|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
ANACHOFANYA MUNGU AKITUMIA SEMINA ZA
NENO LA Salamu
katika Jina la Yesu,
Mwaka 1985 Mungu alisema na sisi mambo mengi yaliyokuwa yanahusu huduma
aliyokuwa ametupa na kutupangia. Kati ya mambo hayo ilikuwa ni juu ya
huduma hiyo kwamba ataitumia “kuiponya nchi yetu”. Wakati huo
hatukuelewa maana yake nini maneno hayo, na ni kwa jinsi gani
yatatimizwa. Na isitoshe tulikuwa hata bado hatujaanza semina hizi
tunazofanya sehemu mbalimbali katika miaka hii ya sasa. Jambo
tulilolifanya ni kuendelea kuomba.
Lakini siku moja tulipokuwa tukisoma biblia tulikutana na mstari huu: “Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya
na shida zao. Hulituma Neno lake, huwaponya; huwatoa katika maangamizo
yao” (Zaburi 107:19,20)
Kwa hiyo tulijua ya kuwa Mungu ataitumia huduma aliyotupa kuiponya nchi
yetu kwa kutumia Neno alilotupa na analotupa kulifundisha.
Mwaka 2001 mwezi wa nane – ukurasa mpya ulifunguka katika huduma hii
ya kufundisha neno la Mungu – wakati tulipofunguliwa mlango wa kuanza
kutangaza mafundisho ya neno kwa njia ya Radio Sauti ya Injili – Moshi.
Wakati huo matangazo yake yalikuwa yanaifikia mikoa ya Kilimanjaro na
Arusha tu – na kwa sasa mkoa wa Tanga umeongezeka. Tunafundisha kila
Jumamosi na Jumapili saa 3 had saa 4 usiku.
Mwezi wa Tisa mwaka 2001, kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga lilitupa
nafasi ya kurusha vipindi vyetu vya neno la Mungu kupitia radio yao ya
‘Radio Faraja”. Hadi sasa tunaendelea kurusha vipindi hivi mara
mbili kila wiki siku ya Jumamosi na Jumapili kwa saa moja – moja (saa
3 hadi saa 4 usiku).
Mwaka 2002 mwezi wa sita tukaanza kurusha vipindi vya semina ya Neno la
Mungu kwa kutumia ‘Radio Free Africa’ (RFA). Kwa hiyo tangu wakati
huo kila jumapili kwa saa moja (saa 12.30 – 1.30 jioni) tumekuwa
hewani katika nchi sita ambazo RFA inasikika kwa kutumia mitambo yake ya
(MW/AM) masafa ya kati – mitabendi 1377.
Mwezi Januari 2003 tumeanza kurusha vipindi vya semina ya Neno la Mungu
kupitia ‘Radio WAPO’ ya mjini Dar es Salaam, kila wiki siku ya
Jumatano saa 3 hadi saa 4 usiku.
Hakika huu ni ukurasa mpya ambao hatua kwa hatua unatuonyesha mwanzo wa
udhihirisho wa maneno ambayo Mungu alisema nasi mwaka 1985 – juu ya
kuiponya nchi yetu kwa kutumia neno analotupa kulifundisha. Maana kwa
njia hii tunawafikia maelfu maelfu ya watu na neno la Mungu kila wiki. -
Uponyaji wa Miili -
Tulipokuwa Moshi mjini kwa semina ya siku tisa mwezi Januari 2002, mtu
mmoja alisimama kushuhudia alivyopona baada ya kupokea maombi kupitia
vipindi vyetu vya Radio Sauti ya Injili (RSI). Alisema mbele ya umati wa
maelfu ya watu waliokuwapo wakati huo ya kuwa yeye ni mlinzi wa usiku,
na wikiendi moja alipokuwa akisikiliza kipindi chetu usiku wakati wa
maombi aliweka mkono juu ya kichwa chake maana alikuwa anaumwa homa.
Akasema baada ya maombi homa ilimwacha na akapona kabisa tangu saa ile.
Na akaanza kuwaeleza walinzi wengine usiku huo huo mambo ambayo Yesu
ameyatenda na kumponya kwa njia ya maombi katika RSI.
Mwezi wa saba 2002, tulikuwa Iringa mjini kwenye semina ya siku sita.
Wakati wa shuhuda, mama mmoja alisimama na kusema ya kuwa alipona wakati
wa maombi ya wagonjwa kupitia kipindi chetu cha RFA kila Jumapili jioni.
Alisema kwanza hakuamini ya kuwa anaweza kupona, lakini wakati wa maombi
aliweka mkono wake kwenye kiuno upande wa kulia mahali ambapo amekuwa na
maumivu kwa muda mrefu sana. Alishangaa sana na kumshukuru Mungu baada
ya kuona amepona na maumivu kutoweka mara tu baada ya maombi hayo ya
radioni tunayoyafanya katika kipindi hicho kila mwisho wa mafundisho.
