|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
JE UMEKUMBUKA KUIOMBEA NCHI YAKO LEO? Salaamu na Shukrani; Tunakusalimu wewe unayeusoma barua hii sasa ni kwa jina hili lipitalo majina yote, jina la YESU KRISTO, Mwana wa Mungu aliye hai, aliye Baba wa milele, Bwana na Mwokozi wetu. Mioyo yetu imejaa shukrani nyingi kwa Mungu kwa kutupa nafasi ya kuyaandika mambo ambayo ameyaweka mioyoni mwetu kwa ajili ya watu wake. Roho Mtakatifu amekuwa mwaminifu sana kama ilivyo kawaida yake, ametuwezesha kuandika barua hii, na kuifikisha mbele yako katika muda uliokubalika. Tunapenda kumshukuru Mungu sana katika Yesu Kristo kwa ajili ya kila mtu ambaye amemwinua kutuombea sisi pamoja na huduma tuliyopewa na Bwana. Pia, tunalitukuza jina la Bwana wetu aliye Jemedari wa vita; na Jehova-yire; na El-shaddai kwa ajili ya kila mtu aliyemgusa kutoa muda wake, mali yake, fedha yake kwa ajili yetu na kwa ajili ya huduma tuliyopewa na Bwana. Kujitolea kwako si bure machoni pake Bwana, kwani neema ya Bwana Yesu Kristo inayookoa, inayoponya, inayohuisha, na iliyojaa baraka iko pamoja na wewe ikuneemeshe. Nchi yetu inahitaji maombi yako: Kwa muda wa miaka kadhaa sasa, Roho Mtakatifu ameweka mzigo ndani ya mioyo yetu wa kuomba juu ya nchi yetu; kama vile alivyoweka kwa wakristo wengine pia. Hivi karibuni Roho Mtakatifu amezidi kutuhimiza kuiombea nchi yetu, pamoja na kuwaombea wote wanaopaza sauti zao kuombea nchi hii, ili wasichoke bali wazidi kuomba bila kukoma kwa ajili ya nchi hii. Katika barua hii tunataka tukuulize swali hili muhimu; Je! umekumbuka kuiombea nchi yako leo? Tunajua utakubaliana nasi tukisema ya kuwa jambo lililo muhimu kwako ndilo linalopata nafasi katika muda wako wa maombi. Je! unafahamu umuhimu wa kuikumbuka nchi yako katika maombi kila siku? Sababu tano zifuatazo tunaamini zitasaidia kukukumbusha na kuchochea umuhimu wa maombi haya ndani yako, ili kila siku kuwe na watu au mtu ambaye anaisogeza nchi yetu mbele ya kiti cha enzi cha Mungu katika maombi. Sababu ya Kwanza: ILI TUISHI KWA AMANI KUSUDI INJILI IHUBIRIWE. “Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli. Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.” (1Timotheo 2:1-6) Tanzania inakadiriwa kuwa na watu wasiopungua millioni 30. Watu wote hawa wanaishi katika eneo la kilomita za mraba 937,062 wakiwa wanatoka katika makabila yenye mila mbalimbali yasiyopungua 120. Tunahitaji kumshukuru Mungu sana kwa sababu muujiza huu mkubwa wa kuishi kwa amani na utulivu kwa miaka yote hii tangu tupate uhuru toka utawala wa Waingereza. Ili amani hii idumu na utulivu huu uzidi kudumu maombi yako yanahitajika SASA usingoje kutokee machafuko ndipo uombe- omba sasa! Ndilo jambo ambalo Mtume Paulo anazidi kutukumbusha katika waraka wake wa kwanza kwa Timotheo. Ingekuwa Mtume Paulo anaandika kwa wakristo wa Tanzania peke yao, maneno yake yangesomeka hivi; “Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala na maombezi, na shukrani, zifanyike kwa ajili ya Watanzania wote; kwa ajili ya viongozi na wote wenye mamlaka Tanzania, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa (utakatifu) wote na ustahivu (uvumilivu).” Kwa nini Roho Mtakatifu alimhimiza Mtume Paulo kutuandikia ili tufanye maombi ya namna