Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Novemba 2004                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


UMOJA WA ROHO HAUTOSHI
BILA
UMOJA WA IMANI

Salamu katika Jina la Yesu.

Katika kitabu cha Waefeso 4: 3 tunasoma habari za “Umoja wa Roho” na katika Waefeso 4: 13 tunasoma habari za “Umoja wa Imani”. Kwa hiyo katika kanisa tunahitaji si tu umoja wa Roho bali umoja wa Roho pamoja na umoja wa imani. Watumishi mbalimbali tunahitaji kushirikiana ili kuimarisha umoja wa imani.

Imeandikwa katika kitabu cha Waebrania sura ya kumi na moja na mstari wa kwanza kuwa; " Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana."

Na pia tuna soma katika Warumi 10:17 kuwa:

"Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo".

Kwa kutumia maana ya neno imani kama tulivyosoma hapa juu tunaona ya kuwa umoja wa imani ni umoja wa 'kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo na bayana ya mambo yasiyoonekana.'

Ni kazi ya Mtume, manabii, wainjilisti, wachungaji na waalimu wakifanya kazi wote kwa kushirikiana, kutufikisha wakristo wote katika umoja wa 'kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, na bayana ya mambo yasi yoonekana.'

Kuna kuwa na tofauti kati ya wakristo juu ya hakika ya mambo yatarajiwayo, na tofauti yakuyangalia mambo yasiyoonekana, matokeo yake ni ukosefu wa umoja imani.

Na chanzo cha umoja wa imani ya kikristo ni kusikia na huku huja kwa

neno la Kristo.

lkiwa tunafundishwa neno la Kristo na Roho mmoja wote, na kulisikia wote, tutakuwa na imani ya aina moja; na Roho huyo aliyetufundisha neno la Kristo hilo atatufikisha katika umoja wa imani.

Huwa inashangaza kuona kuwa wakristo wa madhehebu mbali mbali ulimwenguni, wanatumia Biblia ya aina moja wote, na wanadai wote kuongozwa na Roho wa Mungu, lakini wanapingana juu ya tafsiri ya maandiko. Ni lazima pana tatizo katika kuitafsiri na kuifafanua Biblia.

Siku hizi ingawa wengi wanaitwa wakristo utaona wazi ya kuwa umoja wa imani ya kikristo KIMATENDO haupo. Na hii imetokana na tofauti ya mafundisho yanayotolewa ya neno la Kristo.

Na ndipo hapa tunahitaji huduma zote zifanye kazi. Kila mtumishi wa Kristo awe mtume au nabii au mwinjilisti, au mchungaji au mwalimu amepewa sehemu tu ya neno la Kristo. Huduma zote zikifanya kazi tunapata sehemu tu ya neno la Kristo.

Na ili tuwe na umoja wa imani tunalihitaji neno la Kristo lote na lililo kamilifu. Tukipata sehemu tu ya neno la Kristo tunapata ugonjwa wa utapiamlo wa Kiroho, hasara yake ni kukosa Umoja wa imani kati ya wakristo.

Na Roho wa Mungu anawaunganisha wakristo katika umoja wa imani,

kwa kulitumia neno la Kristo.

Na tujifunze toka kwa Yesu Kristo alipowagawia wanafunzi wake mkate;

Imeandikwa: "Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa akisema, Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu."  (Luka 22: 19)

Biblia haisemi alitwaa 'Mikate' bali alitwaa 'Mkate'.

Hii ina maana ni mkate mmoja tu ambao aliugawanya vipande kumi na

vitatu na kuwapa wanafunzi wake na kipande kingine akala yeye. Kila mmoja alipata sehemu ya mkate huo. Hakuna aliyepewa mkate mzima. Na vipande hivyo vya mkate vikikusanywa unapata mkate mzima.

          Hapa kuna jambo kubwa la kujifunza.

          Vivyo hivyo Yesu Kristo alipopaa aliteka mateka, na akagawa vipawa. Alimpa mtume sehemu, na nabii sehemu, na mwinjilisti sehemu na mchungaji sehemu, na mwalimu sehemu. Na wote hawa wakikusanywa na kila mmoja atoe sehemu ya Neno la Kristo alilopewa, utapata neno zima la Kristo; na ndilo litakalotufikisha katika umoja wa imani.

