Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi Novemba 2002

KUTAFAKARI NENO

Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo,

"Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali YATAFAKARI MANENO YAKE MCHANA NA USIKU, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana". (Yoshua 1:8)

Mtu mmoja aliwahi kutuuliza swali hili: "Je, kutafakari maana yake nini?" Kila mara tunapofundisha somo hili tunakutana na swali la jinsi hii.

Tunaamini kuwa swali hili linawatatanisha wengi kwa sababu bado hawajatofautisha kati ya kusoma neno na kutafakari neno.

Kusoma neno ni tofauti na kutafakari neno. Kulitafakari neno ni zaidi ya kulisoma neno. Watu wengi huwa wanasoma neno zaidi kuliko kutafakari.

Kutafakari maana yake nini?

Maana ya karibu sana ya neno kutafakari ni kuwaza. Ni kusoma neno huku unalicheua na kulitafakari au kuliwaza rohoni mwako.

Kutafakari ni njia mojawapo kubwa ya kuweza kuilisha roho yako. Yesu Kristo alisema Imeandikwa, "mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu" (Mathayo 4:4)

Mkate ni chakula cha mwili wa nje wa nyama na damu; neno la Mungu ni chakula cha mwili wa kiroho. Kinywa kinapokea chakula na meno yanatafuna, na kukivunja huku kikilainishwa na mate, tayari kwa kumezwa.

Kusoma neno ni kama kinywa, kazi yake ni kulipokea neno. Kutafakari ni kuvunjavunja hilo neno huku Roho wa Mungu akililainisha liwe tayari kumezwa na roho yako.

Kutafakari neno kunamletea mtu siri ya ajabu ya uhakika na ushindi ndani ya Kristo.

Sisi ni watenda kazi pamoja na neno la Mungu hapa ulimwenguni. Tunaliwakilisha Neno la Kristo mahali tulipo na ulimwenguni pote.

Na kwa sababu hiyo, Imeandikwa, "Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote" (Wakolosai 3:160

Huwezi ukawa na Neno la Kristo moyoni mwako bila ya kuitumia siri ya kutafakari. Kukariri neno la Kristo hukukuletei uhakika na ushindi kiroho na kimwili kama vile kutafakari kunavyofanya ndani ya mtu.

Kutafakari ni kuwaza.

Tatizo kubwa sana ambalo linawapata watu ni tatizo la mawazo. Na huu ni ugonjwa mkubwa sana ambao umewakwamisha wengi katika maisha yao ya kiroho.

Kutafakari na kuwaza ni jambo la rohoni, ni jambo la moyoni.

Mtu anapowaza, au kutafakari jambo huwa ni jambo linalofanyika moyoni mwake, ingawa utadhani linafanyika katika ubongo.

Je! wewe unayesoma somo hili sasa hivi unawaza nini moyoni mwako, unatafakari nini? Mara nyingi utaona mtu anaposoma mawazo yake (roho yake) yanakuwa mbali sana, kwa hiyo hakuna anachoelewa katika hayo anayosoma.

Pia, hata wakati watu wanasikiliza neno la Mungu, mara nyingi mawazo yao yanakuwa mbali sana na neno linalofundishwa. Hii inajidhihirisha hasa ukimuuliza ya baada muda mchache baadaye, juu ya neno lililofundishwa maana hatakumbuka.

Unapoumwa huwa unawaza nini? Wengi wanautafakari ugonjwa, na wengine hata kukata tamaa anapoona hauponi haraka. Wengine wanapoumwa wanawaza na kutafakari kufa kuliko kuishi.

Unapokuwa una matatizo huwa unawaza nini? Unapokosa maelewano na mwezako, nyumbani, kazini au mahali popote, huwa mawazo yako yanawaza nini?

Unapokuwa huna fedha au vitu fulani vya kimwili huwa unawaza au kutafakari nini?

Tunaweza kusema mengi, lakini swali kubwa ni hili’ "kila wakati huwa unawaza nini na kutafakari nini?"

