Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Desemba 2003                                                        Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


MUNGU AKITEMBEA……
….. TEMBEA PAMOJA NAYE!

Salamu katika Jina la Yesu Kristo,

Tunachoamini sisi ni kwamba hiki ni kipindi ambacho Mungu ameamua kuitembelea Tanzania kwa namna ya kipekee kabisa! Kwa wale ambao wanafuatilia mambo ya kiroho ya nchi ya Tanzania, watakubaliana nasi juu ya jambo hili. Hiki ni kipindi ambacho tunahitaji kukitumia vizuri sana kwa utukufu wa Jina la Yesu Kristo.

          Kwa hiyo tunachosema ni hivi “ Mungu akitembea katika nchi yako – basi inakubidi na wewe utembee pamoja naye!”Tunapofanya semina katika sehemu mbalimbali hapa nchini – tunajitahidi kutembea na Yesu katika maeneo hayo na tumeshuhudia mambo mengi ya ajabu ambayo amekuwa akiyafanya.

          Hii ni ripoti ya mambo ambayo tumeona Yesu akaiyafanya Arusha Mjini (28 Septemba – 5 Oktoba 2003 ), Alabama, Marekani (17 - 19 Oktoba 2003 ), Mbeya Mjini (05– 09 Novemba 2003),    na Kilombero (12 – 16 Novemba 2003). Tulimwona Mungu katika maeneo haya akijidhihirisha kwa “dalili za nguvu na za Roho Mtakatifu”. Hatuna maneno ya kutosha ya kuelezea shukrani tulizonazo kwa Mungu huyu aliyetuita katika Yesu Kristo tutumike chini ya uongozi wake katika kizazi hiki. Sifa na utukufu tunamrudishia Yeye peke yake, maana anastahili!

          Tunatarajia pia kuona na kushuhudia mambo makuu Yesu akiyafanya katika semina ya kumalizia mwaka huu (2003), tutakayokuwa nayo Dar es Salaam tarehe 17-21 Disemba, katika ukumbi wa PTA katika uwanja  wa maonyesho ya sabasaba. Karibu sana kwako wewe unayeweza kufika. Pia, usisahau kutuombea ili Jina la Yesu Kristo likapate kutukuzwa katika hali zote wakati wa semina hii.

Watu wengi waokoka….
…. Wachungaji wajadiliana cha kufanya!

          Jambo mojawapo katika semina hizi ambazo zote zimefanyika ndani ya hema kubwa tulilonalo (kasoro ile semina tuliyoifanya Alabama, Marekani) – ni mahudhurio ya watu kuwa makubwa sana. Kwa mfano semina ya Arusha, ambayo ilikuwa ya pili kuifanya mjini hapa kwa mwaka huu yaliyokisiwa kuwa na watu 30,000 ( hasa katika zile siku tatu za mwisho wa semina – maana semina ilikuwa ya siku nane na siku ya tisa ilikuwa ya shukrani, shuhuda, maombi na uimbaji.

          Katika semina hizi za Arusha, Mbeya na Kilombero tuliona kwa uchache wa wastani wa watu elfu kumi na sita wakiokoka. Na kuna wengi ambao ingawa waliokoka hatukuweza kuwaandika kwa ajili ya uchache wa wahudumu tuliokuwa nao. Lakini tunaamini mbinguni kuna kumbukumbu ya majina yao katika “kitabu cha uzima cha Mwana Kondoo.”

          Hii ni idadi kubwa kuokoka kwa muda mfupi namna hii katika semina hizi tunazozifanya. Na jambo hili limeleta changamoto kubwa kati ya wachungaji tulioshirikiana nao juu ya namna ya kulea na kutunza kondoo hao wasije wakapotea au wakarudi nyuma au wakafa!

          Lakini tunajua Yesu ni “Mchungaji Mkuu” wa kondoo, ni maombi yetu na imani yetu ya kuwa atawahekimisha na kuwaelekeza watumishi wake katika kutunza mavuno haya makubwa.

Masomo yalikuwa changamoto
kwa maisha ya kila siku!

          Utamu mmojawapo wa biblia ni kuona jinsi ambavyo Mungu anajihusisha na kutatua matatizo ya maisha ambayo mwanadamu anakumbana nayo kila wakati katika jamii anamoishi. Ingawa sisi tulikuwa katika nafasi ya kufundisha katika semina hizi, lakini tulijikuta ‘tukifaidi’ mafundisho hayo na kuhuishwa nayo kama vile ilivyokuwa ikitokea kwa wale tuliokuwa tunawafundisha!

