|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Salamu katika Jina la Yesu Kristo. “Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu” Luka 22:20 · Kuifahamu Damu ya Yesu bila ya kujua namna ya kuitumia, haiwi na msaada kwako katika kukunufaisha yaliyomo katika agano jipya. · Kumbuka unaweza kuitumia Damu ya Yesu kwa KUIBEBA – KUINYUNYIZA – KUIMWAGA – KUINYWA lakini kwa jinsi ya rohoni kwa kuwa agano jipya ni agano la rohoni au linaloanza rohoni. · Leo tujifunze na kuimarisha IMANI tuliyonayo katika Damu ya Yesu. Unakuwa una hamu zaidi ya kukitumia kile kitu ulicho na imani nacho zaidi. Hata mtu uliye na imani naye zaidi ndiye unayemtumia zaidi. “kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa” Warumi 3:23-25 · Kwa nini tujifunze na kuimarisha Imani katika Damu ya Yesu? Kwa kuwa tunatakiwa kuitumia kwa imani kuibeba kwa imani; kunyunyiza kwa imani, kuimwaga kwa imani na kuinywa kwa imani! Pia tunatakaswa, tunanunuliwa, tunasafishwa, tunakombolewa, tunashinda, tunalindwa kwa imani katika Damu ya Yesu. · Kufuatana na Waebrania 11:1 – Imani katika Damu ya Yesu ni kuwa na uhakika ya mambo yatarajiwayo na bayana ya mambo yasiyoonekana juu ya yale yaliyotamkwa juu ya Damu ya Yesu. Au Imani katika Damu ya Yesu ni kuamini ya kuwa alichokisema Mungu juu ya Damu ya Yesu ndivyo kilivyo na ndivyo kitakavyotokea. · Lakini kufuatana na Yakobo 2:26 Imani pasipo matendo imekufa au haizai au haileti matokeo yaliyotarajiwa. Au Usitegemee matokeo yo yote katika neno alilolisema Mungu (juu ya Damu ya Yesu – kwa mfano) kama hutataka kutii au kutekeleza kile uchotakiwa kukifanya wewe kilichomo katika neno hilo. Mifano: 1. Damu katika Miimo ya Milango – (Kutoka 12:1-7, 12,13). Nguvu ya ulinzi ya Damu ile ilitokana na maneno ya makubaliano (agano) yaliyosemwa na Mungu – Na Utii wa wana wa Israeli juu ya maagizo waliyopewa kufanya juu ya Damu ile. Damu: - bila Neno la anayeahidi….. - bila Utii wa yule anayeahidiwa juu ya Neno kuhusu Damu lililoambatana na ahadi….. - HAINA NGUVU YOYOTE KIROHO! Tunauhakika Wamisri wengine waliona Wana wa Israeli wakiweka damu katika miimo lakini au hawakuelewa na hawakuuliza, na hata kama waliuliza na kujua sababu walidharau – kwa sababu hawakuamini maneno ya makubaliano (agano) yaliyosemwa juu ya Damu hiyo; lakini hata hivyo wala makubaliano hayo hayakuwahusu. 2. Kamba nyekundu (Ishara ya Damu) – Yoshua 6:22-25 – Uwezo wa ‘Kamba Nyekundu’ wa kumlinda na kumwokoa Rahabu na familia yake ulitoka wapi? Ulitoka katika maneno ya ahadi ya Watumishi wa Mungu pamoja na Utii wa Rahabu katika maagizo aliyopewa ya kamba nyekundu na kitu cha kuifanyia. Lazima kuna waliiona kamba nyekundu lakini hawakuelewa, wala hawakuwa sehemu ya mapatano-kwa hiyo hawakunufaika nayo! 3. Pete ya Harusi Ni alama ya nje ya makubaliano ya watu wawili kuishi pamoja kama mume na mke. Kitu gani kinafanya pete hiyo iwe na maana ni maneno ya ahadi yanayotamkwa na maarusi na matendo yanayoambatana na ahadi hiyo. Ndiyo maana maneno matupu katika ndoa bila matendo hayasaidii ndoa kuwa imara. 4. Katika Agano Jipya kitu gani kimefanya Damu ya Yesu ikubalike na ile ya mafahali isikubalike? Ni Neno la Mungu. Ili nguvu zake zionekane tii, tenda kilichoagizwa juu ya Damu ya Yesu. MUHIMU ufahamu hili ya kuwa: Nguvu ya Damu ya Yesu katika maisha yako inategemea KUSEMA KWAKO MANENO UNAYOTAKA DAMU IFANYE SAWASAWA NA AGANO LINAVYOSEMA NA KUTII AU KUTENDA SAWA NA HAYO MANENO ULIYOSEMA. TENA kumbuka ya kuwa: Kufuatana na Kutoka 12:12,13 – unapoiweka Damu ya Yesu (kwa kusema) juu ya Nyumba, gari, mtu, mtoto, mke, mume, juu yake mwenyewe. Si tu kwamba Mungu analinda dhidi ya madhara ya adui, na madhara ya pigo lake LAKINI pia anafanya hukumu juu ya nguvu za giza lakini vile vile na juu ya yule anayetaka kudhuru hicho kitu au huyo mtu (Hesabu 33:4, Kutoka 18:11). Tunachotaka ujifunze ni kwamba: 1. Ili damu ya Yesu iweze kukunufaisha kupata yaliyomo katika Agano Jipya ni muhimu ujue namna ya kuitumia. 2. Imani yako katika damu ya Yesu ikiongezeka inakuwa rahisi kwako kuwa na hamu zaidi ya kujifunza namna ya kuitumia. 