Salamu za
Krismas
KRISMASI HII JIFUNZE JAMBO TOKA KWA MARIAMU
Salamu katika Jina
la Yesu.
Kila wakati
tunaposoma habari za mambo mbalimbali yaliyotokea Yesu alipozaliwa huwa
tunapata jambo au mambo ya kujifunza. Katika mwezi huu wa Disemba, hata
wale ambao si wakristo wanafuatilia kwa karibu sherehe zinazoambatana na
kuzaliwa kwa Yesu; bila kutafakari kwa undani juu ya ujumbe unaopatikana
wakati tunapokumbuka kuzaliwa kwa Yesu.
Kwa mwaka huu
tunataka tujifunze alichofanya Mariamu alipoambiwa juu ya kuzaliwa kwa
Yesu duniani.
Mungu alimtuma
Malaika Gabrieli kwa Mariamu kusema hivi: “Tazama, utachukua mimba
na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu” (Luka 1:31).
Hili lilikuwa neno
la ahadi kwa Mariamu toka kwa Mungu. Mariamu akataka kujua jambo hili
litatokeaje katika maisha yake; naye akamuuliza malaika, “Litakuwaje
neno hili, maana sijui mume?” (Luka 1:34)
Malaika Gabrieli
akamweleza Mariamu jinsi ambavyo nguvu za au upako wa Roho Mtakatifu
utakavyohusika katika kuifanya hiyo ahadi ya Mungu ya kuzaliwa kwa Yesu
katika maisha yake itakavyodhihirika katika maisha yake. Malaika
Gabrieli akamwambia, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu
zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho
kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu” (Luka 1:35)
Mariamu aliposikia
hayo alisema hivi: “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu
kama ulivyosema” (Luka 1:38)
Hakuna neno
lisilowezekana
kwa Mungu
Kabla Mariamu
hajajibu alivyojibu, Malaika Gabrieli alimwambia ya kuwa; “…. Hakuna
neno lisilowezekana kwa Mungu” (Luka 1: 37)
Mariamu aliambiwa
hivi kwa sababu ndani ya moyo wake alikuwa anajiuliza kama jambo hilo
linawezekana. Alijiuliza jambo hilo kwa sababu kibinadamu alikuwa ni
bikira – hamjui mume kwa hiyo isingekuwa rahisi kupata mtoto!
Unaona kabisa ya
kuwa alikuwa anatafakari juu ya upatikanaji wa ahadi au neno la Mungu
kwake kwa jinsi ya kibinadamu. Katika kutafakari huko akagundua ya kuwa
jambo hilo haliwezekani!
Hii ndio sababu
iliyomfanya Malaika Gabrieli atoe ushuhuda kwanza juu jambo kama hilo
lilivyotokea kwa Elizabeti aliyekuwa jamaa ya Mariamu ya Karibu. Na
baada ya ushuhuda huo akasema yametokea hayo kwa Elizabeti; kwa kuwa
hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu (Luka 1:37)
Kwa kusema maneno
hayo alitaka Mariamu pia alitazame jambo la kuipata ahadi yake ya
kuzaliwa kwa Yesu – ya kuwa litafanyika kwa msaada wa Mungu vile vile.
Alitakiwa aone na akubali ya kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.
Mariamu
alipotambua hivyo akasema; “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe
kwangu kama ulivyosema”. Nasi tunajua alipokea alichosema, maana
baada ya miezi tisa, alizaa mtoto mwanamume, na jina lake akamwita Yesu.
Inawezekana
Krismasi hii imekukuta katika hali ya subira – ukisubiri ahadi ya Mungu
itimie kwako; - na inawezekana imechukua muda mrefu kutimia kwako.
Sisi tunataka
tukuulize hivi; je! Umewahi kusema kama Mariamu alivyosema ya kuwa
“na iwe kwangu kama ahadi ya Mungu inavyosema”?