          Hebu hapa tukumegee angalau kwa muhtasari tu yale tuliyojifunza. Katika semina ya Arusha tulikuwa na somo lililokuwa na kichwa hiki: “Mambo Unayohitaji Kuyajua juu ya Mpango wa Mungu katika Maisha yako”. Tulijifunza ya kuwa yako mambo mengi tunayohitaji kuyajua – lakini muda tuliokuwa nao tulijifunza yafuatayo: Tukiongozwa na neno la Yeremia 29:11 – 14.

·         Amua au chagua kuutafuta na kuufuata mpango wa Mungu katika maisha yako kuliko mipango mingine yeyote!

·         Kuchagua na kuamua kuufahamu na kuufuata mpango wa Mungu kuliko mipango mingine Bila ndani yako kuwa na hamu kubwa au KIU  ya  kuufahamu na kuufuata huo mpango wa Mungu – hakutakusaidia sana!

·         Kwa sababu Hamu Kubwa au KIU yoyote ina mvuto ---mvuto huu unakuvuta kuelekea mahali kiu hiyo inataka. Kiu hii ya kuufahamu mpango wa Mungu inategemea thamani unayoiona ipo katika mpango wa Mungu kwako. Na itakuvuta kumtafuta Huyo aliye na huo mpango wako yaani Kristo. Soma Yohana 7:47-39.

·         Soma Neno la Mungu yaani biblia kwa lengo la kupata mawazo ya Mungu na mbinu za Mungu juu ya kujua na kutekeleza mipango yake.

·         Jifunze kumweka Mungu awe wa Kwanza katika kila eneo la maisha yako.

Tulipokuwa Mbeya tulikuwa na somo lililokuwa na kichwa kinachosema; “Kwa nini watu wengi hawafanikiwi katika maisha yao?” Tuliongozwa katika somo hili na mstari wa 3 Yohana 1:2 unaosema “ Mpenzi, naomba ufanikiwe katika mambo yote, na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo.”

Tuliangalia mambo yafuatayo kama sababu mojawapo zinazofanya watu wasifanikiwe katika maisha yao:

·         Watu wengi wanaishi bila kuwa na lengo la kufanikiwa. Au kufanikiwa siyo sehemu ya lengo katika maisha yao.

·         Watu wengi siyo waangalifu juu ya maamuzi wanayofanya kila siku.

·         Wengi hawafuatilii maneno wanayojisemea wala yale yanayosemwa na wengine juu yao.

·         Wengi wameishiwa maarifa ya kuwasaidia ili wafanikiwa, hata kama wanataka kufanikiwa.

Katika semina ya Kilombero tulijifunza somo lililokuwa na kichwa kinachosema; “Mambo ya kufanya ili ahadi za Mungu zitimie kwako”. Kwa siku tano tulizokuwa nazo kwa semina hiyo tulijifunza mambo yafuatayo ya kuwa:

·         Fahamu kwanza kama ahadi hiyo unayoitaka inakuhusu na una haki ya kuipata kabla ya kuamua uiombeje.

·         Jiulize kama ahadi hiyo unayoitaka inatokana na agano la namna gani – maana kila agano lina mapatano au makubaliano yanayotafautiana.

·         Totautisha kati ya sababu ya ahadi kuwepo, na njia inayoleta hiyo ahadi kwetu. Halafu wewe weka hamu yako na lengo lako kupata kile ambacho ni sababu ya ahadi kuwepo.

·         Jizoeze kuitafakari ahadi hiyo unayoitaka hadi uione moyoni (mawazoni), ingawa bado haijajitokeza kimwili au kwa nje.

Somo hili la semina ya Kilombero liliongozwa na neno toka 2 Petro 1:3,4. Na tulipokuwa Alabama, Marekani tulijifunza mambo ya ndoa, na pia somo lililohusu Namna ya Kushughulikia madeni.

Mungu ajibu maombi ya watu wengi!

Ni tabia ya Mungu kujibu maombi! Yeye mwenyewe amekaribisha maombi – watu wamwombe mahitaji yao kwa utaratibu alioweka katika biblia. Kwa wale wote walioamua kuitikia  wito huu wa kuomba – tunaamini wameona Mungu akiwajibu!

Tunapokuwa kwenye semina za namna hii kama tunazozifanya sehemu mbalimbali – ni jambo la kawaida kuwa ni vipindi vya shuhuda. Katika vipindi hivi tunawahimiza watu kujitokeza kushuhudia matendo makuu ambayo Mungu amewatendea katika huduma Mungu alizotupa za semina, radio, kanda na vitabu.

