Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi Aprili 2003

SEHEMU YA ISHARA NA MIUJIZA KATIKA UINJILISTI

Mpendwa katika Kristo.

Salamu katika Jina la Yesu Kristo tunakupa tukijua ya kuwa Mungu anakupenda na anazidi kukupigania na kukushindia. Tunafurahi ya kuwa Roho Mtakatifu ametupa nafasi hii tena tuseme na wewe angalau kwa uchache habari za Bwana Yesu kwa siku hizi za sasa.

Yesu alipokuwa Yerusalemu Biblia inatuambia ya kwamba: “Watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizozifanya” (Yohana 2:23). Na alipokuwa akienda zake ng’ambo ya Bahari ya Galilaya, Biblia inasema; “Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa” (Yohana 6:2)

Unaweza ukaona kabisa unaposoma maisha ya Yesu na huduma yake alipokuwa duniani, ishara na miujiza vilikuwa vivutio vikubwa vilivyowafanya watu wamfuate, wamsikilize na kumwamini. Tunajua ya kuwa Yesu Kristo yuko hai sasa. Je! unadhani amebadilika? Waebrania 13:8 inasema hajabadilika!

Ikiwa ishara na miujiza vilikuwa muhimu katika huduma yake wakati ule, na kwa kuwa hajabadilika tunaamini vitakuwa muhimu katika huduma yake hata leo ndani ya wale wote waliompokea katika maisha yao.

Imeandikwa katika Yohana 20:30,31 ya kuwa; “ Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa ħkatika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.”

Uinjilisti katika mwanzo wa kanisa

Ukisoma maagizo ya Bwana Yesu utaona wazi ya kuwa alitaka huduma ya wanafunzi wake ya uinjilisti na kulitangaza neno la ufalme wa Mungu, isiwe kwa maneno matupu. Bali iandamane na ishara na miujiza! Soma Mathayo 10: 7, 8; Luka 9:1,2 na Marko 16: 17-20.

Hebu tuangalie mifano ifuatayo jinsi inavyounganisha uinjilisti pamoja na ishara na miujiza.

Mfano wa Kwanza:

Matendo 2:1-41. Ilipotokea ishara ya kunena kwa lugha, Mtume Petro alipata nafasi ya kuhubiri kwa lile kundi lililokusanyika kushangaa hiyo ishara. Matokeo yake ni “ Watu wapata elfu tatu” kuokoka na kuwa wakristo.

Mfano wa Pili:

Matendo ya Mitume sura ya 3 na ya 4: Ulipotokea muujiza wa kiwete kusimama na kutembea, Mtume Petro alipata nafasi tena ya kuwahubiri watu waliokuwa wanashangaa muujiza huo habari za Yesu. Matokeo yake ni watu wengine elfu tano kuokoka na kumfuata Yesu.

Mfano wa Tatu:

Matendo 8:5-8: Filipo alipohubiri katika mji wa samaria, Biblia inasema hivi: “ Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa.

Mtume Paulo anapowaandikia wakristo waliokuwa Korintho anasema:

“Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu…..”

Kwa nini:

“….ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu” (1Wakorintho 2:4,5).

Lengo kuu la uinjilisti ni kuwapelekea watu habari za Yesu Kristo ili wapate kumjua na kumwamini kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao ya kila siku. Kibiblia, tunajua ya kuwa Yesu Kristo ndiye ‘njia’ pekee ya kwenda mbinguni. Yesu aliwahi kusema kuwa “….. mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi” (Yohana 14:6). Kwa lugha iliyo nyepesi ni kwamba hakuna mtu atakayekwenda mbinguni ikiwa hajapatana na Bwana Yesu kabla hajafa.

Huu ndio ukweli, na ni ukweli ulio na msukumo ndani yake. Msukumo huu ni ule wa kutaka kila mtu apate nafasi ya kuisikia injili (habari njema za Yesu Kristo). Mtu yeyote anayemwamini Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wake hawezi kukosa msukumo huu ndani yake; kwa sababu anajua ya kuwa mtu akifa bila Yesu, anaishia jehanamu.

Je! unajua hili?

Je! unajua ya kuwa nusu ya watanzania siyo wakristo? Makisio ya karibuni ya takwimu mbalimbali yanaonyesha ya kuwa asilimia 47 tu ya watanzania wote ndiyo wakristo. Nasi tunajua ya kuwa si wakristo wote hawa wameokoka. Wengine ni wakristo wa jina tu, lakini maisha yao hayana ushuhuda wowote ya kuwa wana- Yesu ndani yao mioyo yao.

Fikiria kwa mfano Yesu arudi leo! Itakuwaje kwa wale ambao hawamjui? Au kwa wale waliomsikia lakini hawakutaka kumwamini? Au kwa wale wanaodhani wanaweza kumkwepa Yesu, wapite “njia” nyingine wapate kufika mbinguni? Ikiwa wewe ni msomaji wa Biblia, basi unajua hali inavyoweza kuwa Yesu akirudi leo.

Kwa sababu hii, ni muhimu tutafute njia au mbinu ya kuwafikishia watanzania injili kwa namna ambayo watampokea Yesu na kumwamini kwa haraka na kuwa uwingi. Kumbuka Biblia haituruhusu kumlazimisha mtu kumwamini Yesu na kuokoka au kuwa mkristo. Ni hiari ya mtu. Ni chaguo lake. Kazi yetu ni kuhakikisha kuwa amemsikia na kumwona Yesu – halafu aamue mwenyewe!

