Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Julai 2005                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


BARUA YA MWEZI JULAI 2005

Salamu katika Jina la Yesu Kristo.

            Tunaamini uko tayari kuendelea tena katika mwezi huu kujifunza zaidi juu ya utendaji kazi wa Mungu alioukusudia Tanzania. Mwezi huu tunataka uone mfano mwingine ambao unaonyesha ya kuwa Mungu huwa anatanguliza kwanza upako wa utajiri kabla ya upako wa uamsho.

Ni muhimu imani yako
juu ya jambo hili iongezeke

Nia ya kukupa mifano hii mbalimbali ni ili imani yako ipate kuongezeka katika jambo hili muhimu ambalo Mungu amesema juu ya Tanzania. Kufuatana na Waebrania 11:1; “imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana”.

Tunatarajia kutembelewa na Mungu tena! Uhakika wa kutembelewa na Mungu tunaupata kwa neno la Kristo. Maana Warumi 10:17 inasema; “Basi imani, chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo”.

Ndio maana ni muhimu uchunguze maandiko pamoja nami, ili upate uhakika (imani) ya kile tunachokitarajia kuwa kunakuja nchini. Ikiwa Mungu aliwahi kulifanya jambo kama hili zamani, basi anao uwezo wa kulifanya jambo kama hili tena!

Ikiwa Mungu alimsaidia Adamu katika bustani ya Edeni, anaweza vile vile akatusaidia katika nchi ya Tanzania. Ngoja nirudie kusisitiza jambo hili ya kuwa: ikiwa Mungu aliwahi kulifanya jambo kama hili zamani, basi anao uwezo wa kulifanya jambo kama hili tena akitaka!

Kwa nini nasisitiza hili?Ni ili tarajio lako liongezeke ndani yako, au hakika ya mambo yatarajiwayo ndani yako iongezeke juu ya Tanzania.

Mungu hana kiegeugeu! Ndivyo Malaki 3:6a anavyotuambia! Tena katika Waebrania 13:8 tunasoma ya kuwa; “Yesu Kristo ni yeye yule yule, jana na leo na hata milele”. Ikiwa na maana ya kuwa alichokifanya jana, anaweza kukifanya na leo pia. Na anachokifanya leo, anaweza kukifanya wakati wowote ujao!

Kwa hiyo kama anasema anakwenda kuitembelea Tanzania tena kwa namna ambayo ataleta kwanza upako wa kupata utajiri, kabla ya kuleta upako wa Uamsho, basi, ndivyo itakavyokuwa, kwa kuwa ndivyo ilivyowahi kuwa huko nyuma!

Ni muhimu imani yako juu ya jambo hili uongezeke, la sivyo maandalizi yako kwa ajili ya kusubiri udhihirisho au utimilifu wa neno la unabii huu yatakuwa hafifu.

Baada ya kukueleza hayo, hebu sasa tuangalie mfano mwingine katika biblia ambapo upako wa kupata utajiri ulitangulia kabla ya kupata uamsho. Je!uko tayari?

Mfano wa Nabii
Eliya

Tunazisoma habari hizi katika kitabu cha 1 Wafalme 17:1-6. Ni habari ambazo wengi wamezisikia na kuzisoma. Zinaanza na mazungumzo kati ya nabii Eliya na Mfalme Ahabu, na kuishia na neno la unabii ya kuwa hakutakuwa na mvua kwa muda wa miaka mitatu na nusu hadi nabii Eliya aseme tena.

Baada ya unabii huo, neno la Bwana likamjia nabii Eliya kusema; “Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani. Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko” (1Wafalme 17:3,4)

Nabii Eliya akafanya kama alivyoambiwa na Bwana, na Kunguru wakafanya walivyoambiwa na Bwana, na nabii Eliya akala na kunywa bila shida katikati ya ukame ulioikumba nchi ile wakati ule!

Jambo la msingi ninalotaka ulione hapa ni kwamba: Mungu aliwatayarisha na kuwaamuru Kunguru wamlishe nabii Eliya KABLA hajampa Eliya maelekezo ya mahali pa kwenda! Kwa lugha iliyo nyepesi ni kwamba aliwaandaa Kunguru kwanza, kabla ya kumwaandaa Eliya.

