|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
ACHA
KULALAMIKA Sala ya Nabii Habakuki: "Ee Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopa; Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka; Katikati ya miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka rehema." (Habakuki 3:1,2) Haya maneno ni sehemu ya maombi ya nabii Habakuki yaliyoandikwa katika sura nzima ya tatu ya Kitabu cha Habakuki. Ukisoma kitabu kizima cha Habakuki utafahamu na kuelewa ya kuwa kuna jambo lililotokea katika maisha ya Habakuki lililomfanya awe mwombaji na kufanya maombi mazito namna hiyo. Tunasema hivi kwa sababu sura ya kwanza ya kitabu cha Habakuki inaonyesha wazi ya kuwa Nabii Habakuki hapo mwanzo hakuwa mwombaji bali alikuwa mlalamikaji! Ukisoma haraka hiyo sura ya kwanza utadhani Habakuki alikuwa anafanya maombi, lakini ukweli wake alikuwa analalamika. Kuna tofauti kubwa kati ya kulalamika na kuomba. Ndani ya kulalamika kuna kukata tamaa, kupoteza tumaini na kupungua kwa imani. Katika kuomba unaonyesha imani uliyo nayo katika uweza wa Mungu kukushindia matatizo au majaribu uliyo nayo. Habakuki aliishi katika kipindi kigumu sana katika maisha yake – kiasi kwamba badala ya kuomba alilalamika karibu juu ya kila kitu. Alilalamika juu ya hali ya dhuluma iliyokuwa inaendelea wakati huo. Alilalamika juu ya udhalimu uliokuwepo wakati ule. Alilalamika juu ya ugomvi na mashindano yaliyokuwepo. Alilalamika akisema: "sheria imelegea, wala hukumu haipatikani, kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki! Kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka." (Habakuki 1:4) Tena alithubutu hata kumlalamikia Mungu kwa ukimya wake! Kwa mfano alisema hivi; " Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa," (Habakuki 1:2) Je! umewahi kujikuta katika hali ya kumlalamikia Mungu namna hii? Ukiendelea kusoma habari hizi za Habakuki utaona ya kuwa aliwahi hata kumlalamikia Mungu juu ya ukimya wake wa kutowaadhibu wale watu waliotajirika kwa sababu ya kuwanyonya wengine. Ni kweli ilikuwa gumu sana kwa Habakuki! Kwani alimjua Mungu wake ya kuwa ni Mungu wa haki – kwa hiyo ilimpa shida kuona udhalimu, dhuluma na unyonyaji ukiendelea na huku Mungu wa haki anakaa kimya! Tena kumbuka Habakuki alikuwa mtumishi wa Mungu – tena nabii. Wito wa Mungu ulikuwa juu yake – lakini alijikuta amekuwa mlalamikaji. Hakujua ya kuwa Mungu amemwita kuwa nabii mwenye mzigo wa maombi, na hakuitwa awe nabii mlalamikaji. KILICHOMBADILISHA HABAKUKI Sura ya pili ya kitabu cha Habakuki inaanza na kutueleza juu ya maamuzi ya Habakuki kutaka kumsikiliza Mungu atasemaje juu ya malalamiko yake. Na Mungu akasema naye! Pamoja na maneno mengi Mungu aliyozungumza naye juu ya kulalamika kwake, alimwambia ya kuwa; pamoja na dhuluma yote iliyopo; pamoja na udhalimu wote uliopo; pamoja na sheria kulegea na hukumu kupotoshwa; pamoja na umaskini uliopo; pamoja na unyonyaji uliopo; "……..Mwenye haki ataishi kwa imani yake" (Habakuki 2:4b) Hili neno lilimbadilisha Habakuki! Neno hili lilimpa Habakuki kitu cha kufanya na mbinu ya kuishi katika hali ngumu iliyokuwa inamzunguka. Ghafla ndani ya moyo wake, Mungu alimpa kutambua ya kuwa mabadiliko ya hali ya kiroho ya jamii ya wakati ule isingeweza kubadilishwa kwa kulalamika, wala kwa hekima na mipango ya kibinadamu bali ingebadilishwa kwa nguvu za Mungu. Na alijua njia mojawapo muhimu ya kumkaribisha Mungu ili abadilishe hali ya jamii ni kwa njia ya maombi. Ndiyo maana mara tu baada ya Mungu kumaliza kusema, Habakuki alianza maombi ya mzigo ambayo tunaamini Roho Mtakatifu alimwongoza kuyafanya. MAOMBI YA HABAKUKI Ule mstari wa pili wa sura ya tatu ya Kitabu cha Habakuki unaonyesha wazi ya kuwa uweza wa Mungu katikati ya kizazi hicho ulikuwa umekufa ulikuwa hauonekani tena kama ilivyokuwa zamani kabla ya wakati huo. Ndiyo maana anaomba anasema, " Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka……" Jambo muhimu hapa tunalotaka uone katika ujumbe huu ni kwamba nabii Habakuki aliacha kulalamika na akaanza kuomba! Kuna nguvu katika maombi. Hasa ukijua ya kuwa Mungu huwa anaheshimu na kujibu maombi ya watu wake walioitwa kwa jina lake- wakiomba kwa uongozi wa neno lake. NA WEWE NI LAZIMA UBADILIKE! Kilichomfanya Nabii Habakuki abadilike ni neno la Mungu. Kwa wasomaji wa biblia wote tunafahamu ya kuwa katika Yohana 1:1-3, 12-14 tunapata maelezo yanayotueleza ya kuwa Yesu Kristo ndiye neno aliyetumwa kwetu ili kubadilisha maisha yetu! Yesu