Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Aprili 2004                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


YESU ALILIPA GHARAMA KUBWA MNO MSALABANI
KWA WEWE KUENDELEA KUBAKI KUWA MASKINI

Salamu katika Jina la Yesu Kristo. Tunamshukuru Mungu sana kwa ajili yako, kwa jinsi ambavyo amekupa neema yake, na ukapata nafasi hii ya kuisoma hii barua yetu kwako. Tunasema ni neema tu ya Mungu, kwa kuwa siku hizi watu wana shughuli nyingi sana kiasi ambacho kwa wengine si rahisi kupata muda hata wa kusoma barua zinazohusu maneno ya Mungu.

          Pamoja na kwamba hatukuoni kwa macho, faraja tuliyonao ni kule kujua ya kuwa “mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa; wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia….” (Isaya 59:1). Tunaamini uaminifu wa Mungu umekuwa ukikutunza usiku na mchana hata ukaifikia siku hii ya leo.

Gharama ya Yesu Kusulubiwa Msalabani

          Yesu alipoamua kuuchukua msalaba na kusulubiwa alikuwa anafanya uamuzi uliokuwa na gharama kubwa sana kwake binafsi. Kwa sababu hiyo tutakuwa hatumtendei haki kama tutaendelea kuchukuliana na hali zile zile zilizomfanya asulubiwe msalabani kwa ajili yetu.

          Biblia inatuambia ya kuwa “Alidharauliwa na kukataliwa na watu, mtu wa huzuni nyingi……alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu….alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu” (Isaya 53:3,4,5).

          Tena tunaambiwa ya kuwa “….uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu ye yote, na umbo lake zaidi ya wanadamu”. (Isaya 52:14)

          Mtume Paulo alipowaandikia Wagalatia alisema, “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, amealaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti….” (Wagalatia 3:13).

            Wafilipi 2:6-8 inatuambia hivi juu ya habari za Yesu ya kuwa; “…yeye  mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”

Yesu alisulubiwa pia kwa sababu ya umaskini wetu

          Si watu wengi wanafahamu ya kuwa jambo mojawapo lililomfanya Yesu Kristo afe msalabani ni umaskini wetu. Wengi wanajua ya kuwa Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, na kwamba alipigwa kwa ajili ya magonjwa yetu. Lakini wengine hawajui  ya kuwa Yesu Kristo alikufa kwa ajili ya umaskini wetu, ili tutoke kwenye umaskini tuwe matajiri.

          Imeandikwa katika 2 Wakorintho 8:9 ya kuwa; “ Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.”

          Yesu alichukua dhambi zetu ili sisi tupokee utakatifu wake; alichukua masikitiko na huzuni zetu ili sisi tupokee furaha yake; alichukua udhaifu wetu ili sisi tupokee nguvu zake; alichukua magonjwa yetu, ili sisi tupokee afya yetu; alichukua mauti yetu, ili sisi tupokee uzima wake; na alichukua umaskini wetu ili sisi tupokee utajiri wake.

          Yesu Kristo kwa kufa msalabani alilipa gharama kubwa mno kwa sisi kuendelea kuwa maskini. Kwa lugha nyingine ni kwamba hakukuwa na sababu ya Yesu Kristo kufa msalabani kama hatutaki kutoka kwenye umaskini.

Ikiwa Mungu hataki uwe maskini
na wewe usitake uwe maskini!

          Ikiwa Mungu hataki uwe maskini na wewe usitake uwe maskini! Mungu hapendi tuwe maskini kiasi ambacho alimtoa mwana wake wa pekee Yesu Kristo ili kila amwaminiye na kumtegemea asiwe maskini tena, ila awe na utajiri wake!

          Milango ya gereza la umaskini limefunguka ila ni wachache wanajua; wengine wanajua lakini hawako tayari kutoka; na wachache wanaojua wameshindwa kutoka kwa sababu:

(i)                 Wamekata tamaa. Hali ya maisha waliyonayo ni duni sana na inakatisha tamaa. Kwa hiyo wanajikuta mara kwa mara wanasema ‘hawawezi’ kuwa matajiri. Na wakisema hivyo hawajui wanasema kinyume na Wafilipi 4:13 inayosema; “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”. Lakini pia hawajui ya kuwa wanaposema hawawezi wanazuia akili zao zisifikiri juu utatuzi wa jambo hilo!

(ii)               Wanaona hali zao za maisha hayo duni ni matokeo ya wao kuonewa na matajiri. Kwa hiyo wanajikuta wananung’unika na kulaumu. Lakini hawajui ya kuwa kutokana na Yakobo 5:9 wanajikuta wameingia kwenye hukumu au kubaguliwa. Au wanajikuta wamekaa katika hali ambayo hawaoni tena fursa (opportunities) za kuwafanya waondokane na hiyo hali ya uduni wa kimaskini.

Amua kutokuwa maskini!

          Hili ndilo tunalokuhimiza katika barua hii. Amua kutokuwa maskini! Maana Yesu alilipa gharama kubwa sana pale msalabani kwa wewe kuendelea kuwa maskini.

          Ni kweli Yesu alisema “sikuzote mnao maskini pamoja nanyi” (Mathayo 26:11); lakini hakuwa ana maana ya wewe uwe mmoja ya hao maskini watakaokuwepo! Kwa hiyo amua kutokuwa maskini na chagua kuwa tajiri katika Kristo!

          Roho Mtakatifu ametumwa kwetu kama msaidizi kufuatana na Yohana 14:26 – kwa hiyo anasubiri uamuzi wako ili akupe msaada wa kutoka kwenye umaskini na kukuingiza kwenye utajiri. “Maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri ….” (Kumbukumbu ya Torati 8:18)

          Wengine wameshindwa kuamua kutokuwa maskini kwa sababu

(i)                 Au, wamejenga undugu na umaskini kutokana na mafundisho potofu waliojifunza;

(ii)               Au, hawajui wakiamua kutokuwa maskini watatokaje;

(iii)              Au, umaskini umewasonga mno tena kwa muda mrefu kiasi ambacho wameupokea kama sehemu yao ya maisha. Hata maombi wala mafundisho hayawasaidii tena mpaka wapate ushauri mzuri ili waweze kujitenga kimawazo mbali na umaskini ili waweze kuukataa na kuuchukia umaskini.

Mwisho

          Tunaamini utatumia busara ya Mungu aliyokupa kufikia uamuzi wa kuukataa uamskini, ili kufa kwa Yesu Msalabani kusiwe ni bure kwa upande wako. Tuombeane.
 

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.