3. Imani inaongezeka juu ya Damu ya Yesu kwa: (i) Kuwa mtendaji wa neno linaloambatana na ahadi ya damu ya Yesu inavyoweza kukusaidia Mfano: Wana wa Israeli na damu ya Pasaka : Rahabu – kahaba na kamba nyekundu. (ii) Kujua kwa nini Damu ya Yesu ina Thamani kuliko damu nyingine yo yote (1 Petro 1: 18,19) Shuhuda za utendaji wa Damu ya Yesu · Kuna wahubiri waliokwenda visiwa vya Bahamas wakitokea Marekani na wakakutana na upinzani. Ilikuwa wakianza kuhubiri kuna watu waliokuwa wanakuja mahali walipokuwa wakifanyia ibada na madebe na makopo na kupiga kelele. Hao wahuburi wakaanza kuzunguka mahali hapo mara kazaa wakisema “Tunanyunyiza Damu ya Yesu”. Usumbufu huo ukakoma – baada ya maombi hayo! · Kati ya miaka ya 1908 na 1909 uamsho mkubwa ulitokea Uingereza na jambo moja lililojitokeza wakati huo ni watu wanaotaka kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu kujikuta wakisema kwa kurudiarudia juu ya Damu ya Yesu. Wakisema “nanyunyiza Damu ya Yesu” au “Damu ya Yesu.” Na Roho Mtakatifu alikuwa anashuka na walikuwa wanajaa na kunena. · Huko huko Uingereza Mchungaji mmoja alijikwaruza na msumari gereji usiku na kuumia. Akaweka mkono juu ya jeraha na kuanza kusema “ Nanyunyiza Damu ya Yesu” – kwa kurudia –rudia. Baada ya nusu saa akapona na alama ya jeraha ikapotea. · Kuna mhubiri na familia yake ambao waliishi wakati wa vita kuu ya pili Uingereza (London). – Walikuwa kila siku wanasema “Tunaifunika nyumba yetu kwa Damu ya Yesu”. Nyumba haikupigwa mabomu wakati wa vita! · Kuna mmisionari mmoja aliyeumwa na ng’e mwenye sumu huko Afrika ya kati. Akashika kidole kilichoumwa na kuanza kusema “Nanyunyiza Damu ya Yesu dhidi ya sumu hii” Akapona ingawa wenyeji walifikiri atakufa! · Kuna mtoto aliyekuwa na jicho moja halioni na la pili linachezacheza na halioni vizuri. Mhubiri akamwekea mikono juu ya macho akasema kwa nguvu “Nanyunyiza Damu ya Yesu” Jicho bovu likaanza kuona mara hiyo hiyo. Lililokuwa linacheza likaanza kupona polepole na baada ya siku chache likatulia na kuona vizuri. Tiliposoma na kusikia shuhuda hizi na zingine nyingi ambao hatuzitaja – zilitufanya na zinatufanya tutamani kujifunza zaidi juu ya damu ya Yesu – maana inaonekana ina THAMANI na NGUVU kuliko tunavyojua. KWA NINI IWE HIVI? Kitu gani kinafanya Damu ya Yesu iwe na nguvu na thamani namna hii? 1. Kwa sababu YA AINA YA UHAI uliomo ndani yake, Soma Mwanzo 9:4; na Mambo ya Walawi 17:11,14 (i) Tafakari haya: Damu ni moja na uhai wa mwenye damu; Damu inabeba roho na nafsi ya mtu. (ii) Kama katika Damu ndiko kuliko na UHAI wa mtu – kwa hiyo Uzima wa Mungu na Uzima wa mtu vinakutana katika hiyo DAMU – AU ili kukutana lazima kuwe na Damu. ‘Blood is a meeting place of Spirits’ (iii) Dhambi ilikuwa na madhara kwenye damu maana huko ndiko kuliko na UHAI. Uhai ulipotea na MAUTI ikaingia. (iv) Kwa sababu dhambi imeleta MAUTI (Kutengwa na Mungu) – ina maana basi ili KUUNGWA NA MUNGU TENA lazima kuwe na damu ya mtu au mnyama aliye hai na asiye na dhambi; ili kwa njia ya uhai huo Mungu aungane na kuwasiliana na mwanadamu aliyetenda dhambi. (v) Na kwa sababu hakukuwa na mwanadamu aliye hai ambaye damu yake ilikuwa safi haina mauti – ndiyo maana Mungu aliagiza damu ya wanyama HADI Yesu alipotokea. (vi) Kwa sababu Dhambi imesababisha mauti na ndio mshahara Mungu anadai. Ili kuwe na ondoleo la dhambi lazima Damu imwagike kwa ajili ya mwenye dhambi (Waebrania 9:22) (vii) Kwa sababu kwenye nafsi kuna (maamuzi,nia na hisia) na nafsi imo katika Damu – shetani anapenda kupata utawala na kuwasiliana na mtu kwa njia ya damu. (viii) Damu ya Yesu ina thamani kwa kuwa ni UHAI wa Mungu na haina dhambi ndani yake wala mauti (Matendo 20:28; Luka 1:34,35) · Kwa hiyo popote ilipo Damu ya Yesu – pana Uhai wa Mungu. · Damu ya Yesu ina thamani kubwa kuliko damu yoyote kwa kuwa pia UHAI wa Mungu una thamani kuliko uhai wowote! Tunaamini haya machache tuliyoyaandika juu ya Damu ya Yesu yamekupa changamoto ya kukuchochea utake kuijua zaidi Damu ya Yesu na kuitumia. Tuzidi kuombeana. Ni sisi katika utumishi wa Kristo, Christopher na Diana Mwakasege |
|