Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi Septemba na Oktoba 2002

MTWIKE YESU KINACHOKUFADHAISHA

 

SALAMU,

       Tunakushukuru ni katika Jina la Yesu Kristo, jina lipitalo kila jina. Tunaamini katika Jina hili la Yesu unapata ulinzi na msaada wa kila siku.

       Kama vile ujuavyo, siku hizi ni za mwisho; na ujio wa Bwana Yesu kuja kulichukua kanisa lake u karibu sana. Tunaamini unazidi kujitakasa na kujitia moyo katika Bwana.

       Mwezi huu tunakuletea ujumbe huu unaosema; “Mtwike Yesu kinachokufadhaisha”. Tunaamini kabisa ya kuwa maneno yaliyomo katika ujumbe huu yatakusaidia kusogea hatua nyingine nzuri zaidi katika Yesu Kristo.

Ni sisi

Christopher na Diana Mwakasege

 

Jambo la KWANZA tunalotaka ujue ni kwamba:

        Si mapenzi ya Mungu, wala kusudi lake, wala mpango wake kufadhaika.

Katika kitabu cha 1Petro 5:7 neno linasema hivi: “Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu”.

         Ni muhimu ufahamu maana ya neno ili ‘fadhaa’. Kwa kuwa ikiwa bado hufahamu maana yake itakuwa vigumu kumtwika Bwana Yesu ‘fadhaa’ usizozijua. Neno hili ‘fadhaa’ maana yake ni mahangaiko; au huzuni; au masikitiko; au kukosa amani; au kuwa na uzito moyoni; au kukosa maamuzi; au bumbuazi la moyo.

Kwa mantiki hii, kumtwika Yesu fadhaa zetu zote kuna maana ifuatayo:

  • Kumtwika Yesu KITU chochote ambacho kinafanya moyo wako ufadhaike, au uhangaike, au usumbuke, au upate woga, au ukose raha, au uhuzunike, au ukose amani, au utiwe uzito, au ukose maamuzi.

  • Kumtwika Yesu JAMBO lolote ambalo linaufanya moyo wako ufadhaike, au uhangaike au usumbuke, au upate woga, au ukose raha, au uhuzunike, au ukose amani, au utiwe uzito, au ukose maamuzi.

  •  Kumtwika Yesu MTU yeyote ambaye anaufanya moyo wako ufadhaike, au uhangaike, au ukose amani, au uhuzunike, au ukose raha, au usumbuke, au upate woga, au utiwe uzito, au ukose maamuzi. Hapa mtu huyu anaweza akawa rafiki yako, au mzazi wako, au mtoto wako, au ndugu yako, au mume wako, au mke wako, au mfanyakazi mwenzako, au ‘bosi’ wako kazini, au jirani yako, au mtumishi mwenzako katika Kristo.

  • Kumtwika Yesu SHUGHULI yo yote ambayo inaufanya moyo wako ufadhaike, au uhangaike, au ukose amani, au uhuzunike, au ukose raha, au usumbuke, au upate woga, au utiwe uzito, au ukose maamuzi. Hapa shughuli hiyo inawezekana ikawa kazi, au biashara, kilimo chako, au huduma, au masomo, au mitihani au sherehe, nakadhalika.

Ni kweli tena ni jambo linatakiwa kukubalika kabisa ya kwamba si mapenzi ya Mungu, wala kusudi lake, wala mpango wake tuishi maisha ya mafadhaiko au ya kuhangaika.

Tunaposoma katika kitabu cha Isaya 53:4 tunaona ya kuwa pale msalabani, Yesu “hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu”. Pale msalabani Yesu alichukua dhambi zetu, kwa kuwa si mapenzi yake tukae na dhambi. Pale msalabani Yesu alichukua magonjwa yetu, kwa kuwa si mapenzi yake tukae na magonjwa. Vile vile pale msalabani Yesu aliyachukua masikitiko yetu, kwa kuwa si mapenzi yake tukae na masikitiko. Vile vile pale msalabani Yesu alijitwika huzuni zetu na fadhaa zetu, kwa kuwa si mapenzi yake tukae na huzuni wala fadhaa.

