Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


B
arua ya Mwezi Februari 2003 

 KUFUNGA HUKO KUNAKUBALIKA?

 Salamu katika Jina la Yesu Kristo.

Kuna Faida katika kufunga

Tunasoma katika Biblia kuwa watu wa Ninawi waliposikia maonyo ya Nabii Yona, ya kuwa Mungu amekusudia kuwaangamiza wasipotubu na kuacha dhambi, wakatangaza maombi ya kufunga.

            “Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; Wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo”. (Yona 3:5)

            “Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya Basi Mungu alighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda, asilitende”. (Yona 3:10)

            Watu wa Ninawi, walifanya maombi ya kufunga wakamlilia Mungu kwa nguvu, na Mungu akawasamehe.

            Yesu Kristo alipokuwa hapa duniani, kabla ya kuanza kazi yake rasmi, alifunga.

            “Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi. Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa” (Mathayo 4:12)

            Huko nyikani alikuwa anajaribiwa na Ibilisi – lakini alishinda. “Kisha Ibilisi akamwacha na Tazama, wakaja malaika wakamtumikia” (Mathayo 4:1)

            Pia, wanafunzi wa Yesu walikuwa na tabia ya kufanya maombi ya kufunga, baada ya Yesu kupaa. “Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana Ibada na kufunga Roho Mtakatifu akasema nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao” (Matendo 13:2,3).

            Hata siku hizi watu wengi wanafanya maombi ya kufunga. Wengine wanajibiwa na wengine hawajibiwi. Wengine ni Wakristo na wengine si wakristo. Mara nyingi mtu anapokuwa katika kufunga, huacha kula chakula kabisa kwa muda fulani au kuacha kula vyakula fulani fulani tu, na vingine anakula kama kawaida.

            Maombi ya namna hii, kuna wakati hufanya baadhi ya watu kudhoofu miili yao licha ya hayo, wakati mwingine hakuna baraka zozote zinazopatikana wala maombi hayajibiwi. Hata ukimuamuru pepo amtoke mtu hukataa, ingawa uliifanya maombi ya kufunga. Wakati mwingine unafunga, na maombi yako yanajibiwa.

Je kuna mtu yeyote katika Biblia ambaye aliomba kwa kufunga na kuona mambo hayabadiliki?

            Ndiyo! Mmojawapo ni Mfalme Daudi.

            Wakati wa mwaka mpya, huko Yerusalemu, Mfalme Daudi alianguka katika dhambi ya uzinzi, baada ya kumtamani mke wa askari wake Uria, Mhiti; Huyo mwanamke aliitwa Bath-Sheba, binti Eliamu.

            “Basi Daudi akapeleka wajumbe, wakamtwaa; naye akaingia kwake, naye akalala naye……kisha akarudi nyumbani kwake. Yule mwanamke akachukua mimba basi akapeleka  na kumwambia Daudi akasema ni mjamzito” (2 Samweli 11:4.5)

            “Hata ikawa asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu waraka, akaupeleka kwa mkono wa Uria. Akaandika katika Waraka huo, akasema, mwekeni Uria mbele ya watu penye vita vikali, kisha ondokeni, ili apigwe akafe” ( 2 Samweli 11:14,15)

            Uria Mhiti, akafa vitani, Daudi akamchukua mke wake na akamzalia mtoto.

          “Lakini jambo lile alilolitenda Daudi likamchukiza Bwana” (2 Samweli11:27)

            Bwana akamkemea Daudi kupitia kwa Nabii Nathani “Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa. Lakini kwa kuwa kwa tendo hili umewapa adui za Bwana nafasi kubwa ya kukufuru, mtoto atayezaliwa hakika yake atakufa” (2 Samweli 12:13,14)

            “Basi Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto Daudi akafunga akaingia akalala usiku kucha chini. Nao wazee wa nyumba yake wakaondoka wakasimama karibu naye, ili wamwinue katika nchi, lakini hakukubali wala hakula chakula pamoja nao. Ikawa siku ya saba yule mtoto akafa” (2 Samweli 12:16,17).

            Licha ya kwamba Daudi alifunga siku saba usiku na mchana, bila kula na kunywa chochote maombi yake hayakukubalika. Kumbuka alikuwa Mfalme mteule wa Israeli, Taifa la Mungu, aliyepakwa mafuta, na aliyesaidiwa sana na Mungu. Lakini wakati huu Mungu hakusikia maombi yake.