hii? Ni wazi kwamba kuiombea nchi yetu kunasaidia watu waishi maisha ya utulivu (yasiyo na ghasia), amani, utakatifu na uvumilivu. Tukiyaelekeza maneno ya Mtume Paulo kwa watanzania, basi tunazidi kusoma yafuatayo: “Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watanzania wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli, kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na watanzania ni mmoja mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya watanzania wote, utakoshuhudiwa kwa majira yake.” Tunajua si kila mtanzania atakubaliana na tafsiri hii ya maneno ya Mtume Paulo, lakini ndivyo anavyotaka sisi tunaomwamini Kristo tufanye – TUOMBE BILA KUKATA TAMAA ili kuwe na utulivu na amani nchini, injili ihubiriwe na watu waokolewe! Ukitaka Tanzania iwe na watu katika kundi litakalomlaki Bwana mawinguni atakaporudi kuchukua kanisa au wateule (1Wathesalonike 4:13-17) – basi usifanye uvivu kuombea nchi yako leo! Kumbuka kila mwaka watu wanaongezeka nchini kwa kuzaliwa ni asilimia 2.8 ya watu wote millioni 30. Hii ina maana ya kuwa kila mwaka nchini wanazaliwa watoto 644,000. Ikiwa tunataka kwenda na wakati basi tuzidishe maombi kila siku, ili tuwe na amani kila siku, ili injili ihubiriwe kila siku (na siyo Jumapili tu!), ili wazaliwe watoto wa kiroho nchini wasiopungua 1766 kila siku ili idadi hii izidi ile ya watoto wa jinsi ya mwili wanaozaliwa kila siku nchini. Hapa pana siri kubwa, asomaye na afahamu, asema Roho Mtakatifu. Sababu ya pili: ILI NCHI YETU IPONYWE “Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na KUOMBA, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na KUIPONYA NCHI YAO” (2 Mambo ya Nyakati 7:14). Nchi inayohitaji kuponywa maana yake ina udhaifu fulani ulio wazi mbele za Mungu na mbele za watu. Mistari hii tuliyosoma toka kitabu cha Mambo ya Nyakati, inatuambia kuwa maombi ya kuombea nchi ni kati ya mambo ambayo yanatakiwa yafanywe na watu walioitwa kwa jina la Yesu Kristo – na kudumu ndani yake. Nchi ambayo Nabii Habakuki alikuwa anaishi kama vile tusomavyo katika Agano la Kale ilikuwa imejaa dhuluma, wizi, uovu, ugomvi, mashindano, udhalimu na mambo mengi yanayofanana na haya. Pia, tunasoma kuwa katika nchi hiyo ya Habakuki, sheria ilikuwa imelegea, wala hukumu ya haki ilikuwa haipatikani. Ndipo Nabii Habakuki alipoamua kumlilia Mungu kwa njia ya maombi juu ya hali hiyo mbaya ambayo ilikuwa imeikumbuka nchi yake. Kati ya maneno yenye uchungu aliyomuuliza Mungu katika maombi hayo ni haya; “Wewe (Mungu) uliye na macho safi hata usiweze kuangalia uovu, wewe usiyeweza kutazama ukaidi, mbona unawaangalia watendao hila; na kunyamaza kimya, hapo mtu mwovu ammezapo mtu aliye mwenye haki kuliko yeye….?” (Habakuki 1;13). Ukisoma Habakuki sura ya Pili utaona jinsi ambavyo Mungu alimjibu Habakuki na kumweleza hatua au adhabu itakayoshuka juu ya nchi na juu ya wote watendao yasiyopendeza machoni pake. Ndipo Nabii Habakuki alipoomba tena akisema; “Ee Bwana, nimesikia habari zako, NAMI NAOGOPA. Ee Bwana, FUFUA KAZI YAKO katikati ya miaka; Katikati ya miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka REHEMA…….” (Habakuki 3:2) Habakuki aliomba naye akajibiwa. Wewe pia ukiomba utajibiwa hakika! Ndivyo Mungu alivyoahidi! Maombi ya Nabii