Mungu alichokuwa anafanya ni kufuata utaratibu na tabia yake ya kutuma kwanza upako wa kuandaa upatikanaji wa utajiri wa mahitaji ya mtu kabla ya kumpa mtu maelekezo ya kufanya. Hili huwa analifanya ili mtu wake anapofanya maelekezo aliyompa, mahitaji yake ya kila siku yawe yanapatikana pia!

Je! Unaliona hili? Ikiwa Mungu alimsaidia Eliya, basi, anaweza kukusaidia na wewe, ikiwa utafuata maelekezo yake!

Ndiyo! Ndivyo ilivyo! Hebu tafakari tena habari hii ya kulishwa kwa Eliya na Kunguru. Kama Kunguru waliagizwa kumlisha Eliya “mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni”; hii inatuonyesha ya kuwa Mungu aliandaa ‘mkate na nyama’ (chakula) KABLA ya kuwaandaa Kunguru; na aliwaandaa Kunguru kukichukua hicho chakula kwa utaratibu huo, KABLA ya kumwambia Eliya kwenda mahali ambako Kunguru wameagizwa wamlishe huko!

Unalipata hili! Mungu aliandaa mkate na nyama (chakula kwa ajili ya asubuhi na jioni – no lunch! – bila chakula cha mchana), na Kunguru wakapewa kipimo cha kubeba kwa kila mlo. Haya yalifanyika KABLA Eliya hajaelezwa au hajaelewa kinachofuata katika maisha yake.

Eliya alipoelezwa kwenda kwenye kijito cha Kerithi, TAYARI mipango ya kutunzwa kwake ilikuwa imeandaliwa.

Naamini unajua ya kuwa Mungu anamtumia Roho wake Mtakatifu kufanya mapenzi yake hapa duniani. Tena, naamini unajua ya kuwa Roho Mtakatifu anatumia upako wake katika kuyatimiza mapenzi na makusudi mbalimbali ya Mungu.

Ikiwa ndivyo unavyoamini, basi, ni rahisi kwako pia kuamini ya kuwa Mungu alimtuma Roho wake kuandaa chakula cha Eliya, na kuwaandaa Kunguru kumpelekea Eliya chakula hicho. Hii ina maana upako wa kupata utajiri wa mahitaji, ulitumwa kufanya kazi kwa ajili ya Eliya kabla ya upako wa utumishi kumpa maagizo zaidi.

Mungu anasema na watu wake katika nchi ya Tanzania ya kuwa anakwenda kufanya jambo kama hili kwa Watanzania, kama vile alivyofanya kwa Eliya!Anatuma kwanza upako wa kupata utajiri wa mahitaji ya watanzania, kabla ya kuleta upako wa uamsho, ili gharama za mahitaji zitakazotokea wakati wa uamsho ziweze kutunzwa ipasavyo!

Jambo jingine muhimu katika habari hii ya Eliya na Kunguru ni juu ya utii wao kwa neno la Mungu lililowapa maagizo ya vitu vya kufanya. Utunzwaji wa gharama za Eliya kuhusu mahitaji yake ya chakula ulitegemea utii wa Eliya na kutii wa Kunguru kwa pamoja kufanya walichoagizwa na neno la Bwana lililowaagiza kukutana kwenye kijito cha Kerithi!

Je! Umewahi kufikiri Kunguru wangefanya nini kama Eliya asingekwenda kwenye kijito cha Kerithi kama neno la Bwana lilivyomwelekeza kufanya? Kunguru wasingekwenda kwenye kijito cha Kerithi! Wala Roho Mtakatifu asingewaongoza kumfuata Eliya kumfuata na kumlisha Eliya huko alikokwenda kinyume na agizo la neno la Bwana kwake katika siku hizo.

Ukisoma habari hii vizuri na kuitafakari utaona ya kuwa hata kama Mungu aliwaandaa na kuwaamuru Kunguru wamlishe Eliya kabla ya kumpa Eliya maagizo zaidi katika utumishi wake; Kunguru hawakutekeleza walichoamriwa hadi Eliya alipochukua hatua ya kutii KWANZA alichoagizwa na Mungu.

