|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Salamu katika Jina la Yesu Kristo, Waefeso 6:11,18 inasema: “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za shetani … kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote” · Neno hili “kwa sala zote” lina maana ya “kwa aina zote za sala na maombi”. Kujua aina zote za sala na maombi ni mojawapo ya SILAHA za mkristo dhidi ya shetani. Soma Waefeso 6:11-20. · Kujua aina moja tu au chache za sala na maombi kumefanya wakristo wengi washindwe katika mashindano yao na shetani. Na pia kuomba maombi ambayo si silaha yanafanya shetani asiachie anachong’ang’ania – kwa hiyo anazidi kukuzuia usikipate. · Sala na maombi yanayozungumzwa hapa ni yale ambayo ni silaha mdomoni mwa mwombaji ya kumsaidia katika mashindano yake na shetani anayezuia mapenzi ya Mungu yasifanyike mahali ambapo Mungu anataka yafanyike. · “Vaeni silaha zote za Mungu” ina maana ni silaha ambazo Mungu anampa mtu na siyo mtu anayejitafutia hizo silaha. Kwa hiyo ikiwa maombi ni silaha ina maana ni maombi ambayo chanzo chake ni Mungu, na Mungu anampa mtu ili aombe. Na maombi hayo Mungu atayatumia kumpiga nayo ibilisi ili upinzani dhidi ya mapenzi ya Mungu uondoke. · Kwa nini Mungu anataka tuombe juu ya vitu ambavyo anajua tunahaja navyo? Si atupe tu? Kinachomzuia ni hiki: Mtu ni nafsi huru aliyepewa dunia aitawale, lakini kwa kutenda dhambi, shetani alichukua nafasi hiyo ya kuitawala dunia. Kwa hiyo hadi hapo ‘muhula wa shetani’ (Mathayo 8:28,29) utakapokwisha, Mungu akitaka kufanya mapenzi yake hapa duniani inabidi apate mtu ambaye atamfahamisha mapenzi yake ili aombe ndipo Mungu ashuke kuyafanya. AINA MOJAWAPO YA MAOMBI HAYA NI: Maombi ya kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu “Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba”(1Yohana 5:14,15) Mambo yafuatayo yapo katika aina hii ya maombi na yatakuwa ndani yako hata kabla ya kuomba:
1. Ujasiri mbele za Mungu Kutokuwa na hofu ya kwenda mbele za Mungu kuomba jambo unalotaka kuomba kwa nini? Kwa sababu: Mungu ndiye aliyekukaribisha kuomba juu ya jambo ambalo ni mapenzi yake juu ya jambo analotaka uliombe. Kinachomfanya Mungu akukaribishe ni damu ya agano iliyomwagika inayotupa ushirika na Mungu kwa njia ya maombi katika kuyatimiza mapenzi yake hapa duniani (Waebrania 10:19-23) 2. Kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu Ujue mapenzi ya Mungu juu ya jambo unaloomba kabla hujaliombea. Imeandikwa katika Waebrania 10:23 “maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu….” Unakwenda patakatifu pa Mungu kuomba huku ukijua alichoahidi kufanya katika kile unachokwenda kuomba. Kwa hiyo mapenzi ya Mungu = ahadi ya Mungu itakayokupa (i) ngao ya Imani (ii) upanga wa Roho (iii) maombi mdomoni (Waefeso 6:17-18). 3. Uhakika wa kusikilizwa maombi: Unakuwa na uhakika wa maombi yako kusikilizwa kwa sababu: (i) Mungu ndiye aliyekukaribisha au aliyekupa mzigo huo wa kuomba (ii) Mungu ndiye aliyekupa jambo la kuombea huku ukijua anachokwenda kukujibu au kukupa 4. Uhakika wa kupokea ulichokwenda kuomba: Unakuwa na uhakika wa kupokea utakachoomba kwa sababu: “ Yeye aliyeahidi ni mwaminifu” (Waebrania 10:23) hawezi kusema uongo (Hesabu 23:19). Kwa hiyo hata kama jibu linachelewa kutokea katika ulimwengu wa kimwili pokea katika moyo wako na usibadili usemi wako. Bali endelea kushukuru juu ya jibu hilo (Marko 11:24, Waebrania 10:23). Wafilipi 4:6 -7 anasema “msijisumbue kwa neno…..” – ukipewa ahadi usijisumbue nayo ‘don’t try to work your own way’, lakini kwa kila neno au kwa kila ahadi, omba na kushukuru. Huwezi ukaenda na ahadi ya Mungu juu ya jambo unalohitaji katika maombi na usipate amani ya Mungu. Ukijaribu kuilazimisha ahadi itokee – unakosa amani – ikiwa ni njia ya Roho Mtakatifu kukuambia sivyo inavyotakiwa! Kwa sababu kabla ya mapenzi ya Mungu kutimizwa hapa duniani kama huko mbinguni, ni lazima kwanza ufalme wake ukaribishwe kwanza, ili Mfalme aje atekeleze mapenzi yake hapo yanapohitajika. KUMBUKA! Haya ni maombi ambayo Mungu anakupa ili kukusaidia katika vita. Katika mazingira ya kivita usijaribu kumwomba Mungu kitu kwa ajili ya kutekeleza matakwa yako au ili kutimiza