|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Salamu katika Jina la Yesu. Mungu wetu huyu ambaye tunaamini ya kuwa ni Mungu wako pia katika Kristo Yesu, ni mzuri sana kiasi ambacho ametupa tena nafasi ya kuwasiliana na wewe kwa njia ya barua hii.
Unapokosea kutumia uwezo Mathayo 10:1 tunaona Yesu akiwaita wanafunzi wake na “akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote ya udhaifu wa kila aina” Pamoja na kupewa uwezo wa kuwatoa pepo, tunaona ya kuna siku waliletewa mtoto aliyekuwa na ugonjwa wa kifafa na wakashindwa kumtoa huyo pepo wa kifafa (Mathayo 17:14 – 16). Yule mgonjwa alipoletwa kwa Yesu biblia inasema; “Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile” Kulichofuata katika Mathayo 17:19 ni kwamba: “ Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema, mbona sisi hatukuweza kumtoa?” Hili swali la wanafunzi linalosema: “mbona sisi hatukuweza kumtoa” lina maana kubwa ndani yake juu ya jinsi walivyolichukulia jambo hili la wao kushindwa kumtoa pepo huyo wa kifafa – licha ya kwamba walikuwa tayari wamepewa upako au uweza na agizo la kutoa pepo. Ndani ya swali hili tunaona mambo yafuatayo: Kwanza: Walijua ya kuwa kuna jambo walilokosea katika wao kujitahidi kumtoa pepo kiasi kwamba pepo hakutoka, na mgonjwa hakupona – licha ya kwamba walikuwa wamepewa upako au uwezo wa kutoa pepo. Pili: Inaonekana maneno aliyowaambia Yesu baada ya kuelezwa ya kuwa wameshindwa kumtoa pepo hayakuwafanya wajisikie vibaya, na wala hayakuwakatisha tamaa; na wala hayakuwafanya wasite kumuuliza Yesu juu ya kile kilichosababisha wakakosea na kushindwa kumtoa pepo. Yesu aliwaambia, “Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni kwangu” (Mathayo 17:17). Ungekuwa ni wewe unaambiwa maneno hayo baada ya kukosea ungejisikiaje? Bado ungekuwa na msukumo wa kumwendea aliyekusemesha namna hiyo ili kujua kilichokufanya kukosea? Wengi wangeweza kusema “kama anaweza kufanya mwenyewe na afanye basi kwani sisi kinatuhusu nini?” Lakini wanafunzi hao hawakufanya hivyo, bali walimwendea Yesu na kumuuliza “mbona sisi hatukuweza kumtoa?” Tatu: Inaonyesha ya kuwa wanafunzi hao si tu kwamba walitaka kujua kosa lao au kilichowafanya wakakosea – lakini pia walitaka kujifunza kutoka katika hilo kosa. Kwa kuwa walipouliza “mbona sisi hatukuweza kumtoa?” – Yesu aliwapa jibu ambalo lilikuwa si tu somo muhimu kwao, bali limekuwa somo kwa mtu yeyote yule ambaye ametaka kujifunza toka kwenye kosa lao. Maana “Yesu akawaambia, kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amini, nawaambia, mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. (Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga)” – Mathayo 17:20, 21. Unapokuwa na utayari wa kujifunza toka kwenye kosa ulilofanya – si tu kwamba wewe unapata msaada, ufahamu na hekima zaidi, bali pia watu wengine watajifunza kutokana na kosa ulilofanya na somo ulilolipata toka katika kosa hilo. Nne: Inaonyesha ya kuwa baada ya kupata somo kutokana na kosa walilofanya – walijifunza na kuelewa vizuri hilo somo kiasi cha kutolirudia tena. Ndio maana hatuoni mahali pengine ambapo pameandikwa ya kuwa walishindwa tena kutoa pepo. Baada ya somo hilo, Yesu akawatuma tena wawili wawili (Luka 10:1-16).Hao wanafunzi wakaenda kama walivyotumwa, na wakarudi “kwa furaha wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako” (Luka 10:17). Kwa nini waliporudi hawakuripoti kwa Bwana Yesu mambo mengine yaliyotokea katika utumishi wao – ila wakakumbuka tu lile la kutoa pepo? Ni dhahiri ya kwamba walitaka Yesu ajue ya kuwa somo walilopata toka kwenye kosa walilofanya la kushindwa kumtoa pepo wa kifafa – walilielewa na wamefuzu. Sasa wameweza kutoa pepo bila shida!