Mwezi Novemba 2002 tulipokuwa na semina ya siku nane Arusha Mjini
tulipokea shuhuda zingine zaidi. Kwa mfano, mama mmoja aliyekuwa ametoka
Moshi Mjini na kuja Arusha kwa ajili ya semina, alishuhudia mbele ya
umati wa watu zaidi ya elfu kumi waliokuwapo hapo. Huyu mama alisema
alikuwa ameugua ugonjwa wa saratani (cancer) ya ulimi kiasi cha
kushindwa kula vizuri na kuongea vizuri. Baada ya kulazwa hospitali
mbalimbali bila mafanikio alirudishwa nyumbani kwao akiwa katika hali
mbaya sana. Akasema siku moja alikuwa anasikiliza moja ya kipindi chetu
cha radio kilichorushwa mwezi wa saba 2002 na kituo cha Radio Sauti ya
Injili (Moshi). Wakati wa maombi, yaliyoambatana na somo lile na yeye
alipokea uponyaji! Nyama iliyokuwa imeota katika ulimi ilikatika na
kudondoka. Kuanzia hapo maumivu yalinyamaza na akapata nguvu. Alipokuwa
anakuja Arusha kushuhudia, alikuwa bado anasumbuliwa na masikio kwani
saratani hiyo ilimfanya asisikie pia vizuri. Lakini katika maombi ya
wagonjwa katika semina hiyo ya Arusha – alipona masikio na akaondoka
anasikia vizuri. Jina la Yesu liponyalo libarikiwe sana!
Pia katika semina hiyo ya Arusha ya mwezi Novemba 2002 kijana mmoja
alishuhudia jinsi Mungu alivyomponya ugonjwa wa ukimwi kwa kupitia
maombi tuliyoomba katika kipindi kimojawapo cha mafundisho yetu kwa njia
ya radio.
Hebu sasa soma baadhi ya shuhuda zifuatazo tulizozipata kwa njia ya
barua tunazopata kila siku. Lengo letu ni kwamba umshukuru Mungu pamoja
nasi, na pia utiwe moyo katika kuendelea kutusaidia katika kuifikisha
huduma ya neno la Mungu kwa watu kwa kutumia radio mbalimbali hapa
nchini. Kutoka Geita
(Mwanza) Ndugu
…. Bwana Asifiwe ……. Awali ya yote ningependa kukupongeza kwanza wewe kwa kazi
nzuri sana unayoifanya ya kuhubiri watu kwa njia ya redio. Pili,
ningependa kuwapongeza wafanyakazi wa Radio Free Africa kwa kupeperusha
matangazo ya mahubiri redioni.
Mimi binafsi nimependezwa sana na mahubiri yako niliyoyasikia mara tatu
mfululizo tarehe 6/10, 13/10 na 20/10 na bado ukasema tutakuwa tena
pamoja endapo Mungu atatujalia Jumapili ijayo. Nami bado nasubiri ili
niweze kupata zaidi na zaidi kuhusu neno la Mungu.
Mahubiri yako, ndugu, yamenifurahisha sana na kuniingia sana; lakini
nimeona nimepungukiwa kiasi kwani sijui ulianza lini na utaendelea hadi
lini. Nimeona ni vyema endapo kuna utaratibu wa kupata kanda za mahubiri
hayo, basi itakuwa vyema zaidi kama nitazipata ili niweze kufaidika
vizuri zaidi na kwa karibu zaidi ….. Kutoka Singida ….Bwana Yesu Asifiwe sana.
Ubarikiwe na huduma unayoitoa ya Neno kwa njia ya redio. Mimi nina shida
kubwa sana ya kiroho ambayo inahitaji maombi ya hali ya juu sana. Maana
ni heri uugue mwili na ufe kulikoni kuugua dhambi; pia ni bora ufarakane
na wafalme wa dunia hii kulikoni kufarakana na ufalme wa Mungu ….
Shida yangu ni hii …….. Niliwahi kumwomba Mungu anipe kazi kwa
kufunga na kuomba, na baada ya miaka mitatu nikapata kazi. Baada ya
kuanza hiyo kazi mwaka 1998 nilifunga na kuomba kwa siku 7 (saba) ili
Bwana anisaidie nisife kiroho na anieleze kusudi la kuniweka hapo kazini
lakini hakunijibu. Nikaomba na kufunga tena kwa siku 21, lakini sikupata
jibu. Nikaomba tena na kufunga kwa siku 40, lakini pia sikupata jibu.