            Je kuna wakati katika maisha yako umewahi kuwa na hali kama ya Daudi?

            Ingawa umeokoka, umeomba kwa kufunga na kwa kulia siku nyingi lakini hujajibiwa? Tatizo ulilotaka litatuliwe na Mungu, bado unalo na limekuwa mwiba maishani mwako.

            Wakati mwengine umeomba kwa kufunga ili ubarikiwe kiroho – unaona hakuna kitu. Unaona ni kama unapiga ukuta. Na wengine wameomba kwa kufunga juu ya wokovu wa ndugu zao na watoto wao lakini wanaona hakuna mabadiliko.

            Umewahi kujiuliza ni kwa nini haya yatokee? Je umewahi kuwa na mawazo ya namna hii ya kumuuliza Mungu? Mbona tumefunga, lakini huoni? “Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii?” (Isaya 58:3)

            Kama umewahi kuwa na maswali ya namna hii, Bwana anakujibu hivi katika Isaya 58:3-5 “Fahamuni siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je kufunga namna hii ni saumu niliyochagua mimi? Je! ni siku ya mtu kujitaabisha Nafsi yake? Ni kuinama kichwa cha unyasi, na kutanda nguo za magunia na majibu chini yake? Je! utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana.”

            Hebu soma tena maswali haya “Je! kufunga namna hii ni saumu niliyochaugua mimi? ……. Je! utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana?”

            Maana yake nini maswali haya? Maana yake ni kwamba si kila maombi ya kufunga yanakubalika mbele ya uso wa Bwana. Na yasipokubalika mbele ya Mungu, hayawezi kujibiwa.

            Inawezekana kabisa kuwa, maombi yako uliyofanya kwa kufunga hayajajibiwa, kwa kuwa kufunga ulikofanya hakujakubalika mbele za Bwana. Una uhakika gani kuwa, Mungu anakufurahia kujinyima chakula kwako unapoomba juu ya jambo fulani? Je! kufunga namna hiyo ni Bwana amekuongoza, au umeona wenzio wakifanya hivyo na wewe ukafuata.

Kwa nini ufanye maombi ya kufunga?

            Maombi ya kufunga ni maombi ya wito. Hakuna mtu anayefanya maombi ya kufunga bure. Lazima kunakuwa na sababu.

            Kuna wito wa kutoka nje. Mtu anaambiwa kufunga kwa kusikia toka kwa mtu mwingine. Watu wa Ninawi walisikia wito toka nje nao wakafunga “ Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga…..” (Yona 3:5)

            Yesu Kristo alipofunga siku arobaini usiku na mchana, hakuamua kwa akili yake. Alisikia wito wa Roho Mtakatifu toka ndani yake, kuwa anahitaji kufunga.

            Biblia inasema hivi, “Kisha Yesu alipandishwa na Roho Nyikani ili ajaribiwe na ibilisi. Akafunga siku arobaini mchana na usiku” (Mathayo 4:12)

            Yesu alipandishwa na Roho wa Mungu ili apate kufanya maombi ya kufunga, yatakayomwandaa kwa makabiliano na Ibilisi. Yesu hakuambiwa na mtu yeyote. Huo ulikuwa wito wa kutoka ndani yake kwa uongozi wa Roho wa Mungu aliyekuwa ndani yake. Hata siku hizi wengi wanasikia wito wa namna hii, wanatii na kufunga.

            Kuna wito wa kutoka ndani na nje, ambao unawafikia watu na wanafanya maombi ya kufunga “Ndipo nikaamuru kufunga, hapo penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za Mungu na kutafuta kwake njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote. Maana naliona haya kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapanda farasi, ili kutusaidia juu ya adui njiani, kwa maana tulikuwa tumesema juu na mfalme, tukinena, Mkono wa Mungu u juu ya watu wote wamtafutao, kuwatendea mema; bali uwezo wake na ghadhabu yake ni kinyume cha wote wamwachao. Basi tukafunga, tukamsihi Mungu wetu kwa ajili ya hayo; naye akatutakabali” (Ezra 8:21 – 23)

            Anayesema maneno hayo ni Ezra, kuhani, “mwandishi wa torati ya Mungu wa Mbinguni” (Ezra 7:21)

            Ezra alikuwa na Roho wa Mungu, kama vile watumishi wote wa Mungu, walivyokuwa naye wakati wa agano la kale.