Je! unafahamu ya kuwa matendo yako na maneno yako, ni matokeo ya mawazo uliyonayo? Mtu husema anachokitafakari au kukiwaza, na pia hutenda anachokitafakari au kukiwaza moyoni mwake.

Ukitaka kumfahamu mtu alivyo moyoni mwake, sikiliza maneno anayosema na angalia matendo anayoyatenda.

Hakuna katika biblia ambapo mtu wa Mungu ameambiwa haitafakari shida yake, awaze juu ya ugonjwa wake au udhaifu wake.

Kumbuka kuwa maneno ni chakula cha roho, hali ya roho yako inategemea sana ni maneno gani unayasikia kila wakati na kuyatafakari.

Unapotafakari maneno unailisha roho yako. Ukitafakari neno la Mungu roho yako inajengeka katika kumjua Mungu.

Ukitafakari shida, magonjwa, hofu, unaifanya roho yako ijengeke katika hayo.

Watu wengi sana wamejengeka katika kumwogopa shetani kuliko Mungu. Hii hali ipo hata kwa watu wa Mungu. Hayo ni matokeo ya kumtafakari shetani na majaribu anayowajaribu, kuliko kumtafakari Mungu na uweza wake.

Neno la Kristo linakosa nafasi katika mioyo ya watu, kwa sababu mioyo ya watu imejaa mawazo ya dunia hii na shida zake. Mioyo ya watu imejaa mawazo yanayopinga na kwenda kinyume kabisa na neno la Kristo.

Moyo wa mtu ni uwanja wa vita. Ukishinda vita katika mawazo, utakuwa umeshinda vita katika mwili, katika roho na katika maneno.

Je umewahi kujiuliza kwa nini Nabii Ezekieli aliambiwa ale gombo la chuo, na Yohana aliambiwa ale kitabu kilichofunguliwa.

Kwa nini hawa kuambiwa kusoma tu ambayo yalikuwa yameandikwa bila kula gombo la chuo na kitabu kilichofunguliwa?

Nini tofauti ya kusoma na kula. Kunatofauti kubwa kati ya kusoma ujumbe wa Mungu na kula ujumbe wa Mungu.

Soma Ezekeili 2:7-10; 3:1-3 na Ufunuo wa Yohana 10:1,2, 8-11.

Mtu anapokula chakula, huwa kinatafunwa na kulainishwa kabla ya kumezwa. Na kikimezwa na kuingia tumboni, kinanyonywa na kuingia katika mishipa ya damu inayozunguka mwili mzima kukisambaza chakula hicho katika sehemu zinazohitajika.

Mtu anapotembea, ukweli ni kwamba ni chakula kile alichokula ndicho kinachotembea, INGAWA yeye ndiye anayeonekana anatembea.

Kwa hiyo Ezekieli na Yohana walipokula ujumbe wa Bwana uliokuwa umeandikwa katika gombo la chuo na katika kitabu kilichofunuliwa, ujumbe huo uliingia ndani yao kama vile ambavyo wangekula nyama.

Ujumbe huo iliingia kwenye damu yao na ukajenga misuli. Kila sehemu ili kuwa imejaa ujumbe wa Mungu. Ujumbe huo ndiyo uliowafanya wapate nguvu ya kutembea, na kuishi, na kusema.

Kwa mtazamo mwingine tunaweza kusema, Ezekieli na Yohana walikuwa ni ujumbe wa Mungu uliokuwa unatembea.

Na sisi tukilitafakari neno la Kristo, na likijaa ndani yetu kwa wingi, tunakuwa ni neno la Kristo linalotembea; tunakuwa ni neno la Kristo, linalosema; tunakuwa ni neno la Kristo linaloponya; tunakuwa neno la Kristo linaloshauri; tunakuwa Nuru ya Mungu kwa wengine!

Tunafika mahali ambapo kuishi kwetu kunakuwa ni neno (Kristo) – kama vile Paulo alivyosema "kuishi ni Kristo" (Wafilipi 1:21)

Mtu anashindwa kuwa mtendaji wa Neno kwa kuwa moyoni mwake hakuna neno. Anabaki kuwa mtendaji wa maneno mengine aliyonayo mawazoni mwake tu.

"Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha MAWAZO na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara KILA FIKRA ipate kumtii Kristo" (2 Wakoritho 10:3-5) Hii ina maana kuwa fikra zako ziwaze sambasamba na Neno (Kristo).

Katika kuishi kwetu na kuenenda kwetu tuwe tunatafakari nini mioyoni mwetu, ili roho zetu zipate chakula safi cha kiroho?

"Hatimaye, ndugu zangu, mambo yoyote yaliyo ya kweli, yoyote yaliyo ya staha, yoyote yaliyo ya haki, yoyote yaliyo safi, yoyote yenye kupendeza, yoyote yenye sifa njema; ukiwapo wema wowote, ikiwapo sifa nzuri yoyote, YATAFAKARINI HAYO" (Wafilipi 4:8)

Mambo yote haya yaliyotajwa utayakuta katika neno la Mungu. Kwa kutafakari neno la Kristo usiku na mchana katika mambo yote ndipo utakapoifanikisha njia yako ya wokovu na ndipo utakapositawi sana kiroho na kimwili.

Na biblia inasema mtu anayelitafakari neno la Mungu usiku na mchana; anakuwa mtu wa namna hii:

"KILA ALITENDALO LITAFANIKIWA" (Zaburi 1:3)

Fanya hivyo na wewe utafanikiwa.

Unapoumwa usitafakari ugonjwa, wala kuwaza maumivu yake, bali tafakari neno la Mungu juu ya uponyaji nalo litakuwa afya mwilini mwako. Maana imeandikwa hivi:

"Mwanangu, sikiliza maneno yangu; Tega sikio lako, uzisikie kauli zangu. Zisiondoke machoni pako; Uzihifadhi NDANI YA MOYO WAKO. Maana ni uhai kwa wale wazipatao, Na AFYA ya mwili wao wote." (Mithali 4:20-22)

Unapolitafakari neno la Mungu ndipo unapolihifadhi neno hilo ndani ya moyo wako. Na neno la Mungu likihifadhiwa ndani ya moyo wako linakuwa AFYA mwilini mwako, na magonjwa hayatakusumbua tena.

Ukilihifadhi neno la Mungu lenye nguvu za uponyaji ndani ya moyo wako utajua hakika kwamba kwa kupigwa kwake (Yesu Kristo) sisi tumepona". (Isaya 53:5)

Wengi wanapata matatizo katika kupokea uponyaji kwa sababu wanaamini kuwa Mungu atawaponya siku moja akipenda kwa sababu wameomba au wameombewa. Hili ni tumaini na siyo imani. Tumaini siku zote muda wake ni baadaye na imani siku zote muda wake ni sasa.

Imani ya uponyaji huja kwa kusikia na kutenda neno la Mungu linalozungumzia uponyaji. Neno linatuambia ya kuwa tulipona siku nyingi zilizopita kwa kupigwa kwake Yesu Kristo na SIYO tutapona siku moja. Unapompokea Kristo moyoni mwako, magonjwa yanakuwa hayana tena mamlaka juu yako.

Na ili uwe na uhakika wa afya ya mwili wako kila wakati, inakubidi uwe na tabia ya kulihifadhi neno la Kristo moyoni kwa kulitafakari.

Siku moja mtu mmoja aliyekuwa anaumwa alituambia kwa huzuni; "Mimi nimeombewa kwenye mkutano wa injili lakini bado sijapona, ingawa niliwaona wenzangu wengi wakisimama kushuhudia kuwa wamepona".

Tukamwambia; "Na wewe umepona lakini tatizo lako ni kwamba hujui ya kuwa umepona"

Akauliza kwa mshangao; " Inawezekana wapi mtu asijijue ya kuwa amepona na huku bado maumivu anayo hata baada ya maombezi?"

Roho wa Mungu akatuonyesha kwa undani zaidi kwa nini mtu huyo alishindwa kupokea uponyaji.