ni maombi ya mtu aliyemjua Mungu wake alivyo Mtakatifu na wa Haki – na pia aliyejua mambo ambayo anaweza kuyafanya juu ya nchi itendayo maombi mbele yake. Ndiyo maana alisema “ Ee Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopa……” Tunajua kuwa Nabii Habakuki alikufa siku nyingi, wala hatuwezi kumpata aje Tanzania nyakati hizi atusaidie kuomba. Lakini tunataka tukuambie jambo muhimu- nalo ni hili. Roho Mtakatifu yupo katika nchi hii ya Tanzania na anatafuta watu wenye hofu ya Mungu, ILI asimame pamoja nao katika maombi ya kuiombea nchi hii ya Tanzania ILI KAZI YA BWANA IFUFUKE NDANI YA WATANZANIA – MUNGU AIPONYE NCHI YETU – KATIKA GHADHABU AKUMBUKE REHEMA – ATUREHEMU! Je! huwa unafurahi unaposoma kwenye magazeti na kusikia katika redio jinsi wizi, ajali, ujambazi, ugonjwa wa ukimwi, na kadhalika vinavyozidi nchini? Kama moyo wako unahuzunishwa na hayo, Roho Mtakatifu anakualika uombe pamoja naye (Warumi 8:26-27) – ILI MUNGU AIPONYE NCHI YETU. Sababu ya Tatu: ILI NCHI YETU ISIPATE MAPIGO “Nami Nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu. Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao; nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu; nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao, asema Bwana Mungu” (Ezekiel 22:30,31). Katika maneno haya ya kusikitisha, Mungu anasema alitafuta mtu kati ya Wana wa Israeli atakayeomba toba kwa niaba ya nchi yao nzima akamkosa. Kwa sababu ya kukosekana kwa mtu MMOJA wa kusimama mbele za Mungu kwa niaba ya wenzake – nchi nzima ilipata mapigo! Kama unakumbuka habari za Abrahamu utaona ya kuwa Mungu alikuwa tayari kuisamehe miji ya Sodoma na Gomora kama angekuta watu kumi wenye haki ndani yake. (Mwanzo 18:28-32). Lakini kwa maneno yaliyotoka kwa kinywa cha Nabii Ezekiel, Mungu yuko tayari kuiponya nchi, ikiwa mtu mmoja atapatikana wa kusimama mbele zake! Je! unafahamu ya kuwa damu ya Yesu Kristo imekupa ujasiri wa kusimama mbele za Mungu kwa ajili ya nchi yako pia? Kama hufahamu somo mistari ifuatayo katika Biblia:- Waebrania 10:19 na 1Petro 2:5,9,10. Je! uko tayari kusimama mbele za Mungu na kuomba toba kwa ajili ya nchi yetu ili nchi nzima isipate mapigo na mabalaa? Kama uko tayari anza leo! Sababu ya Nne: ILI TUISHI PAMOJA KWA UMOJA TUPATE BARAKA ZA MUNGU “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja….. Maana ndiko Bwana alikoamuru Baraka, Naam, Uzima hata milele” (Zaburi 133:1,3) Kumbuka kuomba kuwa tuishi na kukaa PAMOJA na kwa UMOJA kwa jina la YESU KRISTO hapa nchini. Soma Kumbukumbu la Torati 28:1-14, Waefeso 1:3,4; Wagalatia 3:13,14. Sababu ya Tano: ILI KUZIVUNJA KAZI ZA SHETANI JUU YA NCHI YETU “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuzipinga hila za shetani, kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu waroho.” (Waefeso 6:11,12). “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru” (Luka 10:19). Popote unapoziona kazi za ibilisi zikijiinua nchini, tumia jina la Yesu Kristo kuzivunja na kuusimamisha uongozi wa Roho Mtakatifu mahali pale. Nataka ufahamu mambo haya yafuatayo ambayo ni muhimu katika kuombea nchi. Kila nchi inayoonekana inatawaliwa na nchi ya kiroho isiyoonekana. Tabia ya nchi inayoonekana inachukua tabia ya nchi ya kiroho isiyoonekana. Kwa