Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi Januari 2002

JE! UMEPATA NENO LA KUKUONGOZA MWAKA 2002

Mpendwa katika Kristo Yesu;

            Salamu za upendo tunakuletea katika Jina la Yesu Kristo, Mwana wa Mungu na Mwokozi wetu.

            Tunaamini umemaliza mwaka 2001 vizuri na kwa neema ya Mungu umeingia na kuanza mwaka huu wa 2002. Sisi tunamshukuru Mungu kwa kutupa nafasi nyingine tena ya kutumika pamoja naye katika shamba lake. Na Mungu, kwa njia ya Roho wake Mtakatifu, ametupa Neno la kutusaidia na kutuongoza mwaka huu. Neno lenyewe ni hili:

“ Basi, ‘Bwana’ ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru”  (2 Wakorintho 3:17)

            Hili ndilo Neno tulilopewa sisi kwa ajili ya mwaka 2002. Kila mwaka Mungu huwa  anatupa Neno la kusimama nalo kwa mwaka unaohusika. Nasi tumeona katika barua hii tukuulize ikiwa Mungu amekupa Neno la kukuongoza mwaka 2002. Na kama bado hujapata, basi umwombe Mungu ili akupe Neno kwa ajili yako. Ni muhimu sana!

            Ikiwa unaamini ya kuwa ni Mungu aliyekupa neema na nafasi ya kuufikia na kuishi katika mwaka 2002 – basi liko Neno aliloliandaa kwa ajili yako! Inawezekana jambo hili ni jipya kabisa machoni pako. Pia, inawezekana unalijua, lakini siyo jambo unaloliwekea umuhimu unaostahili.

            Kumwomba Mungu akupe Neno lake kwa ajili ya mwaka huu ni muhimu kwa sababu zifuatazo:

1.     Neno hilo linakusaidia kujua mawazo ambayo Mungu anakuwazia kwa mwaka huu:

Mungu anasema katika Yeremia 29:11 ya kuwa; “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani, wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” Pia katika kitabu cha Isaya 55:8-9 anasema hivi; “ Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu”.

      Halafu katika Isaya 55:10,11 anaendelea kutuambia ya kuwa,

“ Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu ampandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma”.

      Hapa tunajifunza ya kwamba katika neno analotupa toka katika kinywa chake tunapata kujua mawazo yake anayotuwazia; njia zake anazotuongoza ili tupite humo.

      Lakini pia kwa wale wapandaji (yaani wapelekaji)  wa neno lake kama sisi neno hilo tunapopewa linatupa mbegu ya kupanda, pia, linatusaidia kunyweshea maji kama mvua mioyo (ardhi) ya watu ili zile mbegu tulizopanda mwaka jana zichupue! Wakati huo huo ambapo neno hilo linapokuwa mbegu ya kupanda mkononi mwa mpanzi; pia na wakati huo huo, neno hilo hilo linakuwa chakula kwa alaye!

      Kwa mfano kwetu sisi tumepewa neno hili la 2 Wakorintho 3:17 ina maana katika neno hili tunapata yafuatayo:

  •      Mawazo anayotuwazia sisi na wale aliotupangia tuwahudumie mwaka 2002. Kwamba tukusudie kumpa Roho Mtakatifu nafasi anayostahili ili kutuweka huru katika maeneo yote maishani mwetu ambayo hayako huru kama ipasavyo katika Kristo Yesu!

  •      Njia au mipango yake kwa mwaka 2002. Kwa sababu imeandikiwa; “Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu” (Zaburi 119:105)

  •       Tutaona Bwana akilithibitisha neno hili kwa ishara na miujiza (Marko 16:20); kwa kuwa Mungu ana tabia ya kuliangalia na kulifuatilia neno lake na kulitimiza (Yeremia 1:12). Kwa hiyo imani inaongezeka ndani yetu (Warumi 10:17) ya kutegemea na kutarajia kumwona Mungu kwa upya na kwa nguvu zaidi kuliko miaka iliyopita!

2.       Neno hilo unalopewa ndilo linalokupa tarajio la kupokea mema toka kwa Mungu. Maana imeandikwa hivi; “Umemtendea mema mtumishi wako, Ee, Bwana, sawasawa na neno lako” (Zaburi 119:65). Mema aliyokuandalia Mungu kwa mwaka huu, yatakujia sawa sawa na Neno analolituma kwako.

3.      Neno hilo unalopewa linakupa msingi mzuri wa maombi yako kwa mwaka 2002. Maana imeandikwa hivi; “ Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba” (1Yohana 5:14,15). ‘ Sawasawa na mapenzi yake’, maana yake ‘ sawasawa na neno lake’.

Ziko sababu nyingine ambazo tungeweza kukupa ili kukuhumiza upende kumwomba Mungu akupe neno la kusimama nalo katika maisha yako kwa mwaka huu. Lakini hizi chache tulizokuandikia katika barua hii tunaamini zinatosha kukupa changamoto ya kulifuatilia jambo hili zaidi

      Kumbuka mwaka mmoja hauna siku nyingi, na siku moja haina masaa mengi hata ukadhani unaweza kufanya kila kitu unavyotaka na wakati utakapo. Kwa hiyo ili uwe ‘focused’ au uwe na lengo au matazamo kwa mwaka huu kusudia kufahamu na kufanya kile Mungu anachotaka ufanye mwaka huu!

      Kumbuka pia Mungu ametupa mwaka huu ili tumzalie matunda. Na huwezi kumzalia Mungu matunda peke yako bila neno lake.

      Kumbuka pia ya kuwa kwa kukupa neno la mwaka huu usifikiri Mungu hatakupa maneno mengine baadaye mwaka huu. Tega sikio lako, Mungu anaweza kukupa maneno mengine ya kukusaidia wakati wowote kufuatana na hitaji unalokuwa nalo, na pia kufuatana na kile anachotaka ukijue wakati huo.

Mwisho  

Tuzidi kuombeana. Tunaamini utasimama pamoja nasi tena mwaka huu ili Kanisa la Bwana lilishwe, Ufalme wa Mungu ujengwe na Jina la Yesu litukuzwe. Semina tulizonazo mbele yetu mwaka huu ni Moshi tarehe 27 Januari hadi tarehe 3 Februari , Tanga tarehe 12 –17 Februari, Arusha tarehe 25 Februari hadi tarehe 3 Machi. Unaweza ukaona ratiba yetu nzima katika sehemu ya ratiba katika mtandao wetu (www.mwakasege.org) au wasiliana nasi kwa simu hii 2504289

Mungu akubariki kila siku,  

Ni sisi katika utumishi wa Kristo, 

Christopher na Diana Mwakasege.

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.