|
|
| ||
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
|
Bwana Yesu Kristo Asifiwe milele! Salamu katika jina la Yesu Kristo. Hali yako ya kiroho inaendeleaje? Ile tu kwamba umepata muda wa kuisoma barua yetu ya mwezi huu, tunaamini Roho Mtakatifu ameweka kiu ndani yako ya kujifunza zaidi juu ya neno la Mungu. Mungu anataka kuitembelea Tanzania tena. Upako wake wa utajiri anauleta kwanza kabla hajatuletea upako wa uamsho. Mwezi huu tunakuletea mfano mwingine unaofundisha juu ya jambo hili.
Mfano wa Ujenzi Nehemia alipokuwa akifanya kazi ugenini kama mnyweshaji wa mfalme Artashasta, aliletewa habari na Hanani mmoja wa ndugu zake juu ya uharibifu uliotokea juu ya mji wa Yerusalemu. Nehemia aliambiwa ya kuwa : “Ukuta wa Yerusalemu umebomolewa, na malango yake kwa moto” (Nehemia 1:3) Ukiendelea kuisoma habari hii utaona ya kuwa Nehemia alimshirikisha Mfalme Artashasta juu ya hali ya mji wa Yerusalemu, na akaomba kibali cha kwenda kuujenga. Jambo mojawapo lililomkabili Nehemia ni namna ya kugharamia ujenzi wa ukuta wa Yerusalemu! Ingawa aliomba msaada wa Mfalme, lakini hakujua kiwango cha uharibifu kilichokuwepo huko Yerusalemu: Kwa hiyo haikuwa rahisi sana kwake kuwa na usahihi wa mahitaji ya gharama za kazi iliyokuwa inamkabili mbele yake. Lakini Mungu aliyeweka mzigo na msukumo wa kuifanya kazi hii ndani ya moyo wake alijua jinsi alivyokusudia kumsaidia Nehemia. Mungu akampa Nehemia kibali na kukubalika mbele ya mfalme wake kwa ajili ya kupata msaada wa vifaa vya kumsaidia kuujenga ukuta wa Yerusalemu. Nehemia mwenyewe aliandika akasema: “Naye Mfalme akanipa, kama mkono mwema wa Mungu wangu ulivyokuwa juu yangu” (Nehemia 2:8) Tunaona hapa ya kuwa Nehemia alipewa hivyo vifaa alivyohitaji toka kwa mfalme, siyo kama mahitaji aliyoyataja, bali “kama mkono mwema wa Mungu” ulivyokuwa juu yake. Kwa nini Nehemia hakupewa sawasawa na mahitaji aliyoyataja mbele za mfalme, bali alipewa kama mkono mwema wa Mungu ulivyokuwa juu yake? Ukilitafakari swali hili kwa undani utaelewa kwa nini ilikuwa hivyo. Sababu kubwa ya Mungu kufanya hivyo ni kwa kuwa Nehemia alikuwa hajui ukubwa wa uharibifu wa Yerusalemu, kwa hiyo isingekuwa rahisi kwake kujua gharama halisi za kazi iliyokuwa inamkabili. Ili kazi anayoiendea isikwame, upako wa Mungu (au mkono mwema wa Mungu) uliokuwa juu ya Nehemia ulimvuvia mfalme Artashasta kumpa Nehemia mahitaji yaliyokuwa mbele yake hata ambayo alikuwa hajayaomba! Unaliona jambo hili linavyofanana sana na unabii tuliopewa katika nchi ya Tanzania juu ya upako wa utajiri kutangulia kufunuliwa kabla ya upako wa uamsho? Mfalme Artashasta aliwezaje kuwa na mahitaji ambayo hata Nehemia mwenyewe alikuwa hayajui? Ni lazima kabla ya upako wa kuujenga Yerusalemu kushuka juu ya Nehemia, Mungu alimshushia mfalme Artashasta upako au uwezo wa kutajirika uliomsaidia kukusanya mali na vifaa ambavyo vilikusudiwa kutumiwa na Nahemia baadaye! Kumbuka: Kabla Mungu hajamwinua mtumishi wake na kumwagiza kazi ya kufanya, huwa kwanza anamwinua mtu mwingine na kumwandaa kwa ajili ya kumgharamia huyo mtumishi wa Mungu atakapokuwa anafanya utumishi aliopewa na Mungu. Jambo kama hili tumeliona likitokea mara kwa mara katika utumishi huu tuliopewa na Mungu. Nakumbuka kuna wakati fulani mimi na mke wangu tuliamua tuwakaribishe kwenye chakula cha jioni familia kadhaa katika mji wa Dar es Salaam zilizotusaidia kifedha kwa huduma tuliyokuwa nayo Kigoma. Familia hizo zilifika, na tukala nao chakula cha jioni, na kumshukuru Mungu kwa utumishi tulioufanya Kigoma. Na tukawaeleza ya kuwa huduma iliyokuwa inafuata wakati huo ilikuwa ni semina yetu ya kwanza jijini Mwanza. Tukawaomba wasiache kutuombea kwa ajili ya semina hiyo. Tulipotaka kumaliza kula na kuondoka, mmoja wa wale tuliwaalika akaomba fursa ya kuzungumza. Nafasi hiyo tukaampa. Akatumia nafasi hiyo kuwaambia wenzake ya kuwa ingawa hatujaambiwa kuchangia kifedha safari ya Mwanza, ni vizuri waliopo wachangie ili baraka za Mwanza zisiwapite. Na waalikwa wakaitikia vizuri na wakachangia safari yetu ya Mwanza kwa kadri Mungu alivyowajalia. Mimi na mke wangu tulishangaa sana. Lakini tulijua lazima Mwanza tutakutana na gharama ambazo hatuzijui bado wala ambazo tulikuwa hatuzitarajii ya kuwa itatubidi tuzilipie wenyewe. Na tulipofika Mwanza na kuifanya ile semina yetu ya kwanza jijini Mwanza tulijikuta tunakabiliwa na gharama ambazo hatukuzitarajia. Tukatumia fedha tulizochangiwa siku ile Dar es Salaam kulipia hizo gharama. Ndipo tulipopata ufahamu ya kuwa Mungu ametufanyia sisi kama alivyomfanyia Nehemia. Mungu alitupa fedha za kugharamia semina ya Mwanza, si sawa sawa na mahitaji yetu, bali sawa sawa na upako wa Mungu (mkono wa Mungu) uliokuwa juu yetu kwa ajili ya kazi iliyokuwa Mwanza. Tulipotamka tu juu ya semina ya Mwanza tunaamini upako uliokuwa juu yetu uliwavuvia na kuwaongoza wale watu ktugharamia kama vile waliotugharamia. Tunaamini utakuwa pamoja nasi tena mwezi ujao (Octoba 2005) tutakapokuletea mfano mwingine juu ya jambo hili. Mungu wetu
ambaye tunaamini ni Mungu wako pia – azidi kukubariki. |
|