Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi wa Machi 2003

UNAFANYAJE MUNGU ANAPOFANYA MAKUBWA KULIKO ULIVYOTEGEMEA?

Salamu katika Jina la Yesu Kristo;

            Ndiyo kwanza tumemaliza semina ya siku nane iliyofanyika Arusha tarehe 16 – 23 Februari 2003 tuliyoifanya katika viwanja vya shule ya sekondari ya Arusha – Meru – ndani ya hema. Mungu amefanya mambo makubwa kuliko mawazo yetu yalivyotegemea. Imeandikwa katika kitabu cha Waefeso 3:20,21 ya kuwa:

“Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya  ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam,  atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina”

            Tunaamini Mtume Paulo aliongozwa na Roho wa Mungu kuandika maneno haya baada ya kuona Mungu amemfanyia mambo makubwa mno kuliko yote aliyoyaomba au aliyoyawaza! Ndivyo yalivyotokea katika siku nane za semina ya Arusha – Mungu amefanya mambo makubwa mno kuliko tulivyoomba au tulivyowaza! Paulo akaandika, “Basi atukuzwe yeye …..” Kwa hiyo

Na Sisi tunamtukuza Yesu!

            Sisi tunamtukuza Mungu katika Yesu Kristo ambaye ametufanyia mambo makubwa sana wakati wa semina. Si rahisi kukueleza yote kwa jinsi yalivyo mengi, lakini tutajitahidi kukueleza mambo kadhaa. Nia yetu ya kukueleza haya yote ni ili na wewe upate kumtukuza Mungu pamoja nasi! Lakini pia upate kujua ya kuwa kama umekuwa ukituombea basi Mungu amejibu maombi yako. Kama umekuwa ukimtolea Mungu sadaka kutusaidia kuifanya kazi hii ya Mungu, basi ujue katika ulimwengu wa roho ulikuwa pamoja nasi katika semina hiyo tukihudumu pamoja. Na Mungu wetu atakujaza kila unachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake “katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu”  (Wafilipi 4:19)

Ishara ya mambo

 mazuri mbele!

Siku ya kwanza ya semina kulizuka ghafula upepo na mvua kubwa ambayo kwa muda mfupi iliharibu baadhi ya mahema tuliyokuwa tumeyafunga. Watu kadhaa wakanyeshewa na mvua. Lakini watu wakamwomba Mungu kwa pamoja na kumkemea shetani kwa nguvu – na baada ya muda mfupi tu upepo ulitulia na mvua ikanyamaza.

            Kwetu sisi hii ilikuwa ishara. Ishara ya mambo mazuri yaliyokuwa mbele yetu katika semina hiyo. Tulijua shetani ameona ushindi tuliopewa na Yesu katika semina na hakufurahi. Kwa hiyo alitaka kuivuruga semina tokea siku ya kwanza. Lakini Mungu akatupigania – hila za shetani zikakwama. Siku hiyo semina iliendelea na watu wakazidi kumiminika kuja kwenye kiwanja tulichofanyia semina. Neno likafundishwa, wagonjwa wakaponywa wengi na mamia kwa mamia ya watu wakaokoka siku hiyo hiyo ya kwanza ya semina

Miujiza yathibitisha

Yesu Yuko hai!

Katika Yohana 20:30,31 imeandikwa ya kuwa; “Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake”

            Mungu anapolithibitisha neno lake kwa ishara na miujiza – jina la Yesu hutukuzwa sana. Kwa hiyo katika semina hizi tunazofanya sehemu ya shuhuda ni muhimu sana. Tatizo tunaloliona ni kwamba muda tunaokuwa  naona unakuwa hautoshi kumpa nafasi kila mtu aliyepona kutoa ushuhuda wake. Hata katika waraka huu tutakushirikisha shuhuda chache ili kila mtu apate kujua ya kuwa Yesu Kristo yuko hai, tena ya kwamba ndiye Kristo, Mwana wa Mungu.

            Watu waliojitokeza kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha, wengine walikuwa wamepokea miujiza yao katika semina za mwaka jana; wengine walipona kupitia kwenye vipindi vyetu vya radio; na wengine walipona katika semina hii ya mwezi Februari 2003.

