Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi Mei 2002

MFIKIRIE MUNGU KWANZA KATIKA MAISHA YAKO

Mpendwa katika Kristo,

Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo.

            Mwezi huu tunakuja kwako na swali hili: “Ni njia zipi unazozitumia kumwonyesha Mungu ya kuwa Yeye ndiye wa kwanza katika maisha yako?”

            Kama unavyofahamu sisi huwa tunasafiri sana sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi kwa ajili ya kufanya semina za neno la Mungu. Siku moja tulipofika katika mji fulani, mtu mmoja alikuja na akatupatia fedha akisema zitusaidie kulipia gharama za safari za kupeleka neno la Mungu.

Tukamshukuru Mungu kwa ajili yake na kwa ajili ya fedha hizo, kwa kuwa ni kweli tulikuwa tunazihitaji wakati huo. Kwa kuwa tulikuwa safarini na tulikuwa tunazihitaji tukaanza kuzitumia mara moja kulipia gharama za mizigo ya vyombo vya huduma tulivyokuwa tumesafiri navyo.

Lakini tulipochukua kiasi cha fedha na kulipia mizigo ya vyombo tulikosa amani mioyoni mwetu. Tulijua mara moja ya kuwa jambo hilo halikumfurahisha Roho Mtakatifu – kwa hiyo tukataka kujua tumekosea wapi! Roho Mtakatifu akatuwekea swali hili ndani ya mioyo yetu; “Je! Mungu ni wa kwanza katika maisha yenu na kila siku?” Wakati tunashangaa juu ya swali hilo, akaongeza lingine; “ Ikiwa Mungu ni wa kwanza katika maisha yenu, mbona mlipopokea hizo fedha hamkutoa kwanza zaka ya Mungu kabla ya kuanza kuzitumia hizo fedha?”

            Ghafla tukatambua kosa letu na tukatubu wakati huo huo. Na tunaamini Mungu ametusamehe!

Wewe ungekuwa umeulizwa swali kama tuliloulizwa sisi ungelijibu namna gani? Au hata sasa utajibu namna gani tukikuuliza ya kuwa je, Mungu ana nafasi ya kwanza katika maisha yako kabla au kuliko mtu au kitu chochote. Ni rahisi sana kujibu ‘ndiyo’ bila kutafakari kwa undani ikiwa kama ndivyo Mungu anavyokuona.

Je! unaelewa maana ya maneno haya aliyoyasema Yesu juu ya Mafarisayo aliposema; “Watu hawa huniheshimu kwa midomo, ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure ……” (Mathayo 15:8,9). Kwa lugha rahisi alitaka wajue ya kuwa wanachosema, wanachowaza na wanachofanya havifanani! Hawawezi wakasema wanampenda Mungu huku mioyo yao inawaza mawazo yanayoonyesha kutokumpenda Mungu, na kwa sababu hiyo hata matendo yao yatakuwa ‘bure’ mbele za Mungu maana yake hayatawaletea ‘faida’ au ‘baraka’ yoyote.

Kama Mungu ni wa kwanza katika maisha yako na unamwabudu yeye basi jizoeze umfikirie Mungu kwanza katika matumizi yako ya fedha, ya mali ulizonazo, ya muda ulionao, nakadhalika.

Tuzidi kuombeana.

ni sisi katika utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.