|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Tunakusalimu katika Jina la Yesu. Jina lipitalo kila jina! Jina hili la Yesu litukuzwe milele katika maisha yako! Ndicho tunachokuombea kwa Mungu kwa wakati huu. Sisi tunaamini ya kwamba kile alichotuambia Mungu ya kuwa atatutembelea tena hapa Tanzania kitatokea hakika. Tena kitatokea kwa utaratibu aliousema – kwamba upako wa utajiri utakuja kabla ya upako wa uamsho. Hata biblia inathibitisha hili kama tulivyoona katika barua tulizokuandikia miezi iliyotangulia.
Ikiwa Mungu aliwahi
kufanya jambo kama Ni kweli kabisa! Na ni jambo linalotakiwa kuaminika kabisa, na mtu yule anayefuatilia mambo ya Mungu anayoyafanya duniani. Ninachotaka ujue na kuamini ni kwamba, ikiwa Mungu aliwahi kufanya jambo kama hili zamani, basi, hata leo uwe na uhakika anaweza kulifanya tena! Kwa nini ninasema hivi kwa msisitizo mkubwa namna hii? Ni kwa sababu, “Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele” (Waebrania 13:8). Kwa maneno mengine tunaweza kusema Yesu Kristo habadiliki, jana na leo na hata milele! Alichokifanya jana, ana uwezo wa kukifanya leo, na ana uwezo wa kukifanya hata baadaye. Wazo hili tunalipata pia katika kitabu cha Malaki 2:6a, Mungu anaposema: “…..mimi ni Bwana sina kigeugeu …..” Nataka kurudia tena kusisitiza ya kuwa, ikiwa Mungu aliwahi kufanya jambo kama hili zamani, basi, hata leo uwe na uhakika anaweza kulifanya tena! Katika mfulululizo wa barua zilizopita nimekueleza, tena kwa uthibitisho wa mistari kadhaa ya neno la Mungu ya kuwa, Mungu amekusudia kuitembelea Tanzania tena. Na atakapoitembelea ataleta kwanza upako wa kupata utajiri kabla ya upako wa uamsho. Sababu kubwa ya kufanya hivi, ni ili kuwasaidia watu wake, wawe na utajiri wa kuweza kulipia gharama, ambazo ki-kawaida huwa zinaambatana na uamsho. Kwa kuwa si watu wengi wameliona hili likitokea katika maisha yao, wanakuwa wazito kuliamini, hata kama wana uthibitisho wa neno la Mungu juu ya jambo lenyewe. Ndio maana nimeona nikuonyeshe tena katika biblia ya kuwa hivi ndivyo Mungu alivyokuwa anafanya mara nyingi pamoja na watu wake. Je!uko tayari nikuletee mifano hiyo? Kama uko tayari, sema kwa sauti “niko tayari”. Ni maombi yangu ya kuwa upako wa Roho Mtakatifu utakuhuisha kwa upya ndani yako, ili ufahamu wako uongezeke katika kuujua na kuuelewa mfumo wa Mungu unavyofanya kazi.
Mfano wa Je!Unajua au unakumbuka jinsi Mungu alivyoumba ulimwengu? Mwanadamu aliumbwa katika siku ya ngapi? Mwanadamu aliumbwa katika siku ya sita! Tunasoma katika biblia ya kuwa: “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba mwanamume na mwanamke aliwaumba ….Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita” (Mwanzo 1:27,31) Mungu aliufurahia uumbaji wake, na tunafahamu siku iliyofuata baada ya kumuumba mwanadamu, ile siku ya saba, alipumzika! Unaelewa ni kwa nini mwanadamu aliumbwa katika siku ya sita, na hakuumbwa katika siku ya kwanza? Au katika siku ya pili, au katika siku ya tatu; au katika siku ya nne; au katika siku ya tano? Kwa nini amuumbe mwanadamu katika siku ya sita? Jibu tunalipata kwa kuangalia na kutafakari juu ya kile ambacho alifanya katika siku hizo tano za uumbaji. Nikitafakari na kuchambua yale yaliyofanyika ndani ya siku hizo tano, ninapata ufahamu ya kuwa; Mungu alikuwa anamwandalia mwanadamu, mambo yote muhimu atakayoyahitaji, kabla hajamuumba ili apate kulitimiza kusudi la Mungu akiwa hapa duniani. Unaliona hilo? Mungu alimwandalia mwanadamu kwanza utajiri wa mahitaji yake, kabla hata mwanadamu hajaumbwa. Na maandalizi hayo yalikuwa muhimu sana na mengi kiasi ambacho Mungu hakutaka kuyafanyia haraka. Mungu aliamua