Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Oktoba 2005                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


BARUA YA MWEZI OKTOBA 2005

Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo.

            Tunajua unahamu ya kujua juu ya mfano mwingine ambao tunakuletea katika barua ya mwezi huu. Kumbuka nia yetu ni kuona imani yako inaongezeka katika kujua na kutarajia utendaji wa Mungu aliokusudia juu ya Tanzania. Mungu analeta kwanza upako wa utajiri kabla ya upako wa uamsho. Hata biblia imeliweka wazi jambo hili.

Mfano
wa Ujenzi wa Hekalu

Hekalu ninalolisema hapa ni lile ambalo mfalme Sulemani alilijenga, akiongozwa na Roho Mtakatifu.

Wito wa kwanza katika maisha ya Mfalme Sulemani, si awe mfalme, bali ajenge hekalu la Bwana ambalo baba yake Daudi alikatazwa kulijenga. Lakini ili aweze kufanikiwa katika kuijenga hiyo nyumba (Hekalu) ya Bwana, alipewa pia nafasi awe mfalme juu ya Israeli.

Soma mwenyewe ilivyoandikwa katika kitabu cha 1 Mambo ya Nyakati 28:20. “Kisha Daudi akamwombia Sulemani mwanawe, uwe hodari, mwenye moyo mkuu, ukatende hivyo; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu, Mungu wangu, yu pamoja nawe; yeye hatakupungukia wala kukuacha, hata itakapomalizika kazi yote ya huo utumishi wa nyumba ya Bwana”

Kwa maneno haya, ni dhahiri ya kuwa wito wa mfalme Sulemani ulikuwa ni kujenga (hekalu) nyumba ya Bwana! Nafasi ya kuwa mfalme alipewa (pamoja na sababu nyingine), ili imsaidie kutekeleza wito wake vizuri na kwa ufanisi zaidi.

Watu wengi huwa wanashindwa kutumia nafasi ambazo Mungu amewapa katika kanisa au katika serikali au katika jamii au mahali popote pale, ili kulitimiza kusudi waliloitiwa kwa kuwa wanashindwa kutofautisha kati ya wito waliopewa na nafasi waliyopewa ili kutimiza wito wao!

Usichanganye kati ya nafasi uliyonayo na wito ulionao. Nafasi uliyonayo sio wito! Ila Mungu amekuweka katika hiyo nafasi ili utimize na kutekeleza wito aliokuitia! Sulemani alipewa nafasi awe mfalme – lakini huu haukuwa wito wake au wajibu wake akiwa katika hiyo nafasi! Wito wa kwanza aliopewa kuufanya akiwa katika hiyo nafasi ni kujenga nyumba ya Bwana!

Baada ya kujua hili, ni muhimu ufahamu ya kuwa kufuatana na utaratibu wa Mungu, asingeweza kumpa mfalme Sulemani wajibu wa kumjengea nyumba bila ya kwanza kumwandalia utajiri wa kumsaidia kugharamia huo ujenzi!

Je!Unalipata wazo hili hapa? Utajiri kabla ya uamsho, ili utajiri uweze kulipia gharama zinazoambatana na uamsho! La sivyo mfalme Sulemani angeweza akawa na maono/mzigo wa kujenga nyumba ya Bwana, lakini bila ya Mungu kumwandalia utaratibu wa kugharamia ujenzi huo;- asingeweza kujenga na kuimaliza nyumba ya Bwana!

Watu wengi wana maono mazuri sana ya kazi ya Mungu ndani yao,lakini kwa sababu ya ukosefu wa fedha, wanajikuta wanashindwa kutekeleza na kuyatimiza maono waliyopewa. Unafikiri hii ni sawa? Ni dhahiri hii si sawa!

Maana Mungu akikupa kazi uifanye huwa pia anao utaratibu tayari wa namna ya kuigharamia. Ni jukumu la mtu mwenyewe kuomba hadi aunganishwe na huo mpango wa kuigharamia kazi aliyopewa na Mungu.

Ndivyo ilivyotokea kwa mfalme Sulemani alipopewa maagizo ya kujenga nyumba ya Bwana. Kabla hata Sulemani hajaanza kutawala Mungu alimtumia mfalme Daudi kuiwekea “akiba nyumba ya Mungu” (1 Mambo ya Nyakati 29:2)

Ukisoma habari hii katika kitabu cha 1 Mambo ya Nyakati 29:1-9 utaona ya kuwa upako wa utajiri uliwasaidia mfalme Daudi na watu wake “kwa hiari yao” kuweka vitu vingi kwa ajili ya Sulemani ili avitumie kugharamia ujenzi wa nyumba ya Mungu muda utakapofika.

Akiba iliyowekwa ilikuwa ni ya dhahabu, fedha, chuma, shaba, miti, vito mbalimbali, rangi mbalimbali, na marimari tele!

Je! Unaelewa kwa nini mfalme Sulemani alipoomba apewe hekima ili aongoze vizuri, Mungu aliimpa na utajiri pia? (1 Wafalme 3:7-14)

Sababu mojawapo ni ili hekima aliyopewa iwe kusikilizwa na wale aanaowaongoza na wale wanaomsikiliza! Kwa nini? Kwa sababu kitabu cha Mhubiri 9:16 inatuambia: “….hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi”.

Unaona jambo hili? Mungu alijua hekima peke yake haitoshi – kwa hiyo akaampa Sulemani utajiri pia ili hekima aliyopewa na Mungu isidharauliwe na maneno yake yaweze kusikilizwa na kufuatwa!

Hata hivi leo tunaliona hili likitokea katika kanisa na katika jamii kwa ujumla! Utaona mtu akiwa maskini lakini ana hekima, si mara nyingi hekima yake inafuatwa, na maneno yake yanasikilizwa. Lakini mtu akiwa tajiri hata kama hana hekima, bado anapewa heshima katika kanisa na katika jamii, na maneno yake mara nyingi husikilizwa.

Ndio maana Mungu alipompa Sulemani hekima akamwongea na utajiri pia – ili awe na vyote viwili – hekima na utajiri!

Sababu nyingine iliyomfanya Mungu ampe Sulemani utajiri pamoja na hekima ni kwa sababu katika kitabu cha Mithali 9:1 hekima ilipo kazi yake mojawapo ni kujenga. Na kila inachokijenga inakijenga imara!

Kwa hiyo lilikuwa ni jambo lililo wazi ya kuwa ikiwa wito wa Sulemani ulikuwa ni kujenga nyumba ya Bwana, basi ilikuwa ni sahihi apewe hekima na utajiri kwa pamoja! Hekima ili imsaidie kujenga; na utajiri umsaidie kulipia gharama za ujenzi huo!

Jambo la msingi ninalotaka uone hapa ni kwamba Sulemani alipewa hekima na utajiri kabla ya kuanza kuutekeleza wito wake wa kumjengea Mungu nyumba!

Asante kwa kusoma barua hii. Usisahau kutuombea ili Mungu azidi kutupa nguvu zaidi kwa ajili ya kazi yake aliyotushirikisha maishani mwetu.
 

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.