|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
TUMETUMWA KAMA KRISTO ALIVYOTUMWA Mpendwa katika Kristo, Salamu katika Jina la Yesu, Mwezi huu tunasukumwa ndani yetu kukusalimu kwa kukumbusha tu ya kuwa “Tumetumwa kama Kristo Alivyotumwa”. Ikiwa umeokoka, basi, umetumwa kama Kristo alivyotumwa! Tunaona wazi kwa msaada wa Maandiko Matakatifu, kuwa watu wote waliookoka, tuliozaliwa mara ya pili, ni wenyeji wa mbinguni (Waefeso 2:19). Sisi si wa ulimwengu huu kama Kristo asivyo wa ulimwengu huu (Yohana 17:14). Ikiwa sisi ni wenyeji wa mbinguni, kwa nini basi bado tumo duniani? Ikiwa sisi si wa ulimwengu kama Kristo asivyo wa ulimwengu huu, kwa nini wakati huu tusiwe tumekufa na kuondoka hapa duniani? Kuna sababu gani hasa ambayo inamfanya Mungu kutuweka hapa duniani katika ufalme wa shetani (2Wakorintho 4:4), ulio jaa chuki, magonjwa na mahangaiko? Kwa nini Mungu anatulinda na jeshi lake la Malaika (Zaburi 91:11-12) na kutuzunguka kwa utukufu wake (Isaya 58:8) hapa duniani? Watu waliookoka wametapakaa ulimwengu mzima karibu sehemu nyingi. Utawakuta kwenye madhehebu mbalimbali ya kikristo, serikalini, katika mashirika ya umma, mashirika ya watu binafsi, mashirika ya kimataifa. Wapo waliookoka wanafunzi, kuanzia shule ya msingi mpaka chuo kikuu, Wapo walimu waliokoka, wapo wakulima na wafanya biashara waliookoka. Na wapo waliookoka wasio na kazi. Na sehemu nyingine ambazo hatujazitaja. Wote hawa ni wenyeji wa mbinguni, lakini hivi sasa wapo hapa duniani – kwa nini iwe hivi? Unadhani Mungu ni baba anayependa sisi tulio watoto wake katika Kristo tubaki katika dunia hii ya mateso bila sababu muhimu katika moyo wake? Baba yetu aliye mbinguni ambaye pia ni Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, hapendi tuanguke katika dhambi, hapendi jinsi shetani anavyotutesa, hapendi tuugue, wala tuwe maskini. Lakini, swali linabaki palepale, kuwa, ikiwa hapendi hayo yatokee kwetu, kwa nini kutuacha hapa duniani, ambapo mambo hayo yanaweza kutupata? Ni lazima tuijue sababu hiyo. Tusipofahamu ni kwa nini wakati huu tumo duniani, wakati tungetakiwa tuwe mbinguni, tutashindwa kufanya yale ambayo Mungu amepanga na kukusudia tuyafanye. Yesu Kristo, Bwana wetu anatupa jibu: “Kama vile (Baba) ulivyonituma mimi ulimwenguni nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni” (Yohana 17:18) “Kama Baba alivyonituma mimi nami nawapeleka ninyi” (Yohana 20:21) Kwa mistari hii miwili tunaona kuwa tupo hapa duniani kwa sababu tumetumwa na Kristo. Sisi “Tu wajumbe (mabalozi) kwa ajili ya Kristo” (2Wakorintho 5:20). Maana yake ni kwamba sisi ni wawakilishi wa Kristo hapa duniani tukifanya kazi (kwa uweza wake) ambayo yeye mwenyewe angependa kuifanya angekuwa hapa duniani katika mwili. Ndiyo maana amesema “Kama vile” alivyotumwa na Baba toka mbinguni kuja duniani, na yeye “vivyo hivyo” ametutuma ulimwenguni toka mbinguni ambako ndiko kwetu kiroho. “Kama vile” na “vivyo hivyo” ni maneno muhimu sana yatakayotusaidia kuifafanua kazi hii ya kuwa mjumbe wa Kristo. “Kama vile” maana yake ni kwa jinsi na namna, na katika hali zote alivyotumwa Kristo duniani, “ vivyo hivyo” maana yake na sisi tumetumwa kwa jinsi na namna na katika hali zote kama Kristo alivyotumwa. Sasa