|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Mpendwa katika Kristo, Salamu tunakupa ni katika jina lile lipitalo majina yote – Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Maisha ya mtu ni matunda ya maamuzi ya mtu mwenyewe binafsi, lakini pia yanaweza yakawa yamechanganyika na maamuzi ya watu wengine yanayogusa maisha yake. Wanadamu tunafanya maamuzi mengi sana kila siku – lakini bila tahadhari ya madhara yake kwa sasa na kwa baadaye; na madhara yake kwetu na kwa watu wengine. Nabii Yoeli aliwahi kuonyeshwa maono ya jambo hili aliposema hivi katika Yoeli 2:14
“Makutano makubwa,
makutano makubwa, wamo Kwa tafsiri nyingine alikuwa anasema ameona makusanyiko au mkutano mkubwa wa watu katika bonde wakifanya maamuzi mbalimbali. Nabii Yoeli aliona nini? Nabii Yoeli aliona mkusanyiko wa watu wakiwa katika bonde au katika dunia. Tunalitafsiri bonde hili analolisema ya kuwa anazungumza habari ya dunia kwa sababu kabla mtu hajazaliwa hana uwezo wa kuamua lolote; na baada ya kufa mtu hana uwezo wa kuamua lolote. Kwa hiyo huo mkusanyiko mkubwa wa watu aliouona ulikuwa umekusanyika katika ‘bonde’ au katika dunia hii. Tukiwa hapa duniani wanadamu tuna uwezo wa kufanya maamuzi, na tena maamuzi mengi sana. Maisha ya mtu ni matokeo ya maamuzi mbalimbali – ya kwake na ya watu wengine. Tena maisha ya kila siku ni mtiririko wa maamuzi mbalimbali yanayofanyika na watu mbalimbali. Kwa mantiki hii jambo la kufanya maamuzi sio la kulifanyia mzaha wala uzembe; wala si jambo tunalotakiwa kulifanya kwa mazoea tu. Tumeona tukuandikie amri 10 ambazo ukizifuata zitakusaidia uweze kufanya maamuzi vizuri na yaliyo mazuri. Amri ya 1 Usijisumbue wala kuhangaika katika kufanya uamuzi wowote! Kuna maamuzi mengi ambayo huwa yanaambatana na mahangaiko na usumbufu mwingi ndani ya moyo wa mtu. Lakini maamuzi mengine huwa hayana mahangaiko wala usumbufu; na kwa sababu hiyo unajikuta unayafanya kirahisi. Usije ukaingia kwenye mtego wa kuona maamuzi yaliyo magumu ndiyo ya kumshirikisha Mungu, na yale yaliyo mepesi ndiyo unayoyaamua bila kumshirikisha Mungu. Neno la Mungu linatushauri hivi:
“Msijisumbue
kwa neno lolote; bali katika Yesu Kristo aliwahi kusema hivi: “…..pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote” (Yohana 15:5). Hii ina maana ni pamoja na kufanya maamuzi! Hatuwezi kufanya maamuzi mazuri bila msaada na uongozi wa Bwana Yesu. Ndiyo maana tunaambiwa hivi: “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu” (1Petro 5:6,7). Hebu linganisha maneno hayo na haya ya Mithali 3:5,6 yanayosema hivi: “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe: katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyoosha mapito yako”. Ukijua haya utajizoeza kumwomba Mungu kila siku ili aongoze maisha yako, ambapo hasa utakuwa una maana ya kwamba unataka aongoze maamuzi yako. Kumbuka maisha ni mtiririko wa maamuzi ya mtu na ya watu wengine. Amri ya 2
Acha amani ya
Kristo iamue ndani yako juu ya jambo halafu wewe fuata Katika Wafilipi 4:7 neno la Mungu linasema hivi “ Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu” Hii sentensi imeanza na maneno haya: “Na amani ya Mungu…..”. Kwa kuanza na neno ‘na’ inaonyesha ya kwamba kuna jambo linalofanyika kwanza kabla ya amani ya Mungu kujidhihirisha ndani ya mtu. Jambo hili tunalipata katika Wafilipi 4:6 anaposema: “Msijisumbue kwa neno lo lote, bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru haja zenu na zijulikane na Mungu”. Watu wa Mungu walio wengi “wanajisumbua” kwanza juu ya jambo na wakiona hawafanikiwi ndipo wanapoomba. Lakini Wafilipi 4:6 inatushauri ‘tusijisumbue katika jambo lo lote kwanza’! Tunatakiwa tujizoeze kuomba au kumkabidhi Mungu mambo yetu yote. Haijalishi ikiwa jambo ulilonalo unaliona ni dogo au ni kubwa, au ni la kawaida, - yote tunatakiwa kumshirikisha Mungu katika sala zetu, maombi yetu na katika shukrani zetu kwake. Tukifanya hivi au tukiishi kwa namna hii ndipo: “Na amani ya Mungu ipitayo akili zote”, itatuhifadhi mioyo yetu na nia zetu (makusudi, au malengo na mipango) yetu katika Kristo Yesu. Ndiyo maana katika Wakolosai 3:15 tunaambiwa hivi: “ Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu, ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani” Hii ina maana usiamue jambo kabla amani ya Kristo haijaamua! Iache amani ya Kristo iamue, halafu wewe fuata kile ambacho amani ya Kristo imeamua. Unaweza ukatuuliza utajuaje kama amani ya Kristo imeamua. Ukikosa amani ndani yako ina maana amani ya Kristo haikubaliani na hilo jambo unaloliombea au unalolitafakari. Ikiwa unapata amani ndani yako ina maana amani ya Kristo inakubaliana na hilo jambo unaloliombea au unalolitafakari.