            Kwa mfano; kuna mama mmoja alishuhudia ya kuwa alikuwa anaumwa na ukimwi na Mungu amemponya. Tulipomuuliza ya kuwa amejuaje ya kuwa amepona, - akasema ni kwa sababu dalili zote za ugonjwa wa ukimwi alizokuwa nazo mwilini zimeondoka baada ya maombi. Tukamshukuru Mungu pamoja naye na kumshauri aende hospitalini akapime tena – ili vipimo vya hospitali vikithibitisha uponyaji – wengine wapate kumwamini Yesu na kumfuata.

            Kuna mwanamke mwingine aliyekuwa na shida ya ‘kutokwa damu’ kwa muda wa miaka mitatu mfululizo, alishuhudia jinsi Mungu alivyomponya katika semina ya Novemba 2002. Na tangu wakati huo ni mzima na shida hiyo haijamrudia tena!

            Kijana mmoja alieleza mbele ya maelfu ya watu jinsi mguu wake wa kushoto ulivyokuwa na matatizo; na jinsi alivyokuwa amekwenda hospitali kubwa za Shinyanga, Mwanza, Musoma na Arusha bila kufanikiwa kupona. Na alikuwa anajiandaa kwenda hospitali ya KCMC ya Moshi aliposikia habari za semina na akaamua kuja. Matokeo yake Mungu alimponya. Akiwa madhabahuni akasema ingawa mguu wake huo wa kushoto ulikuwa umepona, bado alikuwa anatembea kwa shida maana ulikuwa mfupi. Kwa hiyo tukamwomba Mungu ili mguu huo mfupi ukue na kuongezeka urefu. Mbele ya maelfu ya watu tuliona mguu ukitingishwa kwa nguvu za Mungu na kukua hadi kufikia urefu wa kufanana na ule mwingine wa kulia uliokuwa mzima. Maelfu ya watu walioshuhudia muujiza huo walishangilia na kumtukuza Mungu sana.

            Kuna mama mwingine alishuhudia Mungu alivyomponya katika semina hiyo hali ya kupoteza fahamu na kukosa nguvu upande wake wa kushoto kutoka na ugonjwa wa ‘stroke’. Hiyo ‘stroke’ ilifanya mdomo wake upindie upande mmoja alipokuwa anaongea na jicho la kushoto kushindwa kufunguka na kutokuwa nafahamu akiguswa upande huo wa kushoto. Na alikuwa anatembea kwa shida sana. Lakini Mungu alivyo mwingi wa rehema akamponya katika semina hii na akaweza kuona tena vizuri, mdomo ukarudi mahali pake, na fahamu zikarudi katika upande wake wa kushoto – na akaweza kutembea vizuri.

            Shuhuda zilikuwa nyingi sana. Kuna walioshuhudia mifupa iliyounga na kupona; kuna waliopona matatizo ya macho, na magonjwa mwengine mengi. Sisi tunamtukuza Mungu sana kwa uponyaji huu wa ajabu. Jina la Yesu libarikiwe milele!

Waliojazwa Roho Mtakatifu

ni wengi sana!

            Katika eneo hili Bwana Yesu alifanya mambo ya ajabu sana. Si tu kwamba aliwajaza Roho Mtakatifu wale waliokuwa na kiu naye; bali hata wale ambao walikuwa wanapinga habari za kunena kwa lugha mpya; na hata wale ambao hawakujua kilichokuwa kinaendelea.

            Kuna watu waliotueleza jinsi walivyosubiri kwa hamu wapate ‘Double Dose’ ya upako lakini hawakufanikiwa. Walipokuwa wakirudi nyumbani kwao wakiwa ndani ya ‘taxi’ walianza kusimuliana habari za yule kijana aliyepona mguu na wakauona ukikua. Wakiwa katika kuongea juu ya habari hiyo wakataja jina la Yesu – na mara hiyo hiyo wakashukiwa na nguvu za Mungu na kuanza kuomba hadi walipofikishwa nyumbani, kwao, na hata hivyo mmoja wao alishindwa kutembea maana alipotelemka tu toka kwenye ‘taxi’ alianguka chini na kuendelea kuomba. Watu wengi wakawazunguka na kushangaa kulikoni! Pamoja na kwamba Yesu hakuwapa ‘Double Dose’ ya upako pale uwanjani, aliamua kuwapa ndani ya ‘taxi’!