Ndiyo maana Yesu alisema “Msisumbuke maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini …. Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? (Mathayo 7:25,27)

Hatutaki ubaki na mawazo ya kuwa kufanya kazi ni kujisumbua. Biblia inasema mtu asiyefanya kazi na asile (2Wathesalonike 3:10). Alichokuwa anazungumzia Yesu ni lengo au nia uliyonayo unapofanya jambo au kitu – huwa unatafuta nini? Ufalme wa Mungu au fedha kwa ajili ya chakula na mavazi? Watu wasiomjua Mungu huwa wanatafuta chakula na mavazi, lakini watu wa Mungu tunatakiwa KWANZA tuutafute au tutimize kwanza matakwa ya ufalme wa Mungu katika jambo tunalolifanya HALAFU hayo mengine – mavazi na chakula – havitapungua bali tutaongezewa.

Jambo la PILI tunalotaka ujue ni kwamba kuna madhara ya kukaa katika fadhaa au kuishi na mafadhaiko.

Kama kuna jambo ambalo Mungu hataki tukae nalo ina maana lina madhara mabaya kwetu. Hasa tukiangalia gharama ambayo Yesu aliingia ili kuliondoa jambo hilo – gharama ya kifo cha mateso msalabani.

Yesu alichukua dhambi zetu pale msalabani kwa sababu ni mbaya kwetu na hakutaka tuendelee kukaa nazo. Pia, Yesu alichukua masikitiko yetu, huzuni zetu, na fadhaa zetu kwa kuwa ni mbaya kwetu kuendelea kuwa nazo.

Madhara mabayo mtu anaweza kupata akikaa na fadhaa ni pamoja na magonjwa (Mithali 14:30); Mithali 17:22); kukosa furaha (Mithali 15:13); kukosa maamuzi ya busara (Wakolosai 3:15); mauti (2Wakorintho 7:10); na upendo kupotea ( 1 Yohana 4:18)

Wakati mwingine tunaweza tusijue kwa undani ubaya wa jambo kabla ya kufikia uamuzi wa kulikataa. Lakini kama watoto watiifu tunawajibika kutii lile ambalo Baba yetu wa mbinguni anatutaka tulifanye. Kwa mfano, kama anataka tumtwike fadhaa zetu zote tunatakiwa kutii jambo hili. Kwa hiyo tumtwike fadhaa zetu zote wala si fadhaa chache, naye atatupumzisha kwa kutupa utulivu, amani na raha nafsini mwetu.

Jambo la TATU tunalotaka ujue ni hili ya kuwa mambo yafuatayo ukiyafanya yatakusaidia upate kuondokana na fadhaa, huzuni, mahangaiko na mambo yanayofanana na haya pamoja na madhara yake

  1. Nyenyekea chini ya mkono wa Mungu:

           Katika kitabu cha 1 Petro 5:6 tunasoma maneno haya; “ Basi  nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake”

           Ukiambiwa ‘nyenyekea’ kwa jinsi neno hili lilivyotumika katika mstari huu maana yake:

  • Kubali ya kuwa unahitaji msaada wa “mkono wa Mungu” ambao ni Roho Mtakatifu katika jambo hilo linalokufadhaisha;

  • Kubali kuwa chini ya uongozi wa Mungu na kufuata mipango yake katika jambo hilo linalokufadhaisha.

Kumbuka kinyume cha unyenyekevu ni kiburi. Kiburi mara zote kinasema, “Sihitaji msaada wa mtu wala wa Mungu”. Lakini unyenyekevu unasema siku zote; “pasipo msaada wa Mungu mimi siwezi lolote”. Matokeo ya kiburi ni kupingwa na kushushwa na Mungu. Na matokeo ya unyenyekevu ni kukwezwa, kusaidiwa na kuinuliwa na Mungu.

Kwa hiyo hatua ya kwanza katika kuondokana na fadhaa ni kunyenyekea kwa kumwomba Mungu akupe msaada au akusaidie na kukuhekimisha la kufanya katika jambo hilo linalokufadhaisha.

