|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
"Kama
Kristo hakufufuka….." Mpendwa katika Yesu Kristo.
Salamu!
Tunafurahia mioyoni mwetu ya kuwa Mungu ametupa tuwasiliane tena mwezi
huu wa Machi 2002 kwa njia ya barua hii. Tunaamini Roho Mtakatifu
amekuongoza uisome barua hii kwa makusudi kamili yenye lengo la
kukusogeza hatua zaidi mbele katika maisha uliyonayo ndani ya Kristo.
Je! unajua ni hali gani tungekuwa nayo kama Kristo asingekuwa amefufuka?
Umewahi kutulia angalau kwa muda mfupi ukatafakari juu ya swali hili? Je!
unajua umuhimu wa kuwa na uhakika wewe binafsi ya kuwa Yesu
amefufuka? Hata ukisoma katika biblia utaona ya kuwa Yesu baada ya kufa
na kufufuka lakini kabla ya kupaa aliwadhihirishia wanafunzi
wake; "…. kwa dalili nyingi…..ya kwamba yu hai, akiwatokea
siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyohusu ufalme wa Mungu" (Matendo
ya Mitume 1:3). Lazima kulikuwa na sababu muhimu sana zilizomfanya
ajidhihirishe namna hiyo kwa wanafunzi wake ya kuwa amefufuka na kwamba
yu hai! Je!
unaamini kwa furaha ya kuwa Yesu amefufuka?
Kuna wakati wanafunzi wa Yesu walipoambiwa ya kuwa amefufuka,
hawakuamini (Luka 24:10-12; 36-43). Lakini baadaye walipokwenda kaburini
na kukuta mwili haupo – walijua na kuamini ya kuwa amefufuka lakini si
kwa furaha. Hata baada ya kuwatokea wakiwa wamejifungia ndani ya nyumba
hawakuamini kwa furaha hadi alipokula nao chakula walichokuwa
nacho?
Je! unajua ya kuwa hata sasa hata kama unaamini ya kuwa Yesu amefufuka
– huwezi kuwa na furaha kama Yesu huyu aliyefufuka asipojifunua katika
maisha yako ya kila siku na "kula chakula ulichonacho mbele yako"?
Maana yake ajifunue katika maisha yako ya kila siku – hapo ndipo
furaha ya wengi inaongezeka katika kumwamini Kristo.
Imeandikwa katika kitabu cha Luka 24:40,41 ya kuwa; " Na baada
ya kusema hayo aliwaonyesha mikono yake na miguu yake. Basi walipokuwa
hawajaamini kwa furaha wakistaajabu, aliwaambia, mna chakula cho chote
hapa? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala mbele yao."
Ikiwa umeokoka na huna furaha au ikiwa unaamini ya kuwa Yesu Kristo
amefufuka na huna furaha – mara nyingi ni kwa sababu mbili kubwa. Kwanza,
ni kwa sababu humwoni Yesu akajifunua na kujidhihirisha katika maisha
yako ya kila siku kwa mfano kazini kwako au katika masomo yako au katika
biashara yako, au katika ndoa yako. Je!unamwona Yesu aliyefufuka katika
maisha yako? Ikiwa humwoni basi ni maombi yetu kwa Mungu ya kuwa Yesu
ajifunue katika maisha yako ya kila siku na uone baraka za kufufuka
kwake.
Pili: Huna furaha hata kama
umeokoka na unaamini ya kuwa Yesu amefufuka kwa sababu unashindwa kupata
ufunuo ndani yako unaoweza kulinganisha neno la Mungu na kujifunua kwa
Yesu katika maisha yako ya kila siku. Ndiyo maana baada ya Yesu kula
samaki "mbele yao", aliwaambia; " Hayo ndiyo
maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima
yatimizwe yote niliyoandikiwa katika torati ya Musa, na katika Manabii,
na Zaburi" (Luka 24:44). Na katika mstari unaofuata wa 45
tunasoma ya kuwa;l "Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa
na maandiko".
