Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Septemba 2004                                                        Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


ZIJUE TABIA ZA UPAKO WA ROHO MTAKATIFU ILI UWEZE
KUUTUMIA MSAADA WA MUNGU IPASAVYO
(Sehemu ya Pili)

Salamu katika Jina la Yesu.

          Mwezi uliopita tulikuelezea juu ya tabia mbili za upako wa Roho Mtakatifu. Mwezi huu tunataka tukuelezee tabia nyingine zaidi za upako wa Roho Mtakatifu.

Tabia ya Upako No. 3:-

Upako ulio ndani yako unaweza kuwasaidia wengine wavuke katika matatizo waliyonayo lakini usitoshe kukusaidia wewe kuvuka kwenye matatizo yako.  Ukisoma Waefeso 3:20 ni wazi ya kuwa:-

    • Unapokea majibu ya maombi au ya mawazo yako kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yako.
    • Hata kama una upako mwingi kiasi gani majibu ya maombi au mawazo yako ni matokeo ya kiwango cha utendaji wa upako (nguvu) ulio ndani yako.

Kwa hiyo tunaweza kusema UPAKO unaweza kupimika. Kwa sababu neno ‘kwa kadri….’ Lina maana ‘kwa kiwango’ au ‘ kwa kipimo’. Lakini pia ukisoma  Zaburi 23:5 neno ‘kikombe’ – Limetumika kama ‘container’ au kuonyesha upako unaweza kubebeka tena kwa kiwango au kwa kipimo fulani. Ukiisoma  Waebrania 1:9 utaona neno hili:  ‘kuliko wenzio’ - lina maana ‘kiwango tofauti’

Lakini hata kama nguvu/upako unao mwingi kwa kiasi cha kujaa nyumba nzima, na nguvu zinazotumika ni za kiwango cha kutosha chumba kimoja kilichomo ndani ya nyumba hiyo – majibu ya maombi  yako yatakuwa ni matokeo ya nguvu zilizotumika (yaani za kutosha chumba kimoja),  na siyo matokeo ya nguvu zilizopo katika vyumba vingine lakini hazifanyi au hazikufanyishwa kazi.

Upako usiofanya kazi au usiofanyishwa kazi ni sawa na msaada ulioletwa kwako lakini hautumiki. Na matokeo yake yatakuwa sawa na ya yule ambaye hakupata ‘msaada’ au ‘ upako’ kabisa!

Kuna gari ambalo lina nguvu ndani yake za kukuvusha katika matope au katika mchanga kama zitatumika ipasavyo. Usipojua kuzitumia nguvu hizo unaweza ukakwama na usivuke ulipokwama, si kwa sababu gari halina nguvu za kukuvusha, ila ni kwa sababu hakujua namna ya kuzitumia hizo nguvu.

Ukiwa una umeme ndani ya nyumba yako unaweza kulala na giza kama hujui kuuwasha au kama hakuna mtu wa kukusaidia kuuwasha! Na kama mko wengi kwenye ‘line’ moja ya umeme na ukazimika: tizama kwanza taa za nyumba za wenzako. Kama zote zimezimika, basi chanzo cha tatizo la kuzimika umeme haliko ndani ya nyumba yako. Lakini kama kwa wenzako kunawaka taa wakati kwako kumezimika basi tatizo la kuzimika taa kwako limo kwenye nyumba yako.

Kanisa, vikundi vya maombi, vikundi vya huduma n.k mara nyingi vinafungiwa ‘line’ inayofanana ya upako au umeme kutoka kwa Mungu. Ukiona wenzako wanaendelea vizuri wakati wewe huendelei vizuri, tatizo liko kwako wala si kwa kundi zima.

Hata kama ni kundi zima upako wao umezimika;  kama unayo  ‘generator’ (kunena kwa lugha) iwashe ili taa yako iendelee kuwaka hadi hapo ‘line’ ya wote itakapokuwa imetengemaa.

Fahamu hili ya kuwa kiwango cha upako unaofanya kazi ndani yako kinaweza kuwasaidia wengine wavuke katika matatizo yao, lakini kiwango hicho hicho kisikusaidie wewe.