mfano: Ezekiel 28:1-10 inazungumza juu ya mkuu wa Tiro aliye mwanadamu. Lakini Ezekiel 28:11-19 inazungumza juu ya mfalme wa Tiro aliye kerubi aliyekuwa katika bustani ya Adeni. Kerubi maana yake ni malaika. Kwa hiyo ni wazi kuwa mkuu wa Tiro aliyekuwa mwanadamu alikuwa anatawala nchi hiyo kwa kufuata maongozi ya Mfalme wa Tiro aliyekuwa kerubi, au malaika, au shetani. Kiburi cha mfalme wa Tiro (Kerubi) kilionekana ndani ya Mkuu wa Tiro (mwanadamu). Ufalme wa Tiro wa kiroho ulitawala ufalme wa Tiro wa kibinadamu. Mipaka ya nchi ya Tiro ilifanana na mipaka ya nchi ya Tiro ya kibinadamu. Mfalme wa Tiro wa kiroho (kerubi) anaitwa “kerubi ufunikaye” maana ya “malaika afunikaye’ au “roho ifunikayo” – ni ufalme wa kiroho unaofunika ufalme wa kibinadamu; - ni ufalme wa giza unaoifunika nchi ya kibinadamu kwa giza. Soma pia Daniel 10:12,13,20 – inazungumza juu ya vita vya malaika Gabriel alipokuwa ametumwa na Mungu apeleke ujumbe kwa Danieli. Tunafahamu ya kuwa Malaika Gabriel ni roho; kwa hiyo vita vyake ni vya kiroho na vipingamizi alivyokutana navyo vilikuwa ni vya kiroho. Aliyempinga njiani ni Mfalme wa falme ya uajemi ya kiroho na siyo ya kibinadamu. Hii ina maana ya kuwa ufalme wa Uajemi wa kiroho ndio uliokuwa unatawala juu ya ufalme wa Uajemi wa kibinadamu uliokuwa unatawaliwa na Koreshi. Soma pia Yeremia 25:11,12. Katika kitabu cha Danieli 10:13, Malaika Gabriel anasema “Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi (mmoja) ……….pamoja na wafalme wa uajemi (wengi). Hii inamaanisha kulikuwepo falme ndogo ndogo katika uajemi zilizotawaliwa na wafalme ambao pia walikuwa na mkuu mmoja juu yao. Hivi ndivyo ulivyo pia ufalme wa giza wa shetani juu ya nchi mbalimbali hapa duniani. Waefeso 6:12 inatuambia kuwa: “Kwa maana kushindana kwetu sisi (wakristo) si juu ya damu na nyama, bali ni juu ya:
Uwanja wetu wa vita ni katika ulimwengu waroho. Ili wana wa Israeli waliokuwa wanatawaliwa na ufalme wa uajemi watoke katika utumwa, ilibidi kwanza Malaika Gabrieli amshinde shetani aliyekuwa anatawala juu ya ufalme wa Uajemi. Malaika Gabrieli alijua ya kuwa ili aweze kubadilisha mawazo ya mfalme wa Uajemi aliye mwanadamu juu ya wana wa Israeli, ni budi kwanza avunje utawala wa shetani uliokuwa juu ya mfalme wa Uajemi. Na sisi tukitaka ndugu zetu katika nchi yetu watoke katika utumwa wa giza, dhambi, uongo, rushwa, dhuluma, ulevi, uasherati, na kadhalika, ni budi tuingie katika ulimwengu waroho juu ya nchi yetu na ndugu zetu. Ukitaka kubadilisha mambo ya sehemu fulani yaliyo kinyume na neno la Kristo, badilisha mambo ya ulimwengu wa kiroho unaotawala juu ya sehemu hiyo- kwa kuwa tunayo mamlaka juu ya ulimwengu wa kiroho na wa kimwili katika jina la Yesu Kristo. MASHAURI MUHIMU Nia na kusudi la kuiombea nchi kila siku ni zaidi ya sababu hizi tano zilizozitajwa katika barua hii. Nimeziandika hizi chache ili kufufua na kuchochea kazi hii muhimu ya kuiombea nchi yetu ndani ya moyo wako. Tunapenda kukushauri yafuatayo ili kama huyafanyi basi, uanze kuyafanya tangu leo:
Neema ya Bwana Yesu Kristo; na Upendo wa Mungu Baba; na ushirika wa Roho Mtakatifu uwe pamoja nawe siku zote hata milele na milele, Amina. Ni sisi katika utumishi wa Kristo, Christopher na Diana Mwakasege |
|