Barua ya Mwezi June 2003
“MTAPOKEA NGUVU ZA
ROHO MTAKATIFU”
Kwa ajili ya nini?
Salamu
Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo; tukiamini ya kuwa rehema zake
ndizo lizokupa nafasi hii ya kusoma ujumbe huu tunaokuletea leo.
Ni
furaha kujua ya kuwa rehema za Mungu ni nyingi tena hazikomi, na ni mpya
kila asubuhi. Na sisi katika rehema hizi hizi tunazidi kumtumikia zaidi.
Tunaomba utuombee semina yetu inayofuata ya tarehe 10 –13 Julai 2003
pale Kigoma mjini.
Ujumbe
Je! Umewahi
kujiuliza kwa nini wakati mwingine nguvu za Mungu zinakushukia kwa
uwingi halafu baada ya muda zinapungua au zinaondoka – unabaki hali kama
vile hujawahi kushukiwa hata siku moja?
Inawezakana
umewahi kujiuliza swali hili na inawezekana hujawahi kujiuliza. Na pia
inawezekana hali hii tunayoiuliza hapa juu haijawahi kukutokea.
Kumbuka kuwa nguvu
za Mungu zinaweza kupungua ndani yako – kwa sababu mbalimbali – ambazo
ni pamoja na kutozitumia kwa kiwango kilichokusudiwa.
Unakumbuka Yesu
alipoulilia mji wa Yerusalemu? Alisema;
“Laiti ungalijua,
hata wewe, katika siku hii, yapasayo amani!”
(Luka 19:42).
Alichokuwa anataka wajue ni kwamba ndani yake kulikuwa na nguvu au upako
wa Roho Mtakatifu uletao amani. Lakini tunaona wazi ya kuwa Yerusalemu
hawakutumia upako huu na amani ya Mungu ikaondoka pia. Tatizo la
Yerusalemu lilikuwa ni kwa sababu hakutambua majira ya ‘kujiliwa’ kwake.
Kwa lugha nyingine
Yerusalemu ‘ulijiliwa’ au ulitembelewa na nguvu za Mungu ziletazo amani
– lakini hawakutambua! Na kwa sababu hawakutambua hilo, kwa hiyo hata
nguvu za Mungu hawakuzitambua wala kuzitumia. – Kilichotokea ni kwamba
nguvu hizo (1Wakorintho
1:18,24)
ziliondoka wasiweze kuzitumia.
Tunaona pia katika
Yohana 1:11 ya kuwa
“ Alikuja kwake,
wala walio wake hawakumpokea.”
Yesu anaweza kuja kwako. Nguvu zake (ambazo ndizo nguvu za Roho
Mtakatifu) zinaweza kuja kwako – usipozipokea itakuwa vigumu kuzitumia
kwa kiwango kinachotakiwa. Maana katika mstari unaofuata wa 12, Yohana
anaendelea kusema hivi:
“
Bali
wote waliompokea aliwa uwezo wa kufanyika …..”
Ili
uweze kuzipokea na kuzitumia nguvu za Mungu ipasavyo ni vizuri ujue
Mungu amezituma nguvu zake kwetu kwa ajili ya nini. Zipo sababu nyingi
katika biblia, lakini sisi tunataka tukupe angalau chache wakati huu ili
ziwe changamoto kwako.
Sababu ya
Kwanza: TUWE MASHAHIDI WAKE
Ili
tuonekane na kujulikana ya kuwa sisi tu wanafunzi wa Yesu –
tunachohitajika kufanya ni kupendana (Yohana 13:35). Huu ni upendo ambao
watu wasiomjua huyu Mungu wetu wanatakiwa wauone kwetu. Wakiona
tunavyopendana, basi watajua ya kuwa sisi tu wanafunzi wa Yesu.
