Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Agosti 2005                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


BARUA YA MWEZI AGOSTI 2005

Salamu katika Jina la Yesu Kristo.

            Tunamshukuru Mungu ya kuwa umepata muda wa kusoma barua yetu ya mwezi huu. Tunaendelea kukuletea mifano zaidi inayothibitisha uhalisi wa uhalali wa kila ambacho Mungu ameamua kukifanya Tanzania. Ikiwa hujui ni nini Mungu alituambia, ni vizuri uzisome barua zetu za miezi ya nyuma.

Mfano wa Ujenzi wa
Hema

Tunaposoma habari za Wana wa Israeli walipokuwa wanatoka Misri, tunaona ya kuwa walitoka wakiwa na fedha na mali nyingi sana. Mungu aliwapa fedha na mali ambazo walikuwa hawazihitaji kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Zaburi 105:37a inatuambia ya kuwa: “Akawatoa hali wana fedha na dhahabu….”

Fedha walizihitaji za nini wakati jangwani walikokuwa wanaelekea kulikuwa hakuna maduka? Na dhahabu je! Zilikuwa ni kwa ajili ya nini, wakati ingekuwa vigumu wao kujipamba vizuri wakiwa katika safari ambayo usafi kwao ingekuwa shida?

Hili lilikuwa jambo la kushangaza, na la ajabu, na ambalo halikutegemewa na wana wa Israeli ya kuwa Mungu atawafanyia!

“Wana wa Israeli wakafanya kama neno lile la Musa; wakataka kwa Wamisri vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu, na mavazi. Bwana akawajalia kupendelewa na Wamisri hata wakawapa kila walichokitaka.Nao wakawateka Wamisri nyara” (Kutoka 12:35,36)

Lazima Mungu alikuwa na sababu nyingine iliyomfanya awape hizo mali nyingi hao wana wa Israeli wakati alijua hawatazihitaji kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao ya kila siku!

Nasema Mungu alijua ya kuwa hawahitaji utajiri huo kwa matumizi ya mahitaji yao ya kila siku, kwa sababu Mungu alikuwa na utaratibu mwingine wa kuwatunza watakapokuwa safarini. Kila aliyewahi kuisoma habari yote ya safari ya wana wa Israeli toka Misri na kwenda Kaanani, anajua ya kuwa Mungu aliwalisha Mana na Kware. Pia, aliwapa muujiza ambao uliwasaidia nguo zao zisichakae, na miguu yao isivimbe!

Tatizo ni kwamba Wana wa Israeli walipewa utajiri mwingi ambao hawakuuhitaji kwa matumizi yao ya kila siku; na hata walipojua ya kuwa wana mali na utajiri uliozidi mahitaji yao,hawakumuuliza Mungu wala Musa juu ya matumizi yake!

Kilichotokea ni wao kutengeneza ‘ndama’ kwa kutumia utajiri huo, walipoona Musa amechelewa kuleta ‘taarifa’ ya kikao chake na Mungu kilichohusu matumizi yaliyokusudiwa juu ya utajiri wao! Soma Kutoka 32:1-7!

Kabla Musa hajawaeleza sababu ya wao kupewa utajiri uliozidi mahitaji yao ya wakati ule, wakautumia utajiri huo kutengeneza ‘ndama’, - na hali yao ya kiroho na kiuchumi ikaharibika!

Ukifuatilia habari hii kwa makini, kufuatana na ujumbe wa unabii kwa Tanzania, utaona ya kuwa wana wa Israeli walipewa utajiri kwa msaada wa upako wa Mungu KABLA Musa hajapewa maagizo na maelekezo ya ujenzi wa hema.

Hii ilikuwa ni kufuatana utaratibu wa ki-Mungu wa kutayarisha utajiri wa upatikanaji mahitaji ya kazi yake KABLA hajaagiza kazi yake kufanywa!

Musa alipopanda mlimani (Kutoka 25:1-9), jambo la kwanza aliloambiwa ni matumizi ya utajiri waliokuwa nao wana wa Israeli waliopewa walipokuwa wakitolewa Misri. Kazi yake ilikuwa ni kujengea hema!

Kila mtu anayepewa utajiri mwingi kuliko mahitaji yake, na hajui kwa nini amepewa, - asipokuwa mvumilivu kusubiri maagizo ya Mungu, -atajikuta ametengeneza ‘ndama’, - na tangu wakati huo hali yake ya kiroho na ya kiuchumi inaharibika!

Je!unajua kwa nini una mali nyingi zaidi ya mahitaji yako ya kawaida? Inawezekana una fedha, magari, nyumba, na mali zingine kuliko mahitaji yako ya kawaida, - kwa nini?

Kwa nini Mungu akupe utajiri mwingi namna hiyo unaozidi mahitaji yako? Sababu yake ni hii: Kuna maagizo atakayopewa ‘Musa’ yatakayohitaji sehemu ya utajiri wako, ili maagizo hayo yatekelezeke kikamilifu katika muda uliopangwa, na bila ‘Musa’ kuhangaika juu ya upatikanaji wake!

Utajiri waliopewa wana wa Israeli wakati ule uliokuwa sio wa mtu mmoja, bali taifa zima la Israeli lilitajirishwa! Ikiwa Mungu aliweza kutajirisha taifa zima la watu wake wakati ule, basi, anaweza tena kutajirisha taifa zima la watu wake nchini Tanzania!

Je! Unaamini hili linawezekana? Mimi ninaamini kwa moyo wangu wote! Na ndiyo maana nakupa mifano hii mbalimbali ya kibiblia juu ya utaratibu wa Mungu, ili na wewe imani yako iongezeke juu ya kutimizwa kwa neno alilosema Mungu juu ya Tanzania.

Alimwandaa Adamu kwa njia hii hii! Alimtunza nabii Eliya kwa utaratibu huu huu! Alimsaidia Musa kwa kutumia njia hii hii! Na sisi ninauhakika utatusaidia na kututunza kwa njia hii hii aliyotumia kwa wenzetu waliotutangulia!Hebu tuangalie mfano mwingine tena mwezi ujao wa Septemba 2005! Naamini hujachoka na mifano hii!

Mungu wetu akubariki kwa baraka zote alizozikusudia kwa ajili yako.
 

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.