ni budi tufahamu kwa undani kwa nini Yesu Kristo alitumwa, alitumwa kwa nani, na alikuwa na ujumbe gani, na katika hali gani. Bila kuyajibu maswali haya, kazi yetu ya ubalozi itakuwa ngumu sana, na mwisho wake itakosa maana. BARAKA NA LAANA Baba Mungu alipowaumba mwanaume na mwanamke, biblia inasema, “ akawabarikia” (Mwanzo 1:28). Mungu alikuwa anaweka nini ndani ya mwanadamu alipombariki? Kubariki maana yake ni kutabaruku, kuneemesha, kufanya heri, kusitawisha, kufurahisha. Biblia inaposema, “Mungu akawabarikia” ina maana kuwa Mungu akawaneemesha; Mungu akawafanya wawe heri; Mungu akawastawisha; Mungu akawafurahisha. Hii baraka ndiyo iliyokuwa nguvu ya mafanikio katika maisha ya mwanadamu. Mungu alikusudia kuwa kwa kuwabarikia angemweka mwanadamu duniani kuwa chanzo cha mafanikio kwa mazingira yaliyokuwa yanamzunguka. Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake, kwa sura yake aliwaumba mwanaume na mwanamke. Sura ya Mungu ni upendo kwa kuwa Mungu ni upendo. Mungu alimuumba mtu bila dhambi, wala bila ugonjwa wowote. Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake; Mungu hafi kwa hiyo alimuumba mwanadamu kwa mfano wake asife – adumu milele kama yeye adumuvyo. Lakini fikra za mwanadamu zilipodanganywa na ibilisi, alipoteza mfano wa Mungu ndani yake na sura ya Mungu haikuonekana ndani yake. Baraka zote zilipotea na badala yake, mtu na vitu vyote vilivyomzunguka viliingia katika laana. Hii ni kwa sababu walikataa kumtii Mungu aliye chanzo cha baraka, badala yake walimtii shetani aliye chanzo cha laana (Mwanzo 3:11-19). Nguvu ya mafanikio ilipotea na badala yake ikaingia nguvu ya kutokufanikiwa, ikaingia nguvu ya kushindwa. Upendo ulipotea, na chuki ikaingia. Haki ilipotea, dhambi ikapata nafasi. Uzima ulipotea na badala yake mauti na magonjwa vikaingia duniani. Mauti maana yake ni kutengwa na uso wa Mungu. Adamu alipoambiwa utakufa, haikuwa kifo cha kimwili bali ni kifo cha kiroho. Kifo cha kimwili ni matokeo ya mtu kufa kiroho kwanza katika bustani ya Edeni. Mungu alikuwa anamwambia utakufa akiwa anamaanisha kuwa Adamu atatengwa na yeye aliye chanzo cha uzima, upendo, baraka na kufanikiwa. Hali hii ndiyo iliyoleta kifo cha mwili. SURA YA MUNGU NDANI YA KRISTO Mungu aliamua kuirudisha sura yake ndani ya mwanadamu kwa njia ya Yesu Kristo, kwa kuwa yeye ni sura ya Mungu. “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao Mungu wa dunia hii (shetani) amepofusha fikra zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye SURA YAKE MUNGU”. (2 Wakorintho 4:3,4) Tangu nabii Malaki alipopata ufunuo wa neno la Bwana kwa Israeli hadi wakati wa kutokea kwa Yesu Kristo duniani, kulipita karibu miaka mia nne. Kwa muda wa miaka mia nne, Mwanadamu hakuisikia sauti ya Mungu. Ndipo shetani alipopata nafasi ya kulipaka matope jina la Mungu wetu. Kwa kuwa aliweka katika fikra za watu kuwa Mungu ndiye chanzo cha mabaya yote yaliyopo duniani. Aliwafanya watu wamuone Mungu kama hakimu asiye na huruma. Aliwafanya wamuone Mungu kuwa ndiye aliyeleta magonjwa ili kuwaadhibu. Na hii ipo katika fikra za watu hata leo. Utawasikia wakiyagawa magonjwa kuwa mengine ni ya Mungu mengine ni ya watu. Lakini elewa neno hili: Hakuna ugonjwa wa Mungu wala