Soma mwenyewe ujionee!Biblia inasema; Eliya “akaenda akafanya kama alivyosema Bwana; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerithi, kinachokabili Yordani. Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito”

Ikiwa rahisi kwa Kunguru kutekeleza walichoamriwa, baada ya Eliya kutekeleza alichoambiwa! Eliya hakupewa mahitaji yake ya chakula cha kila siku kwa kuwa alikuwa mtumishi wa Bwana; bali alitunzwa kwa sababu alikuwa mwaminifu kutii neno la siku au neno la wakati huo lililotumwa kwake na Bwana!

Jifunze jambo hapa! Unaweza ukawa mtumishi wa Mungu uliyepakwa mafuta; lakini fahamu hili, Mungu hatatunza mahitaji yako ya kila siku kwa sababu tu wewe ni mtumishi wake, la hasha! Bali atatunza mahitaji yako ya kila siku kwa kuwa umesikia na umetii neno la siku au neno la wakati ulilopewa na Bwana!

Usipokuwa mtii wa neno uliloagizwa ujue hutaonana na ‘kunguru’ wako au yule aliyeagizwa akutunze na kukulisha wakati unatekeleza neno hilo!

Hili ni muhimu kwa sababu tunaona ya kuwa neno la siku lilipobadilika kwa Eliya hata utunzwaji wa mahitaji ya Eliya ulibadilika! Kutunzwa na kulishwa kwake kulitegemea utii wa neno hili la pili au kwa wakati huo kwake lilikuwa neno la ‘sasa’.

‘Kunguru’ waliagizwa kumtunza wakati anatekeleza neno au agizo la kwanza.Lakini hawakuamiriwa kumtunza wakati anatekeleza neno la pili, kwa sababu mama mjane wa Sarepta alikuwa amepewa agizo hilo au ‘tenda’ hiyo!

Tunasoma katika 1 Wafalme 17:8,9 ya kuwa: “Neno la Bwana likamjia (Eliya), kusema, ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni,ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe”

Roho Mtakatifu na upako wake aliingia kazini tena! Utaratibu wake ule ule! Mungu alimwamuru mjane wa Sarepta amlishe Eliya KABLA Mungu hajamwambia Eliya kwenda Sarepta!

Tunaona tena upako wa kupata utajiri wa mahitaji ukifanya kazi KABLA ya upako wa utumishi uliokuwa mbele ya Eliya!

Ilikuwa wazi wa nabii Eliya ya kuwa muda wa kulishwa na ‘kunguru’ umekwisha, na kulishwa kwake na mama mjane wa Sarepta kulitegemea utii wake juu ya agizo la kwenda Sarepta!Asingekwenda asingekula! Kunguru wangemtunza Sarepta kama wangeamriwa kufanya hivyo, lakini agizo walilopewa halikuhusu safari ya Eliya ya kwenda Sarepta! Safari ya Sarepta aliandaliwa mtu mwingine kumtunza!

Kumbuka: Mungu akikupa kazi au agizo la kufanya, anakupa pia ndani yako neno linalokupa hakika (imani) ya kutunzwa kwa mahitaji yako ya kila siku utakapokuwa unatekeleza ulichoagizwa!

Ndivyo inavyotakiwa kuwa wakati wote, na hasa wakati wa uamsho utakapokuja. Kutunzwa kwa mahitaji ya kila siku ya watu wa Mungu kutategemea utii wao wa maagizo ya Mungu watakayopewa wakati huo!

Jiambie peke yako kwa kusudi la kujitia moyo ya kuwa: “kama Mungu alifanya kwa Eliya alipotii neno lake, ndivyo atakavyofanya na kwangu ninapotii neno lake!” Kwa nini? Kwa sababu Mungu hana upendeleo, wala hana kigeugeu!

Usisahau kusoma barua yetu ya mwezi ujao wa Agosti 2005. Tutaendelea kukushirikisha zaidi juu ya jambo hili kwa kukupa mfano mwingine wa kukusaidia.

Tuzidi kuombeana.
 

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.