|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Neema hii ya Mungu ambayo ndiyo inayotuwezesha kuwasiliana na wewe kwa njia hii ya barua – iwe pamoja nawe unaposoma ujumbe uliomo humu. Salamu zetu zinakujia katika Jina la Yesu Kristo, tukiamini ya kuwa unaendelea kusonga mbele na kukua katika kumjua Yesu Kristo. Mwezi huu Roho Mtakatifu ameweka ndani ya mioyo yetu kukuandikia angalau kwa kifupi juu ya kile unachotakiwa kukifanya unaposongwa na majaribu. Inawezekana huna jaribu lolote lililokusonga kwa sasa, lakini tunza ujumbe huu kama ‘chakula’ chako utakachokihitaji katika safari yako ya maisha hapa duniani. Kwa nini tunakushauri hivi? Ni kwa sababu tunaamini kila mtu kwa wakati wake huwa anaingia katika majaribu kwa namna moja au nyingine – na kuna wengine ambao hawajajua la kufanya. Majaribu ni nini? Majaribu: · Ni matatizo yanayomkumba mtu na kumfikisha njia panda au mahali pa kujiuliza maswali haya, kwa mfano; kama Mungu yuko pamoja naye au la! · Ni matatizo yanayomkumba mtu na kumfikisha njia panda – mahali ambapo anajikuta anajiuliza swali kama hili kwa mfano; kama bado aendelee na wokovu au auache! · Ni matatizo yanayomsonga mtu na kumfikisha njia panda – mahali ambapo anajikuta anajiuliza swali kama hili; je, aendelee na utumishi huo, au kikundi hicho, au kanisa hilo, au kamati hiyo, au aache! · Ni matatizo ambayo mtu anakutana nayo na yanamfikisha njia panda na kujikuta katika hali anayojiuliza kwa mfano, ikiwa kama ahadi za Mungu ni za kweli au la. Na wakati mwingine ni jambo ambalo ameliombea kwa muda mrefu bila kupata majibu yake au utatuzi wake, kwa hiyo jambo hili likimfikisha njia panda, mtu huyo anajikuta anajiuliza kama aendelee kuliombea jambo hilo au aache! Si kila tatizo ni Jaribu! Kwa hiyo si kila tatizo unalokutana nalo katika maisha ni jaribu! Maadamu tatizo hilo ulilonalo halijakufikisha ‘njia panda’ au katika hali ya kujiuliza maswali tuliyoorodhesha hapa basi ujue hilo ni tatizo la ‘kawaida’ tu na bado halijawa jaribu! Lakini pia matatizo mengine ambayo sisi kama wanadamu tunayaona yamekuwa jaribu kwetu – kwa Mungu inawezekana haoni hivyo – bali anajua ni adhabu tunayopata kutokana na kutokutii maagizo yake! Kwa mfano ukikisoma Kitabu cha Yona utaona ya kuwa Yona alipata vyote – jaribu na adhabu! Kwa mfano, lile agizo alilopewa Yona la kwenda Ninawi kupeleka ujumbe wa Mungu lilimfikisha njia panda katika maamuzi yake kiasi cha kujiuliza kama aende Ninawi au asiende. Yona akaamua kutokwenda Ninawi na akaanza safari ya kwenda Tarshishi. Kwa nabii Yona agizo la kwenda Ninawi kwake lilikuwa jaribu! Lakini alipokuwa ndani ya meli akielekea Tarshishi, Mungu alituma upepo mbali sana ambao uliamsha mawimbi makubwa yaliyotaka kusababisha ile meli izame. Kukatokea mahangaiko makubwa kwa watu waliokuwa ndani ya meli. Tatizo hilo la upepo ingawa inawezekana hao watu waliliona ni jaribu kwao – maana walijiuliza waendelee na Yona au la – lakini hali hiyo ya upepo ilikuwa ni adhabu kwa Yona kutoka kwa Mungu! Pia, Yona alipokuwa ndani ya tumbo la samaki – hilo halikuwa jaribu kwake bali adhabu kutoka kwa Mungu! Ukisoma Malaki 3:10-12 utaona ya kuwa kuna matatizo yanayotokea katika maisha ya mtu kwa yeye kutokuwa mtoaji wa zaka. Matatizo hayo yanaweza kuwa makubwa na magumu na ya muda mrefu kiasi kwamba yanamfikisha mtu huyu njia panda katika uhusiano wake na Mungu. Kwa mtu huyu hayo matatizo atayaona ni majaribu kwake, lakini ki-biblia hayo si majaribu bali ni adhabu iliyotokana na