Unapofanya sala ya toba na kumkaribisha Yesu katika maisha yako –
unaokoka. Unaweza ukawa umeokoka lakini usiwe ‘mwanafunzi’ wa Kristo –
kwa tafsiri ya Yesu juu ya nani ni mwanafunzi wake. Ikiwa umeokoka na
huonyeshi upendo wa Kristo kwa waliookoka wenzako unapoteza hadhi ya
kuwa mwanafunzi wa Kristo.
Inapofika hali ya kuwa ‘shahidi’ inabidi upokee nguvu za Roho Mtakatifu.
Yesu alisema katika kitabu cha Matendo ya Mitume 1:8 ya kuwa:
“ Lakini mtapokea
nguvu,; akiisha kuwajilia
juu yenu Roho
Mtakatifu; nanyi mtakuwa
mashahidi wangu
katika Yerusalemu, na
katika Uyahudi
wote, na Samaria, na hata
mwisho wa nchi”
Kazi ya
shahidi ni kusimama upande wa anayeshitaki au anayeshitakiwa kumtetea
huyo ambaye ameamua kuwa shahidi upande wake – akisema na kwa kuonyesha
vithibitisho ili kusisitiza kuwa anachokitetea ndicho sahihi.
Katika
mazingira ya Bwana Yesu, sisi tunakuwa mashahidi kwa kusema na kuonyesha
au kuthibisha kwa vitendo ya kuwa yote ambayo Yesu Kristo amesema na
yamefanyika juu yake ndivyo yalivyo, na ndiyo kweli inayotakiwa kufuatwa
na kila anayemtafuta Mungu wa kweli.
Nguvu za
Roho Mtakatifu zinatufanya tuweze kusimama katika nafasi ya kuwa
mashahidi wa Kristo.
Sababu ya Pili:
Kushinda Dhambi
Ndiyo!
Kushinda dhambi. Unaweza kuishinda dhambi. Katika Mwanzo 4:7 tunaambiwa
inatupasa au ni lazima tuishinde dhambi. Mungu hawezi kusema tuishinde
dhambi kama hakuna mbinu ya sisi kuishinda dhambi. Pia, katika Warumi
tunaambiwa ya kuwa dhambi haitatutawala.
Lakini
ni lazima tujue ya kuwa hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kuishinda
dhambi kwa nguvu zake mwenyewe. Kila mtu lazima ajue kuzitumainia
nguvu za Mungu
tunazozipata katika Roho Mtakatifu kwa sababu ya Kristo kufa msalabani
kwa ajili yetu. Ndiyo maana imeandikwa hivi katika 1 Wakorintho
1:18,23,24:
“ Kwa sababu neno
la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookokolewa ni
nguvu ya Mungu …… sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi
ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa
Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.”
Hiki
ndicho kinachotokea unapookoka; Kristo anaingia ndani yako kwa uwezo wa
Roho Mtakatifu- anakuwa nguvu ya Mungu inayokuwezesha kushinda dhambi.
Kwa hiyo kama iko dhambi inayokusumbua – tubu, halafu omba Mungu
akuongezee nguvu za Roho wake ili upate kushinda dhambi.
Sababu ya Tatu:
Kuwa Tajiri
Jambo
mojawapo lililotokea kwa mwanadamu dhambi ilipoingia ni kuishi maisha ya
umaskini na kupungukiwa. Dhambi pia iliweka matabaka ya matajiri na
maskini. Toka mwanzo na hata sasa na siku zote Mungu hapendi watu wake
wawe maskini (kwa jinsi ya mwili)
Katika 2
Wakorintho 8:9 tunasoma ya kuwa:
“ Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini
kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa
matajiri kwa umaskini wake”
Kwa hiyo
ni mapenzi ya Mungu tuwe matajiri. Njia ambayo Mungu anatumia
kutuwezesha tuwe matajiri ni kwa kutupa nguvu zake. Kwa maana imeandikwa
katika kitabu cha Kumbukumbu ya Torati 8:18 ya kuwa:
“Bali utamkumbuka
Bwana, Mungu wako
maana ndiye
akupaye nguvu za kupata
utajiri, ili
alifanye imara agano
lake
alilowapa
baba zako,
kama
hivi leo”