Kwa kweli nilikata tamaa nikajua Bwana hayuko nami tena, lakini nikiwa
katika kuomba nilisikia unahubiri kwa njia ya Radio Free Africa –
nilitubu upya. Lakini bado sina amani, nahitaji maombi – sina tumaini,
biblia nashindwa kusoma, natamani niwe kama mwanzo ….. Kutoka Mtwara Kwako
Mtumishi wa Mungu,
Nia ya barua hii ni kutaka kukufahamisha ya kwamba nami nimeokoka
nampenda Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yangu. Nilifurahi
sana baada ya kusikia injili inahubiriwa kwa njia ya Radio Free Africa
na Mungu akikutumia kama chombo. Hii inaonyesha jinsi injili
inavyohubiriwa kwa njia ya pekee na hata watu wa vijijini wanaweza sasa
kusikia injili ya Yesu Kristo kwa urahisi – kwa hilo Mungu akubariki
sana.
Baada ya kusikia mahubiri yako kwa njia ya redio nilikuwa nipo wilaya
moja nikifanya kazi za kutafuta maisha. Baada ya muda walikuja watu
wawili kunitembelea na ikabidi na wao wasikilize hiyo injili iliyo
kamili ya Yesu Kristo. Watu hawa walikuwa wapagani wasioamini habari za
Yesu Kristo. Baada ya kusikia, walipenda wapate mafundisho kwa njia ya
posta kutoka kwako ikiwa ni pamoja na kanda zenye mafundisho na masomo
ya vitabu.
Kwa jambo hili namshukuru Mungu kwa sababu anataka kuwaokoa watu kwa
njia kama hii. Tunatumaini ya kwamba watu watazidi kufunguka kwa kupitia
mtazamo huu …….. Kutoka
Nyanza, Kenya ….. Kusudi la waraka huu ni kuwa ningependa kukujulisha
kwamba huduma ya kufundisha “Neno” la Mungu kupitia ‘Radio Free
Africa’ inatufikia vizuri hapa mkoani ‘Nyanza – Kenya’,
isipokuwa wakati mwingine mawimbi hututatiza tusisikie vizuri. Kwa
sababu hiyo ninamshukuru Mungu kwa kukupa maono hayo ya kurekodi kanda
za mahubiri, ili yaweze kuwafikia wale ambao hawaipati ‘Radio Free
Africa’ kwa wepesi. Shukrani kwa maono hayo.
Mimi nimejaribu kuwafahamisha wachungaji na watumishi wa Mungu kuhusu
mafundisho hayo ya kila Jumapili jioni tunayopata kupitia RFA, na watu
wote hao wanashuhuda mbalimbali ya miujiza ambayo Bwana Yesu huitenda
wakati unapoomba maombi ya uponyaji na sala ya toba. Mungu aibariki
huduma hii ienee “kotekote” Kutoka Geita, Mwanza
Ninayofuraha kubwa sana kuweza kuandika kipande hiki cha barua, ili
niweze kutoa shukrani na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mahubiri yako kwa
njia ya ‘Radio Free Africa’ inayosikika kila Jumapili jioni. Ukweli
ninafarijika sana kwa mahubiri hayo.
Mungu azidi kukulinda na kukubariki ili uzidi kutulisha neno lake japo
hata kwa njia hii ya redio. Binafsi nimebarikiwa sana na kipindi hiki.
Pia, nawashukuru wamiliki wa redio hii ya RFA kwa kukupatia kipindi
hicho. Niliguswa sana na mahubiri ya tarehe 25 Agosti 2002 ambayo
yalikuwa yanahusu ‘Kuguswa mara ya Pili na Bwana Yesu …..’ Kutoka Masasi
Nakusalimu katika Jina la Bwana Yesu,
Tunashukuru kuwa tunapata Neno la Mungu kupitia ‘Radio Free Africa’
kila Jumapili kuanzia saa 12:30 jioni.
Namshukuru Mungu ya kuwa nilikuwa naumwa macho ‘vikope’ – wakati
wa kipindi cha maombezi unayoomba redioni mwisho wa kipindi niliweka
vidole vyangu kwenye macho na nimepokea uponyaji!
Tunaomba njia ya kuweza kupata kanda zako, kwa kweli tunahitaji sana!
Maana masomo hayo ni ya manufaa sana kwetu. Mwisho
Hizi ni baadhi tu ya shuhuda nyingi ambazo tumekuwa tukizipata kwa njia
ya barua. Tumekushirikisha ili (i)
Uzidi kumshukuru Mungu pamoja nasi kwa ajili ya mambo anayofanya kwa
kutumia vipindi hivi vya mafundisho katika redio; (ii)
Uzidi kuomba na kutuombea mafanikio zaidi katika huduma hii; (iii)
Uzidi kutiwa moyo zaidi wa kutoa mchango wako wa kifedha unaotusaidia
sana kulipia gharama za vipindi hivi redioni. Kwa sasa tunalipa wastani
wa Shs. 600,000 kila wiki au shs. Millioni 30 kwa mwaka. Tuzidi kuombeana ili tuzidi kudumu katika Bwana, na tuzidi
kuifanya kazi yake kwa ufanisi zaidi chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. ni sisi katika utumishi wa Kristo, Christopher na Diana Mwakasege |
|