Kupewa uwezo wa kupata
utajiri haina Kama vile ilivyotokea kwa wanafunzi wa kwanza ya kwamba, kuwa na uwezo wa Mungu wa kutoa pepo haina maana utamtoa pepo kirahisi; kuna mambo mengine unayohitaji kuyajua na kuyafanya ili uwezo huo uliopewa uweze kukusaidia ili kuwatoa pepo. Vivyo hivyo na kwenye utajiri. Kufuatana na Kumbukumbu ya Torati 8:18. Mungu anaweza kukupa uwezo wa kupata utajiri, lakini haina maana utakuwa tajiri mara moja. Kuna mambo mengine unayohitaji kuyajua na kuyafanya ili uwezo huo uliopewa uweze kukusaidia kupata utajiri ambao Mungu anataka uupate. Lakini pia kuna mambo mengine unayapata na kuyajua baada ya kufanya makosa katika kuutumia huo uwezo uliopewa. Na ukiishakosea – ni muhimu kurudi kwa Mungu katika maombi yenye toba ndani yake ili kujua kwa nini umekosea na hukufanikiwa. Ndiyo maana biblia haikuficha makosa waliyoyafanya waliotutangulia – ni ili tujifunze katika hayo makosa na yale yaliyotokea au waliyojifunza baada ya kukosea. Lengo halikuwa ni kuwaaibisha bali ni ili sisi tunaosoma habari zao siku hizi tusaidike na kupata maarifa na hekima na ufahamu ili tufanikiwe katika maisha.
Wewe Unapokosea jambo kitu
gani Unapokosea haina maana huna akili, bali inamaana ya kuwa hujafanya kilicho sahihi Hofu na aibu ya kukosea imewakwamisha watu wengi kufanya mambo mapya katika maisha yao. Kiu ya kujifunza na kufanikiwa katika kufanya jambo jipya unaloliona ni muhimu katika maisha yako. Kiu hii isipozidi hofu na aibu uliyonayo ya kukosea utakapofanya hilo jambo – huwezi kulifanya wala kuthubutu kuanza kulifanya! Chukia kufanya makosa, lakini makosa yenyewe usiyaogope ikiwa utayafanya. Yatumie kujifunza jambo jipya linalopatikana katika kila kosa. Muhimu: Katika kila kosa mtu analolifanya kuna jambo la kujifunza ikiwa atabadilisha mtazamo wake juu ya jinsi anavyowaza na jinsi anavyoyachukulia makosa anayoyafanya. Makosa uliyoyafanya yasikukwamishe, bali yageuze yawe baraka kwa maisha yako – ya sasa na ya baadaye. Hebu tafakari mifano ifuatayo: → Levi straus aliamua kuelekea Calfonia (U.S.A) ili kujishughulisha na uchimbaji wa dhahabu. Lakini pamoja na jitihada zote alizokuwa nazo, hakufaulu katika uchimbaji huo wa dhahabu na badala yake akaanza kutengeneza suruali na kaptura za wachimbaji kwa kutumia turubai. Huo ndio ukawa mwanzo wa suruali za Levi au Jean’s za Levi, tunazoziona madukani na watu wakizivaa siku hizi. → Thomas Edison – Ndiye aliyevumbua ‘bulb’ ya umeme. Lakini hadi afanikiwe inakisiwa alikosea karibu mara 10,000. Ni mashirika machache kama yapo ambayo yanaweza kuruhusu mfanyakazi akosee mara nyingi namna hiyo bila kumfukuza kazi. → Christopher Columbus – Alipoanza kusafiri toka Uingereza ilikuwa ni kwa nia ya kutafuta njia ya kwenda China ili kufanya biashara. Akakosea njia na kupotea na kujikuta katika bara la Amerika na kupelekea kuanza kwa Taifa la Marekani. → Ukijifunza kutokana na makosa katika kulea mtoto wa