Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma
BARUA ZA MWEZI


Barua ya Mwezi May 2003

Maswali ya Kujiuliza Unaposongwa na Majaribu

Mpendwa Katika Kristo Yesu

          Ni matumaini yetu ya kuwa barua hii inakukuta na unaisoma katika mazingira ya ushindi tulionao kila siku katika Yesu Kristo. Tunaamini Mungu anakutunza na anaendelea kukupigania. Ni maombi yetu kwa Mungu ya kuwa neema yake Kristo itazidi kukufunika ili kiu uliyonayo ya kutaka kumjua zaidi Mungu na kumtumikia uzidi kuwa nayo.

          Katika mwezi huu Roho Mtakatifu ameweka ndani yetu kuhimizwa kukushirikisha juu ya maswali unayopaswa kujiuliza kila wakati unapojikuta umekabiliwa na jaribu au majaribu.

Majaribu ni nini?

          Majaribu ni matatizo yanayomkumba mtu na kumfikisha njia panda au mahali pa kujiuliza mwenyewe; - kama aendelee na Yesu au amwache…; - Au kama Mungu yupo pamoja naye au la …; - Au kama aendelee na wokovu au aache …; - Au kama aendelee na utumishi huo au na kikundi hicho au na kanisa hilo au na kamati hiyo au aache …; - Au kama ahadi za Mungu ni za kweli au la …; - Au aendelee na maombi au aache ….

          Kwa hiyo si kila tatizo ni jaribu! Ingawa kila jaribu ni tatizo kwake yule anayejaribiwa! Kumbuka au fahamu ya kuwa hakuna mtu ambaye hakutani na majaribu. Kila mtu huwa anaingia katika majaribu kwa namna moja au nyingine – na kuna wengine hawajajua la kufanya.

          Pia, inawezekana kabisa ya kuwa lile ambalo kwako wewe unaliona si jaribu, - kwa mwingine linaweza kuwa jaribu – tena jaribu kubwa! Kwa mfano; kuolewa au kuoa kwa mwingine ni jaribu na angetamani asingeolewa au asingeoa kama angejua atakutana na jaribu alilokutana nalo. Wakati huo huo kwa mwingine kutokuolewa au kutokuoa kumekuwa jaribu kwake. Pia, inawezekana kwa mwingine kuzaa na kuwa na mtoto ni jaribu kwake, wakati kwa mwingine kutokuzaa na kutokuwa na mtoto kumekuwa jaribu. Pia, inawezekana kwa mwingine kuwa na pesa ni jaribu, wakati kwa mwingine kutokuwa na pesa ni jaribu! Pia, inawezekana mtu unayemwona wewe ni kikwazo na jaribu kwako, kwa mwingine mtu huyo huyo anaonekana wa maana, wa baraka, na wa msaada!

Maswali ya kujiuliza unapojaribiwa

          Ni jambo la kawaida kwa mwanadamu yeyote kujikuta anajiuliza maswali mengi nafsini mwake – hasa anapotambua ya kuwa yumo katikati ya jaribu. Katika maswali mengi unayokuwa nayo wakati huo unapojaribiwa, tunaomba usisahau kujiuliza maswali mawili muhimu yafuatayo:

Swali la kwanza: Yesu yuko wapi unapojaribiwa – Yumo ndani ya jaribu au nje ya jaribu au hujui yuko wapi?

          Kujua jibu la swali hili kutakusaidia sana katika kuamua uombe maombi ya namna gani juu ya jaribu hilo na uenende kwa namna gani wakati ukiwa unajaribiwa.

          Tunakuambia haya kwa sababu biblia imeweka wazi juu ya mazingira mbalimbali ambayo mtu wa Mungu anaweza kukumbwa na majaribu, na pia kuweka wazi mambo yanayoweza kumsaidia kutoka na ushindi katika jaribu lililomsonga.