Kwa mfano: Yesu pale kwenye bustani ya Getsemani (Luka 22:40 – 46; Mathayo 26:44 – 46):

·         Ingawa Yesu alikuwa na Roho wa Mungu na upako aliokuwa nao uliweza kuwasaidia wengi waliohitaji msaada kwake, hata hivyo haukuweza kumsaidia Yeye katika jaribu lake ili aweze kuvuka hadi alipotiwa nguvu tena wakati akiomba.

    • Nguvu (upako) zilipopungua alikuwa na mahangaiko moyoni na hofu ya kutii maagizo ya Mungu. Hata kuomba alikuwa amechoka.
    • Upako (nguvu) alipoongezewa ulimsaidia kiasi kwamba aliomba zaidi hadi akavuka na kuwa na utulivu katika kufanya mapenzi ya Baba yake.

Hebu tuangalie mfano mwingine huu wa Eliya Mtishbi ( 1 Wafalme 18:36-46):

·         Ingawa Eliya alikuwa na Roho Mtakatifu aliyemtia nguvu (upako) ya kuomba mvua inyeshe au isinyeshe; Mungu ajibu kwa moto, kupiga na kuua nabii wa Baali 400, na kukimbia mbio kuliko farasi wa Ahabu; - upako huu haukumwezesha Eliya kustahimili vitisho vya Yezebeli: Kwa hiyo alimkimbia Yezebeli!

·         Eliya alipata shida ile ile aliyopata Yesu wakati upako ulipopungua, na upako uliobaki kushindwa kumvusha mahali alipotaka ‘kuvuka’. Alipata mahangaiko na kukosa nguvu na ujasiri wa kuendelea katika mapenzi ya Mungu wake – akamkimbia Yezebeli..

·         Eliya alitiwa nguvu kwa kupewa chakula na maji toka mbinguni na malaika, ambavyo ni sawa na kupewa Neno na Roho Mtakatifu kutoka Mbinguni.

·         Naye akaenda kwa nguvu ya hicho chakula na maji kwa siku arobaini. Hii ina maana nguvu zilizofanya kazi ndani yake ni zile zilizotokana na chakula alichokula na maji aliyokunywa Eliya alikuwa ameishiwa nguvu kabisa ya kuendelea hadi alipopokea ‘chakula na maji’ navyo vikamtia nguvu.

·         Upako huo mpya ulimchukua hadi mahali ambapo aliweza kumsikia Mungu akisema naye.

·         Mtu anaweza akaishiwa upako kiasi cha yeye kushindwa kumtii Mungu katika maisha yake. Lakini akipata Neno la Mungu na nguvu mpya za Roho Mtakatifu anahuishwa upya na kupata wepesi wa kumtii Mungu.

Hebu tuangalie habari ya Samsoni ( Waamuzi 15:9-14 – 19):

·         Ingawa alikuwa na nguvu za kuwapiga wafilisti, lakini kiu ikataka kumuua – kwa sababu nguvu zilimtoka.

Kumbuka haya:

·         Yesu alitiwa nguvu baada ya kukubali mapenzi ya Mungu yatimizwe katika maisha yake. Na upako uliongezewa juu yake ili avuke na kuyafanya mapenzi ya Baba yake.

·         Mungu hawezi kukupaka mafuta ili uyatumie kuyafanya mapenzi yako, kwa hiyo kila wakati utakuwa unatafuta upako lakini hupati.

·         Eliya alikuwa ametumika sana bila ya kupata muda wa ‘kula na kunywa’ mezani pa Bwana kiasi ambacho alifika mahali ambapo nguvu au upako wa kumsadia kuendelea ‘kuishi’ katika mapenzi ya Mungu alikuwa ameishiwa.

·         Kilichomsaidia ni kukubali ‘kula na kunywa’ vya mbinguni na nguvu ya hivi vitu zilimsogeza hatua nyingine.

·         Samsoni aliishiwa nguvu alipopigana na Wafilisti, akaomba naye akapewa maji, ‘roho yake ikamrudia’ maana yake upako ukarudi akaburidika.

Kwa hiyo;

·         Kumbuka kumwomba Mungu akuhudumie na wewe wakati huo huo anapohudumia wengine.

·         Ombea watoto/ndugu wakati upako umejidhihirisha, usisubiri umehudumia wengine ndipo uhudumie na hao wakati mwingine – na je kama nguvu zimekwisha itakuwaje?

Tuzidi kuombeana.

Ni sisi katika Kristo,

Christopher na Diana Mwakasege

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.