Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Februari 2006                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


JE UNAKUMBUKA KUWAOMBEA
WATUMISHI WA MUNGU?

Umuhimu wa Kuwaombea Watumishi wa Mungu

Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo.

Siku moja nilipokuwa namalizia kuhubiri katika kanisa fulani, niliwaambia wale waliokuwa wananisikiliza ya kuwa wakiwa nyumbani kwao wawe wananikumbuka katika maombi yao kwa kadri Roho Mtakatifu atakavyowaongoza juu ya mahitaji yangu ya kiroho, kiakili, kimwili, na kifamilia.

Lakini siku mbili baadaye mama mmoja aliyekuwepo kanisani hapo alinifuata nyumbani akaniuliza swali hili: “Uliposema pale kanisani tukukumbuke katika maombi yetu sikukuelewa. Wewe kama mtumishi wa Mungu unayetuombea mara kwa mara –na wewe unahitaji maombi toka kwetu kwa vipi?”

Ni wazi ya kuwa mama huyu alikuwa na mawazo ya kuwa watumishi wa Mungu hawahitaji kuombewa. Je, na wewe una mawazo kama hayo? Je!huwa unawaombea watumishi wa Mungu mara kwa mara au unangoja usikie wanashida au wameanguka kwenye dhambi ndipo unawaombea?

Kipimo cha mtu anayewaombea watumishi wa Mungu ni hiki: Wakati wengine wanawalaumu, yeye anawaombea! Wakati wengine wanawarushia maneno watumishi wa Mungu, yeye anawarushia maombi! Wakati wengine wanawashitaki, yeye anawaombea!

Je!wewe uko kwenye kundi lipi? La waombaji au kundi la walalamikaji?

Mwaka 1990

Mapema Mwaka 1990, nilikuwa katika mji fulani nikihubiri na kufundisha mkutano wa siku kumi mfululizo kila siku jioni. Siku ya tisa usiku, Mungu alisema nami katika roho yangu maneno yafuatayo:-“Kesho ni siku ya mwisho ya mkutano; utakapomaliza kuhubiri, na kuombea watakaookoka na wagonjwa – piga magoti kwenye jukwaa halafu uombe mkutano ukuombee wewe na familia yako kabla ya mkutano kufungwa rasmi”.

Niliposikia maagizo hayo nilishangaa sana, tena maswali mengi yaliingia moyoni mwangu kutaka kujua kwa nini Mungu ameniambia hivyo. Wala sikujua watu watanielewaje nikiwaambia hayo.

Pamoja na maswali yote niliyokuwa nayo nilitii kufanya kama Bwana alivyoniagiza . Baada ya kumaliza kuwaombea waliookoka na wagonjwa niliueleza mkutano maagizo ya Mungu, halafu nikapiga magoti kwenye jukwaa mbele ya watu wote ili waniombee mimi na familia yangu.

Watu karibu elfu moja na mia tano waliokuwa pale wote walimpazia Mungu sauti kwa pamoja kwa muda wa dakika kumi na tano hivi – wote wakiomba kwa sauti juu yangu na familia yangu huku wengi wakiwa wameinua mikono yao juu. Nguvu za Mungu ziliushukia mkutano kwa upya na baada ya maombi kumalizika watu wengi walikuwa wameanguka chini!

NINI MAANA YAKE?

Baada ya mkutano huo niliendelea kumuuliza Mungu katika maombi nikitaka kujua ni nini maana yake jambo hili.

Roho Mtakatifu aliniongoza katika Biblia na kunionyesha umuhimu wa watumishi wa Mungu kuombewa na wenzao. Na si hilo tu bali Roho Mtakatifu aliniongoza katika Biblia na kunionyesha umuhimu wa Watumishi KUWAOMBA Wakristo wenzao wawaombee!

Kumbuka Yesu Kristo anatupa mfano mzuri anapowaomba wanafunzi wake washirikiane naye katika maombi. Imeandikwa hivi:

“Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?” (Mathayo 26:40).

