Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi Februari 2002

Je! Unajua ya kuwa Roho Mtakatifu ni Msaidizi aliyetumwa na Mungu kutusaidia?

Mpendwa katika Kristo,

        Salamu katika Jina la Yesu Kristo!

        Tunajua inawezekana kabisa ya kuwa unamjua Roho Mtakatifu au kama humjui basi umewahi kusikia habari zake au pia inawezekana umewahi kusoma habari zake katika vitabu mbalimbali.

        Tunaona ya kuwa katika kitabu cha Yohana Mtakatifu, Yesu Kristo alimtambulisha Roho Mtakatifu kama ‘Msaidizi’ mara nne! Soma mistari ifuatayo:

        Yohana 14:16,17 inasema hivi:

"Nami nitamwomba Baba, naye atawapa MSAIDIZI     mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu."

        Yohana 14:26 inasema hivi:

"Lakini huyo MSAIDIZI, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba  atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia"

        Yohana 15:26 inasema hivi:

"Lakini ajapo huyo MSAIDIZI, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia."

        Yohana 16:7 inasema hivi:

"Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi nisipoondoka, huyo MSAIDIZI hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu."

Kwa nini MSAIDIZI alitumwa?

        Msaidizi siku zote anatumwa kwa sababu msaada wake ni muhimu kwa yule anayehitaji msaada. Ukisoma maandiko mbalimbali katika biblia utoana ya kuwa Yesu Kristo alipopaa na kuketi mkono wa kuume wa Mungu alimwambia Baba yake ya kuwa sisi tuliomo ulimwenguni tunahitaji msaada ili tuweze kuona, kuingia, kufanya na kudumu katika mapenzi ya Mungu. Kwa hiyo Roho Mtakatifu ambaye ni Msaidizi alitumwa kwetu ili kutusaidia.

        Msaidizi anapotumwa huwa anabeba msaada ambao anajua utamsaidia yule anayehitaji msaada. Si watu wengi wanaojua ya kuwa msaada wanaohitaji ili kutatua matatizo waliyonayo umo ndani ya Roho Mtakatifu. Na si wengi pia wanaojua ya kuwa Roho Mtakatifu anatumia UPAKO kama njia mojawapo ya kutusaidia au ya kutupa msaada tunaouhitaji.

        Neno "Upako" kama linavyotumika sasa katikati ya watu wa Mungu linatokana na maneno katika biblia yanayosema "kutiwa mafuta" (Luka 4:18). Lakini pia neno hili "Upako" limetafsiriwa katika sehemu zingine katika biblia kama ‘nguvu ya Mungu’ (Matendo 1:8), au ‘uweza wa Bwana’ (Luka 5:17), au ‘mkono wa Mungu’ (1Petro 5:6) au ‘kidole cha Mungu’ (Luka 11:20), nakadhalika.

Je! unajua ya kuwa:

Huwezi kutafuta msaada ambao unaona huna shida nao;

Huwezi kutafuta msaada ambao unaona hautakusaidia kutatua shida yako;

Huwezi kutafuta msaada ambao hujui kama upo, na hata kama unajua upo lakini hujui namna ya kuupata;

Huwezi kuletewa msaada wakati hutaki kusaidiwa;

Huwezi kutafuta kusaidiwa kama hutaki kusaidiwa

Unaweza pia ukawa unataka kusaidiwa lakini humtaki huyo anayekuletea msaada!

Unaweza pia ukawa unataka kusaidiwa lakini hutaki msaada unaoletwa hata kama huna tatizo na anayeleta huo msaada!

Imani huja kwa kusikia….

        Warumi 10:17 inasema; "Basi, imani chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo".Mtu anayetaka kusaidiwa mara nyingi kitu kinachomfanya atafute msaada ni KUJUA kitakachotokea baada ya kuupata huo msaada katika eneo analotaka kusaidiwa. Ndiyo maana mtu mgonjwa anayetaka kupona ugonjwa unaomsumbua atatafuta uponyaji kila mahali anaposikia unaweza kupatikana.