Kristo ndiye jibu la matatizo yaliyomo humu ulimwenguni. Kwa hiyo hatua ya kwanza ya mtu yeyote akitaka maisha yake yabadilike, aache kulalamika, ni lazima – NI LAZIMA – akutane na Neno, yaani Bwana Yesu Kristo amwokoe. Ni muhimu na ni lazima mtu aokolewe na Bwana Yesu Kristo akitaka mabadiliko katika maisha yake ya kawaida, na pia katika maisha yake ya maombi. Mabadiliko ambayo hayana Yesu Kristo ndani yake si ya kudumu, na mara nyingi hayaonyeshi utukufu wa Mungu. Mabadiliko anayoyaweka Yesu Kristo ndani ya mtu ni ya kudumu, ya kuaminika, na yenye kuonyesha utukufu wa Mungu. KUOKOKA HAKUTOSHI….! Jambo ambalo limejitokeza wazi ni kuwa; pamoja na kwamba watu wengi wameokoka, bado maisha yao mara kwa mara yanaingia katika mtego wa kulalamika. Hata wengine wamepakwa mafuta kama vile alivyopakwa mafuta Habakuki, lakini na wao wanalalamika. Jibu alilopewa nabii Habakuki la kuwa "Mwenye haki ataishi kwa imani yake"(Habakuki 2:4b), ndilo jibu ambalo Mungu ametupa ndani ya Yesu Kristo katika Injili yake. Katika Warumi 1:16 tunaona ya kuwa "Injili…..ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye…" na katika Warumi 1:17 tunaona ya kuwa, "haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani, kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani". Mtu akiisha okoka anatambuliwa ya kuwa ni "mwenye haki" mbele za Mungu katika Kristo. Kwa kuwa amefanyika kuwa kiumbe kipya, mfumo wake wa maisha ni tofauti na ule wa zamani. Pamoja na kwamba mazingira ya maisha yanayomzunguka yanaweza kuwa hayajabadilika, inatakiwa ayatazame kwa mfumo tofauti. Anapoyaona, lazima aache kulalamika! Ni lazima tufahamu ya kuwa hata kama umeokoka, kulalamika kunaondoa ndani yako upendo, uvumilivu, furaha na amani. Na zaidi ya yote, msukumo wako katika maombi unapotea. Unajikuta unategemea nguvu zako, na msaada wa wanadamu wengine kuliko msaada wa Mungu aliye hai. Dawa ya kulalamika ni neno la Mungu kukaa ndani yako kwa wingi na katika hekima yote. Ndiyo maana Yesu Kristo alisema hivi: "Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa." (Yohana 15:7) Ukitaka kutendewa lolote unaloomba kwa Mungu, au kwa maneno mengine unaweza kusema ukitaka uwe na mafanikio katika maombi, Yesu Kristo anasema fanya mambo mawili: Jambo la kwanza: Kaa ndani yake. Anasema hivi, "Ninyi mkikaa ndani yangu……." Kwa maneno mengine anasema, "Ninyi mkiamini au mkiokoka….." Hatua ya kwanza ni kuokoka na kuamini ukitaka kufanikiwa katika maombi. Jambo la pili: Neno lake likae ndani yako. Anasema hivi, " maneno yangu yakikaa ndani yenu…." Hiki ndicho kipengele kinachofanya watu wengi wasifanikiwe katika maombi yao- hawana neno la Kristo ndani yao juu ya mambo wanayoyaombea. Na kwa kuwa hawapokei wanachoomba-wanajikuta wanalalamika kila wakati. Ukiona umeokoka, na maombi yako hayawi ya mafanikio- kazana kulisoma na kulitafakari neno la Mungu juu ya jambo unaloliombea! Maana Yesu Kristo anasema tufanye maombi baada ya kukaa ndani yake na maneno yake kukaa ndani yetu. Anasema hivi; " Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni……" Agizo la "Ombeni….." linakuja baada ya sisi kutuambia tukae ndani yake na maneno yake kukaa ndani yetu! Neno lake ni muhimu sana kama unataka ufanikiwe katika maombi yako kwa sababu Mungu mwenyewe anasema juu ya neno lake ya kuwa, "Neno …..litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma" (Isaya 55:11). Maisha yako yatabadilika ukijifunza kuwa na neno ndani yako siku zote. Kulalamika kutatoweka. Kama vile ilivyokuwa kwa nabii Habakuki – utaacha kulalamika juu ya matatizo yanayokuzunguka na yanayokukabili, na utakuwa mtu wa maombi! Kwa kuwa utajua ya kuwa dawa si kulalamika bali ni kufanya maombi! Kwa mfano: Ikiwa ndoa yako imefika mahali pagumu pa kutaka kuvunjika – hutalalamika na kukata tamaa bali utaomba kwa sababu utajua ya kuwa Mungu anasema, "Mimi nakuchukia kuachana…." Kama Mungu anachukia kuachana, na wewe chukia kuachana na mume au mke wako – na kwa njia ya maombi Mungu anaweza kuwapatanisha tena. Unapokuwa una neno la Mungu ndani yako utajifunza kuwa mwombaji badala ya kuwa mlalamikaji. Badala ya kulalamika juu ya mchungaji wako, au wazee wa Kanisa, au serikali yako au tabia za vijana, au uonevu kazini, au katika lolote lile- ukiwa na neno la Mungu ndani yako – utaongozwa na kuhimizwa na Roho Mtakatifu kufanya maombi. Na maombi yako yatafanyikiwa. Tuzidi kuombeana. Ni sisi katika utumishi wa Kristo, Christopher na Diana Mwakasege |
|