|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Salamu katika Jina la Yesu Kristo, Tulipokuwa Mwanza Septemba 2004 siku mbili kabla ya kuanza ile semina, kuna maswali machache ambayo nilikuwa namuuliza Mungu moyoni mwangu, hasa juu ya mzigo ambao ameweka ndani yangu wa kuwafundisha watu juu ya masuala ya mafanikio ya kiuchumi kibiblia. Nimejaribu kuweka hili somo pembeni ili nifundishe mengine lakini imeshindikana kwa muda mrefu sana! Ni sehemu chache tu peke yake ambazo nimefundisha masomo mengine kwa mwaka wote wa 2004. Lakini karibu mwaka mzima toka mwaka 2003 mwishoni, huku ndani yangu, hata nifanyeje, hata nikiomba, nikilala, nikitembea, kuna huo ujumbe wa watu wa Mungu kufanikiwa kiuchumi unazunguka! Nimeandika na kuandika na kuandika haukatiki! Ni kama ‘mlenda’- haukatiki! Nikaona ninahitaji kumuuliza Mungu juu ya jambo hili! Sijawahi kukaa na somo moja muda mrefu hivi. Ok, nimewahi kukaa na somo la Upako na nikafundisha mpaka mahali fulani, kuna somo la Nafsi likaenda mpaka mahali fulani, la Majeraha mpaka mahali fulani, lakini sio kwa staili hii ya somo la uchumi - na nilitaka kujua kuna nini nyuma ya msukumo huu wa Roho Mtakatifu juu ya somo hili. Kwa hiyo nilipokuwa ninamwomba Mungu juu ya hilo alinisemesha sentensi ya ajabu sana; alisema hivi, Ninakwenda kuitembelea Tanzania tena, na kuleta uamsho ambao hamjawahi kuuona. Lakini kabla sijaleta upako wa uamsho, nitaleta kwanza upako wa utajiri juu ya watu wangu, ili waweze kulipia gharama zitakazoambatana na uamsho unaokuja. Ngoja nirudie tena kwa upana hiyo sentensi; aliniambia anakwenda kuitembelea Tanzania tena, wale wanaoelewa maana ya ‘tena’ maana yake aliwahi kututembelea miaka ya zamani. Lakini kuna ujilio maalum (au “special visitation” inakuja nyingine) na hauko mbali, ambapo Mungu anakwenda kuleta uamsho katika kanisa, na katika nchi hii kwa namna ambayo hatujawahi kuona. Lakini kabla ya kuleta huo uamsho, anakwenda kuleta kwanza upako wa utajiri ili kanisa lake au watu wake wawe na fedha na mali zitakazolipia gharama za uamsho unaokuja. Mungu aliponisemesha namna hiyo, nikamwambia ninaomba mistari ya biblia inayothibitisha ukweli na uhalali wa jambo hili! Sasa unajua si kitu cha kawaida uzungumze na watu wanaofuatilia maandiko sawasawa ya kwamba Mungu anasema ya kuwa kabla sijaleta upako wa uamsho analeta kwanza upako wa utajiri. Akili haikubali! Kwa hiyo nikamwambia Mungu naomba mistari ya kuthibitisha anachosema. Sijawahi kuona biblia kwa namna hiyo na kwa msisitizo niliouona baada ya kuomba nipewe mistari ya biblia. Ok, nilikuwa ninaona hivi vitu kwenye biblia na hilo jambo ambalo Mungu analizungumzia huko nyuma, lakini nilikuwa sijawahi kuona kwa msisitizo wa namna hiyo. Niliona msukumo na uhuisho mpya katika mistari ya biblia niliyopewa. Ndio maana kwa mwaka huu wa 2005 nataka nikuletee kwa njia ya barua mambo kadhaa ambayo Mungu alinieleza juu ya jambo hili. Naamini utapata nafasi ya kuzifuatilia na kuzisoma na kuzitafakari barua zote 12 za mwaka huu. Mimi na mke
wangu tunakutakia baraka za Bwana Yesu. Tuombeane. Usiache kusoma barua
yetu ya mwezi ujao (Februari) ili ujue upate kujua zaidi kile ambacho
Mungu ametueleza juu ya jambo hili. |
|