Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Februari 2005                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


BARUA YA MWEZI FEBRUARI 2005

Bwana Yesu yu Hai! Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo!

            Mwezi uliopita (Januari) tulianza kwa kukueleza yale ambayo Mungu alisema na sisi juu ya mipango yake ya kuitembelea Tanzania – kwa upako wa utajiri na ule wa uamsho. Na kwamba upako wa uamsho utakuja baada ya upako wa utajiri kuletwa kwanza. 

Katika barua ya mwezi huu tunataka tukupe uthibitisho wa kwanza wa kibiblia juu ya jambo hili.

Je kuna uthibitisho wa kibiblia juu ya mungu kuleta upako
 wa kupata utajiri kwanza kabla ya upako wa uamsho?

Ndiyo! Kuna sehemu nyingi katika biblia zinazothibithisha jambo hili. Ninaamini uthibitisho utakaouona katika sehemu hizi nne utakupa uhakika ya kuwa ni Roho Mtakatifu aliyasema nasi juu ya jambo hili.

Uthibitisho wa Kwanza

Kumbukumbu la Torati 8:18

Ngoja twende pole pole halafu Mungu atasema na wewe na kila asomaye baru hii kila mtu kwa nafasi yake; maana ninaamini Mungu amekuongoza kuisoma barua hii kwa makusudi muhimu, na si kukupotezea muda. Maana kuna shughuli nyingi sana ambazo ungekuwa unafanya wakati huu badala ya kusoma barua hii, lakini Mungu amekuweka hapo uisome yote. Kuna sababu muhimu!

Kumbukumbu.8:18 anasema hivi, “Bali utamkumbuka Bwana Mungu wako, maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri, ili kulifanya imara agano lake alilowaahidia baba zako hata hivi leo”

Huu mstari ni mzuri sana, na watu wanausoma sana, lakini utazame leo kwa namna hii; Bwana ndiye atupaye nguvu, (nguvu tafsiri nyingine ni upako); upako wa kupata utajiri. Kama vile ambavyo kuna upako wa kuhubiri, kuna upako wa kufundisha, kuna upako wa kuwa mchungaji, kuna upako pia wa kuwa tajiri.

“ Upako” maana yake ni uweza wa Mungu ulioko ndani ya Roho Mtakatifu kwa ajili yetu sisi kutuwezesha tuwe jinsi Mungu anavyotaka tuwe, na tufanye kile ambacho Mungu anataka tufanye, Bwana Yesu asifiwe!

Hiyo ni sehemu ya kazi ya upako. Kazi mojawapo ya upako ni kutuwezesha, na ndio maana Roho Mtakatifu anaitwa Msaidizi.

Ukiomba msaada kwa Mungu hamtumi Yesu wakati huu, maana alikwishamtuma, alikwishakuja akafanya kazi yake na akaimaliza akasema, ‘Imekwisha’ akarudi juu. Na kabla ya kuondoka Yesu Kristo akasema ataletwa msaidizi mwingine anayeitwa Roho Mtakatifu. (Soma Yohana 16:7-15). Roho Mtakatifu ndiye anayewakilisha uungu wote wa Yesu na Mungu Baba hapa duniani wakati huu.

 Roho Mtakatifu alipoteremka hakuja hivi hivi, ndani yake alibeba msaada kutoka kwa Mungu, huo msaada unaitwa upako, Bwana Yesu asifiwe!

Sasa, inategemea unataka msaada wa namna gani, kama unataka msaada wa kuhubiri, uko upako mahususi (very specific) kwa ajili ya kuhubiri. Kama unataka upako wa kuwa mchungaji, upo upako wa kufanya kazi hiyo; ikiwa unataka upako wa kuendesha gari upo, unataka upako wa kusonga ugali utapata; hakuna shida kabisa! Ukitaka upako wa kuwa tajiri upo pia!