kwanza, mtoto wa pili utamlea vizuri zaidi kuliko yule wa kwanza. → Kuna mfanya biashara aliyekuwa anataka kupata mkopo benki; lakini kila benki aliyokwenda alinyimwa mkopo huo alikuwa naomba apewe. Alipitia benki saba na zote zilimkatalia. Lakini hakukata tamaa, na alikuwa kila benki wakimkatalia anawauliza sababu zilizowafanya wasimpe mkopo. Walipokuwa wanamueleza sababu hizo alikuwa anajifunza jambo na kurekebisha andiko lake kila mara. Alipokwenda benki ya nane kuomba mkopo – walimpa – lakini ni kwa sababu ya kujifunza katika kukosea mara saba! → ‘Masomo’ yanayotokana na ajali za magari na ndege yamezaa uundaji mzuri zaidi wa magari na ndege ili kupunguza hizo ajali. Katika kila kosa unalolifanya una nafasi ya kujifunza angalau mambo matatu (i) kujifunza zaidi juu yako mwenyewe; (ii) kujifunza jambo jipya ambalo ulikuwa hulijui; (iii) kukutana na watu ambao bila kujikuta katika hilo ‘kosa’ labda usingekutana nao. Kutokujua namna ya kujifunza kutokana na kosa kutakufanya uendelee kufanya kosa hilo hilo mara kwa mara, na kukukwamisha kusonga mbele. → Akina Wright wale ndugu wawili wa Columbus, Ohio kule Marekani ndio waliounda ndege ya kwanza – walijaribu na kukosea mara nyingi sana kabla ya kuweza kuruka hewani. Na katika kuruka huko waliruka uumbali wa mita 75 tu. Ingawa umbali huo unaonekana ni mdogo, lakini huo ndio uliokuwa mwanzo wa uvumbuzi wa ndege! Na kila ajali inapotokea inazaa ‘somo’ linalowafanya wataalamu wa ndege kuzifanya ndege zinazoundwa ziwe salama zaidi kuliko zile za mwanzo.
Shule za aina mbili;
soma Kuna shule mbili kubwa hapa duniani. Kuna shule ya darasani na kuna shule ya maisha – yaani nje ya darasa. Katika shule ya darasani unapewa kwanza somo halafu jaribio au mtihani ua maswali yanafuata baada ya somo ili ijulikane kama umeelewa somo au la. Ukikosea katika kujibu maswali inategemea mwalimu wa hilo somo anakujengea kuona nini katika makosa yako: - : au atakufanya ujisikie vibaya, au utakufanya ujione huna akili na kujidharau, au atakusema vibaya na udharaulike mbele ya wenzako – na hii inaweza kuzaa ‘inferiority complex’ (kujisikia duni mbele ya wengine); au atakusaidia ujifunze na kusahihisha kosa na kwa kufanya hivyo kukusaidia ujifunze jambo jipya kutokana na makosa uliyofanya. Katika shule ya maisha – yaani nje ya darasa mara nyingi unajikuta umefanya makosa bila kujua au kwa kujua. Ni juu yako na jukumu lako kujifunza kutokana na makosa hayo – ili upate somo la kukusaidia uvuke hapo na usirudie hilo kosa tena. Mara nyingi shule ya maisha haina ‘mwalimu’ wa kukuhimiza kusahihisha kosa, au kukutia moyo kwa kupewa cheti cha kufuzu. Hali yako ya maisha na hekima utakayokuwa nayo ndiyo itaonyesha umefuzu kiasi gani shule ya maisha. Watu wengi wanafaulu shule ya darasani na kufeli shule ya maisha, na matokeo yake ni maisha yao yanakuwa si mazuri. Kuna wengine wanafeli shule ya darasani lakini wanafuzu shule ya maisha, na matokeo yake