            Ezra alikuwa kiongozi, aliyekabiliwa na safari ambayo alikuwa anahitajika kuwaongoza watu waifanye. Akasema, “Ndipo nikaamuru kufunga ……maana naliona……..”

            Kwa namna nyingine tunaweza kusema, “aliona kwanza ndipo akaamuru kufunga.”

            Alisikia kwanza wito wa ndani, ndipo wito wa nje ukajitokeza, ili yeye na wenzie wajikabidhi mbele za Bwana kwa maombi ya kufunga.

            Neno “nikaamuru” linasimama kwa ajili ya wito wa nje. Neno “naliona” linasimama kwa ajili ya wito wa ndani.

            Kitu kikubwa kinachojitokeza hapa ni kwamba maombi ya kufunga yanaongozwa na Roho Mtakatifu. Ni maombi yanayosimamiwa na Mungu mwenyewe kwa njia ya Roho wake. Hebu soma na kutafakari maneno yafuatayo:

            “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako” (Mithali 3:5,6)

“Kwa kuwa watu wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu….Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Warumi 8:14,16).

            “Yesu alipandishwa na Roho nyikani……akafunga siku arobaini mchana na usiku” (Mathayo 4:1,2)

            Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji, walimwendea Yesu na kutaka kujua kwa nini wanafunzi wake hawafungi wakati wao na Mafarisayo walikuwa wakifunga.

            “Yesu akawaambia, walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda Bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa Bwana arusi; ndipo watakapofunga”. (Mathayo 9:15)

            Kwa nini Yesu alisema hivyo?

            Yesu alikuwa ana uhakika kuwa hawana haja ya kuacha kula na kunywa wakati yeye bado yupo kimwili.

            “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa Kweli atawaongoza awatie kwenye kweli yote kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo, atawapasha habari yake” (Yohana 16:13).

            Yesu Kristo anatuambia kuwa kazi kubwa ya Roho Mtakatifu ni kututia katika kweli yote.

Kweli hiyo ni ipi?

            Neno la Mungu ndiyo kweli tunayotakiwa kuifahamu. “Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndiyo kweli.” (Yohana 17:17). Hii ni sehemu ya sala ambayo Yesu aliwaombea wanafunzi wake popote walipo ulimwenguni.

            Baada ya Yesu Kristo kupaa na Roho Mtakatifu, kuwashukia ndipo, wanafunzi wake walipoanza kufunga. Kwa mfano tunasoma hivi:

            “Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana Ibada ya kufunga, Roho Mtakatifu akasema, nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao” (Matendo ya Mitume 13:2,3)

Tunauliza tena……Kwa nini mtu inakubidi ufunge?

            Kuna sababu nyingi, lakini zinaweza kujumulishwa katika maneno yafuatayo:.

            Tunafanya maombi ya kufunga, ili tupate “kujinyenyekeza mbele za Mungu na kutafuta kwake njia iliyonyooka kwa ajili yetu sisi wenyewe na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote” (Ezra 8:21)

            Duniani tumo safarini lengo letu ni kufika mbinguni kwa Mungu kwenye makao ya milele. Kila wakati tunakuwa na haja ya kuyafahamu mapenzi ya Mungu juu ya maisha yetu ili tupite katika njia iliyonyooka. Mapenzi ya Mungu tunayapata katika Biblia, ambayo ni neno la Mungu kwa wanadamu.

            Yesu Kristo alisema, “Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu, ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwajua njia. Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia na kweli, na uzima; mtu haji kwa baba, ila kwa njia ya mimi” (Yohana 14:3-6)

            Yesu ni “njia iliyonyooka” tunayoitafuta tunapofanya maombi ya kufunga.

            Sasa unaweza kuelewa kwa nini Yesu alisema wanafunzi wake hawawezi kufunga wakati yeye yupo kimwili. Ni kwa sababu yeye alikuwa Njia yao iliyonyooka. Hawakuhitaji kufunga ili wamuone au kumuuliza wafanye nini.Yeye Kristo alikuwa pamoja nao, akiwaongoza, akiwafundisha, akiwaonya na kuwaagiza.

            Hawakuwa na haja ya kuacha kula na kunywa wakati Yesu yupo pamoja nao.