            Mama mwingine alishuhudia mbele ya maelfu ya watu kuwa alikuwa anapinga habari za kunena kwa lugha, na kwamba wale waliokuwa wanadai wananena kwa lugha mpya walikuwa wakijifanya tu. Lakini Mungu aliamua kumthibitishia jinsi alivyokosea katika kuwaza kwake! Alisimulia ya kuwa alikuwa amekaa kwenye kiti wakati wa somo likiendelea alishitukia ameanza kunena kwa lugha mpya! Na wakati wa maombi mwishoni mwa somo alisogea na yeye mbele ya jukwaa, nguvu zikamshukia na kunena tena kwa lugha mpya lakini pia na kucheka sana. Aliondoka uwanjani kwenda nyumbani na kupanda basi huku akiendelea kucheka katika Roho Mtakatifu. Tangu siku hiyo ubishi ulikwisha na ana uhakika wanaonena kwa lugha hawajifanya – bali ni halisi na ni kweli tupu!

            Mama mwingine alitusimulia jinsi alivyojikuta anazungumza ‘lugha asiyoijua’ akiwa amekaa kwenye kiti wakati wa maombi ya ujazo wa Roho Mtakatifu. Hakujua ni kitu gani kimetokea hadi tulipokutana naye baada ya semina na kutueleza kulichotokea. Tukamwambia ya kuwa kilichotokea ni kwamba alijazwa Roho Mtakatifu na ishara iliyotokea kuthibitisha hili ni yeye kunena kwa lugha mpya. Alipopata ufafanuzi huo alifurahi sana. Na sisi tunamtukuza Mungu pamoja naye! Sifa ni kwa Yesu Kristo!

            Maelfu ya watu walijazwa Roho Mtakatifu hata wengine kushindwa kutembea na kubebwa kwenda nyumbani; na wengine kushindwa hata kuongea kwa muda! Laiti ungekuwepo na uone jinsi Mungu alivyotembelea na kuwajaza upako wa Roho Mtakatifu vijana!

Utayari wa kuokoka ulikuwa mkubwa!

            Watu walivyokuwa wanaokoka ‘kirahisi’ utadhani walikuwa wanatoka nyumbani wakiwa wamepania kuokoka! Maana ilikuwa haijalishi unaita watu kuokoka wakati gani, kabla au baada ya neno – walikuwa wanaokoka tena kwa uwingi sana. Kwa siku nane zote ni wastani wa watu 9500 waliokoka! Siku zingine walikuwa wanaokoka watu wengi kiasi ambacho wahudumu hawakuweza kuwaandika wote. Lakini tuna uhakika mbinguni wana kumbukumbu nzuri zaidi ya majina ya wote waliookoka katika semina hiyo!

            Siku moja baba mmoja ambaye alikuwa hajaokoka alielezea ushuhuda uliofanya watu wengi waokoke pamoja na yeye mwenyewe! Alisema siku moja aliamua ‘kunyata’ usiku ili asimwamshe mke wake aliyekuwa amelala, - akachukua mkanda wa video wa moja ya semina zetu na kwenda sebuleni kuuangalia. Wakati wa maombi ulipofika katika video, naye akasimama na kuweka mkono juu ya kifua chake – kwani alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo na wa shinikizo la damu. Baada ya maombi hayo ya kwenye video akapona! Kwa hiyo wakati wa semina akaamua kutoa ushuhuda wa uponyaji huo, na kuomba aombewe aokoke pia! Watu waliosikia wakashangilia kwa nguvu, na sisi tukakaribisha watu wengine ambao hawajaokoka waje mbele ili waombewe na waokoke pamoja naye. Mamia ya watu walijitokeza kuokoka! Mke wa baba huyo ambaye yeye alikuwa ameokoka alikuja mbele kushuhudia kwa macho yake na masikio mume wake akiokoka! Jina la Yesu lihimidiwe milele!

Mwisho

            Tunatamani tuendelee kukueleza mambo mengi zaidi ambayo Bwana aliyofanya – lakini tunaona tuliyokuandikia hapa yanatosha kwa leo. Watu waliohudhuria walikuwa wengi sana – si chini ya 10,000 kila siku. Siku ya mwisho wa semina walikuwa wengi zaidi kiasi kama 20,000!

            Tuzidi kuombeana. Ni kweli Mungu amefanya kuliko tulivyokuwa tumetegemea. Sifa na utukufu ni wake. Semina zinazofuatana ni Dar es Salaam tarehe 1 –9 Machi 2003 (Kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee) na tarehe 18 – 24 Machi 2003 Tanga mjini. Tuombee ili Mungu akajitukuze tena. Ukiweza kufika kwenye semina hizo karibu sana tushirikiane baraka za Mungu.

ni sisi katika utumishi wa Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.