ugonjwa wa mtu, bali magonjwa yote ni ya shetani. Kwa hiyo kama unaumwa ujue huyo ni shetani aliyejificha katika ugonjwa. Shetani aliwadanganya watu wajue kuwa yeye ndiye Mungu, na kwamba hakuna mwingine zaidi yake. Na watu waliamini na wakaanza kumwabudu kwa njia nyingi. Hata leo wapo watu wa namna hii – wanaomwabudu shetani na kazi zake. Kwa kuwa shetani hapendi mwanadamu afanikiwe, tangu alipopata nafasi ya kumtawala wakati wa Adamu mpaka hivi leo, anavuruga mipango ya mtu isifanikiwe. Hufanikiwi katika kazi yako, ndoa yako, biashara yako na maisha yako, kwa kuwa kwa sehemu kubwa ni shetani ndiye aliyekufungia njia na kuharibu mafanikio ya nafsi yako. Ndiye anayeleta chuki na utengano katika ndoa. Ndiye anayekufanya ushindwe kufuata taratibu zilizowekwa za kazi. Ndiye anayekufanya upate hasara katika biashara yako. Yesu Kristo anamsema shetani kuwa kazi yake ni kuiba, kuchinja na kuharibu (Yohana 10:10). Na jinsi shetani asivyopenda ajulikane alivyo, amediriki kuwadanganya watu kuwa hakuna kitu kinaitwa shetani. Na ametumia vitu vingi kuingiza wazo hilo katika watu, kuanzia elimu mpaka mila na desturi za watu. Mtu pamoja na vitu vyote ulimwenguni, walikuwa wamefarakana na Mungu kabisa. Na dunia hii ikawa chini ya shetani na vitu vyote vilivyomo pamoja na mtu-shetani alivitumia jinsi alivyopenda mwenyewe. Mtu akiwa bado katika hali hiyo, Baba Mungu akamtoa Mwana wake wa pekee Yesu Kristo, aje hapa duniani toka mbinguni alikokuwa ili kufanya mambo matatu makubwa. YESU BALOZI WA KWANZA DUNIANI Yesu Kristo alikuwa ndiye raia (mwenyeji) wa kwanza wa ufalme wa Mungu aliyekuja duniani ili kufanya kazi ya “ubalozi”, akiwa mjumbe aliyetumwa na Mungu kwa kusudi maalum. Na alikuja na majukumu matatu makubwa, kwanza ilikuwa kumfunua Mungu kwa wanadamu au kuileta tena duniani sura ya Mungu kwa kuyafanya mapenzi yake mbele za watu. Ndiyo maana aliomba hivi; “Mimi (Yesu Kristo) nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye….. Jina lako nimewadhihirishia (nimewadhihirishia jinsi ulivyo) watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika. Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako. Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao, nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma” (Yohana 17:4,6-8). Na jukumu la pili lilikuwa ni kuziharibu kazi za ibilisi ndani ya mtu na katika mazingira yake. Imeandikwa hivi, “Atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. (Yohana 3:8) Jukumu la tatu ni kuwapa wanadamu wale wanaomwamini uzima wa Milele – Yohana 3:16. Kazi za Ibilisi zimegawanyika katika sehemu kuu nne, dhambi, magonjwa, mauti na umaskini. Na Yesu Kristo alipokuwa akipaa kurudi Mbinguni, alikuwa amemaliza kazi hizi zote kwa mafanikio makubwa. Majukumu yote haya aliyafanya kwa wakati mmoja. Alilidhihirisha Jina la Baba yetu kwa kuzivunja kazi na hila za Ibilisi na kuwapa watu uzima wa Milele. Yesu Kristo alikuwa balozi wa kwanza wa Mungu, kutumwa duniani, kuuwakilisha ufalme wa Mbinguni. Lakini kabla ya kuanza kazi yake rasmi ya ubalozi, ilibidi kwanza lazima apewe vitambulisho ambavyo vina mhuri na sahihi ya Baba aliye mfalme wa ufalme wa mbinguni. ILI ulimwengu ujue kuwa Yesu Kristo yupo duniani