            Katika torati ya Musa kufunga ilikuwa ni Lazima – ni sheria. Lakini sisi tulio ndani ya Kristo hatufungwi na Sheria (Warumi 8:1-4). Wanafunzi wa Yesu hawakufungwa na Sheria hasa Yesu alipokuwa pamoja nao. Wanafunzi wa Yohana na Mafarisayo walikuwa bado chini ya sheria ndiyo maana iliwabidi wafunge.

            Baada ya Yesu Kristo kupaa, Roho Mtakatifu alichukua nafasi ya Kristo ndani ya wanafunzi. Roho Mtakatifu anaongoza (Wagalatia 5:16,18, 25), anafundisha (Yohana 16:13) anaonya (Ufunuo 2:7,11,17,29), na anaagiza (Ufunuo 22:17)

            Roho Mtakatifu peke yake ndiye chanzo cha wito wa  kufunga katika Kanisa la Kristo na siyo sheria. Lakini utaona watu wengi wanafanya maombi ya kufunga kwa sababu wamesikia au wameona au wameambiwa na watu juu ya kufunga. Na kwa sababu hiyo wanakuta wanajitesa muda mrefu bila kula wala kunywa na maombi yasijibiwe. Wengi wanafanya maombi ya kufunga kimazoea tu bila ya kuongozwa na Roho Mtakatifu. Matokeo yake ni kutokujibiwa na Mungu.

            Biblia inakataza watu kutegemea akili zao wenyewe na kuwategemea binadamu wengine katika safari hii ya Mbinguni (Mithali 3:5,6).

            Mtegemee Roho Mtakatifu peke yake ambaye atakufunulia Yesu alivyo katika maandiko. Na Yesu ni Njia unayoitafuta ili kutatua tatizo ulilo nalo.

Lengo Letu

            Lengo letu ni kuona ya kuwa kila mtu anayemjua Yesu kama Bwana na Mwokozi wake – anaongonzwa na Roho Mtakatifu katika kila jambo kufuatana na Warumi 8:14. Hii ni pamoja na maombi yanayohusisha kufunga pia. Maombi ya kufunga yanafaida kubwa ikiwa yatafanyika kwa kusudi la Mungu na kwa uongozi wa Roho Mtakatifu.

            Kwa hiyo jitahidi kusoma biblia kwa makini ili upate kujifunza zaidi juu ya jambo hili. Tunaamini Roho Mtakatifu atakuonyesha mambo mengi – sisi tulichotaka katika waraka huu ni kuchokoza fikra zako ili kulitazama jambo hili la maombi ya kufunga kwa jicho la neno la Mungu na si kwa jicho la mazoea. Kwa mfano:

  • Je! Unajua ya kwamba kuna tofauti ya kufunga ya Agano la Kale na kufunga ya Agano Jipya? Maana Agano la Kale lilifungwa ‘mwilini’ na Agano Jipya lilifungwa ‘rohoni’. Katika Agano la Kale walitahiriwa mwilini na katika Agano Jipya wanatahiriwa rohoni. Kwa hiyo na kufunga kwa Agano la Kale kulianzia ‘mwilini’ na kufunga kwa Agano Jipya kunaanzia rohoni.
  • Je! Unajua ya kuwa kufunga hakumbadilishi Mungu wala hakumbadilishi shetani? Mungu ni Yeye yule kabla ya wewe kuanza kufunga, wakati unafunga, na baada ya kufunga – Mungu ni Mungu – habadiliki wala kufunga kwetu hakuubadilishi uungu wake. Na juu ya shetani ni hivi: kabla hujaanza kufunga ‘ameshindwa,’ wakati unafunga ‘ameshindwa,’ na baada ya kufunga ‘ameshindwa’. Shetani ameshindwa juu ya maisha yako  na wewe ni mshindi dhidi yake si kwa sababu ya kufunga bali ni kwa sababu ya kazi ambayo Yesu aliifanya msalabani na kuimaliza. Kufunga kunakusaidia wewe ili kuuweka mwili wako na nafsi yako na roho yako katika hali ambayo mapenzi ya Mungu yanatimizwa katika maisha yako kwa urahisi zaidi – hasa katika kuimarisha maombi yako. Soma mistari ifuatayo: Zaburi 35:13; Mathayo 6:16,17; Mathayo 17:21 na Danieli 10:1-3.

Tuzidi kuombeana

ni sisi katika utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.