|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
NAMNA YA KUTUNZA UWEPO WA MUNGU Je, unafahamu ni nini chanzo cha wakristo kupoa kiroho? Kitu gani kinakufanya wakati mwingine uwe na maisha ya uvuguvugu kiroho? Imekuwa ni kitu cha kawaida kwa wakristo siku hizi kuwa na maisha ya kiroho yanayobadilika – badilika. Leo yanakuwa ya moto na kesho yanakuwa ya baridi – je, ndivyo Mungu anavyotaka tuwe? Kuna wakati mwingine hata inafikia wakati mtu anaanza kujiuliza kama Mungu yupo pamoja naye au amekwisha – mwacha na yeye hana habari. Jambo muhimu kwa mtu yeyote aliyeokolewa kwa damu yenye thamani kuu – damu ya Yesu Kristo ni kuona ya kuwa uwepo wa Mungu unakuwa pamoja naye, SIKUZOTE, KILA WAKATI na KILA MAHALI. KIUTunaamini ya kuwa una kiu ya kuona nguvu za Mungu zinazidi kuonekana kwako kila siku. Tunaamini ya kuwa unatamani uwepo wa upako wa Roho Mtakatifu uwe wazi na wenye kuzidi kila siku katika kila ufanyalo. Ni wazi ya kuwa unapookoka – Yesu Kristo anaingia ndani ya roho yako na kufanya makao ndani yako kwa uwezo wa Roho wake Mtakatifu. Lakini je! Huyu Yesu Kristo aliye ndani yako anaonekana katika kila unalolifanya? Je! Wanaokuzunguka na kusikia unachosema – wanamwona Yesu Kristo aliye hai katika maisha yako? Ni kweli kabisa ya kuwa pasipo uwepo wa Yesu Kristo katika maisha yetu, hatuwezi kufanikiwa katika lolote lile tufanyalo. Yesu Kristo yupo pamoja nasi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Tufanyaje basi, ili uwepo huu wa Roho Mtakatifu katika maisha yetu udumu na uzidi KATIKA KILA TUFANYALO? Kumbuka Yesu Kristo alituambia hivi katika kitabu cha Yohana 15:5; “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana PASIPO MIMI NINYI HAMWEZI KUFANYA LOLOTE” TUJIFUNZE TOKA KWA YESU KRISTOSiku moja Yesu Kristo aliwaambia wanafunzi wake kwa mshangao, akasema, “ Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini BABA AKAAYE NDANI YANGU huzifanya kazi zake (Yohana 14:10). Ni wazi kabisa ya kuwa Mungu Baba alikuwa pamoja na Yesu Kristo kila siku, katika kila alilolifanya na katika kila alilolisema. Ndugu zake, rafiki zake na adui zake, wote walishuhudia ya kuwa Yesu Kristo alikuwa na uwezo na hekima isiyo ya kawaida – kwa jinsi ya kibinadamu. Kuna wakati Fulani watu waliotumwa na Mafarisayo kumshika walirudi mikono mitupu huku wakisema “ Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena” (Yohana 7:46.) Roho wa Baba yaani Roho Mtakatifu alikuwa pamoja na ndani ya Kristo kila wakati. Jambo hili lilimfanya Yesu Kristo awe na uwepo wa Baba yake kila wakati – na Yeye alijua hilo. Mafanikio ya maisha na huduma yake hapa ulimwenguni ilitegemea sana uhusiano aliokuwa nao na Baba yake. Baba yake asingekuwa naye kila siku – huduma yake isingekuwa na matunda wala maisha yake yasingekuwa na maana kwetu. YESU ALIFANYA NINI? Yesu Kristo Mwenyewe anatuagiza ya kuwa vivyo hivyo na sisi – bila ya uwepo wake kuwa pamoja nasi na ndani yetu – matunda ya ukristo wetu hayataonekana na huduma aliyotupa tuifanye itakwama. Ni jambo gani lililomfanya Baba Mungu awe na mtoto wake Yesu Kristo kila wakati? Yesu Kristo anatupa jibu anaposema hivi katika kitabu cha Yohana 8:28,29 ya kuwa: “…..Sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba ALIVYONIFUNDISHA ndivyo ninenavyo. Naye aliyenipeleka yu pamoja nami; hakuniacha peke yangu; kwa sababu NAFANYA SIKUZOTE YALE YAMPENDEZAYO.” Kwa sababu SIKUZOTE alifanya yale yampendezayo. Yesu Kristo alifanya mapenzi ya Baba yake siku zote. Na