Ingawa wanafunzi hao walilala badala ya kuomba – jambo muhimu la kujifunza hapa ni kwamba Yesu Kristo aliwaomba wanafunzi wake washirikiane naye katika maombi aliyokuwa nayo kabla ya kusulubiwa.

Kama Yesu Kristo aliona umuhimu wa maombi ya wengine, si zaidi sisi tulio watumishi wake?

Ni kwa ajili hiyo Roho Mtakatifu ameweka mzigo wa maombi ndani ya wakristo wengi kuwaombea watumishi wa Mungu mara kwa mara. Je huwa unawaombea nini?- Mungu awafanyie nini?

MAHITAJI YA PAULO

Tukisoma nyaraka za Mtume Paulo tunaona wazi ya kuwa aliyaweka wazi mahitaji yake ya maombi kwa wakristo wa makanisa mbali mbali ili wamwombee. Naamini ya kuwa Roho Mtakatifu alimwongoza kuwaandikia hivyo. Mahitaji hayo ya Mtume Paulo yanatusaidia hata sisi leo kuona UMUHIMU wa kuwaombea watumishi wa Mungu, na MAMBO ya kuwaombea:

1.     Milango ya kueneza Neno la Mungu ifunguliwe:

Mtume Paulo akiwaandikia wakristo waliokuwa Kolosai aliwaambia hivi katika Wakolosai 4:2-4:

“Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa, ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena”

Tunahitaji kuwaombea watumishi wa Mungu popote, wafunguliwe milango ya kuhubiri neno la Mungu.

Wakati mwingine mnatamani mtumishi wa Mungu mmojawapo awafikie na kila mkimtafuta hamumpati – msikate tamaa upesi – mwombee kwa Mungu afunguliwe mlango wa kufika kwenu. Ndiyo maana Mtume Paulo aliwaomba Wakristo waliokuwa Rumi wamwombee ili apate kufika kwao kwa furaha, kama apendavyo Mungu (Warumi 15:32).

2.     Wahubiri Injili kwa Ujasiri:

Tatizo moja kubwa kwa watumishi wengi wa Mungu ni kujaa hofu na kukosa ujasiri wa kuihubiri injili iwapasavyo – hasa pakiwa na vitisho kwao toka kwa wapinzani wa injili.

Kwa hiyo ni vizuri kuwakumbuka katika maombi – tukikemea roho ya hofu itoke kwao na kuwaombea wavikwe ujasiri wa kuinena injili kama iwapasavyo kuinena. Maombi ya jinsi hii hata Mtume Paulo aliomba wakristo wamwombee akisema:

“…..ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya injili,….hata nipate ujasiri katika hiyo kunena jinsi inipasavyo kunena” (Waefeso 6:19,20).

Tafadhali chukua biblia yako na usome Matendo ya Mitume 4:29-31 uone matokeo ya maombi ya jinsi hii yalivyo kwa watumishi wa Mungu.

3.     Waokolewe na hila za Wapinga Wokovu:

Naamini unafahamu jinsi watu wanaopinga wokovu na injili ya Kristo wanavyojitahidi usiku na mchana kuwadhuru kwa njia mbali mbali Watumishi wa Mungu wanaohubiri injili inayookoa.

Kumbuka kuwaombea ili Mungu awaepushe na hila hizo na kuwalinda. Mtume Paulo akijua hila hizo aliwaomba wakristo wamwombee. “Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokokewe na wale wasioamini katika Uyahudi….” (Warumi 15:30,31). Soma pia 2 Wathesalonike 3:1,2.

4.     Waombewe wawe na hekima:

Jambo lililo wazi katika maisha ya utumishi aliyokuwa nayo Yesu Kristo hapa duniani ni maisha ya utumishi yaliyojaa hekima ya Mungu katika utendaji wake, na katika kujibu maswali mengi aliyokuwa anaulizwa. Hebu na tuisome mistari hii pamoja:

“Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri jinsi ya kumtega kwa maneno. Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifahamu katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hujatazama sura za watu. Basi utuambie, waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?” (Mathayo 22:15-17).