mtu huyo kutokuwa mtoaji wa zaka! Maswali ya Kujiuliza Ikiwa umo katikati ya majaribu; au umo katikati ya matatizo yanayotaka kugeuka kuwa jaribu; au utakapokumbana na majaribu, jiulize na utafute majibu ya maswali yafuatayo: Je! Yesu yuko wapi wakati huo unapojaribiwa? – ndani ya jaribu? Au nje ya jaribu? Au hujui yuko nje au ndani ya hilo jaribu? Ndani ya Jaribu: Yesu anaweza kuwa pamoja na wewe unapokuwa katika jaribu lakini akanyamaza kimya wala asikusaidie. Je unajua ni kwa nini afanye hivyo? Kwa mfano ukisoma habari hii iliyoko katika Luka 8:22-25 utaona ya kuwa Yesu alikuwemo ndani ya ‘boti’ amelala wakati hali ya bahari ilipokuwa imechafuka na kusababisha wanafunzi wahangaike sana! Kwa nini ‘mwanzo’ wa tatizo la kuchafuka kwa bahari hawakumwamsha? Inaonyesha dhahiri ya kuwa Yesu hakuwa kiongozi wao katika kila eneo la maisha yao! La sivyo tokea mwanzo wa safari wangempa uongozi wa ‘boti’! Lakini hawakumpa kwa kuwa labda waliona hana utaalamu wala uzoefu wa kuendesha ‘boti’. Na hata matatizo ya kuchafuka bahari yalipoanza hawakumwamsha mapema – maana hawakujua kama anaweza kuwa na ufumbuzi wa tatizo walilokuwa nalo. Ndiyo maana Yesu alipokemea upepo na kuituliza bahari wakamaka na kusema wao kwa wao “Ni nani huyu basi hata anaamuru upepo na maji, navyo vyamtii?” (Luka 8:25) Sisi tunakushauri uumpe Yesu uongozi wa kila eneo la maisha yako ili akuongoze na kukupigania. Wanafunzi hawakumjua Yesu vizuri katika mapana ya uweza wake. Wewe usikwame kama walivyokwama wao, bali soma neno la Mungu mara kwa mara ili umjue na kumfahamu Yesu uliyenaye, huku ukiwa umekwisha umpa uongozi wa kila eneo la maisha yako. Ili utakapojikuta umo ndani ya jaribu ‘asilale usingizi’ bali awe wa kwanza kukupigania na wewe ukifuata maelekezo yake namna ya kushinda au kutoka katika hilo jaribu. Nje ya Jaribu: Kuna wakati unaweza ukajikuta umo katikati ya jaribu ukijua kabisa ya kuwa Yesu hayuko pamoja na wewe katika hilo jaribu.Lakini pia wewe unaweza ukafikiri Yesu yuko pamoja na wewe ila amenyamaza wakati kwa kweli hayuko pamoja na wewe – yuko nje ya jaribu! Kwa mfano, ukisoma habari hii iliyopo katika kitabu cha Mathayo 14:22-33 utaona ya kuwa hawa wanafunzi walijikuta wamekubwa na machafuko wakiwa ndani ya ‘boti’ wakati Yesu hayumo humo. Walikuwa wameamua kusafiri bila Yesu. Tatizo lilipotokea hawakuwa na wa kuwasaidia hadi hapo Yesu alipowaona na kuwafuata na kuwasaidia. Na wewe usifanye kosa kama hili la kutaka kumwita Yesu wakati una matatizo tu – lakini ni bora ukampa Yesu nafasi katika maisha yako, kiasi ambacho huanzi kufanya chochote bila Yeye kuwepo. Kumbuka Yesu mwenyewe alisema katika Yohana 15:5 ya kuwa “…..maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote”. Umewahi kujiuliza kwa nini wanafunzi waliamua kuanza safari ya kuvuka bahari bila Yesu? Kwa nini hawakumsubiri hata kama inaonekana aliwashurutisha kuondoka? Safari zote walikuwa wanasafiri wote, kwa nini wakati huo waliamua kumwacha? Na baada ya kuondoka, walidhani atasafiri na kuvuka bahari kwa namna gani? – maana wakati huo walikuwa hawajui wala hawajawahi kumuona Yesu akitembea juu ya maji. Labda kulitokea kutokuelewana kati yao na Yesu, au waliona anawachelewesha! Je! umewahi kufika hali ya kuona umeliombea jambo muda mrefu kiasi kwamba unaona Mungu anachelewa kujibu kwa hiyo unaamua kuchukua hatua unayochukua bila uongozi wake? Usifanye kosa kama hili, maana biblia inasema. “…….aaminiye hatafanya haraka” (Isaya 28:16), na pia inasema “…bali