Ni dhahiri ya kwamba Yesu aliwahi kusema nao juu ya maandiko yaliyohusu
maisha yake katikati yao na hawakuyaelewa. Kwa hiyo akawafunulia akili
zao wapate kuyaelewa hayo maandiko – yaani wapate kulinganisha kuwepo
kwa Yesu katikati yao na maandiko! Kwa hiyo baada ya kumwona Yesu akipaa
na kuchukuliwa juu mbinguni, biblia inasema; "Wakamwabudu;
kisha wakarudi Yerusalemu wenye
furaha kuu" (Luka 24:52)
Kwa hiyo ni muhimu na wewe uweze kulinganisha neno la Mungu na kuwepo
kwa Yesu aliye hai katikati yako. Bila hili furaha yako inapungua. Ni
maombi yetu kwa Mungu ya kuwa "atakuwa anakufunulia akili zako kila
siku upate kuyaelewa maandiko." Kama
Kristo hakufufuka…..…… hakuna aliyekufa atakayefufuka!
Ndiyo! Kama Kristo hajafufuka, basi hakuna kiyama ya wafu au hakuna
aliyekufa atakayefufuka! Imeandikwa hivi: "Basi, ikiwa Kristo nahubiriwa
ya kwambaamefufuka katika wafu, mbona baadhi yenuhusema kwamba hakuna
kiyama ya wafu?Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristonaye hakufufuka…..
Maana kama wafuhawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka….. Na hapowao nao
waliolala katika Kristo wamepotea(1Wakorintho 15:12,13,16,18)
Lakini tunajua ya kuwa Yesu amefufuka – Yuko hai na kwa sababu hiyo
iko siku atayowafufua wote waliokufa. Wengine watapata nafasi ya kukaa
naye milele mbinguni na wengine watatupwa katika Ziwa la Moto katika
mateso ya milele. Soma Ufunuo wa Yohana 20:11-15 na 1Wathesalonike
4:13-17) Kama
Kristo hakufufuka……...…..basi, imani yetu ni bure!
Imani ya Kikristo imesimama kwenye kitu gani? Imesimama katika Yesu
Kristo aliyesulubiwa, akafa, akazikwa, na akafufuka. Kama Kristo
asingekuwa amefufuka, kusulubiwa kwake, kufa kwake na kuzikwa kwake
kusingekuwa na faida yo yote kwetu wakati huu. Ndiyo maana imeandikwa: "Na kama Kristo hakufufuka,
imani yenu ni bure;mngalimo katika dhambi zenu na kama katika maishahaya
tumemtumaini Kristo, sisi tu maskinikuliko watu wote" (1
Wakorintho 15:17,190
Ikiwa Yesu hakufufuka isingekuwa rahisi kwa sasa kupata msamaha wa
dhambi, au kupata ondoleo la dhambi au kupata uzima wa milele! Hii ni
kwa sababu haya yote tunayapata kwa njia ya Roho Mtakatifu. Na Roho
Mtakatifu asingeweza kuja na kufanya hayo kwa kila anayemwamini Yesu
aliyefufuka kama Yesu asingekuwa amefufuka. Hii ni kwa sababu
Roho Mtakatifu hakuja kwetu hadi Yesu alipotukuzwa na kuketi mkono wa
kuume wa Mungu baada ya kufufuka. Soma Yohana 7:37-39; Yohana 16:7-16. Kama
Kristo hakufufuka…...…..basi, kuhubiri kwetu ni bure!
