Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Mei 2005                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


BARUA YA MWEZI MEI 2005

Bwana Yesu Asifiwe!

            Salamu kwako katika Jina la Yesu Kristo ambalo linastahili kusifiwa na kuheshimiwa na kila mtu anayempenda Mungu wa kweli.

            Mungu amekusudia kuitembelea Tanzania. Na katika utaratibu wake analeta kwanza upako wa utajiri kabla ya upako wa uamsho. Katika barua hii tunakuonyesha uthibitisho wa nne wa kibiblia juu ya uhalisi na uhalali wa jambo hili kutokea nchini.

Uthibitisho wa Nne
 

2 Wakorintho 9:10 –13

Ngoja tuangalie 2Kor.9:10-13 inasema hivi, “Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu. Mkitajirishwa katika vitu vyote, mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu. Maana utumishi wa huduma hii hauwatimizii watakatifu riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu. Kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo wanamtukuza Mungu”.

Hapa anaangalia habari ya utumishi kwa jinsi ya utoaji, watoaji ni watumishi, utoaji ni utumishi! Anasema “mkijaribiwa kwa utumishi huo”! Labda nisome ule mstari wa kumi na moja, labda hujawahi kuuona kwa namna hii, anasema, “Mkitajirishwa katika vitu vyote (hebu sema vitu vyote) anasema “mpate kuwa na ukarimu wote (sema ukarimu wote). Unisikilize, huwezi kuwa na ukarimu wote isipokuwa umekuwa tajiri katika vitu vyote!

Hainisaidii sana kuniambia Mwakasege nilitaka kukusaidia kwenye huduma lakini sina fedha za kukupa. Ndani ya moyo wako unataka sana kunisaidia kwa kulipia sehemu ya gharama na huduma niliyonayo lakini huna fedha hizo!

 Mungu anataka akufungue kwenye hilo, ili uwe tajiri katika vitu vyote uweze kuwa na ukarimu wote. Hasaidii kusema kwa kweli nitakuombea tu peke yake siihitaji maombi tu peke yake ila nahitaji maombi pamoja na fedha.

 Sasa, sikuambii ya kuwa maombi hayana sehemu yake, lazima ufahamu ya kwamba maombi yana sehemu yake, lakini Mungu hakusema toa maombi wakati unatakiwa kutoa fedha! Watumishi wengi watakuambia juu ya hali hii. Wana watu wengi wanaowaombea lakini wana watu wachache ambao wako tayari kuwapa fedha za kugharimia huo utumishi walionao unaoombewa. Matokeo ni kazi ya Mungu kukwama au kwenda polepole pamoja na maombi mengi kufanyika juu ya hiyo kazi.

Mungu anataka akufikishe mahali ndani ya moyo wako akikugusa kutoa uwe una kitu cha kutoa; hapo ndipo mahali Mungu anapokupeleka. Hana sababu ya kukuwekea mzigo kwa ajili ya kuigharamia huduma fulani halafu asikupe pesa za kuisadia hiyo huduma. Lazima kuna tatizo mahali fulani linalosababisha hali hii kwako.

  Kwa sababu ule upako unaompeleka yule mtumishi lazima kuna mahali unakusanya fedha atazozihitaji kwenye utumishi huo.Lazima huu uhusiano uwepo. Au hujatumwa na Mungu katika hilo unalofanya au umepewa fedha lakini umezitumia si katika kugharamia huduma Mungu aliyokupa.

Ngoja nikuambie namna hii; serikali za huku duniani zinavyoendesha mambo yao ni kivuli cha serikali ya mbinguni. Kama vile huku duniani kuna bajeti, na serikali ya mbinguni ina bajeti.  Kama vile huku duniani kuna ‘ministries’, zinazoitwa Wizara, na mbinguni kuna ‘ministries’, kibiblia haziitwi wizara bali zinaitwa huduma.

Kila mwaka serikali inapanga mgawo wa fedha kwa ajili ya wizara zake kufuatana na mipango iliyoko ili kutimiza kusudi la serikali; na mbinguni vile vile kuna  mgawo wa fedha unayopangwa kwa ajili ya ministries au huduma zilizoko huku duniani kutimiza kusudi la Mungu, - kumbuka hili siku zote!