wamgojeao Bwana watapata nguvu mpya…” (Isaya 40:31). Labda hujui kama Yesu yumo ndani ya jaribu ulilonalo au yuko nje! Ukijikuta katika hali ya namna hii ujue wewe si wa kwanza kukumbana na mazingira kama haya. Kitabu cha Danieli sura ya tatu na mstari wa kwanza hadi wa ishirini na tano kinaeleza habari za akina Abednego, Meshaki na Shadraka. Hawa vijana walijikuta katika mazingira ambayo hawakujua kama Mungu atawasaidia katika tatizo lililokuwa linawakababili. Mfalme Nebukadreza aliwauliza “Ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu?” (Danieli 3:15). Akina Shedraka, Meshaki na Abednego hawakuwa na uhakika na jibu la swali hili, ila wakamwambia huyo mfalme ya kuwa Mungu wao anaweza kuwaokoa akitaka, lakini hata kama hatawaokoa, wako tayari kufa kuliko kuitumikia miungu ya mfalme! Unajua kilichotokea! Mungu hakuwasaidia wasitupwe kwenye tanuru la moto, bali alisubiri watupwe ndani ya tanuru la moto wamkute humo na awatoe bila madhara yo yote. Wakati mwingine usingetamani uingie katika tanuru la majaribu, lakini Mungu anasubiri uingie ndani ya tanuru la majaribu ndipo akujibu na kukutoa bila kudhurika na hayo majaribu! Lengo lake ni kuimarisha imani yako kufuatana na maneno yaliyoandikwa katika kitabu cha Yakobo 1:2-4. Swali lingine la kujiuliza Ikiwa umo katikati ya majaribu; au umo katikati ya matatizo yanayotaka kugeuka kuwa jaribu; au utakapokumbana na majaribu jiulize na utafute pia jibu la swali hili. Je, chanzo cha jaribu ulilonalo ni nini? – Ni Mungu? – au ni shetani? – au ni mwili? Mungu akimjaribu mtu kama ilivyotokea kwa Ibrahimu katika kitabu cha Mwanzo 22:1,2 – si kwa nia ya kumwangusha au kumkwamisha mtu. Bali Mungu akikujaribu ujue ‘anakupima’ au anakupa mtihani ili kupima uwezo wako wa kuingia ngazi nyingine inayofuata ya baraka au utumishi aliokupangia. Lakini pia ni ili akupe kutokutulia katika ngazi uliopo ili usonge mbele katika hatua au eneo lingine la huduma aliyokuitia. Shetani akikujaribu kama ilivyotokea kwa Yesu katika kitabu cha Mathayo 4:1-3 ni kwa lengo la kukujengea mazingira ambayo yatakufanya iwe rahisi kwako kuona sababu ya kumwacha Mungu au iwe rahisi kwako kutotii neno la Mungu au maagizo ya Mungu. Mwili ukikujaribu kama tunavyosoma katika kitabu cha Yakobo 1:13-15 ni kwa lengo la kutaka roho na nafsi yako vifuate nia ya matakwa ya mwili. Ndio maana kila wakati “mwili hutamani ukishindana na roho, na roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka” (Wagalatia 5:17). Na kufuatana na Warumi 8:5-8 ukiifuata nia ya mwili na matakwa yake huwezi kamwe kumpendeza Mungu. Kwa hiyo ni muhimu sana uweze kujua chanzo cha jaribu ulilonalo – kama ni Mungu, au ni shetani, au ni mwili. Hili ni muhimu ujue kwa kuwa hata namna ya kushughulikia majaribu hayo inatofautiana kutokana na tofauti ya vyanzo vyake. Fahamu jinsi Mungu anavyoyatazama majaribu Kwa kuwa kufuatana na Wakolosai 3:1-3,10 na Waefeso 2:6 tumefufuliwa na tumeketi pamoja na Kristo, kwa hiyo ni muhimu tujizoeze kuyaona majaribu yetu kwa jinsi ambayo Mungu anayaona. Kwa mfano: · Jaribu likija kwako ni ‘saizi yako’. Na kama si saizi yako, basi Mungu atakupa mlango wa kutokea toka kwenye hilo jaribu (1Wakorintho 10:13) · Katika kila jaribu Mungu anategemea ushinde – kwa sababu umeumbwa na umeundwa ili ushinde unapokuwa ndani ya Kristo na si ushindwe. Kufuatana na Warumi 8:35,37-39 tumetangaziwa ushindi kabla ya jaribu kuanza au kuisha! · Katika kila jaribu hata kama limetoka kwa shetani au katika mwili – Mungu ataligeuza liwe baraka kwako. Ukisoma Warumi 8:28 inasema: “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake”. · Kumbuka matatizo mengine ambayo sisi kama wanadamu tunayaita majaribu – kwa Mungu anajua ni adhabu tunayopata kutokana na kutokutii maagizo yake. Kwa mfano katika kitabu cha Yoshua 7:1-26 wana wa Israeli walijikuta kwenye matatizo ya kupigwa na adui zao, si kwa sababu walikuwa wanajaribiwa, ila ni kwa sababu walikuwa wanapata adhabu ya kutokutii kwao maagizo ya Mungu. Na katika mazingira ya namna hii huwezi kusonga mbele kwa ushindi bila ya kwanza kutubia kosa ulilolifanya, na kuendelea kuyatii maagizo ambayo ulikuwa huyatii! · Kuna mazingira mengine tunayoishi ambayo kwetu kama wanadamu ni magumu na yanatuweka majaribuni,lakini Mungu anajua hayo ni maeneo ya kawaida ya kazi aliyotupangia; kwa mfano, tokea mwanzo Mungu hakupanga msalaba uwe jaribu kwa Yesu bali uwe sehemu ya wito wake. Lakini katika Mathayo 26:36-46, msalaba uligeuka kuwa jaribu kwa Yesu, lakini maombi aliyoyafanya pale Getsemani yalimvusha na kumsaidia kumalizia wito wake vizuri. Kwa hiyo anaposema nasi katika Luka 9:23 juu ya kuchukua misalaba yetu hana maana ya majaribu yetu – bali ana maana ya wito aliotuitia. Lakini mazingira magumu ya kazi ambayo Mungu anaweza kukupangia ni kwa mfano; katikati ya mbwa mwitu (Luka 10:1-4); katikati ya nyoka na nge (Luka 10:19 na Ezekieli 2:1-6); au penye giza ili wewe uwe nuru hapo (Mathayo 5:14-16), au kupigana kama askari ili kuwafungua wafungwa na kuwarudisha waliotekwa (Wagalatia 6:1,2); au kuwa ‘chumvi’ katika mazingira yasiyo na ‘ladha’ (Mathayo 5:13). Haya ni baadhi ya mazingira ambayo ni magumu kwa mtu kufanya kazi au kuishi ndani yake – lakini ndio sehemu ya wito wa kuwa mkristo.
Mambo ya msingi ya
kukumbuka Kila mtu anaingia katika majaribu kwa namna moja au nyingine. Pia, lile ambalo wewe usiloliona ni jaribu, kwa mwingine linaweza likawa ni jaribu kubwa. Kwa mfano, kwa mwingine kuwa na fedha ni jaribu wakati kwa mwingine kutokuwa na fedha ni jaribu. Au mtu huyo huyo ambaye wewe unamwona ni jaribu kwako au kikwazo kwa mwingine anamwona ni baraka. Inawezekana kuolewa au kuoa kwa mwingine ni jaribu wakati kwa mwingine kutokuolewa au kutokuoa ni jaribu. Mambo ya msingi ambayo unahitaji kuyakumbuka kila wakati ili ushinde majaribu uliyonayo au utakayokuwa nayo ni haya: 1. Usiharibu uhusiano wako na Mungu. Kujaribiwa si dhambi – lakini cha muhimu ni kuwa mwangalifu na makini kujua unafanya nini unapojaribiwa. Biblia inatuambia ya kuwa: Yesu –“mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa” (Waebrania 2:18). “Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuliana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi” (Waebrania 4:15). Ikiwa Yesu hakuharibu uhusiano na Mungu alipojaribiwa, na wewe usiharibu uhusiano wako na Mungu unapojaribiwa. 2. Jenga maisha yako au utumishi wako au ndoa yako katika namna ambayo itastahimili ‘mafuriko’ ya majaribu yanapokuja. · Kufuatana na Mathayo 7:24-27 majaribu yanaweza kulinganishwa na ‘mafuriko’ yanayosemwa katika habari hii – yanampitia kila mtu. · Kufuatana na Mathayo 6:13, Mungu anaweza kuzuia aina fulani ya majaribu toka kwa shetani, hasa kama anaona si ‘saizi yako’! · Angalia kutafakari mistari hii: → Kama ulimwenguni kuna dhiki (Yohana 16:13), kwa hiyo andaa maisha yako kushinda mafuriko ya ‘dhiki’. → Kama kuna wakati tutachukiwa kwa sababu ya Jina la Yesu (Mathayo 10:22), kwa hiyo andaa maisha yako kushinda