sisi tukitaka kuwa na Baba Mungu na Kristo Yesu sikuzote (si jumapili tu au wakati Fulani tu bali sikuzote) inatupasa tuyafanye mapenzi yake siku zote. Maana yake tuwe watendaji wa Neno lake siku zote na kila mahali, ndiyo maana Yesu Kristo alisema hivi; “Mtu akinipenda, atalishika Neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” (Yohana 14:23) TUJIFUNZE TOKA KWA WAKRISTO WA KWANZATunaposoma jinsi Ukristo ulivyoanza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Matendo ya Mitume tunaona ya kuwa Ukristo ulianza kwa nguvu na uliendelea kwa nguvu sana! Wakati huo, “kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume” (Matendo ya Mitume 2:43). Si hivyo tu, bali Wakristo hao wa kwanza walikuwa SIKUZOTE, “Wakimsifu, Mungu na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa KILA SIKU kwa wale waliokuwa wakiokolewa” (Matendo ya Mitume 2:47) Hebu fikiria ilivyo vema kushuhudia muujiza huu wa KILA SIKU watu kuokoka! Siyo kila mwezi tu, siyo kila wakati wa mkutano wa kiroho tu, wala si kila Jumapili tu – bali KILA SIKU Bwana aliokoa watu! Nini chanzo cha siri hii ya wenzetu kushuhudia na kutembea na Nguvu za Mungu namna hii? Kwa nini mambo haya hayaonekani siku hizi? Kwa nini mahali pengine pana ukame sana wa kiroho, - hata ishara na miujiza ya Mungu haionekani – wala watu hawaokoki kwa wingi? Je! Tunaweza kujifunza kitu kutokana na maisha ya wakristo wenzetu hawa? Maana walimwamini na kumtumikia Mungu yule yule tunayemwamini na kumtumikia sasa katika Kristo Yesu. Kwa nini basi kuna tofauti ya uwepo wa Mungu kwa kiasi kikubwa hivyo. Kitu gani kilimfanya Mungu aonekane sana katika maisha ya wenzetu kuliko ilivyo sasa? Siri ya wakristo wa kwanza waliyoitumia ili nguvu za Mungu ziweze kuonekana katika maisha yao imo katika maneno ya mstari huu, “ Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali” (Matendo ya Mitume Mambo matatu makubwa yanajitokeza katika mstari huu ambayo waliyafanya wakristo wenzetu na hata uwepo wa Mungu ulikuwa pamoja nao kwa nguvu wakati wote; Mambo hayo matatu ni haya yafuatayo;
Ukisoma zaidi katika Matendo ya Mitume 2:43-47 utaona jinsi hawa wenzetu walivyoishi na kuuonyesha ukristo wao. Pia wazo hili unalipata katika Matendo ya Mitume 4:23-37. Matokeo yake ni kwamba Neno la Mungu lilienea haraka sehemu nyingi, Ishara na Miujiza ilifanyika kwa jina la Yesu Kristo, na watu waliokolewa kila siku. Si hivyo tu bali Biblia inaongeza kusema hivi; “Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu” (Matendo ya Mitume 13:52) Hata hivi leo tukitaka kuuona uwepo wa Mungu ukiwa pamoja nasi kwa nguvu kama ulivyokuwa pamoja na wenzetu; inatupasa na sisi tuishi kama walivyoishi. Siku zote tunatakiwa tuishi maisha ya kudumu. 1. Katika maombi na 2. Katika kusoma na kulitenda Neno la Kristo; na 3. Katika kushirikiana ili kuonyesha tunavyopendana. Matokeo yake ni kuona sikuzote tumejaa furaha na Roho Mtakatifu. Hakutakuwepo kupoa kiroho, bali wakati wote tutakuwa tunatembea na kuishi katika uwepo wa Mungu wetu ulio katika Roho Mtakatifu. Mambo hayo matatu tuliyoyataja hapo juu yakitendeka, kunatokea uamsho katikati ya watu. Uamsho unapotokea katikati ya watu wa Mungu, kuna mambo mengi yanayotokea, lakini mambo makubwa matatu hujitokeza. Haya mambo matatu ndiyo pia yanayoonyesha tabia za Uamsho zilivyo:
Palipo na uamsho pana hofu ya Mungu. Kuna wakati unafika ambapo watu wa Mungu wanapoa na kutokujali sana mambo ya Mungu, na kutokupenda maombi ya muda mrefu, na hata kufikia kutokwenda kanisani au kwenye vipindi vya masomo ya Biblia, kwa kujisingizia shughuli nyingi. Ukiona haya yanajitokeza au yamejitokeza, basi ujue ya kuwa hofu ya Mungu haipo kati yao. Na Mungu anapoamua kujidhihirisha upya katikati yao kwa uwezo wa Roho wake Mtakatifu, kunatokea uamsho, na uwepo wa Mungu unakuwa wazi kwa kila mtu. Na palipo na uwepo wa Mungu, pana hofu ya Mungu. Lakini hofu ya Mungu inaporudi katikati yao kwa sababu ya uamsho wa Roho Mtakatifu, wanaanza upya kutembea katika hekima. Je, unafahamu ni kwa nini? Kwa kuwa imeandikwa “ Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima, …….” (Zaburi 111:10) Tafsiri nyingine ya hofu ya Mungu ni kumcha Bwana. Mungu anapojidhihirisha upya katikati ya watu wake, kila mmoja wao anaona kama vile Mungu ameshuka kwa ajili yake tu na ameshuka kumshughulikia yeye tu! Kwa hiyo utaona watu wakiwa wepesi kutubu dhambi zao na kutengeneza au kurekebisha maisha yao. Na kinachofuata ni watu hao kuanza kujishughulisha upya na mambo ya Mungu. Utaona wanapenda utakatifu, - utaona wanapenda maombi na kumtumikia Mungu. Kunapotokea uamsho watu huona Mungu yuko karibu nao zaidi kuliko alivyokuwa zamani. Tunakumbuka tulikuwa tunahubiri mahali fulani hapa nchini, na tuliposema wale wanaotaka kutubu waje mbele, watu wengi walikuja na kutubu kwa machozi. Roho wa Mungu alishuka kwa nguvu katika mkutano ule. Na tulipowafuatilia hao waliotubu, tukaona ya kuwa robo tatu yao walikuwa ni watu waliokuwa wameokoka zamani lakini wakarudi nyuma na kuanguka dhambini. Na neno lilipohubiriwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, wakachomwa mioyo yao, wakawa kama watu walioamshwa toka usingizini, wakaamua kutubu na kumrudia Mungu. Na matokeo yake ni vikundi vya maombi kuanza kwa upya, na ‘fellowship’ kupata nguvu mpya, na watu kushuhudia kwa ujasiri na bila woga. Hii si kazi ya mtu, ni kazi ya Roho Mtakatifu aichunguzaye mioyo ya watu na kuijua ilivyo.
Watu wa Mungu wakipoa, hata watu wanaozaliwa upya mara ya pili wanakuwa wachache. Watu wa Mungu wakiamka upya kiroho, watu wengi wanaokoka. Ni wazi kwamba kunapotokea uamsho, mavuno ya roho za watu yanakuwa mengi – kwa kuwa watu wanapata msukumo mpya wa kushuhudia. Hivi ndivyo ilivyokuwa wakati wa wanafunzi wa kwanza wa Yesu Kristo. Siku ya Pentekoste ilipotimia Roho wa Uamsho aliwashukia wale wanafunzi wa kwanza wa Kristo, ambao walikuwa wamejaa hofu na wasiwasi; na baada ya kuwaamsha na kuwavika ujasiri walianza kumsifu Mungu kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Uamsho huu katikati ya wanafunzi wa Kristo, ulileta mafadhaiko na mshangao kwa wale ambao hawakuwa wanafunzi wa Kristo. Imeandikwa; “ Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa …. Wakashangaa wote …..” (Matendo ya Mitume 2:6,7) Na wakati ule ule Petro ambaye alikuwa amewahi kumkana Yesu Kristo mara tatu, Roho Mtakatifu alimpa ujasiri wa kusimama na kuhubiri kwa nguvu habari za Yesu Kristo. Mtume Petro aliyeamshwa na Roho Mtakatifu akisema maneno yake huwa yamejaa moto ambao huwachoma wale ambao wanamsikiliza! “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina la Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie. Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi. Nao waliolipokea neno lake (walioamua kuokoka) wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu” (Matendo ya Mitume 2:37 – 41) Kwa sababu ya uamsho wa Roho Mtakatifu katikati ya watu wa Kristo, watu wengine ELFU TATU walikoka kwa siku moja na kwa mahubiri ya mtu mmoja. Hii ni kazi ya Roho Mtakatifu. Na hawa waliookoka si kwamba walitubu na kutawanyika bali Biblia inasema, “ Wakawa wakidumu katika fundisho la Mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali. Kila mtu akaigiwa na hofu ……….Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa”. (Matendo ya Mitume 2:42 – 47)
