Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Aprili 2005                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


BARUA YA MWEZI APRILI 2005

Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo aliye hai!

            Katika barua ya mwezi huu tunakuletea uthibitisho wa tatu kutoka katika biblia juu ya ujumbe aliotupa Mungu ya kwamba anakwenda kuletea Tanzania upako wa utajiri kwanza kabla ya kuletea upako wa uamsho.

Uthibitisho wa Tatu

Warumi 10:13-15

Angalia kitabu cha Warumi.10:13-15 anasema hivi, “Kwa kuwa kila atakayeliitia jina la Bwana ataokoka, basi wamwiteje yeye wasiyemwamini, tena wamwaminije yeye wasiyemsikia, tena wamsikieje pasipo mhubiri, tena wahubirije wasipopelekwa”.

Umeona hayo maneno! Unisikilize! Kuna uhusiano na muunganiko kati ya mtu anayepeleka mhubiri wa injili, na yule mtu anayeokoka baada ya kuhubiriwa. Maana anasema, kila atakayeliitia jina la Bwana ataokoka, lakini wamwiteje yeye wasiyemwamini, tena wamwaminije yeye wasiyemsikia, wasikieje pasipo mhubiri, (angalia hii sentensi) wahubirije wasipopelekwa?

 Kwa hiyo kabla Mungu hajaandaa mhubiri, anaandaa kwanza mtu wa kumpeleka mhubiri, maana atahuribije asipopelekwa? Iko faida gani ya kuandaa wahubiri bila kuandaa wapelekaji? Mungu haeindi hivyo! Mungu anaendesha kazi yake kwa staili yake ya kwamba anaandaa kwanza wapelekaji, halafu anainua wahubiri! Wahubiri wanapojitokeza kuhubiri maana yake wapelekaji wako tayari.

Fedha haianguki kwenye miti! Inachukua muda kuipata ya kutosha.Kwa hiyo kama Mungu anaandaa mhubiri mwaka ujao, lazima atakayempeleka na kumgharamia huyo mhubiri ameshaanza kuandaliwa mapema. Lazima uuone huo uhusiano, ni uhusiano wa ajabu na wa muhimu sana.

Matendo ya Mitume 13:1-5 anasema , “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba na Simeon aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hao walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia, ndipo wakiisha kufunga na kuomba wakaweka mikono yao juu yao wakawaacha waende zao. Basi watu hao wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu, wakateremkia Seleukia na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro”

Nataka uone hapa anaposema hivi, “wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu”.  Kumbuka tulikotoka; tulisoma “wahubirije wasipopelekwa”. Kwa kuna uhusiano kati ya upako unaomnyanyua mtumishi na kumpeleka mtumishi kazini na upako wa utajiri unaokaa juu ya mtu kwa ajili ya kugharamia safari na utumishi wa yule mtumishi, anapokuwa kazini.

Kama Roho Mtakatifu amewapeleka inamaanisha kuna gharama ambazo zinatakiwa kulipwa wakiwa katika safari hizo za kihuduma. Kwa sababu ni Roho Mtakatifu ndiye anayewapeleka; uwe na uhakika Roho Mtakatifu amekwisha wafunika upako wale wote aliowaandaa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hawa watumishi wanakokwenda utumishi wao unafanikiwa bila kukwamishwa na gharama za safari na huduma hiyo.

Tatizo lililopo ni kwamba kuna ukosefu wa mawasiliano kati ya upako ulioko juu ya watumishi na upako ulioko juu ya wale watu ambao wamepewa fedha kwa ajili ya kuwatunza watumishi. Na hakuna kitu kibaya kama hicho!

 Kwa sababu huyu ambaye amepewa fedha nyingi hajui sababu kwa nini amepewa fedha nyingi. Hapa sizungumzii suala la kutoa fungu la kumi, maana fungu la kumi ni jukumu la kila mkristo kumtolea Mungu. Utoaji wa kutunza watumishi ni maagizo maalumu toka kwa Roho Mtakatifu ambayo mara nyingi yanahusisha utoaji mkubwa kuliko ule wa fungu la kumi peke yake.

 Huu ni utajiri ulio na kazi maalumu, na unapokuja kwa mtu unakuwa mwingi kuliko mahitaji yake binafsi. Si kila mtu atapewa, isipokuwa yule ambaye amekuwa na uhuru wa kifedha kwa namna ambavyo hawezi kula pesa ya Mungu ikija mkononi mwake.

La sivyo kama hujawa na uhuru kifedha huu upako hauwezi kukusaidia kitu, kwa sababu hiyo pesa ikija nyingi kwako fikiria kitu cha kwanza utakachowaza. Si wengi watawaza kuutumia huo utajiri waliojaliwa kuwa nao katika kugharamia pia gharama za kazi ya Mungu na watumishi wake.

Utasema ‘lakini Mungu nimempa fungu la kumi’! Mungu hakuleta utajiri kwako wewe kutoa kwa ajili ya fungu la kumi tu peke yake, kuna kazi yake, inayohitaji utoaji mkubwa zaidi ya fungu la kumi.

Lazima kuwe na uhusiano kati ya utajiri huo uliopewa na uhitaji wa gharama za kazi ya Mungu mahali fulani. Lakini kwa sababu wengi walio na utajiri huo hawajui au wanachelewa kujua, wanajikuta wakitumia utajiri walionao kwa shughuli zingine ambazo hazihusiani na kazi ya Mungu.

Lakini vile vile, kazi ya Mungu inakwama kwa kukosa mtu wa kuigharamia. Kumbe huyo mtu yupo, ila hajui ya kuwa anatakiwa kuigharamia kazi hiyo. Na watumishi wa Mungu wanaosimamia hiyo kazi ya Mungu iliyokwama hawajui kama kuna mtu aliyeandaliwa kuitunza hiyo kazi waliyopewa. Kukosa mawasiliano mazuri kati ya makundi haya mawili kumeifanya kazi ya kugharamia huduma iwe ngumu.

Huu ni uthibitisho wa tatu wa kibiblia niliopewa juu ya kile ambacho Mungu anataka kukifanya Tanzania. Hebu sasa tuangalie uthibitisho wa nne juu ya jambo hili – katika barua ya mwezi ujao (Mei 2005). Usiache kuisoma!

Nasi tunakutakia na kukuombea mafanikio katika kila eneo la maisha yako sawasawa na 3 Yohana 1:2. Usisahau kutukumbuka katika maombi yako ili tuzidi kukua zaidi katika neema ya Bwana na katika kumjua Yesu zaidi.
 

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.