Fikiria wewe unaulizwa swali kama hili ungejibu kwa namna gani? Maana siku hizi tunalipa kodi pia; je ni halali kulipa kodi? Watumishi wa Mungu wakiulizwa swali kama hili watajibuje? Hekima ya Mungu ilimsaidia Kristo katika kulijibu, kama tunavyosoma katika Mathayo 22:18-22:

“Lakini Yesu akaufahamu uovu wao akasema, mbona mnanijaribu, enyi wanafiki? Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. Akawambia, ni ya nani sanamu hii, na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao”.

Ni muhimu tukumbuke kuwaombea watumishi wa Kristo hekima zaidi ya kimbingu ili waweze kushinda mitego mingi ya maswali inayowajia kila siku.

Si hilo tu bali hekima hiyo ya Mungu itawasaidia kutatua matatizo mengi ya ugomvi yaliyopo katikati ya wakristo kwa sababu mbalimbali. Ndiyo maana mfalme Sulemaini aliomba apewe hekima (1Mambo ya Nyakati 1:7-10)- katika uongozi na utumishi wake.

5.     Huduma zao zikubalike na wakristo wenzao:

Mtume Paulo alipokuwa anaanza huduma yake hakukubaliwa na wanafunzi wa Yesu Kristo kwa haraka. Biblia inasema: “Alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi” (Matendo ya Mitume 9:26).

Hata siku hizi si watu wote waliookoka ambao huduma zao zinakubaliwa. Wengine wanakataliwa kwa sababu ya dhehebu wanalotoka; wengine wanakataliwa kwa sababu hawajaenda chuo cho chote cha Biblia; wengine wanakataliwa kwa sababu ya umri wao mdogo; na wengine wanakataliwa kwa sababu ni wasichana au wanawake; na wengine wanakataliwa kwa sababu zingine mbali mbali.

Mtume Paulo akiijua shida hii aliwaandikia wakristo waliokuwa Rumi ya kuwa “….jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu….huduma yangu niliyonayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu….” (Warumi 15:30,31). Kumbuka kuwaombea watumishi wa Mungu huduma zao zikubalike na watakatifu mahali Mungu anapowapeleka kuhudumu.

6.     Watiwe nguvu upya baada ya kuchoka:

Ukisoma kitabu cha Kutoka 17:8-16 utaona jinsi ambavyo Musa alivyosaidiwa na wenzake baada ya kuchoka akiwa katikati ya vita. Hebu fikiria hao wenzake wasingekuwapo – kungetokea nini? Watumishi wa Mungu huwa wakati mwingine wanachoka kiroho, kiakili na hata kimwili; kwa hiyo wanahitaji maombi yako ili watiwe nguvu upya na Mungu, ili waendelee na kazi – walizoitiwa..

MKARIBISHE ROHO MTAKATIFU

Ndiyo!Mkaribishe Roho Mtakatifu akusaidie katika kuwaombea watumishi wa Mungu. Maana tunasoma katika Warumi 8:26,27 ya kuwa Roho Mtakatifu ametumwa kutusaidia katika maombi.

Ukimkaribisha Roho Mtakatifu, atakukumbusha kuwaombea watumishi wa Mungu na wakati mwingine hata kwa majina yao – atakupa mambo ya kuwaombea na namna ya kuwaombea.

Mambo niliyoyataja katika somo hili ni baadhi tu ya mambo mengi ambayo watumishi wanahitaji kuombewa. Mambo mengine ni; maisha yao ya ndoa (1 Timotheo 3:4,5); wawe na mwenendo mzuri (Waebrania 13:18); na kadhalika.

Ni maombi yangu ya kuwa Roho Mtakatifu aliyekuongoza kusoma barua hii atakuhimiza na kukuongoza pia katika jambo hili muhimu la kuwaombea watumishi wa Mungu. Anza sasa!

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.