Watu wa Mungu wakipoa kiroho, matengano, magomvi na mashindano hutokea katikati yao. Watu wa Mungu wakipoa kiroho, huwa wanapambana wao kwa wao badala ya kupambana na shetani. Watu wa Mungu wakipoa kiroho hata baraka za Mungu hazionekani katika makusanyiko yao, ndoa zao, na kazi zao. Wanakuwa ni watu wanaoshi kwa kujitahidi, na siyo kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Imeandikwa hivi: “Tuishi kwa roho, na tuenende kwa Roho. Tusijifu bure, tukichokozana na kuhusudiana” (Wagalatia 5:25,26) “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa UMOJA ……….. Maana ndiko Bwana ALIKOAMURU BARAKA, Naam, uzima hata milele” (Zaburi 133:1-3) Hii ni habari njema kusikia kwamba BWANA AMEAMURU BARAKA ZAKE ZIENDE KWA WATU WANAOKAA PAMOJA NA KWA UMOJA! Ni kweli kwamba vitu vingi vinaweza kutukusanya pamoja, kama vile ndoa, harusi, msiba, mikutano, ibada, ugomvi, mashauri; nakadhalika. Lakini kuwa pamoja haimaanishi kuwa mna umoja. Tunarudia tena: Lakini kuwa pamoja haimaanishi kuwa mna umoja. Mnaweza kuwa pamoja katika ibada au harusi huku moyoni hampatani. Na hivi ndivyo ilivyo, kwa watu wengi wa Kristo. Wanakaa au wanakutana pamoja lakini hawana umoja. Umoja wa kweli hauletwi na taratibu za kibinadamu hata kama ni nzuri sana. Zinaweza kutufanya tuwe pamoja, lakini haziwezi kutufanya tuwe na umoja. Umoja wa kweli huletwa na Roho Mtakatifu. Ndiyo maana Roho Mtakatifu akijidhihirisha kwa upya katikati ya watu wa Mungu, huwa wanapatana na kuwa kitu kimoja bila kujali tofauti ya madhehebu yao. Ndivyo ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Kristo wa kwanza walipohuishwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Imeandikwa hivi: “Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu, Wakawa wakidumu katika fundisha Mitume, na katika USHIRIKA, na katika kuumega mkate, na katika KUSALI ……. Na wote waliaoamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. Na siku zote kwa MOYO MMOJA walidumu katika hekalu, wakimega mkate NYUMBA KWA NYUMBA na kushiriki chakula chao kwa FURAHA na kwa MOYO MWEUPE, wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa WAKIOKOLEWA” (Matendo ya Mitume 2:41-47) Kunapotokea uamsho, umoja wa kweli hutokea. Kulipo na uamsho wa Roho Mtakatifu, ushirikiano wa kweli hutokea. Kunapotokea uamsho, uchoyo unahama, ugomvi unahama, wivu unahama, uvivu unahama, na ubinafsi unahama. Ni tabia ya uamsho kuleta umoja wa kweli – watu waliopoa kiroho wanaamka toka katika uchoyo, toka katika ugomvi, toka katika ubinafsi na wivu, na badala yake wanaanza kushirikiana, kusaidiana, kupendana na kusali pamoja katika Roho Mtakatifu. Tena Imeandikwa hivi: “Na jamii ya watu walioamini (waliookoka) walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu chochote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali WALIKUWA NA VITU VYOTE SHIRIKA. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye MAHITAJI; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile walivyouza, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadri ya alivyohitaji” (Matendo ya Mitume 4:32-35). |
|