Tukamwambia; "Uponyaji huwa unapokelewa kwanza katika roho na ndipo unajidhihirisha katika mwili. Wewe ulitaka kwanza uone maumivu yamekwisha, ndipo uamini moyoni mwako ya kwamba umepona. Unatakiwa uwe na uhakika kuwa umepona kwa sababu neno la Mungu linasema umepona na siyo mwili unasemaje"

Mtu huyu alikuwa na tatizo ambalo watu wengi wanalo. Ni tatizo la kukosa uhakika unaodumu wa kuhusu roho zao na miili yao.

Neno la Mungu ndilo kweli inayodumu milele. Neno la Mungu ndilo linalompa mtu uhakika wa jambo ambao hauwezi kuyumbishwa na kitu chochote.

Neno la Mungu linahifadhiwa ndani ya moyo wa mtu kwa kulitafakari na siyo kwa kukariri. Mtu anayekariri mistari ya biblia ni sawa sawa na mtu anayekula mahindi au chakula chochote bila kutafuna.

Neno la Kristo na likae moyoni mwako kwa uwingi katika hekima yote (Wakolosai 3:16).

Kumbuka, Neno la Mungu moyoni mwako ndilo linalokupa uhakika wa mambo yako yote; (wokovu, uponyaji, ushindi katika majaribu, mamlaka yako juu ya shetani na kazi zake, uzima wa milele, na kadhalika.)

Na huo ndio msingi mkubwa wa imani, kwa kuwa "imani ni kuwa na hakika ya mambo….." (Waebrania 11:1).

Kabla imani yako katika Kristo haijaonekana katika matendo yako na maneno yako, ni lazima ijengeke kwanza katika moyo wako kwa njia ya kulitafakari au kuliwaza neno la Mungu katika mambo yako yote.

Matokeo yake ni kwamba utakuwa na uhakika wa jambo lolote moyoni mwako na kwa ajili hiyo utakuwa na ujasiri wa kulisema na kulitenda.

Usipokuwa na uhakika wa jambo moyoni mwako, huwezi ukawa na ujasiri wa kulisema na kulitenda.

Neno la Mungu ndilo nuru na taa miguuni petu sisi tulio ndani yake (Zaburi 119:105); na kwa sababu hiyo tunaishi katika imani iliyo na uhakika udumuo, na wala si wa kubahatisha.

Je, umewahi kuutafakari mstari huu ufuatao:

"Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi, kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu" (1Yohana 3:9)

Swali kubwa tulilojiuliza kwa siku nyingi mpaka Bwana alipotusaidia, lilikuwa, ninawezaje kuishi hapa duniani na tusiweze kutenda dhambi?

Tunaamini hili ni swali ambalo wengi linawasumbua; na hata ambao si wakristo au hawajaokoka wanajiuliza swali.

Mstari huu unatupa maana ya kwamba mtu yeyote aliyezaliwa na Mungu mara ya pili kwa uweza wa neno lake (1Petro 1:23), anatakiwa aishi kuanzia hapa duniani katika utakatifu kama vile Baba yake (Mungu) alivyo mtakatifu, WALA ASITENDE DHAMBI!

Unaweza ukajiuliza na hata kukataa kuwa hii haiwezekani. Lakini kabla ya kukataa naomba ujibu swali hili; "Unadhani Mungu ni dhalimu kiasi hicho kukwambia ufanye jambo ambalo anajua huna uwezo wa kufanya?"

Mungu si dhalimu, maagizo yote aliyotupa, ametupa pia na njia ya kuyafanya.

Kwa hiyo unaweza ukaishi katika utakatifu bila kutenda dhambi!

Imeandikwa:

"Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, NISIJE NIKAKUTENDA DHAMBI" (Zaburi 119:11)

Ukiliweka neno la Mungu moyoni mwako kwa kulitafakari, unaweza ukaishi bila kutenda dhambi, kwa kuwa neno hilo litakuwa nuru na taa miguuni pako (Zaburi 119:105)

Unaanguka mara kwa mara katika dhambi kwa kuwa HUNA NENO LA KRISTO KWA UWINGI MOYONI MWAKO; na kwa sababu hiyo unashindwa kuwa mtendaji wa Neno.