mapenzi yako: Ukiomba nje ya mapenzi ya Mungu, mambo mawili yanaweza kutokea: (i) Mungu kutokukupa ulichoomba (Yakobo 4:2-3) (ii) Mungu kukupa unachotaka lakini ukakonda kiroho (Zaburi 106:13-15) na hata wakati mwingine kufa kiroho (Hesabu 11:4-6-34) MIFANO ya kuomba maombi sawasawa na mapenzi ya Mungu! Mfano No. 1. Daniel 9:1-3, 17,18 – akiomba juu kurudishwa wana wa Israeli Yerusalemu · Kabla ya kuingia katika maombi hayo ilibidi lazima awe na mambo manne yaliyotajwa hapo juu kabla ya kuingia katika maombi. Aliyapataje? “Kwa kuvisoma vitabu” akapata ufahamu (Daniel 9:1-3,17,18). Alisoma vitabu vipi? Alisoma vitabu hivi: Yeremia 25:11,12, 2 Nyakati 36:21-23, Ezra 1:1-5, Yeremia 29:10 – 14. · Pamoja na kwamba ilikuwa ni mapenzi ya Mungu ya kuwa baada ya miaka sabini awarudishe wana wa Israeli nchini mwao na kuujenga Yerusalemu – lakini alitaka waombe au wamwombe kwanza: Soma pia Ezekieli 36:33-37 anaposema “nitaulizwa” au “nitaombwa” · Baada ya Danieli “kuvisoma vitabu” hivi na kupata ufahamu – ilikuwa ni mwaliko wa Mungu kwa Danieli ili aombe sawasawa na mapenzi au ahadi ya Mungu. Danieli alipoomba mara ya kwanza katika sura ya 9 hakujibiwa maombi yake ila alipewa ufahamu zaidi juu ya mtiririko wa miaka sabini au majuma sabini yaliyokuwa yameamuliwa juu ya wana wa Israeli. Katika sura ya 10 anaonyeshwa maono ya vitu na akapata ufahamu ya kuwa ili mapenzi ya Mungu juu ya watu wake yatimizwe lazima aombe ili shetani asizuie kutimizwa kwa ahadi au mapenzi ya Mungu. Mfano No. 2. Simeoni aliomba juu ya kuzaliwa kwa Yesu duniani. Luka 2:22 – 35. · Kabla ya kuingia katika maombi hayo ilibidi kwanza ndani yake awe na mambo manne yanayotakiwa ukitaka kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu. Aliyapataje? Kwa kuonywa na Roho Mtakatifu aliyekuwa juu yake (Luka 2:22- 26 – 35). “Ameonywa” = “Ameangalizwa”. · Kwa kule kufanya maombi ya shukrani baada ya kumwona Yesu hekaluni, huku akisema “sasa Bwana, wamruhusu mtumishi wako”; inaonyesha wazi ya kuwa Simeoni alikuwa anaomba ‘aondoke’ au ‘afe’ lakini hakuruhusiwa. Kwa nini? Ni ili akae katika maombi kwa ajili ya kuzaliwa kwa Yesu ili shetani asije akazuia kutimizwa mapenzi ya Mungu au ahadi ya Mungu juu ya kuzaliwa kwa Yesu duniani! Mfano No. 3. Yesu akimwombea Petro akiongoka awaimarishe ndugu zake (Luka 22:31 – 24) · Ili Yesu aweze kumwombea Petro sawasawa na mapenzi ya Mungu ilibidi ndani yake awe na mambo manne yanayotakiwa ndani ya mtu yeyote anayetaka kuomba maombi ya namna hii. Aliyapataje? Kwa kusikia toka kwa Baba yake – Yohana 5:19. Maana angejuaje ya kuwa shetani ‘amepewa kibali’ cha kuwajaribu/kuwapepeta kama ngano. Kwa nini shetani aliomba awapepete wanafunzi wa Yesu? Ili mapenzi ya Mungu yasitimizwe baada ya Yesu kufa na kufufuka na kupaa – kusiwepo wa kuendeleza kazi alizoanza Yesu kuzifanya. · Kujua huku ndiko kulikompa Yesu ujasiri wa kuwaombea (Yohana 17:15) na kumwombea Petro ili shetani asifanikiwe. Mfano No. 4. Anania akimwombea Sauli/Paulo ili apate kuona (Matendo ya Mitume 9:17-19). · Ili Anania aweze kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu ilibidi ndani yake kuwe na mambo manne anayotakiwa mtu awe nayo kabla ya kuomba maombi ya namna hii. Aliyapataje? Kwa njia ya maono wakati Yesu alipomtokea (Matendo 9:10-19) · Shetani alitaka kumzuia Paulo asifanye mapenzi ya Mungu kwa kumfanya kipofu (Matendo 9:1-9). Ilibidi apate kuona, kabla ya kuanza kuutumia wito aliopewa. · Anania aliomba juu ya Paulo sawasawa na mapenzi ya Mungu, na ndipo Paulo alipoweza kuendelea na kile alichotakiwa na Yesu kufanya akiwa mjini Dameski. Kumbuka: · Mungu atatumia njia mbalimbali kukujulisha mapenzi yake juu ya jambo analotaka uliombee – lakini si nje ya neno lake. · Aina hii ya maombi ni pale upinzani wa shetani unapokuwepo dhidi ya mapenzi ya Mungu. · Unawezaje kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu bila kuyajua mapenzi ya Mungu juu ya jambo unalotaka kuliombea? Kwa kuomba kwa lugha mpya au kwa kunena kwa lugha kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Soma 1 Wakorintho 14:2 na Warumi 8:26,27. Tuzidi kuombeana. Ni sisi katika utumishi wa Kristo, Christopher na Diana Mwakasege |
|