kutumia siku tano kumwandalia mwanadamu utajiri wa mahitaji yake, utakaomsaidia katika wito wake atakapokuwa duniani! Ilikuwa ni muhimu kwa Mungu kuandaa kwanza mahali pa mtu kuja kukaa, na pia ahakikishe ana kila haja atakayoihitaji, kwa ajili ya kutembea vizuri kwenye lile kusudi la Mungu. Kwa sababu ya umuhimu wa jambo lenyewe, ilimchukua siku tano kutayarisha hayo mazingira na utajiri wake! Ili sasa, mwanadamu akiumbwa au akiletwa eneo hilo katika siku aliyoikusudia, aweze kukuta mambo muhimu yote atakayoyahitaji yako tayari. Baada ya kufanya hayo, siku ya saba Mungu akapumzika! Ikiwa Mungu alifanya jambo hili kwenye bustani ya Edeni, ili ampe maandalizi muhimu mtu wake, uwe na uhakika anaweza kulifanya jambo hili tena kwa watu wake waliomo Tanzania! Kwa nini nasema hivi?Kwa sababu Yesu Kristo ni Bwana, hana kigeugeu, ni yeye yule, jana, na leo, na hata milele! Sasa unisikilize! Mungu akikuweka mahali kwa utumishi wake, au kwa kusudi lake, ujue basi tayari amekuwa na “siku tano” za kukuandalia mazingira na utajiri wa mahitaji utakaokusaidia kulipia gharama za utumishi uliopewa mahali hapo! Je!unalipata hili? Sema ‘ndiyo nalipata!’ – Kama unalipata! Siku tano zako ni zipi na ni ngapi siwezi kujua, ila ya kwamba zipo nina uhakika! Siku tano zako zinaweza kuwa siku kadhaa, au wiki kadhaa, au miezi kadhaa, au miaka kadhaa…… Hii ni siri ya ajabu sana! Mimi sizijui ‘siku tano’ zako ni zipi na ni ngapi! Lakini ya kwamba zipo nina uhakika, labda kama unafanya kile ambacho Mungu hakukupangia kukifanya! Na labda kama upo mahali ambapo Mungu hakukupangia ili kufanya alichokuitia kukifanya ukiwa hapa duniani. Na pia,inawezekana upo katika eneo ambalo Mungu amekupangia, na unafanya kile ambacho Mungu amekupangia,lakini kwa namna moja au nyingine muunganiko wako wa utajiri wa mahitaji ulioandaliwa tayari kwa ajili yako si mzuri. Inawezekana kabisa dhambi ikawa chanzo cha kuvurugika kwa uchumi wa mtu, kama ilivyokuwa kwa Adamu katika bustani ya Edeni. Na dawa yake ni toba! Hii ni kwa sababu dhambi ilipoingia duniani kupitia katika bustani ya Edeni ilibadili sana mfumo wa uchumi wa dunia mzima. Watu wengi sana wanafahamu dhambi ilivyoleta shida, na kwa ajili hiyo watu wanashindwa kwenda mbinguni; lakini si wote hao wanajua ni kwa kiasi gani dhambi imeathiri pia uchumi wa dunia hii! Fungua kitabu cha Mwanzo sura ya tatu utaona mambo kadhaa juu ya jambo hili la kuathirika kwa uchumi. Lakini kumbuka si kila wakati dhambi ndio chanzo cha kuvurugika uchumi wa mtu. Wakati mwingine zinaweza zakawa ni sababu zingine kabisa mbali na dhambi. La msingi nililotaka ujue ni kwamba mahitaji ya Adamu yaliandaliwa kwanza kabla hajaumbwa. Unaelewa sasa kwa nini mwanadamu aliumbwa siku ya sita na hakuumbwa siku ya kwanza? Ni kwa sababu Mungu alikuwa anamwandalia kila kitu anachokihitaji kufanikisha wito wake uliomleta duniani. Mungu alitumia siku tano kumwandalia mwanadamu ‘utajiri’ wa kumsaidia katika wito wake atakapokuwa duniani. Ilikuwa muhimu kwa Mungu kuandaa mahali pa mtu kuja kukaa na kuhakikisha ana kila haja anayohitaji kwa ajili ya kutembea vizuri kwenye lile kusudi la Mungu kiasi ambacho ilimchukua Mungu siku tano kutayarisha hayo mazingira na utajiri wake . Ili siku ya sita mwanadamu akiletwa akute kila kitu kimewekwa tayari. Siku ya saba Mungu akapumzika! Katika barua ya mwezi ujao wa Julai 2005, tutaendelea kukuletea mifano mingine iliomo ndani ya biblia juu ya kufanyika kwa jambo kama hili duniani katika siku za nyuma. Kumbuka kama Mungu aliweza kumsaidia Adamu, ujue basi anaweza kukusaidia na wewe – maana ni Mungu asiye na upendeleo. Ubarikiwe Milele
na Mungu wetu! |
|