|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Salamu katika Jina la Yesu. Mimi na mke wangu, Diana, tunajua ya kuwa Roho Mtakatifu amekuongoza kuisoma barua yetu hii ya Machi 2005, ili upate kujua uthibitisho wa kibiblia juu ya mipango aliyonayo Mungu juu ya Tanzania. Katika barua ya Februari 2005 tulikushirikisha uthibitisho wa kwanza juu ya Mungu kuleta upako wa utajiri kwanza kabla ya upako wa uamsho katika Tanzania. Sasa tukuangalize juu ya uthibitisho wa pili. Uthibitisho wa Pili 1 Wakorintho 9:7 Angalia mstari huu: 1Wakorintho.9:7 anasema hivi, “Ni askari gani aendaye vitani wakati wowote kwa gharama zake mwenyewe?” Unajua maana yake nini mstari huu? Maana yake ni kwamba kabla Mungu hajanyanyua askari aende vitani, ananyanyua na kumwandaa kwanza mtu wa kumgharamia askari huyo atakapokuwa vitani. Na akimnyanyua mtu wa kumgharamia askari, hawezi kumpa utajiri kwa ajili ya gharama zake tu yeye mwenyewe ili aweze kugharamia maisha yake tu peke yake, lazima katika utajiri atakaomletea kwenye maisha yake, utakuwa mwingi ili aweze pia kulipa mahitaji ya askari vitani. Kabla mtumishi hajanyanyuliwa kwa ajili ya kazi ya Mungu, lazima Mungu anyanyue kwanza mtu atakayemgharamia katika huo utumishi. Kabla askari hajaenda vitani, gharama yake ya kuwa vitani, huwa kwanza anaandaliwa mtu atakayeitunza. Wale ambao walikuwepo wakati wa ile vita ya Tanzania na Idd Amin wa Uganda wanaelewa kitu ninachosema. Sisi tuliokuwa tunakwenda kwenye hiyo vita hatukuwa na muda wa kufikiri juu ya jinsi ya kugharamia gharama za vita. Ila tulijua aliyetutuma atatugharamia. Kupata mahitaji yako vitani kunategemea mawasiliano yako ukiwa vitani na yule aliyekutuma. Kupata mahitaji yako vitani kunategemea utii wako wa maagizo kutoka kwa kamanda wako; inategemea mahali ulipo kule vitani kama kiongozi wako wa vita anaweza akakuletea na kukufikishia mahitaji yako. Askari aliyeko vitani huwa hawazi atakula nini, au atapata wapi chakula, anajua muda wa kula ukifika chakula kitakuwepo, kisipokuwepo amefundishwa mbinu za kuishi na kutafuta chakula akiwa vitani. Mungu anataka kututeremshia upako kwa ajili ya uamsho hapa nchini. Hatuzungumzii juu ya uamsho mdogo. Ikiwa umepita na kuhudhuria kwenye semina tunazofanya, utatambua ya kuwa hata nusu hatujafika kwenye kitu ambacho Mungu anataka kufanya nchini, pamoja na uwingi wa watu wanaokuja katika semina hizi wakati huu. Lakini hujawahi kuona ukubwa wa uamsho unaokuja. Utaona Waarabu wakiokoka kweupe! Utaona Wahindi wakija ki-familia kuokoka kweupe! Kwa sasa hapa nchini unaenda mikoa mingine unakuta hakuna kanisa ambalo lina mkristo wa asili ya ki-hindi, wala hakuna mchungaji ambaye ameandaliwa kuwalea Wahindi kiroho. Nilipokuwa Moshi wakati fulani ikaja familia ya wahindi wanataka maombi na wanamtaka huyu Yesu tunayemhubiri. Baada ya semina inakuwaje? Nikaanza kuuliza ikiwa kuna mtu yeyote pale Moshi ambaye anatunza Wahindi kikanisa; wakaniambia hakuna. Huwezi kuwatunza wahindi walio wengi sawasawa na wakristo wengine, kwa sababu watamwona Yesu kama Mungu mwingine kati ya miungu mingi waliyonayo. Lazima awepo mtu ambaye ameandaliwa na Mungu kuwatunza na kuwasaidia pole pole mpaka waweze kuvuka katika hilo. Kuwaandaa watumishi wa namna hiyo kuna gharama. Hakuna sababu ya kuomba watoto wengi wa kiroho, halafu tunakuwa na vinyumba vya makanisa vidogo. Hakuna sababu ya kuomba uamsho mkubwa, halafu bado makanisa yana wachungaji wachache. Hakuna sababu ya kuomba uamsho mkubwa halafu bado unakuwa na kanisa lenye uwezo wa kukalisha watu kidogo. Tunazungumza habari za kuwa na kanisa linaloweza kukalisha watu elfu kumi, au elfu ishirini au zaidi. Kuyaandaa na kuyajenga makanisa makubwa hivi yanahitaji fedha nyingi. (Sikiliza) tunazungumza habari za watu wengi kuokoka kwa wingi kila siku. Mwaka 2004 waliokoka watu 50,000 katika semina tulizozifanya na uamsho bado, je, uamsho ambao Mungu anasema atauleta nchini ukija itakuwaje? Nilikuwa nimekaa kwenye hoteli