          “Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika.” (1 Wakorintho 13:9,10)

          Tatizo huwa linaanza kutokea mara tu mtu anaposikia wito wa kumtumika Mungu ukiwaka ndani yake. Na kwa sababu ya mazingira tuliyolelewa, wazo la kwanza linalomjia ni kutaka kuwa mchungaji.

          Lakini ni lazima tufahamu ya kuwa si wote walioitwa na Mungu kumtumikia, wameitwa wawe wachungaji.

          Kuna wengine wameitwa wawe mitume lakini hawajui na kama wanajua hawaifanyi kazi hiyo kwa kuwaogopa wanadamu.

          Kuna wengine wameitwa wawe wainjilisti lakini utakuta wanakwenda kwenye vyuo vya biblia kusomea uchungaji. Na hawafahamu ya kuwa uinjilisti ni huduma nyingine tofauti na uchungaji.Na mara nyingi watu wa namna hii wanapata shida katika utumishi. Utakuta mtu amebarikiwa kuwa mchungaji lakini kuishi kwake, kusema kwake na kuenenda kwake anaenenda kama mwinjilisti. Na anashindwa kufanya kazi ya uchungaji vizuri.

          Ni kitu gani kinakuwa kimetokea?

          Hebu soma mstari huu wa Waefeso 4:1

          “Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa.”

          Maana ya mstari huu ni hii: Ikiwa umeitwa kuwa nabii enenda kama nabii. Ikiwa umeitwa kuwa mwinjilisti, enenda kama mwinjilisti. Ikiwa umeitwa kuwa mchungaji enenda kama mchungaji. Ikiwa umeitwa kuwa mtume, enenda kama mtume. Na ikiwa umeitwa kuwa mwalimu, enenda kama mwalimu.

          Tusichanganye huduma kama vile ambavyo wengine wanataka wao wenyewe wawe wachungaji, wainjilisti, manabii, mitume, na waalimu kwa wakati mmoja. Huu ni uchoyo na ni ubinafsi.

          “Mkaribishane ninyi kwa ninyi, pasipo kunung’unika kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbali mbali za Mungu. Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina.” ( 1Petro 4:9-11)

          Na tena tunasoma yafuatayo:

"Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, vyote havitendi kazi moja; vivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbali mbali, kwa kadiri ya neema tuliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake mwenye kuonya katika kuonya kwake; mwenye kukirimu , kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia, kwa bidii; mwenye kurehemu, kwa furaha. Pendo na lisiwe na unafiki; lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; Kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu." (Warumi 12:4-10)

Laiti basi tungekuwa waaminifu kuyatii na kuyafuata maongozi ya neno la Mungu, matatizo mengi tuliyonayo yasingekuwapo.

Tafadhali tusichanganye huduma na karama tulizopewa. Kama vile mafundisho yaliyochanganywa, yanavyowachanganya wanafunzi vile vile na huduma zilizochanganywa, zinawachanganya wanaohudumiwa. Na kwa kuwa kuna kuchanganisha huduma na karama katikati ya wakristo, na wakristo, nao wamechanganishwa. Hawajui waamini lipi na wamwamini nani. Kila dhehebu lina mikazo yake, na wakristo wengi wanaifuata bila kujiuliza. Matokeo yake ni kukosa umoja wa imani kati ya wakristo wa madhehebu mbali mbali.

Kitu gani kimetutenganisha?

Ni mafundisho yanayotoka kwa baadhi ya wafundishaji wa neno la Kristo, ambao huingiza kipengele cha kuwadharau wakristo wengine katika mafundisho yao.

Wanapanda chuki badala ya upendo. Wanapanda ugomvi badala ya amani. Wanapanda utengano badala ya Umoja.

Kukosekana kwa huduma zingine katika kanisa kumeathiri sana maisha ya kiroho ya wakristo.

Kwa mfano biblia inasema;

 "Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni." (Waefeso 2:19-20)

Ndani ya mitume na manabii, Kristo ameweka Neno lake lililo na kazi ya kujenga msingi wa maisha ya kiroho ya wakristo. Mitume na manabii, wakikosekana siku hizi za leo, wakristo wanakosa msingi ulio imara na mara nyingi huyumbishwa, na wakati mwingine hata kuanguka kiroho. Tukiwa kama viungo vya Kristo, kila mmoja na afanye wajibu wake, na Kristo atauunganisha na kuukuza mwili wake yaani kanisa, ili upate kujijenga wenyewe katika upendo (Waefeso 3:16) .

Tuzidi kuombeana.

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.