Anza sasa kuwa na tabia ya kulitafakari au kuliwaza neno la Mungu usiku na mchana, utakuwa na akiba ya kutosha ya kukufanikisha wewe na wenzako.

Neno la Mungu ndicho chakula cha roho yako. Lisha roho yako kwa Neno la Mungu kama vile ambavyo unaulisha mwili wako chakula kinachotoka kwenye udongo.

Yesu Kristo ndiye chakula cha uzima kilichoshuka toka mbinguni. Unapomtafakari Kristo, unaifanya sura yake na tabia yake viumbike moyoni mwako.

"Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu" (Yohana 6:51)

Kumtafakari Kristo (Neno) ni kula na kutafuna na kumeza chakula cha uzima. Na chakula hiki (Kristo) kinatufanya tuwe wazima kiroho na kimwili.

"Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, MTAFAKARINI SANA Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, Yesu" (Waebrania 3:1)

Kuna habari ya kweli ambayo ilitokea katika mji mmoja hapa Tanzania, itakayokupa picha ya umuhimu wa kulitafakari neno ili kula chakula cha kiroho.

Kuna mtu mmoja tajiri sana kwa mali ya dunia hii. Ana fedha za kutosha, ana magari mengi ya kwake binafsi, ana nyumba zake, na mali nyingine nyingi.

Siku moja alianguka chini ghafla na kuzimia. Basi, rafiki zake walimbeba haraka sana na kumpeleka hospitalini. Alipofika hospitalini huku bado amezimia, madaktari walimpima kwa vipimo vingi bila kufanikiwa kuona kilichomfanya aanguke na kuzimia.

Na walipokuwa wanachunguza zaidi jambo hili waliona kuwa mtu huyo tajiri alikuwa na tatizo la kutokula chakula vizuri. Kwa hiyo wakamwekea "drip’ ya maji ya "glucose" (maji yenye sukari).

Mara baada ya kumwekea hiyo "drip" aliamka na akashangaa alipojikuta yuko hospitalini na madaktari wamemzunguka. Alipewa chakula zaidi, akapata nguvu na akarudi nyumbani akiwa mzima bila kupewa dawa yoyote ila chakula tu.

Tatizo la mtu huyo ni kwamba ingawa alikuwa na kila kitu cha kumwezesha kupata chakula, alikuwa hana muda wa kukaa chini na kula chakula. Kila wakati alikuwa ni mtu wa shughuli nyingi.

Tulipoambiwa habari hii, Roho wa Mungu alitukumbusha hali ya watu wa Mungu wengi walivyo hivi sasa. Wamezimia kiroho, moto wa injili na maombi umepoa ndani yao kwa sababu hawana nafasi ya kukaa chini na kula chakula cha kiroho.

Kwa sababu wana shughuli nyingi, hawapati kabisa wakati wa kula neno la Mungu kwa kutafakari. Matokeo yake ni kuzimia kiroho. Wakipewa "drip" ya maombi wanasimama na kuendelea kiroho. Lakini kuendelea huku hakudumu kama hawapati nafasi ya kutulia mbele za Mungu na kulitafakari Neno lake – wao wenyewe binafsi.

Kwa hiyo hatua ya kwanza katika kuwa mtendaji wa Neno ni KULITAFAKARI NENO LA MUNGU USIKU NA MCHANA.

Hii ni muhimu sana kwa kuwa katika Kristo (Neno) tunaishi, tunakwenda, na tunakuwa na uhai wetu.

"Kwa maana ndani yake yeye (Kristo au Neno) tunaishi, tunakwenda, na kuwa na uhai wetu" (Matendo 17:28).

Tuzidi kuombeana. Semina tulizonazo mwezi huu ni tarehe 2-3 Novemba 2002 tutakuwa BIRMINGHAM, ALABAMA, U.S.A na terehe 17-24 Novemba 2002 tutakuwa Arusha mjini. Ombea semina hizi, na fika mwenyewe ukiweza.

Ni sisi katika utumishi wa Kristo

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.