Lengo kubwa linalotufanya tuwahimize watu watoe shuhuda hizi ni kwamba:

·         Shuhuda hizo zipate kumtukuza Mungu katika Jina la Mwana wake Yesu Kristo.

·         Shuhuda hizo zinathibitisha ya kuwa Yesu Kristo yuko hai na hajabadilika (Waebrania 13:8) na ya kwamba Yeye ndiye Kristo – Mwana wa Mungu (Yohana 20:30,31); na ya kwamba neno tunalofundisha linatoka kwake (Marko 16:20).

·         Lakini, pia shuhuda hizo zinawatia moyo na kuwapa matumaini watu wengi ambao wana mahitaji kama ya wale waliojibiwa – ya kuwa kama vile Mungu alivyowasaidia wengine; atawasaidia na wao pia.

Vipindi hivi vya shuhuda, ni muda hata sisi ambao pia tunausubiri kwa hamu sana – kwa sababu tulizozitaja hapo juu. Mambo tuliyoona na kusikia Mungu ameyafanya kwa watu wake Arusha, Mbeya na Kilombero ni mengi sana, na haitakuwa rahisi kuyaandika yote. Lakini tungetaka kukushirikisha haya machache:

Shuhuda mojawapo iliyojitokeza  mara kwa mara ni juu ya familia zilizokuwa na shida ya kupata watoto na Mungu akawajibu. Tulishuhudia akina mama zaidi ya kumi wakisimama kushuhudia pamoja na watoto wao waliowazaa. Laiti ungekuwepo na kuona furaha walizokuwa nazo na jinsi mioyo na midomo yao ilivyojaa shukrani na sifa kwa Yesu aliyewajalia kuzaa watoto hao.

Tuliona wengine wakishuhudia jinsi walivyosubiri kupata watoto bila mafanikio hadi mmoja kufikia miaka 15! Miaka 15 ni mingi sana kusubiri mtoto ingawa Ibrahimu na Sara katika biblia walimpata Isaka baada ya kusubiri miaka 25!

Familia moja mtu na mke wake walisimama na kushuhudia jinsi ambavyo walimwomba Mungu awape watoto mapacha wakati wa maombi katika semina ya mwaka jana tuliyoifanya Arusha. Na Mungu akawasikia na amewajalia kupata watoto mapacha wawili – mmoja wa kike na mwingine wa kiume.

Mama mwingine alishuhudia jinsi alivyojaliwa kupata mtoto akiwa hai baada ya mimba mbili zilitangulia watoto kufia tumboni kabla hawajazaliwa!

Mama mwingine aliomba Mungu ampe mtoto wa kiume, na ndani ya moyo wake alikuwa na uhakika wa kujibiwa kiasi kwamba alinunua nguo za mtoto wa kiume na kumpa jina la kiume kabla mtoto hajazaliwa. Na alipojifungua - alizaa mtoto wa kiume! Jina la Bwana libarikiwe!

Mama mwingine tulipokuwa kwenye semina Mbeya alieleza ya kuwa yeye hakufika kwenye semina ya mwaka jana tuliyoifanya Mbeya – ila wenzake walifika na kuweka ombi kwenye ‘box’ la maombi juu ya mama huyo aliyebaki nyumbani ili apate mtoto. Mungu akayasikia maombi hayo, na akamjalia kupata huyo mtoto. Akaja na huyo mtoto aliyemzaa katika semina ya mwaka huu tuliyoifanya Mbeya ili kumpa Mungu utukufu.

Hizi ni baadhi tu ya shuhuda za wale walioomba Mungu awape watoto na akawapa! Inawezekana unayesoma habari hizi unashida ya kupata mtoto na umemwomba Mungu na bado hujajibiwa. Inawezekana pia ya kuwa wewe huna tatizo la namna hii, lakini unaifahamu familia yenye hitaji la namna hii, na wamemwomba Mungu lakini hadi sasa bado hawajajaliwa kupata mtoto!

Tunataka tukutie moyo kwa maneno ya biblia yafuatayo – ya kuwa – imetupasa kumwomba Mungu siku zote wala tusikate tama (Luka 18:1). Maana imeandikwa katika Zaburi 113:9 ya kuwa; “ Huweka nyumbani mwanamke aliye tasa, awe mama ya watoto mwenye furaha.” Tena imeandikwa katika Kutoka 23:26 ya kuwa; “Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako …..” Tena Mungu anauliza katika Isaya 66:9 ya kuwa; “Je, mimi nilete wana karibu na kuzaliwa, nisizalishe? asema Bwana; mimi nizalishaye, je, nilifunge tumbo? asema Mungu wako.”