Amri ya 3
Usinie makuu
kupita imani uliyonayo maana maamuzi yako na utekelezaji Ushauri huu tunaupata katika kitabu cha Warumi 12:3 tunaposoma ya kuwa: “ Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani” Kwa lugha nyepesi tunaambiwa tusijaribu kuamua kufanya jambo ambalo ni juu ya imani tuliyonayo, au lililo kubwa kuliko uwezo wa imani tuliyonayo kulibeba, – bali tulifanye “…..kwa kadri ya imani” (Warumi 12:6). Ikiwa tunatakiwa kuishi kwa imani (Warumi 1:17, Wagalatia 2:20) na siyo kwa kubahatisha, maana yake vile vile tunatakiwa kufanya maamuzi yetu kwa imani na sio kwa kubahatisha. Kumbuka maisha yetu ya kila siku ni matokeo ya maamuzi yetu wenyewe na ya watu wengine. Maamuzi ya kubahatisha yanazaa maisha ya kubahatisha vilevile. Ikiwa tunatakiwa kuenenda kwa imani ( 2 Wakorintho 5:7) na siyo kwa kuona, maana yake vile vile tunatakiwa kuenenda katika maamuzi yetu kwa imani hiyo hiyo. Ikiwa “…..aaminiye hatafanya haraka” (Isaya 28:16) – basi inabidi maamuzi yake pia asiyafanye ‘kwa haraka’ kiasi ambacho anakuwa hana uhakika na alichoamua. Hii ni kwa sababu, “Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Waebrania 11:1). Unahitaji imani kwa ajili ya maamuzi yako kwa sababu Mungu anaweza kukuongoza kuamua jambo ambalo kibinadamu haliwezekani au ni kubwa kuliko uwezo wako kulitekeleza. Amri ya 4 Usifanya Maamuzi kwa Mazoea tu , bali jifunze kumtegemea Roho Mtakatifu. Ni rahisi sana kwa watu wengi kufanya maamuzi yao ya kila siku kimazoea maana ndivyo walivyozeoa au ndivyo walivyozoeshwa. Lakini mtu anapokuwa ndani ya Kristo, biblia inatuambia amekuwa “kiumbe kipya” (2 Wakorintho 5:17); na maisha yake ni mapya. Ikiwa maisha ni mapya maana yake na mfumo wake wa kufanya maamuzi na kuenenda kila siku ni mpya pia. Kwa nini? “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti” (Warumi 8:2). Kwa nini? “Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu” (Warumi 8:14) Kwa nini? “ Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia Aba, yaani, Baba” (Warumi 8:15). Tunaambiwa pia katika Wagalatia 5:16,17 ya kuwa: “….enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka” Tatizo ni kwamba pamoja na watu wengi kujua umuhimu wa kuongozwa na Roho wa Mungu bado hawajui huyu Roho wa Mungu anaongozaje mtu! Kwa mfano utajuaje ikiwa katika jambo unalofanya au unalotaka kufanya, ni Roho wa Mungu anayekuongoza? Biblia inatuonyesha njia kadhaa ambazo Roho wa Mungu anazitumia kuongoza watu. Mojawapo ni hii – utasikia ndani yako uhuru au utasikia ndani yako kufungika! Ukisikia uhuru au uko huru kufanya jambo hilo au unapolifanya jambo hilo – ujue Roho Mtakatifu anataka ulifanye. Ikiwa utasikia au unasikia kufungika kufanya jambo unalolifanya ujue Roho Mtakatifu anakuongoza usilifanye au usiendelee kulifanya. Kwa nini iwe hivi? “ Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru……” (Warumi 8:2). ‘Sheria’ maana yake ‘utaratibu’. Kwa hiyo ‘sheria ya Roho wa Uzima’ maana yake utaratibu wa Roho wa uzima. Kwa tafsiri nyepesi maana yake utaratibu wa Roho wa uzima ukikuongoza katika jambo ‘unakuacha huru’ ulifanye hilo jambo. Unajisikia huru kulifanya! Ikiwa Roho hakubaliani na hilo unalolifanya au unalotaka kulifanya hatakuacha huru ulifanye – maana yake utasikia kufungika na unasikia hofu! Kwa nini iwe hivi? “Kwa kuwa hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu ….” (Warumi 8:15). Tena imeandikwa hivi: “ Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria” (Wagalatia 5:18). Hampo chini ya sheria maana yake hamfanyi lo lote kwa kulazimishwa ila kwa upendo wa Kristo ulio ndani yetu unaotufanya tuwe huru kufanya tunachotakiwa kukifanya tukiongozwa na Roho wa Mungu. Kwa mantiki hii tunasema usifanye maamuzi yoyote kwa mazoea tu – bali jifunze kuongozwa na Roho Mtakatifu – hutazitimiza kamwe tamaa za mwili. Itakuwa rahisi kwako kufanya maamuzi yako yote sawa sawa na mapenzi ya Mungu juu yako. Ujumbe huu tutaendelea nao mwezi ujao. Tunaomba usikose kuisoma barua yetu ya mwezi ujao maana ndani yake tunataweka amri zilizobaki sita za kukusaidia katika maamuzi yako. Tuzidi kuombeana. Ni sisi katika utumishi wa Kristo, Christopher na Diana Mwakasege |
|