Mbinu mmojawapo muhimu ya kutusaidia kufanya uinjilisti wa namna hii ni kwa kutumia ishara na miujiza anayofanya Bwana Yesu mwenyewe – kama tutampa nafasi afanye!

Yesu alipokuwa duniani

Unaposoma habari za Yesu Kristo katika injili zote nne za Mathayo, Marko, Luka na Yohana utaona ya kuwa: Watu wengi walimwamini Yesu kwa kuona ishara alizofanya na miujiza aliyofanya kuliko kwa maneno aliyosema. Utaona wazi ya kuwa ishara na miujiza vilikuwa vitendea kazi muhimu katika kuwathibitishia watu; Yeye ni nani na ametoka wapi. Hebu tafakari maneno haya ambayo Yesu alisema;

“Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba” (Yohana 10:37,38)

Yesu Kristo alipoulizwa na Wayahudi kama yeye ndiye Kristo akawajibu akasema, “Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki; Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia” (Yohana 10:24,25. Wanafunzi wa Yohana walipouliza swali kama hilo la Wayahudi baada ya kutumwa na Yohana alipokuwa gerezani; - Yesu aliwajibu kwa vitendo kwanza! Biblia inasema, “ Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona. Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia. Vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema.” ( Luka 7:19-22).

Nikodemo alipokwenda kumwona Yesu usiku alianza kwa kusema, “ Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye” (Yohana 3:2). Kwa hiyo tunajua ya kwamba kilichomvuta Nikodemo amfuate Yesu ni zile ishara alizoziona na kusikia Yesu Kristo akizifanya.

Je! unafikiri Yesu aliyekuwa ndani ya wanafunzi wa kwanza, akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha neno walilohubiri na kufundisha kwa ishara na miujiza amebadilika? Hapana! Ikiwa hajabadilika siku hizi je! yuko wapi?

Hata leo inawezekana!

Tunajua Yesu yuko hai leo. Hajabadilika. Alichofanya “jana” anao uwezo wa kukifanya hata “leo”.

Utaona mara nyingine kama kukitokea muujiza au ishara watu wanakusanyika kutaka kujua “kulikoni”. Hapo ndipo nafasi nzuri yakuwaambia habari za Yesu anayefanya ishara mpaka leo. Tumeona hili likitokea mara kwa mara.

Wakati fulani tulipokuwa Tanga mjini tuliona watu wengi wakiongezeka kuja kwenye semina tuliyokuwa tunafundisha mwanzoni mwa mwaka huo waliposikia jinsi wagonjwa walivyokuwa wanapona. Mtu mmoja ambaye alikuwa hajaokoka alikuja akitaka uponyaji katika sikio lake lililokuwa limeziba na kutokusikia kwa muda wa miaka mitatu. Wakati wa maombi ya wagonjwa akapona na akaanza kusikia tena katika sikio lililokuwa limeziba. Na wagonjwa wengine walipona pia. Tulipotangaza ya kuwa wanaotaka kumpokea Yesu huyu anayeponya apate kuwaokoa, wengi walitoka mbele kuombewa ili waokoke, pamoja na yule aliyepona sikio!

Usiseme mimi siwezi! Nenda kasome katika Biblia alichosema Yesu! Katika Marko 16:17-20 alisema; “Kila aaminiye….”. Kama unamwamini Yesu ya kuwa ni Mwana wa Mungu, amefufuka na ni Mwokozi – neno ‘kila’ linakuhusisha na wewe! Katika Yohana 14:12 anasema, “ Yeye aniaminiye mimi ……” Hii inakuhusisha na wewe! Chukua hatua. Tumia nafasi Mungu anayokupa unapokutana na mgonjwa. Mwombee akikuruhusu umwombee au ndugu zake wakikuruhusu. Kazi yako ni kuomba. Kazi ya Bwana Yesu uliye naye ni kuponya. Sifa na heshima si zako bali za Bwana Yesu anayeponya hata leo!

La kukusaidia!

Inawezekana una hofu. Ujasiri wa kuchukua hatua huna. Au uliwahi kuombea mtu hakupona au ulipata vitisho. Jizoeze kuomba maombi haya:

“Basi, Bwana, yaangalie matisho ya wanaonitisha na kunikatisha tamaa katika huduma hii. Unijalie mtumishi wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyoosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako Mtakatifu Yesu. Amina”.

Sala hii tumeichukua katika maneno ya maombi ya wanafunzi katika kitabu cha Matendo 4:29-31. Sisi wenyewe tumekuwa tukiomba mara kwa mara kwa ajili yetu na mahali tunapokwenda kuhudumu. Na tumeona matokeo yake yanavyozidi kujitokeza, na bado tunaendelea kuomba sala hii mara kwa mara.

Unaweza na wewe ukaomba sala hii au kwa maneno mengine jinsi Roho Mtakatifu atakavyokupa. Omba kwa ajili yako; na omba kwa ajili ya mahali unaposali au unapoabudu. Lengo: Yesu aonekane watu wamwamini. Anza leo!

Shukrani.

Mzigo ulio nao wa kutusaidia katika maombi kwa ajili ya huduma ambayo Mungu ametupa – zidi kuwa nayo na Mungu akutie nguvu uendelee. Tunahitaji hayo maombi. Ahsante pia kwa kila mtu aliyejitoa kwa mali na/au muda wake kutusaidia tufanikiwe katika huduma ya Bwana. Mungu wetu na azidi kukuzidishia sawa sawa na ahadi zake.

ni sisi katika utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.