ni maisha yao yanakuwa mazuri. Hii ni kwa sababu shule nyingi za darasani hazimsaidii mtu kupata maarifa katika elimu anayopata, bali zinamsaidia atoke na elimu peke yake. Elimu bila maarifa haitoshi kukusaidia kutatua matatizo yalimo katika ‘maisha’. Shule ya maisha inatoa maarifa moja kwa moja bila elimu. Mungu alisema katika Hosea 4:6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa…..” Na hakusema kwa kukosa elimu! Ukiweza kusoma shule zote mbili ni vizuri zaidi kwako ikiwa utalenga kutoka na maarifa katika shule hizo mbili. Shule ya maisha ina madarasa mengi pia, mojawapo ni darasa la makosa. Unapokosea kosa hili linakuwa ni darasa. Maana yake kuna somo au masomo ndani yake ya kujifunza kama utakuwa tayari kujifunza. Labda ulikuwa unajaribu kufanya jambo jipya kabisa ambalo hujawahi kulifanya maishani na ukakosea; badala ya kusita au kukata tamaa au kuogopa kujaribu tena kwa kuhofia kukosea tena, wewe amua kufungua macho yako ya ndani ujifunze jambo, ujirekebishe na usonge mbele!
Je unajua kosa lako Kutokujua kuwa umekosea wapi au kutokujua kama wewe ndio mwenye makosa na ukasababisha kutokee kitu ambacho hakikutakiwa kitokee, kutokujua huko kunaweza kuzaa ndani yako hali au tabia kati ya zifuatazo:
Unajikuta unawaza au/ na kusema “siyo mimi” “sihusiki” “Tatizo siyo langu wala sikulisababisha mimi” “ Nisingeweza kufanya kosa la namna hii”
Unajikuta unasema “Ni kosa lako na si langu,” au “wewe ndiye ulisababisha nikakosea,” au “Mke wangu angekuwa na matumizi mazuri ya fedha ningekuwa mbali kimaisha” au “ Isingekuwa kulipa ada ya shule ya watoto ningekuwa tajiri sana,” au “Wateja hawanunui bidhaa zangu ndio maana sifanikiwi,” au “Hakutoa maelekezo vizuri,” au “Wafanyakazi wamekuwa wazembe ndio maana makosa ni mengi,” au “Serikali haijanisaidia ipasavyo”.
Unajikuta unasema “sina elimu ya kutosha ndio maana nimekosea”.Au “Sina ujuzi wa kutosha ndio maana nimekosea”. Au “Kila mtu alikuwa anafanya hivyo hivyo.” Au “Sikuwa na muda wa kutosha, kwa hiyo nikafanya kwa haraka”
Unajikuta unasema, “Nilisema sitaweza, lakini mkanilazimisha kufanya,” au “Sitarudia kufanya jambo hili tena,” au “Naona aibu kurudia tena,” au “Nitakosea nikirudia tena,” au “ Hakuna faida ya kujaribu tena, maana nitapata hasara,” au “Sioni namna gani nitafaulu katika hili nikurudia kulifanya”
Unajikuta unasema “Hakuna kosa lililofanyika;” au “Sioni kosa langu; ”au “Mimi naona ninavyofanya ni sawa tu,” au “Niambie nimekosea wapi maana mimi sioni”
Ikiwa unaogopa kufanya