        Upako ni msaada uliotumwa kwetu na Mungu katika jina la Yesu Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu. Watu wengi hawautafuti upako wala Roho Mtakatifu ambaye ndani yake kuna upako kwa sababu hawajasikia habari zake wala faida zake! Ikiwa wewe umesikia habari zake na unajua faida zake mbona basi huonyeshi kiu ya kutosha ya kuonyesha ya kuwa unahitaji? Au kuna njia nyingine unayotumia kupata masaada unaouhitaji katika maisha yako? Maana kama unahitaji msaada toka kwa Mungu, ni muhimu ujue ya kuwa Roho Mtakatifu ni Msaidizi aliyetumwa na Mungu ulimwengu akiwa amebeba msaada wa kutusaidia tunaouhitaji.

Tafakari mifano hii!

        Kwa nini nabii Elisha aliomba roho (upako) maradufu iliyokuwa juu ya nabii Eliya imshukie? Soma habari hii vizuri katika kitabu cha 2 Wafalme 2:1-15.

        Ni kwa sababu alijua ya kuwa Eliya anaondolewa kwake na ya kuwa hatakuwa pamoja naye wakati anavuka mto Yordani mara ya pili. Na kwa kuwa alijua siri iliyomsaidia Eliya kuvuka mto Yordani kwamba haikuwa nguo yake bali roho iliyokuwa juu yake; na kwa kuwa alijua atakuwa peke yake bila Eliya atakapovuka mto Yordani tena, akaomba apate roho hiyo maradufu au upako huo maradufu.

        Sikiliza! Kama kuna mtu aliyekusaidia kuvuka mara ya kwanza katika tatizo ulilonalo, tafuta kuijua siri iliyomfanya kukusaidia ukavuka, ili hata kama hayupo uweze kuvuka mwenyewe kwa kuitumia wewe siri hiyo aliyoitumia yeye kwanza.

        Wayahudi wangapi waliovuka bahari ya Shamu wakiongozwa na Musa waliijua siri ya upako (au mkono wa Mungu) uliokuwa juu ya fimbo ya Musa? Soma kitabu cha Kutoka 4:1-5; Kutoka 14:15-18). Hata kama wangetaka kurudi Misri peke yao bila Musa baada ya kuvuka bahari ya Shamu mara ya kwanza wangekwama kwa sababu hawakujua siri iliyomfanya Musa akawavusha mahali pakavu mara ya kwanza.

        Wale waliokuwa karibu na Musa walipokuwa wanavuka bahari ya Shamu, ilikuwa rahisi kuona ya kuwa ni ‘fimbo’ iliyofanya wakavuka. Kwa hiyo kila mtu angeanza kuiga kutembea na fimbo kama Musa na kuishika na kuitumia kama Musa alivyofanya! Tofauti yake ingekuwa fimbo ya Musa siku zote ingekuwa na matokeo tofauti, yaliyo bora, na yenye mafanikio zaidi kuliko ya fimbo zao!

        Kwa hiyo tunakuambia na kukushauri hivi; Don’t just follow METHODS but follow the ANNOINTING behind the success of various methods! Mafanikio hayamo kwenye mbinu au njia unayotumia bali yamo katika upako unaowezesha mbinu au njia fulani ifanikiwe!

        Kumbuka siyo "kupiga maji kwa fimbo" bali upako wa Roho Mtakatifu uliofanya njia hii ya kupiga maji kwa fimbo ifanikiwe kupasua bahari ya Shamu. Tena, siyo "kupiga maji kwa nguo ya Eliya" bali upako wa Roho Mtakatifu uliofanya njia hii ya kupiga maji kwa nguo ya Eliya ikafanikiwa!

Mwisho!

        Ni maombi yetu ya kuwa katika barua hii Mungu ameamsha nia na kiu zaidi ndani yako ya kumjua zaidi Roho Mtakatifu na upako wake. Mungu na akuhekimishe na kukufunulia zaidi juu ya Msaidizi huyu wa ajabu!

        Tuzidi kuombeana!

ni sisi katika utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.