Inawezekana
unasita kusema namna hii kwa sababu unajaribu kufikiri ni kwa namna gani
ahadi hiyo itatimia – na ukitafakari kibinadamu unaona haliwezekani
kabisa.
Kumbuka hata
Mariamu alifika mahali pa kuwaza namna hii. Kibinadamu ahadi aliyopewa
isingewezekana kutimia.
Inawezekana
unaumwa ugonjwa ambao kidaktari inaonekana huwezi kupona – lakini
kumbuka ahadi ya Mungu juu ya uponyaji. Mungu atakuponya! Kwa nini? Kwa
kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu! Ni neno gani hilo
lisilowezekana kwa Mungu? Ni neno lile la ahadi alilolisema katika
biblia juu ya kutuponya magonjwa. Kwa mfano Marko 16:17,18; Mathayo
8:16,17, Kutoka 15:26; 1Petro 2:24.
Tunazungumza juu
ya uponyaji kama mfano mmoja wapo tu. Lakini eneo lolote lile ambalo
kibinadamu ni vigumu kuona ni kwa namna gani ahadi ya Mungu inaweza
kutimia – linaweza kutazamwa kwa namna hii. Kwa nini? Kwa kuwa hakuna
neno lisilowezekana kwa Mungu!
Kama unaona tatizo
kuamini hivi tafakari shuhuda mbalimbali Krismasi hii, zile ambazo
zinaonyesha jinsi ambavyo Mungu amefanikisha jambo kama hilo hilo
unalotaka lifanikiwe kwako. Kama hakuna shuhuda zo zote unazozijua –
tafakari zilizomo katika biblia!
Tunaamini mwishoni
utakubaliana na Malaika Gabrieli ya kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa
Mungu. Na ukifikia mawazo haya ndani yako ni rahisi kwako kusema kama
Mariamu alivyosema ya kuwa “….. na iwe kwangu kama ulivyosema”
Kupokea ahadi za
Mungu kuna
gharama zake – je uko
tayari kuzilipa?
Mariamu alipoamua
kuipokea ahadi ya kuzaliwa kwa Yesu katika maisha yake alijua gharama
ambazo zilikuwa zimeambatana na uamuzi huo; na alikuwa tayari kuzilipa.
Kuna gharama
kadhaa ambazo Mariamu alikuwa tayari kuzilipa ili tu aipate ahadi ya
Mungu katika maisha yake.
Kwa mfano: Alikuwa
tayari kulipokea neno aliloahidiwa pamoja na kwamba ubikira wake
ungeharibika na angekupata uja uzito nje ya ndoa! Gharama ya matukio
haya kwa msichana wakati huo ilikuwa kubwa – kwake mwenyewe na kwa ndugu
na marafiki zake!
Lakini Mariamu
akijua hilo bado alikubali kuipokea ahadi ya Mungu na neno la ahadi hiyo
lijidhihirishe katika maisha yake.
·
Alikuwa tayari kumkosa mume wake mtarajiwa lakini alipate neno
aliloahidiwa!
·
Alikuwa tayari kuharibu uhusiano wake na wazazi wake, ili mradi aipate
ahadi aliyoahidiwa.
·
Alikuwa tayari kuharibu usichana wake na kuhama rika toka kwenye
usichana kwenda kwenye umama. Kikawaida unapohama rika moja kwenda rika
jingine hata marafiki wanabadilika! Lakini pamoja na hayo yote Mariamu
alikuwa tayari kula gharama hiyo ili aipate ahadi ya Mungu iliyokuwa
imesemwa kwa ajili yako.
Je! Wewe uko
tayari kula gharama ya kiasi gani ili tu ahadi ya neno la Mungu litimie
katika maisha yako?
Krisimas hii
usitafakari tu baraka inayokuja kwa Yesu kuzaliwa katika maisha yako, na
neno lake kudhihirishwa kwako; lakini pia tafakari gharama
zinazoambatana na udhihirisho huo.
Tunakutakia
sherehe njema. Tuzidi kuombeana.