2.      Mtwike fadhaa zako zote au mtwike mizigo yako yote.

Katika kitabu cha 1Petro 5:7 tunaambiwa tunyenyekee, “huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu”. Na katika kitabu cha Mathayo 11:28,29 tunaona Yesu akisema; “ Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu”

Baada ya kumwambia Mungu ya kuwa tunahitaji msaada wake katika eneo linalotufadhaisha, tunatakiwa kuchukua hatua nyingine ya ‘kumtwika’ hiyo fadhaa au ‘kumtwika mzigo’ huo unaotufadhaisha na kutulemea.

Neno hili ‘kumtwika’ linaashiria hatua ambayo Mungu anataka sisi tuifanye. Mungu hataki kutunyang’anya fadhaa tulizonazo kama hatutaki kumpa azichukue. Mungu hataki kutunyang’anya mizigo inayotulemea ikiwa hatutaki kumkabidhi atubebee.

Ni kweli kwamba pale msalabani Yesu ‘ alichukua’ dhambi zetu, magonjwa yetu na masikitiko yetu; na pia ‘alijitwika’ ili kuuonyesha ulimwengu nia yake na uwezo wake wa ‘kubeba’ alichochukua na alichojitwika. Sababu ya kufanya hivi ni ili tujue mahali pa kupeleka dhambi, magonjwa, masikitiko, huzuni, fadhaa tunapokabiliwa navyo.

Je! unamtwikaje Bwana Yesu fadhaa ukiwa nazo? Kwa njia ya maombi – maana ndivyo biblia inavyotuagiza. Katika kitabu cha Wafilipi 4:6,7 imeandikwa hivi:

“Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru,haja zenu zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu,  ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu”

Kwa mantiki ya maneno ya mistari hii, maana yake tunatakiwa kumtwika Bwana Yesu fadhaa tulizonazo na mizigo tuliyonayo kwa njia ya maombi.

Ushuhuda no. 1

Tunamfahamu mtu mmoja ambaye ameokoka, tena ni mtumishi wa Mungu aliyewahi kuweka jambo hili katika matendo na akasaidika.

Kuna wakati fulani mmoja kati ya watoto wake wa kike ambao wote wameokoka alipata mimba  kabla ya kuolewa. Jambo hili lilimshitua sana huyu ndugu. Ingawa aliweza kumsamehe huyo mtoto na kumsaidia aweze kutengeneza maisha yake, hata hivyo kitendo cha binti yake huyo kupata mimba kabla hajaolewa kilimfadhaisha sana.

Baada ya hapo alijikuta anaposafiri na mke wake; na watoto wake wanapobaki nyumbani peke yao, moyo wake ulikuwa ukipata mfadhaiko na mahangaiko mengi. Ndani ya moyo wake hakuwa na uhakika ikiwa binti zake watakuwa waaminifu au la. Jambo hili lilitesa nafsi yake na wakati mwingine kumfanya apate usingizi kwa shida.

Hali hii ilikuwa inampata pamoja na kwamba kila siku alikuwa anawaombea watoto wake na kuwakabidhi kwa Mungu katika maombi. Kabla ya binti yake kupata mimba hakuwa na mahangaiko na mfadhaiko huo wanaposafiri, lakini baada ya binti yake kupata mimba alikuwa anapata mafadhaiko kila waliposafiri.

Siku moja aliamua kuiombea hali hii ya mafadhaiko ili Mungu aweze kumpa ufumbuzi. Alipokuwa katika maombi hayo, Mungu akampa jibu kwa kuuweka mistari hii 1 Petro 5:6,7 moyoni mwake.

Ndipo Roho Mtakatifu alipompa ufahamu huu moyoni mwake. Kwamba kabla binti yake hajapata mimba alikuwa akiwaombea watoto wake na moyo wake ulikuwa huru kuwaacha mikononi mwa Mungu. Lakini baada ya binti yake kupata mimba hata pamoja na kuwaombea watoto wake moyo wake haukuwa huru kuwaacha mikononi mwa Mungu. Uzito huu moyoni mwake ulitokana na wazo hili ya kwamba “nilimwamini Mungu kuwalinda watoto hawa lakini bado mmoja wao akapata mimba – je, hata nikiwaombea sasa nina uhakika gani watalindwa vema?”