          Kwa mfano, katika kitabu cha Luka 8:22 – 25 tunaona ya kuwa Yesu alikuwa na wanafunzi wake ndani ya boti wakati walipokuwa wanakumbwa na msukosuko wa upepo na mawimbi wakivuka bahari. Ni mpaka walipomwamsha na Yeye kupata nafasi ya kudhihirisha uwezo aliokuwa nao juu ya tatizo walilokuwa nalo – ndipo upepo ukakoma na mawimbi kutulia. Pia, ukilinganisha na majaribu – mtu anaweza kukumbwa na misukosuko ya majaribu Yesu akiwa ndani ya ‘boti’ au ndani ya maisha yake. Kwa hiyo kukumbwa na majaribu haina maana ya kuwa Yesu amekuacha. Inawezekana kabisa yupo pamoja na wewe katika jaribu hilo – soma pia Zaburi ya 23.

          Lakini pia katika Mathayo 14:22-23 tunaona wanafunzi wa Yesu wakiwa ndani ya boti bila Yesu wakati msukosuko wa mawimbi na upepo ukiwasumbua. Kwa hiyo unaweza pia ukawa katika msukosuko wa jaribu – huku Yesu umemwacha ‘ngambo’ – yaani hukuanza naye ‘safari’ katika hilo unalofanya lililokuingiza majaribuni.

          Pia unaweza ukajikuta hujui kama Yesu yumo ndani ya jaribu au hayumo. Kwa sababu ukisoma kitabu cha Danieli 3:1,2, 16 – 18, 24-25 tunaona jaribu lililowapata Shedraki, Meshaki na Abedinego. Hawakujua kama Mungu atawasaidia au la! Na hata kama atawasaidia – hawakujua kama msaada huo atawaletea wakiwa nje ya ‘tanuru’ (au nje ya jaribu) au ndani ya ‘tanuru’ (au ndani ya jaribu). Kwa hiyo wakaamua kusimama katika ushuhuda wa kumheshimu na kumwamini na kumwabudu Mungu hata ingawa hawakujua kama atawasaidia au hatawasaidia.

          Ikiwa wakati huu unaposoma ujumbe huu umo katika jaribu ni muhimu ujiulize ikiwa Yesu yumo ndani ya jaribu au yupo nje ya jaribu au pia ikiwa hujui yupo wapi ndani au nje ya jaribu!

Swali la Pili: Jiulize – hivi chanzo cha jaribu ulilonalo ni nini? Ni Mungu? Ni Shetani? Ni Mwili?

          Watu wengi huwa wanadhani chanzo cha majaribu yote ni shetani, na wengine ni Mungu. Lakini Biblia imeweka wazi ya kuwa majaribu tunayokutana nayo yanaweza yakawa yanatoka kwa Mungu – soma Mwanzo 22:1,2,9-14; Au yakawa yanatoka kwa shetani – soma Mathayo 4:1-3; Au yakawa yanatoka katika mwili wako – soma Yakobo 1:13-15 na Wagalitia 5:16,17. Na kila jaribu unatakiwa ulikabili tofauti kufuatana na chanzo chake kilivyo tofauti.

          Tofauti za vyanzo hivi ni hizi: Mungu akikujaribu huwa analengo la ‘kukupima’ au kukupa mtihani ambao utamwezesha kupima uwezo wako kama umeiva na uko tayari au umefikia kiwango cha wewe kuingia ngazi nyingine inayofuata ya baraka au ya utumishi aliokupangia. Lakini wakati mwingine Mungu akikujaribu ni ili akupe kutokutulia katika ngazi uliopo ili usonge mbele katika hatua/au katika eneo lingine la huduma au baraka aliyokuitia na kukupangia.

          Shetani akikujaribu huwa siku zote lengo lake ni kukujengea mazingira ambayo yatakufanya iwe rahisi kwako kuona sababu ya kumwacha Mungu au iwe rahisi kwako kuacha kuliamini na kulitii Neno la Mungu au maagizo yake.

          Mwili ukikujaribu unataka roho na nafsi yako vifuate mwili unachotaka hata kama ni kinyume na mapenzi ya Mungu. Na kufuatana na Warumi 8:5-8 ukiufuata mwili hauwezi kuwa na maisha ya kumpendeza Mungu.

Mwisho

          Tunaamini umepata cha kukusaidia katika ujumbe huu. Tuzidi kuombeana ili sote tuzidi kudumu katika mapenzi ya Mungu. Mungu na azidi kukubariki na kukushindia katika jaribu lolote linalokusonga au linaloweza kukusonga.

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.