Je! unajua kwa nini Yesu Kristo alipofufuka alitaka sana na akahakikisha
ya kwamba wanafunzi wake wanapata uhakika ya kuwa amefufuka? Ni kwa
sababu alikuwa anataka wawe ‘mashahidi’ wake ya kuwa yote
aliyoandikiwa yalitokea kama yalivyoandikwa katika " torati ya Musa,
zaburi na Manabii" (Luka 24:36-53). Na ya kwamba wanafunzi wake
wazunguke na kutangaza habari njema za msamaha wa dhambi na uzima wa
milele unaopatikana katika Yesu Kristo aliyefufuka. Mtume Paulo
aliandika hivi; "Tena
kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubirikwetu ni bure na imani yenu ni
bure. Naam,na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongowa Mungu; kwa
maana tulimshuhudia Munguya kuwa alimfufua Kristo, ambaye
hakumfufua,ikiwa wafu hawafufuliwi" (1Wakorintho 15:14,15)
Kwa maneno mengine Mtume Paulo angeweza kusema hakuna sababu ya kuhubiri
habari za Yesu ikiwa hakufufuka. Au Yesu aliyekufa lakini
hakufufuka hana faida yo yote ukimhubiri. Lakini Yesu aliyekufa na
kufufuka ana faida kwa anayemhubiri na kwa anayehubiriwa pia. Uzuri wa
kumhubiri Yesu Kristo aliyefufuka ni kwamba huwa analithibitisha hilo
neno linalohubiriwa juu yake kwa ishara na miujiza. Soma Marko 16:20. Kama
Kristo hakufufuka….…..basi, Jina la Yesu haliwezi kuwa na nguvu!
Hata katika maisha haya ya kawaida kibinadamu, jina la mtu linapoteza
nguvu yake pale anapokufa. Kwa sababu mwenye jina hayupo kufanya yale
ambayo alikuwa anayafanya alipokuwa hai. Akiisha kufa hawezi tena
kuyafanya mambo hayo, na jina lake likiitwa hawezi kujitokeza mwenyewe
– maana amekufa. Jina lake likiitwa baada ya yeye kufa, hawezi
kujitokeza – rafiki au ndugu au majirani zake wanaweza kujitokeza kwa
niaba yake, lakini hawawezi kufanya alivyokuwa anafanya! Wanaweza kuiga
vitendo alivyokuwa akifanya lakini haviwezi vikawa halisi.
Imeandikwa katika Waebrania 13:8 ya kuwa; "Yesu Kristo ni yeye
yule , jana na leo na hata milele". Huu mstari hauwezi kuwa
kweli kama Yesu Kristo hajafufuka. Na kwa kuwa amefufuka, Jina lake lina
nguvu sana, kwa sababu ukimwita anaitika na kufanya yale yale aliyokuwa
anayafanya alipokuwa hai. Kwa mfano, kabla ya kufa alikuwa anaponya
wagonjwa, kwa hiyo hata baada ya kufufuka akiitwa kwa jina lake Yesu
kuponya wagonjwa anakuja anawaponya!
Tunasoma katika kitabu cha Matendo ya Mitume sura ya tatu habari za mtu
aliyekuwa kiwete tangu tumboni na akaponywa kwa Jina la Yesu Kristo
baada ya Petro kumwombea. Watu waliokuwepo walistaajabu sana wakifikiri
akina Petro wamemponya mtu huyo kwa nguvu zao au kwa utakatifu wao.
Ilimbidi Petro aliweke wazi jambo hili ili wajue huyo kiwete kapona kwa
namna gani. Petro akawaambia hivi; "Mungu wa Ibrahimu na wa
Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu,
ambaye ninyi mlimsaliti….mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu
amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake. Na kwa imani katika
Jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua; na
imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu
ninyi nyote"(Matendo ya Mitume 3:13,15,16) Mwisho
Tulitaka katika barua hii tukukumbushe ya kuwa Yesu Kristo amefufuka na
ya kwamba Yuko hai kwa ajili yetu wote; na ulimwengu unatakiwa
kuhubiriwa habari hii njema! Tuzidi kuombeana. ni
sisi katika utumishi wa Kristo, Christopher na Diana Mwakasege |
|