzunguka unapotaka msaada kwa Yesu. Mfano mmojawapo ni watu waliobomoa dari ili kumpitisha mgonjwa wao afike mbele ya Yesu. Soma habari hii katika Marko 2:1-12. Hawa watu wangeweza kukatishwa tamaa na umati wa watu, na kutokuingilika kwa Bwana Yesu. Lakini imani waliyokuwa nayo iliwapa kutafuta njia ya kumfikia Bwana Yesu. Wangekata tamaa wangerudi nyumbani na rafiki yao bado mgonjwa. Yesu aliona ‘imani yao’ katika ‘njia’ waliyotumia kumfikisha mgonjwa mbele yake bila kukatishwa tamaa na mazingira magumu waliyoyakuta mahali Yesu alipokuwa.

Nia yetu ni kuona unajibiwa maombi yako unapoomba kwa Mungu, hasa unapojua ya kuwa ni tabia ya Mungu kujibu maombi ya watoto wake.

                  Tuzidi kuombeana.

ni sisi katika utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.