Huku duniani Waziri hawezi tu akatumia zile fedha alizopewa kwenye wizara yake, nje ya bajeti bila maelezo, lazima atajieleza vizuri. Labda atakwenda mpaka bungeni ajieleze vizuri, kwa nini alitumia kama alivyotumia, na kama alitumia vibaya Wabunge na mkaguzi wa mahesabu ya serikali watambana kwa maswali mengi.

Mimi nataka nikuambie ya kuwa kuna watu wengi sana watakwenda mbinguni na watakuta bajeti yao haijaguswa, wala haijatumika, kwa sababu Mungu hawezi kutoa fedha nje kwa kanisa ya kusudi lake.

Kama Rais hawezi kutoa fedha nje ya kusudi la wizara, kwa nini mnataka Mungu atoe fedha nje ya matumizi ya kusudi lake?

Ukishapata hiyo picha utaelewa ninachokueleza hapa.

Mungu anataka akutajirishe kwanza katika vitu vyote ndipo unapoweza kuwa na ukarimu wote! Unaweza ukawa na ukarimu wote ndani ya moyo wako lakini haisaidii sana kama huna vitu vya kutoa, … itakuumiza tu! Ndio maana kama una moyo wa utoaji inaumiza sana kujua kwamba kuna shida ambayo kwa kweli ungekuwa nacho ungeweza ukasaidia. Lakini kwa kuwa huna cha kutoa, huwezi fanya kitu. Ni afadhali usingeijua.

Kwa wale ambao wanazunguka kama tunavyozunguka wanaelewa hii ni lugha gani  ambayo  Mungu anasema katika ujumbe huu.

Tulipokuwa Dodoma kuna kijana mmoja ambaye alikuwa anavuta bangi ameacha shule, na kila mtu amemkatia tamaa, akarudi kwa Yesu wakati wa semina tuliyoifanya na akaacha kuvuta bangi, akataka kurudi shule, lakini nani anamlipia?

 Tulipokuwa Moshi kuna msichana mmoja alikuwa kichaa, akapelekwa hospitali mbalimbali hakupata msaada wowote wa kupona, akarudishwa kwao kule Moshi. Tulipokuwa na semina Moshi mjini akaletwa uwanjani kafungwa kamba mkononi na miguuni. Lakini tulipomwombea akapona.

Akaletwa pale mbele jukwaani kushuhudia. Akaeleza jinsi alivyoteseka,  na jinsi walivyokuwa wanamfunga kwa kamba. Alipomaliza, akasema, “Mwakasege nataka kusoma shule, wazazi wangu hawana uwezo wa kunisomesha.”

Nikasema, moyoni “ Mungu nisaidie”, Mungu akasema moyoni mwangu “Yuko mtu nimemwandaa kwa ajili ya kumlipia”. Nikasema kwa sauti, “yule mtu aliyeandaliwa kwa ajili ya kumlipia huyu msichana aje mara moja”. Wakatokeza watu wawili.

Nikawaunganisha na mwenyekiti wa semina ili wafuatilie, wajue ni shule gani alikuwa anasoma, anataka kusoma kitu gani sasa,na pia wawasiliane na wazazi wake. Ni watu wengi tunaokutana nao waliona na mahitaji ya namna hiyo na ni wengi, lakini ni nani atawalipia?

Unaliona hili? Bila utajiri wa vitu vyote, huwezi ukawa na ukarimu wote.

Tumeangalia hadi sasa, sehemu nne katika biblia zinazoonyesha ya kuwa neno ambalo Mungu amesema kwa ajili ya Tanzania – linathibitika kibiblia.

Ni unabii na ujumbe muhimu kwa ajili ya Tanzania, ni muhimu tuwe na uhakika ya kuwa unathibitika kibiblia, kabla hatujaanza kuamini, na kujiandaa kwa ujio wake.

Katika barua za mwezi inayofuata, tutaangalia kwa mifano ya kibiblia inayofanana na utekelezaji wa neno hili lililotamkwa kwa ajili ya Tanzania. Tumeona kwa maandiko katika sehemu nne, uthibitisho wa unabii huu. Mifano tunayoiangalia katika barua zijazo zinazofuata miezi ijayo itatupa kujua na kuwa na uhakika ya kuwa ikiwa Mungu aliwahi kufanya jambo kama hili zamani, basi hata leo anaweza kulifanya tena!

Tuzidi kuombeana.

Neema ya Bwana Yesu Kristo izidi kuwa juu yako daima.
 

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.