makosa kumbuka ulivyojifunza kuendesha baiskeli! Kuna mtu ambaye anatamani sana kuhubiri, lakini anasita kuhubiri kwa kuogopa kukosea wakati hapo atakapokuwa anahubiri! Ukiogopa kuhubiri kwa kuwa unaogopa kukosea wakati utakapokuwa unahubiri huwezi kujifunza kuhubiri vizuri. Ni muhimu ujue ya kuwa kukosea ni sehemu ya kujifunza. Mtu yeyote ambaye labda anatamani kufanya biashara au kuwekeza fedha zake katika mradi au kampuni fulani,lakini anasita kuanza kufanya hivyo kwa kuogopa kukosea na kupoteza fedha zake, ni vigumu kwake kuwa mfanya biashara au mwekezaji mzuri! Lazima kujua ya kuwa kukosea katika kufanya jambo unalotaka kufanya ni sehemu ya darasa kwako la kupata somo la kukusaidia ujifunze jambo ambalo ulikuwa hulijui. Kumbuka usilitazame kosa kama kikwazo, bali litazame kama darasa muhimu. Sehemu ya mkakati wa kushinda katika eneo lolote katika maisha yako ni wewe kuwa na moyo wa kutokuogopa kukosea au kushindwa. Ikiwa unaogopa kufanya makosa kumbuka ulivyojifunza kuendesha baiskeli (kama unajua kuendesha baiskeli). Lazima utakumbuka ya kuwa kukosea na kushindwa kuendesha baiskeli hakukuwa kikwazo kwako. Ndani yako ulikuwa na kiu kubwa mno ya kushinda na kujua kuendesha baiskeli, kiasi ambacho ndani yako hofu ya kukosea na kushindwa haikukusumbua. Unaendesha baiskeli vizuri sasa kwa sababu ulijifunza pia toka kwenye makosa uliyofanya ulipokuwa unajifunza kuendesha baiskeli! Kwa hiyo tumia mbinu hii hii na utashi huu huu pia katika mambo unayojifunza katika maisha. Huwezi ukataka kufanya jambo na kufanikiwa wakati ndani yako unaogopa kukosea au kushindwa. Imani na hofu havikai pamoja! Huwezi ukawa na imani ya kushinda jambo unalotaka kufanya, wakati huo huo una hofu ya kushindwa ikiwa utalifanya. Ikiwa ndani yako umebeba imani na hofu juu ya jambo hilo hilo ni vigumu kulifanya! Kumbuka ukichanganya imani na hofu mahali pamoja matokeo yake ni kuwa na moyo wa kusita-sita na kushindwa kufanya maamuzi katika jambo hilo. Biblia inasema: “Mtu wa nia mbili husita-sita katika njia zake zote” (Yakobo 1:8). Huwezi ukawa na nia mbili ndani yako zinazopingana na utegemee mafanikio mazuri katika maisha yako.
Wanaoishi kwa kutegemea Hakuna timu ya mpira inayoingia uwanjani kucheza ikiwa imejiandaa kushindwa! Ingawa timu hiyo inajua imejiandaa kushinda, lakini pia inajua inaweza ikakosea katika kucheza na kujikuta imefungwa na kushindwa. Kitu gani kinawafanya wachezaji waingie katika kushindana na timu nyingine na mawazo hayo? Ni kwa sababu ndani yao imani na hamu yao kushinda ni kubwa kuliko hofu ya kushindwa! Kuna timu zingine zinapokuwa na hofu ya kushindwa, zinaingia uwanjani na mbinu za kujihami zaidi kuliko za kushambulia. Kama timu inataka kushinda, kuzuia kufungwa magoli hakutawasaidia sana, ikiwa timu hiyo haitaifunga magoli timu inayoshindana nayo! Wanaoshi kwa kutegemea mbinu za kujihami tu peke yake, huwa sio washindi katika maisha! Ni vizuri uwe na mbinu zote hizo za aina mbili – kushambulia na kujihami! Shambulia ili upate ushindi ambao ulikuwa huna, halafu jihami kwa kulinda ushindi ulioupata,huku moyo wako umeuelekeza katika kupata ushindi mkubwa zaidi kuliko huo. Kwa kiingereza tunaweza kusema hivi: “ A person who plays only a defensive game of life, does not win or gain. You need to play an offensive game in order to win and gain more than you have now. Then