kuuwakilisha ufalme huo. Na sasa tuone alivyopokea vitambulisho hivyo. “Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunikia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye” (Mathayo 3:16-17) Ingawa wakati huo Yesu Kristo alikuwa amekwisha kaa duniani miaka thelathini, watu walimuona kama mtu mwenzao wa kawaida. Hakuwa na tofauti yo yote na vijana wengine wa kiyahudi. Walikuwa hawamtambui kuwa balozi wa Mungu, kwa kuwa alikuwa hajapewa vitambulisho na kiongozi wa ufalme alikotoka – ufalme wa mbinguni. Na alipokuwa anakua aliwaona watu wengi wenye shida, vilema, vipofu, viziwi, vichaa lakini aliwaacha kama walivyokuwa kwa sababu alikuwa hana kitambulisho cha kumwezesha kufanya kazi hiyo. Lakini siku ya kukabidhiwa vitambulisho ilipofika, jambo kubwa lilitokea duniani. Baada ya miaka mingi ya dunia kukaa katika ukiwa, MBINGU ZIKAFUNUKA, ROHO WA MUNGU AKASHUKA KAMA HUA, NA SAUTI YA MUNGU IKASIKIKA TENA DUNIANI. Hivi ndivyo vitambulisho vya ubalozi wa ufalme wa mbunguni. 1. Mbingu kufunuka; 2. Roho wa Mungu kushuka; 3. Sauti ya Mungu kusikika. Watu wengi wanafikiri kuwa kitambulisho cha mtu wa Mungu ni ubatizo wa maji peke yake. Lakini tukio hili la Kristo linatupa picha ya ndani zaidi. Siku hiyo Yesu Kristo alipobatizwa, watu wengi pia walibatizwa, Lakini ni Yesu Kristo peke yake ambaye mbingu zilifunuka, Roho wa Mungu akamshukia na sauti ya Mungu ikasikika kuthibitisha kuwa amepata kibali mbele za Mungu. JE UNAVYO HIVYO VITAMBULISHO? Hebu tuone neno la Mungu linatuambiaje. Mbingu ni kiti cha enzi cha Mungu (Isaya 66:1). Mbingu ni hazina ya Mungu. Imeandikwa hivi; “Atakufunulia Bwana hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.” (Kumbukumbu la Torati 28:12). Mbingu kufunuka, maana yake hazina ya Mungu imefunuliwa kwa ajili yake, ambayo ni kiti cha enzi – kiti cha kifalme kilicho na vitu vya thamani vya kifalme, siri za kifalme, na uweza wa kifalme…… Mbingu kukufunukia maana yake siri za kiti cha enzi cha Mungu ziko wazi mbele yako, na umekirimiwa (umepewa) mambo yote ya kiti hicho. Sasa, Roho wa Mungu anapokuja juu yako anakuletea mambo mazuri. Imeandikwa hivi: “Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu”. (1 Wakorintho 2:12) Kazi ya Roho wa Mungu ni kutuwezesha kujua ni mambo gani ambayo Mungu ametukirimia baada ya mbingu kutufunukia ambayo ni kiti chake cha enzi kufunuka. Sauti ya Mungu ni ujumbe wa Mungu uliyo ndani yako. Kwa hiyo Yesu Kristo alipopewa vitambulisho hivyo; mbingu kumfunikia, Roho wa Mungu kumshukia, na kusikika kwa sauti ya Mungu, kulimfanya Yesu Kristo asiwe myahudi wa kawaida tena! Kwa kutumia vitambulisho hivyo aliweza kujijua yeye ni nani, na ametoka wapi na amekuja kufanya nini, na matokeo ya kazi hiyo ni nini; na baada ya kumaliza kazi hiyo atakwenda wapi? Yesu Kristo alisema hivi; “Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; nakwenda kwa Baba” (Yohana 16:28) Yesu Kristo alijua kuwa ametoka katika ufalme wa Mungu, na kwamba yupo duniani akiwa balozi (mjumbe) wa ufalme wa huo. SHETANI ASOMA VITAMBULISHO Lakini tunafahamu ya kuwa jambo la kwanza ambalo balozi analifanya kabla ya kufanya kazi katika nchi aliyopelekwa ni kujitambulisha kwa kiongozi au mkuu wa nchi hiyo. Na Yesu Kristo