Wazo hilo ndilo lililofanya moyo wake usiwe huru, na kumfanya ahangaike na kulemewa kila alipowakumbuka watoto wake. Pamoja na kwamba alikuwa anawaombea ulinzi wa Mungu kila siku, nafsi yake haikuwa huru ‘kuwaacha’ mikononi mwa Mungu. Huyo ndugu anasema alipopata huo ufahamu akaenda mbele za Mungu katika maombi na kutubu – kwa sababu ya kutomwamini Mungu asilimia mia moja juu ya ulinzi wa watoto wake, na kisha kuwakabidhi upya tena ili Mungu awalinde. Baada ya maombi hayo uzito aliokuwa nao moyoni uliondoka na hakupata tena shida na kukosa amani juu ya watoto wake.

Watu wengi huwa wana shida kama iliyompata ndugu huyo. Ingawa tatizo linaweza lisifanane, lakini matokeo yake ya kulemewa na kuhangaika moyoni yafanana. Inawezekana hali hii ikatokea kunapotokea kutokuaminiana kazini, au kutokuaminiana katika ndoa; au kutokuaminiana katika biashara au huduma, na maeneo mengine yanayohusu mahusiano baina ya watu mbalimbali. Ukiwa una mahangaiko au kutokutulia au kulemewa moyoni kwa sababu zinazofanana na hizi tulizozitaja hapa, basi tubu kwa kutokuamini kwako, na mkabizi tena Mungu jambo hilo linalokulemea. Endelea kilikabidhi katika maombi hadi usikie moyoni kama vile mtu aliyetua mzigo mzito hata kama kwa nje tatizo hilo bado halijaisha. Utulivu utakaoupata moyoni ni ishara ya kuonyesha ya kuwa Yesu amebeba huo mzigo au hilo tatizo na si wewe; na pia kwamba ‘umefaulu’ kumtwika Bwana Yesu fadhaa hiyo.

Inawezekana ukawa unajiuliza ya kuwa inakuwaje mtu aokoke tena awe mwombaji au analiombea tatizo linalomtatiza na bado ndani yake asimwamini Mungu juu ya tatizo analoliombea? Sisi tunasema inawezekana kabisa, maana biblia imeweka wazi juu ya jambo hili.

Kwa mfano, katika Zaburi ya 42 ambayo Daudi aliiandika akiwa katikati ya majaribu na matatizo, tunaona jinsi ambavyo roho ya Daudi ilikuwa bado inamtumaini Mungu katikati ya shida hizo, lakini nafsi yake ilikuwa imekata tamaa, imeinama na kupoteza tumaini kwa Mungu. Katika Zaburi 42:5, Daudi anaisemesha nafsi yake hivi;

“Nafsi yangu, kwa nini kuinama, na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu…..”

Ni wazi ya kuwa mafadhaiko ambayo Daudi alikuwa nayo ilikuwa ni matokeo ya nafsi yake ‘kuinama’ au kukata tamaa. Kwa hiyo Daudi (roho yake) akaisemehsa nafsi yake na kuitia moyo isikate tamaa bali imtumaini Mungu. Na wewe ukijikuta katika hali hii jizoeze kujitia moyo kwa kuisemesha nafsi yako isikate tamaa bali imtumaini Mungu.

Ushuhuda no.2

Tunamfahamu pia mtumishi wa Mungu mmoja ambaye alijikuta anaumwa kichwa sana na kwa muda mrefu bila kupona – vizuri. Anasema  alitumia dawa za aina mbalimbali bila tatizo na maumivu ya kichwa kuisha. Lakini pia anasema aliombewa pamoja na yeye mwenyewe kujiombea bila kupokea uponyaji wa kudumu. Wakati mwingine alikuwa anapata nafuu kidogo, lakini baada ya muda mfupi, maumivu makali ya kichwa yalikuwa yanamrudia.