Mistari hii ya biblia ikutie moyo, wala usikate tamaa. Muujiza wa mtoto unayemwomba kwa Bwana uko karibu – maana Mungu analiangalia neno lake apate kulitimiza (Yeremia 1:12).

Kwa njia ya radio Mungu
amewahudumia watu pia!

Watu wengi pia walijitokeza kushuhudia jinsi ambavyo Mungu aliwagusa na kuwapa haja ya mioyo yao walipokuwa wakisikiliza vipindi vya semina ya neno la Mungu tunavyorusha katika radio mbalimbali kila wiki.

Kwa mfano mama mmoja alishuhudia katika semina ya Arusha ya kuwa aliokoka na kujazwa Roho Mtakatifu na kuzungumza kwa lugha mpya aliposhiriki maombi yaliyoambatana na kipindi chetu cha neno la Mungu katika Radio Sauti ya Injili. Alieleza maelfu ya watu waliokuwa hapo ya kuwa ingawa yeye ni mhudhuriaji mzuri wa mara kwa mara wa semina zetu lakini alikuwa hajaokoka, wala alikuwa hakubaliani na mambo ya kuokoka, na ya kunena kwa lugha kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Kwa hiyo alipoona watoto wake wakiokoka katika semina tuliyoifanya Arusha mwezi wa pili mwaka huu – hakufurahi hata kidogo. Akawagombeza sana watoto wake kwa kuokoka. Lakini akasema, watoto wake hawakutishika na upinzani huo wa mama yao – na wakamjibu kwa ujasiri na kusema “Kwani, mama kuokoka ni dhambi? Kama wewe hutaki basi baki lakini sisi tumeamua kuokoka!” Yule mama alisema alipouona ujasiri waliokuwa nao ambao hajawahi kuuona wakiwa nao alinyamaza kimya – asiwasemeshe tena juu ya jambo hilo!

Akaendelea kuelezea ya kuwa baada ya siku chache kupita alipokuwa anasikiliza kipindi chetu cha radio – wakati wa maombi kule mwishoni mwa kipindi – aliamua kusimama na kufuatilizia sala tuliyokuwa tunaiongoza. Katika maombi hayo akajikuta ananena kwa lugha kwa karibu nusu saa nzima! Watoto wake wakamuuliza alipokwisha kutulia ya kuwa “ sasa ulikuwa unabisha nini?”

Tulipokuwa Mbeya wakati wa semina tuliona watu watatu kwa muda tofauti wakieleza walivyojazwa Roho Mtakatifu na kunena kwa lugha walipokuwa wanashiriki maombi tunayofanya mwisho wa kipindi cha neno tunachorusha kupitia Radio Free Africa kila Jumapili saa kumi na mbili na nusu hadi saa moja na nusu kila wiki.

Tukiwa Arusha kuna mchungaji mmoja aliyesimama na kushuhudia jinsi alivyopona maumivu ya jino alipokuwa akisikiliza kipindi chetu tunachorusha kupitia Radio Sauti ya Injili.

Tena katika semina hiyo hiyo ya Arusha, msichana mmoja alishuhudia alivyopona uvimbe uliokuwa upande wa kulia wa shingo yake. Alipona kupitia maombi tuliyoyafanya kupitia kipindi chetu tunachorusha kupitia Radio Sauti ya Injili.

Mwisho

Nafasi haitatosha kukuandikia shuhuda zote zilizotolewa wakati wa semina hizi – lakini tunaomba ushirikiane nasi katika kumshukuru Mungu kwa ajili ya mambo hayo yote aliyoyafanya. Na kwako wewe uliyetupa sadaka yako kwa Mungu tuitumie kulipia gharama za semina hizi – tunasema Mungu akubariki na akurudishie mara mia sawasawa na Neno lake.

          Mungu anapotembea nchini kwetu – ni wajibu wetu kutembea pamoja naye. Tuwe na utayari ili atutumie kama apendavyo ili kulitimiza kusudi lake jema kwa nchi yetu. Tunashukuru kwa kuwa umekubali kutembea pamoja nasi wakati huu. Usiache kutuombea mafanikio na ushindi mkubwa kwa ajili ya semina inayofuata ya Dar es Salaam tarehe 17-21 Disemba 2003 itakayofanyika katika ukumbi wa PTA katika uwanja wa Sabasaba. Timu nzima tunayoshirikiana nayo inakusalimu na kukutakia baraka zaidi za Bwana katika maisha yako ya kila siku.

Ni sisi katika utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.