akiwa mjumbe (balozi) wa kwanza wa kutoka katika ufalme wa mbinguni, ilibidi kwanza akutane na mkuu wa dunia hii, kabla ya kuanza kazi yake aliyotumwa kuifanya. Kwa hiyo mara tu baada ya Yesu Kristo kupewa vitambulsho, alipelekwa kwanza kwa Mkuu wa ulimwengu huu, ili atabulishwe kwake kwanza. Soma Mathayo 4:1-11. Ilikuwaje Roho Mtakatifu aliamua kumpeleka Yesu Kristo mikononi mwa Ibilisi, kwa makusudi kabisa, ili ajaribiwe? Ni dhahiri kulikuwa na sababu kubwa. Kumbuka kuwa kila hatua aliyoichukua Yesu Kristo akiwa hapa duniani ilikuwa katika mapenzi ya Mungu; hata kujaribiwa kwake pia. Na kusudi la kufanya hivi ni ili aonyeshe vitambulisho vyake ya kwamba yeye ni nani. Na ndiyo maana aliulizwa maswali matatu, kwa sababu vitambulisho vyake vilikuwa vitatu. Na ili kujaribiwa kwake kutimie Roho wa Mungu alimwacha Ibilisi amchukue Yesu anapotaka. Ibilisi asingeweza kusema “ ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu…..” kama isingekuwa ni kwamba alikuwa amevisoma vitambulisho vya Yesu Kristo. Na kila wakati Yesu Kristo alimjibu kwa maandiko akisema “Imeandikwa ….” Na kwa njia hiyo akamshinda Ibilisi. Kumbuka umetumwa kama Kristo alivyotumwa na umepewa vitambulisho kama alivyopewa Kristo, ili kufanya kazi kama alivyofanya Kristo. Pia basi fahamu utajaribiwa kama Kristo alivyojaribiwa. Kwa hiyo usishangae wakati mwingine unapoona ya kuwa, mtu yeyote anapotangaza kuwa ameokoka au anamtumikia Bwana anaingia katika majaribu mengi. Ndiyo maana mara nyingi maswali hutokea ya namna hii “Ikiwa kweli umeokoka mbona unafanya hiki na kile” Au, utasikia “Ukiwa kweli umeokoka na unamtumikia Bwana, mbona hufanyi hiki na kile? Unaposikia maswali kama haya fahamu kuwa kuna mjaribu nyuma yake. Na wewe ujibu kwa maandiko ukianza kwa kusema Imeandikwa. Lakini usipojijua wewe ni nani, na umetoka wapi, na umekuja kufanya nini, kila wakati utakuwa unashindwa na majaribu. Yesu Kristo alijua kuwa ametoka katika ufalme wa Mungu, na kwamba yupo duniani akiwa balozi (mjumbe) kwa ufalme huo. Na pia alikuwa na uhakika na vitambulisho alivyopewa; - kwa hiyo mara tu baada ya kupewa vitambulisho hivyo alianza kufanya kazi ya ubalozi. Imeandikwa hivi; “Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia”. (Mathayo 4:17) Unaona jinsi Yesu alivyoanza kazi yake. Fungua roho yako, iwe wazi kabisa tuende na Yesu hatua kwa hatua katika kazi yake ya ubalozi, ili na sisi tujue namna ya kuifanya, kwa sababu tumetumwa kama yeye alivyotumwa. FUATA NYAYO ZA YESU Kuna watu wengi siku hizi walioshindwa kumtumikia Mungu, na kuwa mabalozi (wajumbe) wa kweli kwa sababu hawana uhakika na wanakotoka kiroho na vitambulisho walivyonavyo. Siri mojawapo ya mafanikio ya Yesu Kristo katika kazi yake hapa duniani ni kwamba ALIJUA ALIKOTOKA NA ALIKUWA NA UHAKIKA NA VITAMBULISHO VYAKE. HAKUWA NA HOFU YOYOTE! Siku moja alifika mji wa Nazareti, na siku ya Sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake. “ Akapewa Chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo (kitabu) akatafuta mahali palipoandikwa, “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao; na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa (walioonewa), Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubalika. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho, Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. (Luka 4:17-21). Je! umeona jinsi Yesu Kristo alivyojitambulisha ya kuwa yeye ni nani na ametoka wapi na amekuja kufanya nini na vitambulisho vyake ni nini? Hapa alikuwa anajitambulisha mbele ya viongozi wa dini, viongozi wa serikali na watu wote kuwa yeye ni mjumbe (balozi) toka katika ufalme wa Mungu. Yesu Kristo hakuogopa kujisema yeye ni nani na kazi yake ni nini. Hakuwa na hofu hata kidogo. Aliweza kusema: “LEO MAANDIKO HAYA YAMETIMIA MASIKIONI MWENU”. Alijua kuwa ni yeye aliyekuwa ametabiriwa katika Torati, Zaburi na Manabii. Kumbuka umetumwa kama alivyotumwa, kwa hiyo utafanya kama alivyofanya na utasema kama alivyosema ili kuifanikisha kazi yako ya kuwa mjumbe (balozi) kwa ajili ya Kristo. Biblia inasema, “Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake,imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda”. (1 Yohana 2:6). Kufuatana na mstari huu tunatakiwa kuenenda kama Kristo alivyoenenda alipokuwa hapa duniani. KWA NINI UWE NA HOFU? Ukitaka kufanya kazi ya kuwa balozi kwa ajili ya Kristo, lazima ujifunze (inakupasa!) kuenenda bila hofu kama vile yeye alivyoenenda bila hofu. Aliweza kuenenda bila hofu kwa sababu alitoka katika ufalme wa Mungu, ambao ni ufalme wa upendo, na alikuja kuuwakilisha upendo, na ni upendo ndio uliomfanya aishi na kutembea, na kuifanya kazi ya Mungu bila hofu. Imeandikwa hivi; “Katika pendo hamna hofu, lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo. Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza. Mtu akisema, Nampenda Mungu naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake” (1Yohana 4:18-21). Baada ya kusoma mistari hiyo, jibu swali hili, Mbona watu waliojazwa Roho Mtakatifu wa Mungu ni wengi, lakini kazi ya Roho Mtakatifu haionekani katika maisha yao? Je! ni watu wangapi wanaofahamu kuwa unaye Roho yule yule ambaye alimwezesha Yesu Kristo kuhubiri habari njema ya kufunguliwa kwa wafungwa wa dhambi, vilema kutembea, vipofu kuona, na viziwi kusikia? Je hao wanaokuzunguka, nyumbani au kazini au shuleni, wanafahamu kuwa una kitu cha zaidi juu ya Roho Mtakatifu kuliko kunena kwa lugha mpya ambako wanakusikia mara kwa mara ukinena? Kazi za Kristo hazionekani vizuri siku hizi – kwa sababu upendo wa wengi umepoa. Ugomvi umejaa katika kanisa; masengenyo na chuki ni kitu cha kawaida siku hizi kati ya ndugu waliookoka. Manung’uniko ya wazi na ya moyoni ni mengi. Mioyo ya wakristo inajua kutukana kimya – kimya kuliko hata vinywa vyao vinavyotoa matusi na maneno machafu. Unategemea Mungu aonyeshe nguvu zake katika hali ya namna hiyo? Unategemea Mungu akutumie na huku una uchungu na mwenzio namna hiyo? La hasha! Upendo umekwenda wapi siku hizi? Watu wa Mungu wamejaa hofu katika vinywa vyao, na hata wasiposema matendo yao yanajidhihirisha wazi. Hofu ya kushindwa, hofu ya kudharauliwa, hofu ya kufilisika; hofu ya maisha, hofu ya kuugua, hofu – hofu – hofu ……… Mwisho Tuzidi kuombeana. Tukiamini ya kuwa mwezi ujao utakuwa pamoja nasi tena kusoma salamu na ujumbe tutakaokuletea. Mungu akubariki sana. Ni sisi katika utumishi wa Kristo, Christopher na DianaMwakasege |
|