defend or protect your gains while at the same time focusing on being offensive for more future gains” Ndio maana, kwa mfano, mtu ambaye ana fedha na anaogopa kufanya nazo biashara ili ziongezeke kwa hofu yo yote na akaamua ‘kuzificha’ hawezi kutajirika! Kuna uwezekano mkubwa hata hizo alizozificha asikae nazo muda mrefu – akajikuta zimeondolewa mikononi mwake au kwa kuzitumia au kunyang’anywa na yule aliyekupa! Ukisoma kitabu cha Luka 19:20-26 utaona ya kuwa mtu aliyeshindwa kuzalisha fedha alinyang’anywa na akapewa yule aliyeweza kuzizalisha! Unataka kuwa yupi kati ya hao? Anayenyang’anywa au yule anayeongezewa? Ikiwa unataka kuwa yule anayeongezewa, basi unahitaji kujua namna ya kuzizalisha – na uzizalishe kweli ili ziongezeke. Ikiwa unataka kuwa huyo anayeongezewa basi ni muhimu ubadili mfumo wako wa maisha. Usiishi kwa kujihami zaidi inapofika kwenye fedha ulizonazo kiasi cha kutokuwa na mbinu za kuzizalisha kwa kuogopa kuzipoteza wakati umo katika uzalishaji! Huwezi ukawa na mawazo ya kushindwa unapotaka kufanya jambo wakati katika kitabu cha Warumi 8:37 imeandikwa hivi: “Lakini katika mambo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda” Tena katika 2 Timotheo 1:7 tunasoma ya kuwa: “ Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi” Maandiko hayo ni kwa ajili yako ili kukutia moyo katika jitihada ulizonazo za kutaka kuwa na maisha ya ushindi, mafanikio na ya kumpendeza Mungu. Ishi kwa kuwa na mikakati ya kushinda na wala si ya kujihami tu usishindwe! Kusema hutaki kuendelea kuwa maskini hakutoshi kukutoa katika umaskini kama hutakuwa na mikakati ya ki-Mungu ya kukutajirisha!
Tizama kwa upya makosa Hili jambo ni muhimu ulitilie maanani. Inawezekana hujawahi kuyatazama makosa uliyoyafanya kwa namna hii tunayokuonyesha katika ujumbe huu. Je, katika makosa unayojua umewahi kuyafanya katika maisha yako, umejifunza jambo lolote? Ikiwa hujajifunza jambo lo lote, ni vizuri kama utachukua muda wako kidogo na ukatazama upya makosa uliyowahi kuyafanya kwa lengo la kuona kama unaweza kujifunza jambo lolote la kukusaidia. “Utusamehe Makosa yetu…….” Sehemu ya sala ambayo Yesu alifundisha wanafunzi wake ili wawe wanaifanya inasema “Utusamehe makosa yetu, kama sisi nasi tunavyowasamehe waliotukosea”. Katika tafsiri ya mojawapo ya biblia imeandikwa ya kuwa “Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu” (Mathayo 6:12). Tunachotaka uone hapa ni kwamba ni sehemu ya mafundisho ya Bwana Yesu ya kuwa tunapotambua makosa tuliyofanya tunahitaji kutubu. Toba ya kweli ndani yake ina kujua ulichokosea na kujifunza katika hicho ulichokosea. Usipojifunza katika hilo kosa, utajikuta unarudia kosa hilo mara kwa mara, na unakwama katika hilo eneo na kukosa mabadiliko katika maisha. Kufuatana
na kitabu cha Matendo ya Mitume 26:20 – unapotubu unahitaji kumwelekea
Mungu, na kuyatenda matendo yanayopatana na toba yako – ili ubadilike
katika maisha yako. |
|