moja Dar es Salaam, halafu mtu mmoja akaja akanisalimia na akasema, ndugu, wewe huwezi kujua, juzi nilikuwa nasikiliza kipindi kwenye redio Wapo, mke wangu alikuwa anaumwa. Ameingia tu ndani ya nyumba yetu akasikia kipindi chako, akasema “siendi mahali, nakaa hapa, nisikilize mahubiri” na alikuwa anaumwa sana. Akaeleza jinsi ambavyo ilipofika saa ya maombi mke wake akaweka mkono wake kwenye kichwa chake niliposema kwenye mahubiri redioni ya kuwa weka mkono mahali mtu anapoumwa.Maombi yalipoisha mke wake akapona saa hiyo hiyo! Huyo ni mtu mmoja.Huwezi kujua ni wangapi wanapata msaada, wanapona na kuokoka kwa njia ya mafundisho tunayoyarusha kwa njia ya redio. Lakini unajua gharama za kuweka vipindi katika redio kila wiki?Kwa hiyo kanisa nchini linahitaji kuandaa wachungaji, na sio wachungaji watakaowalea watu kidhehebu, bali wachungaji watakaowalea kondoo wa Mungu kiroho hata ambao hawapo chini ya makanisa yao. Kwa sababu Mungu anapotazama kanisa, hatazami kanisa kwa vikundi vikundi vinavyoitwa madhehebu ya kikristo anaangalia kanisa kama mwili wake. Anapotazama wachungaji haoni wachungaji kima dhehebu, bali anaangalia wachungaji wa kondoo kwa ajili ya kanisa lake zima, ingawa wapo katika maeneo tofauti tofauti. Usije ukategemea watu wasiomjua Mungu ndio wawe wanatoa pesa nyingi sana kwa ajili ya kulipia gharama zinazokuwepo katika kumfanya Mungu ajulikane kwa wale wasiomjua. Kanisa linatakiwa kuwa na vipindi kwenye ‘television’ vya kutosha, sio vya kubangaiza - baingaza. Kanisa litahitaji kuwa na redio (tena zaidi ya moja) ambao zitakuwa hewani masaa 24 kila siku, ili mtu akichoka usiku afungue redio na akutane na neno la kumsaidia, au ili akiingia kwenye gari aweze kusikia nyimbo za kusifu na asikie neno la kumtia moyo. Mipango yote hii inahitaji fedha, lakini zitoke wapi wakati watu wa Mungu hawana fedha za kutosha kugharamia mipango hiyo? Mungu anajua ili kuutunza na kuuimarisha uamsho – ni lazima atangulize utajiri kwa watu wake. Wewe tafuta nchi yoyote, tafuta mahali popote, tafuta kanisa lolote ambalo lilikuwa na uamsho bila kuambatana na pesa za kugharamia matunda ya uamsho ule. Uamsho huo haukudumu muda mrefu na matunda yake kwa sehemu kubwa yalipukutika. Huwezi kukaa na uamsho katika kanisa kwa muda mrefu bila ya kuwa na fedha za kutosha kulipia gharama za matunda yanayoambatana na uamsho. Wakristo wengine watahama au watapoa na wengine kufa kabisa kiroho. Wanaanza kutafuta chakula cha kutosha cha kiroho lakini hawana uwezo wa kukigharamia. Watu wengi wanaokoka lakini hawana biblia, wewe mwenyewe huwezi kuwanunulia biblia. Unaamua kuwatafutia agano jipya, agano jipya zenyewe unangojea za msaada watu wakupe, wasipokuwepo unaanza kuhangaika. Lakini uwezo wa kununua ungekuwepo, mahangaiko yasingekuwapo. Kwa hiyo tunapozungumzia habari za nchi hii kutajirika, hatuzungumzi habari za wakristo kupata fedha tu, lakini lazima kuwe na mabadiliko ya miundo mbinu ya kiuchumi katika nchi hii. Tutahubirije injili haraka haraka bila mabadiliko ya kiuchumi yaliyo mazuri? Barabara zinapokuwa mbovu, na injili inapelekwa sehemu mbalimbali kwa shida na kwa polepole sana. Barabara zikiwa nzuri, ni rahisi kuzitumia ili kuipeleka injili sehemu mbalimbali nchini kwa uwepesi na kwa haraka. Katika kumbukumbu ya Torati 8:18 Mungu anatuonyesha ya kuwa kabla ya kuimarisha agano ni lazima kwanza awe ameleta upako wa kutupa utajiri. Katika 1 Wakorintho 9:7 anatuonyesha ya kuwa hawezi akapeleka askari vitani bila wa kumgharamia. Ina maana ya kuwa kwa yule anayemgharamia askari, ndani ya zile baraka anazoletewa kwenye maisha yake kuna mali na fedha kwa ajili ya mahitaji ya askari! Tumeona uthibitisho huu wa pili wa kibiblia juu ya kile ambacho Mungu anataka kukifanya Tanzania. Hebu tuangalie sasa uthibitisho wa tatu – tutakaokuonyesha katika barua yetu ya mwezi ujao (Aprili 2005). Usisahau
kutuombea ili tuendelee kuitenda kazi ya Bwana kwa kiwango kile kile
ambacho Mungu anataka! |
|