mafuriko ya chuki yanapokuja. → Kwa kuwa miili yetu ni hekalu la Mungu (1Wakorintho 3:16,17), kwa hiyo tuandae maisha yetu kushinda mafuriko ya uadui wa mwili juu ya mapenzi ya Mungu (Warumi 8:5-8, Wagalatia 5:16,17). → Kwa kuwa tumo duniani na dhambi bado ipo (Mwanzo 4:6,7), kwa hiyo tujiandae kushinda mafuriko ya dhambi (Warumi 6:14). → Shetani anaitwa mjaribu na mungu wa dunia hii (2 Wakorintho 4:3,4), kwa hiyo tujiandae na ‘mafuriko’ ya upinzani wake ( 2Wakorintho 10:3-5, Waefeso 6:10-13). · Je, mtu anayejua mbele yake kuna mtihani, ataacha kujiandaa vizuri na kisha ategemee kufaulu huo mtihani? La hasha! Lazima ajiandae. Na wewe uishi maisha yaliyotayari kuvuka majaribu au ‘mafuriko’ yaliyomo katika maisha haya kwa kulisoma neno la Mungu na kuwa mtendaji wa neno hilo ulilosoma. Maisha yako yatakuwa yamejengwa juu ya ‘mwamba huu’ kwa kumjua Yesu Kristo zaidi ya kuwa ni kwako nani katika maisha haya na yale ya baadaye. 3. Usiache kuomba wakati unaposongwa na majaribu – bali endelea kuomba. Ukisoma katika Mathayo 26:36 – 46 utaona jinsi maombi yalivyomsaidia Yesu kuvuka katika jaribu alilokuwa nalo la kukinywea ‘kikombe’ cha Baba yake. Na wewe je, ukiwa katika majaribu unafanya nini? Je unaendelea kuomba au unakata tamaa, unachukia na unaacha kuomba? Sisi tunakushauri endelea kuomba ukiona umechoka ujue upako wako umepungua kufuatana na Mithali 24:10 inayosema, “ukizimia siku ya taabu, nguvu zako ni chache” 4. Unapokuwa katika majaribu jitahidi usipoteze furaha yako au uchangamfu wako. Yakobo 1:2 inasema, “….hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali….” Neno hili ‘furaha’ maana yake usiwe na huzuni bali uwe mchangamfu. Neno hili ‘mkiangukia’ limetumika kuonyesha ya kuwa jaribu hili hukupanga wala hukulijua. Lakini wazo hili tunalipata pia katika kitabu cha 1 Petro 4:12,13 maana tunasoma hivi: “Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho. Lakini kama mnavyoshiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe”. Ni muhimu kufurahi ukiwa katika majaribu maana unahitaji nguvu zaidi za Mungu. Na kufuatana na Nehemia 8:10 furaha ya Bwana ndio nguvu zetu. Mfanye Mungu afurahi au akufurahie naye atakupa nguvu zake. Ndio maana ni muhimu mtu aokoke na kumpokea Bwana Yesu katika maisha yake (Zaburi 51:12). Ukipoteza furaha ya Bwana unakuwa mzito kwenye kufikiria, kuamua na kufanya mambo.Lakini pia unakosa nguvu na unajaa huzuni. Kuokoka ni mwanzo tu wa furaha ya Bwana ndani yako – lakini hakutoshi! Ni lazima ujizoeze kuona Mungu anavyoona juu ya jaribu ulilonalo. Mungu anaonaje juu ya jaribu lako? Kwanza analiona kwa kutumia neno lake alilotamka juu yako (Yeremia 1:12). Lakini, pili, anatangaza mwisho wa jaribu lako katika mwanzo wake! (Isaya 46:9,10). Kufuatana na Warumi 8:37 anakutangazia ushindi wako dhidi ya jaribu, siyo mwishoni mwa jaribu bali mwanzoni mwake. Tena anajua matokeo yake yatakuwa mema (Warumi 8:38), na pia imani yako itaimarika (Yakobo 1:2-4) Mwisho kabisa, tunataka tukukumbushe ya kuwa ni muhimu kutafuta wimbo na kuimba unapokuwa ndani ya jaribu. Ndivyo Mtume Paulo na mwenzake Sila walivyofanya walipokuwa gerezani kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Matendo ya Mitume 16:16-25. Walipoimba nyimbo za kumsifu Mungu, nguvu za Mungu ziliwashukia na kuwaweka huru.
Tuzidi kuombeana.
Yesu karibu anarudi. Simama imara usitikisike. Baraka iliyoko mbele yako
ni kubwa kuliko ukubwa wa jaribu lolote ulilonalo au utakalokutana nalo
katika maisha yako. |
|