Basi, ndipo siku moja alipoamua kuingia katika maombi ya kumuuliza Mungu chanzo cha tatizo hilo la maumivu ya kichwa; na kwa nini maumivu yalikuwa hayaishi pamoja na kunywa dawa nyingi na kuombewa. Katika maombi hayo, anasema ndani ya moyo wake ulimjia mstari huu unaosema. “ Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mathayo 11:28)

Baada ya kuletewa mstari huu ndani ya moyo wake, na kuanza kuutafakari, Roho Mtakatifu akampa ufahamu wa kujua ya kuwa maumivu ya kichwa yaliyokuwa yanamsumbua ni matokeo ya ‘mzigo’ kumlemea. Akajua ya kuwa kati ya mambo mbalimbali yaliyomhusu ya kila siku katika huduma, katika familia, katika ofisi, na katika jamii; kuna mojawapo limekuwa ‘mzigo’ kwake na matokeo ni kulemewa na kuumwa kichwa.

Ufahamu huu ulimpeleka katika maombi zaidi ambayo sasa yalilenga katika ‘kumkabidhi’ au ‘kumtwika’ Bwana Yesu kila jambo lililomhusu na kila mtu aliyemhusu. Alikuwa akiomba na kusema maneno yanayofanana na mfano huu; “ Mungu nakukabidhi na kukutwika huduma uliyonipa unisaidie kuibeba isiwe mzigo kwangu……”. Na akaendelea kutaja maeneo mbalimbali. Alipomaliza maombi hayo maumivu ya kichwa yaliyomsumbua muda mrefu yalinyamaza na kupona. Na amani ya Mungu ipitayo fahamu zote ikajaa ndani yake.

Tuliwahi kueleza ushuhuda huu mahali fulani na baada ya siku moja mtu mmoja aliyekuwepo kutusikiliza akatuambia jinsi ambavyo kwa muda mrefu alivyokuwa amesumbuliwa na maumivu ya kifua bila kupona kikamilifu – licha ya maombi aliyoomba na hata dawa alizotumia. Akatuambia ya kuwa mara tu baada ya kusikia ushuhuda wa mtu aliyepona kichwa naye akaanza maombi ya “kumkabidhi na kumtwika” Bwana Yesu mambo yote yaliyomhusu moja baada ya jingine. Akalala usingizi usiku huo bila maumivu ya kifua. Ndipo alipotambua kuwa tatizo la maumivu ya kifua lilitokana na kulemewa mizigo ya kazi nyingi alizokuwa anazifanya!

3.    Angalia na jichunguze unachokitafuta katika hicho kinachokuletea fadhaa

Ndilo tunalokuambia: Angalia na jichunguze unachokitafuta katika hicho kinachokuletea fadhaa. Kwa mfano, kama kazi au huduma au biashara unayofanya inakupa mafadhaiko au huzuni, angalia na jichunguze LENGO lako la  kwanza katika kufanya hiyo kazi au hiyo huduma au hiyo biashara.

Tunakuambia hili kwa sababu Yesu Kristo alisema; “Msisumbukie maisha yenu….. msisumbuke basi, mkisema, tule nini? au tunywe nini? au tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa” (Mathayo 6:25,31,33)

Katika maneno haya Yesu hakuwa anasema ya kuwa kujiuliza kuwa utakula nini leo au utavaa nini leo ni vibaya – bali alitaka tuone ya kuwa katika lo lote tunalofanya iwe kazi, iwe huduma, iwe biashara, iwe ndoa, lengo letu la KWANZA liwe ni kuutafuta ufalme wa Mungu na haki yake, na siyo kutafuta kula na kunywa na kuvaa kwa kuwa hilo litakuwa ni ‘kujisumbua’ na mafadhaiko yatatokea. Lakini tukilenga kwanza kutafuta mapenzi ya Mungu yatimie katika hilo tunalolifanya au tunalohusika nalo, basi na hayo mengine (ya kula, ya kunywa, ya kuvaa) tutazidishiwa na siyo tutapungukiwa.

Kumbuka ‘imani isiyo haba’ hutanguliza kwanza ufalme wa Mungu, na haki yake na mapenzi ya Mungu; na si malengo yake binafsi ya kibinadamu.

Mwisho

Tunaamini katika somo hili umepata cha kukusaidia. Tuandikie upatapo nafasi ili tumshukuru Mungu pamoja nawe katika yale aliyokutendea kupitia katika somo hili. Tuombeane na Mungu wetu na ambaye tunaamini ndiye Mungu wako pia, azidi kukubariki na kukufanikisha katika maisha yako.

Ni sisi katika utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.