Sasa angalia anasema, huu utajiri ambao unakuja kwa staili hii, sio utajiri wa kawaida, anasema “nguvu za kupata utajiri ili” (hebu sema ‘ili’). Ni utajiri ili kulifanya imara agano. Neno “ili” ndilo linalotuonyesha ya kuwa kuna sababu ya mtu kupewa nguvu za kupata utajiri.

 Tunafahamu ya kuwa kuna maagano mawili makubwa kwenye biblia. Kuna agano la kale na kuna agano jipya. Na jumla ya maagano yote mawili maana yake ni hii; Mungu pamoja na wanadamu. Ni mapatano na makubaliano kati ya Mungu na mwanadamu juu ya kupatana na kuishi tena pamoja milele. Kuna mapatano ya kwanza ambayo biblia inasema yalikuwa na mapungufu (Waebrania 8:7). Ndio maana ilibidi yawepo mapatano ya pili.

 Agano la kwanza lilikuwa vivyo hivyo, Mungu alitaka kukaa pamoja na wanadamu, agano la pili katika damu ya Yesu sio tu kwamba anataka kukaa pamoja na wanadamu lakini sasa anataka kukaa ndani yao. Kwa hiyo anaposema kuimarisha agano, maana yake anataka kuimarisha kuwepo kwake katikati ya watu na ndani ya watu.

Wale ambao hawafahamu hili, maana yake ni kuhubiri injili watu waokoke, watu wanapookoka agano linaimarika. Na kadri watu wanaookoka wanapoimarika kutembea ndani ya Bwana, agano linaimarika. Kadiri watu wanavyoendelea kupata faida zilizotokana na msalaba, agano linaimarika, Bwana Yesu asifiwe!

Ukienda na picha ya namna hiyo, maana yake ni kwamba kabla ya agano kuimarishwa lazima upako wa utajiri uje kwanza, ndivyo mstari huu wa kumbukumbu ya Torati 8:18 unavyosema! Unaona ninachoona?

Ok! Anasema hivi, “Bali utamkumbuka Bwana Mungu wako maana ndiye akupaye nguvu za kupata utajiri ili kulifanya imara agano lake”. Maana yake agano haliwezi likafanyika imara mpaka kwanza umepata nguvu za kupata utajiri!

Maana utajiri huo ndio unaokusaidia kuimarisha agano lake. Maana yake kabla injili haijahubiriwa lazima kwanza upako wa utajiri uweze kuja ili kufanya injili ipate kuhubiriwa!

Huu utajiri sio utajiri wa kawaida! Ni utajiri unaokuja sawasawa na mahitaji ya kuimarisha agano! Hauji sawasawa na mahitaji yako ya kawaida, bali, unakuja sawasawa na mahitaji ya kuimarisha agano. Kwa hiyo utapewa utajiri over and above your normal requirements au kwa tafsiri ya kiswahili maana yake utapewa utajiri zaidi ya unavyohitaji kwa ajili ya mahitaji yako ya kawaida!

Si utajiri mdogo, Roho Mtakatifu aliniambia “ninatafuta watu watakaokuwa mawakili wa pesa na mali ninayotaka kuteremsha huku Tanzania kwa ajili ya kazi yangu”. Anatafuta watu.  Kwa sababu hawezi kumpa kila mtu hizo pesa na mali, kwa sababu si kila mtu anaweza akatumia jinsi Mungu anavyotaka.

 Ndio maana ninasema huu ujumbe ni kwa wale wanaotaka kutajirika ki-Mungu na kwa ajili ya kusudi la Mungu. Si ujumbe kwa ajili ya kila mtu. Je! Uko tayari Mungu akutajirishe halafu akuongoze kuutumia huo utajiri kwa kusudi lake?

Huu ni uthibitisho wa kwanza wa kibiblia juu ya jambo hili ambalo Mungu anataka kulifanya Tanzania. Hebu tuangalie uthibitisho wa pili – katika barua ya mwezi ujao (Machi). Kwa hiyo usiache kuisoma.

Tuzidi kuombeana!
 

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.