Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Januari 2006                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


UNA UFAHAMU KWA KIASI GANI
JUU YA HUDUMA ZA MALAIKA
KATIKA MAISHA YAKO?

Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo. Tunaamini umesherehekea vizuri mwezi uliopita kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo katika kizazi cha mwanadamu.

Na sisi tuliungana na wakristo wengine ulimwenguni katika furaha hii. Watu wengi sana wanakichukulia kipindi hiki kuwa ni cha sherehe, bali sisi tulikiona ni kipindi cha sherehe pamoja na kujifunza! Na mambo ya kujifunza yako mengi sana katika habari hii ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Pamoja na kukutakia uwe na mwaka mpya wa mafanikio, tungependa pia, uwe na somo la kutafakari na kujifunza! Tungetaka utafakari na ujifunze juu ya huduma za malaika katika maisha yako.

Tulipokuwa tunamuuliza Mungu juu ya kile cha kukuandikia katika barua hii, tulijiuliza swali hili: “ni jambo gani lililotokea katika kipindi cha kuzaliwa kwa Yesu ambalo si mara zote linakumbukwa?”

Ndani yetu tuliona kabisa Roho Mtakatifu akituwekea jambo la malaika na utumishi waliofanya wakati huo, - na jinsi ambavyo na sisi siku hizi tunahitaji kujifunza juu ya malaika na huduma zao. Maana palipo na Yesu Kristo pana malaika zake pia!

Lililo wazi katika biblia ni kwamba kuzaliwa kwa Yesu, kulifunua na kuweka wazi sehemu ambayo malaika wanayo katika maisha yetu, na katika uhusiano wetu na Mungu. Kumbuka ya kuwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu iko mwishoni mwa mwaka, ili pia tuwe na jambo la kujifunza katika kumbukumbu hiyo tayari kwa ajili ya mwaka mpya unaofuata!

Kabla ya Kuzaliwa
kwa Yesu

Kabla ya kuzaliwa kwa Yesu, Mungu alituma malaika wake watoe habari hizo muhimu kwa wahusika wachache waliokuwa karibu sana na jambo hili.

Tunaona mara ya kwanza malaika Gabrieli akimtokea mzee Zakaria hekaluni alipokuwa akifanya maandalizi ya ibada. Malaika Gabrieli alimweleza Zakaria juu ya mke wake Elizabeti kumzalia mtoto wa kiume atakayemwita Yohana; na akamwambia kazi atakayoifanya Yohana katika kuandaa ujio wa Yesu Kristo.

Habari hii tunaisoma katika kitabu cha Luka 1:8-25. Na tunaona malaika akijitambulisha kwa Zakaria aliposema: “Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema”.

Miezi sita baada ya jambo hili kutokea, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka Nazareti nyumbani kwa bikira Mariamu. Habari hii tunaisoma katika kitabu cha Luka 1:26-38.

Malaika Gabrieli akiwa nyumbani kwa Mariamu akampa ujumbe toka kwa Mungu juu ya kuteuliwa kwake ili atumike katika kumzaa Yesu Kristo duniani. Si hilo tu aliloelezwa, lakini pia aliambiwa jinsi mimba hiyo itakavyotokea; na kazi ambayo Yesu ataifanya atakapokuwa duniani. Katika mazungumzo hayo hayo pia, alielezwa juu ya ujauzito wa Elizabeti.

Mara ya tatu tunaona malaika akimtokea Yusufu aliyekuwa anajiandaa kumwoa Mariamu. Lakini hakumtokea kama alivyowatokea akina Zakaria na Mariamu. Wala jina la malaika huyu biblia haisemi. Lakini alimtokea Yusufu kwenye ndoto!

Katika ndoto hiyo malaika anajibu maamuzi ya siri ambayo Yusufu alikuwa ameamua kuyachukua dhidi ya Mariamu baada ya kujulikana ya kuwa ni mjamzito! Habari hii tunaisoma katika kitabu cha Mathayo 1:18 – 24.

Baada ya Kuzaliwa
kwa Yesu

Ukifuatilia mambo yaliyotokea mara tu baada ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, utaona jinsi malaika walivyohusika katika kipindi hicho.

Malaika wa Bwana alitumwa kupeleka habari za kuzaliwa kwa Yesu kwa wachungaji waliokuwa makondeni wakilinda mifugo yao katika zamu ya usiku.

Katika Luka 2: 9 – 12 tunasoma ya kuwa: “ Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori la kulia ng’ombe”

Lakini tunaona baada ya Malaika kusema hayo: “Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu” (Luka 2:13). Hii inaonyesha ya kuwa Mungu aliandaa kwaya ya malaika ili waimbe mara tu baada ya wachungaji kupewa habari za kuzaliwa kwa Yesu. Pia si tu waimbe lakini waonekane wakiimba! Malaika hao wangeweza kuimba bila ya kuonekana kwa wanadamu! Lakini Mungu alitaka waonekane. Je wewe umewahi kujiuliza ni kwa nini Mungu aliwafunua hao malaika waonekane na wanadamu?

Huduma hii ya malaika kutoa habari za kuzaliwa kwa Yesu haikuishia hapo, bali tunaona pia ya kuwa waliwaongoza mamajusi hadi mahali Yesu alipokuwepo!

Tunajua  ya kuwa mamajusi waliongozwa na nyota hadi wakajua Yesu alipo. Hatuambiwi habari za malaika kuhusika. Lakini ukiichunguza habari hii vizuri na kuitafakari utajua ya kuwa ile “nyota” ilikuwa ni malaika!

Tunalijuaje hili? Tunalijua kwa neno la Mungu! Mamajusi walisema waliiona “nyota yake Mashariki” (Mathayo 2:2). Hii haikuwa nyota ya kawaida! Ilikuwa nyota ya “mfalme wa Wayahudi” au kwa maneno mengine ilikuwa nyota ya Yesu!

Biblia inaposema “nyota yake” ina maana gani? Kufuatana na Ufunuo wa Yohana 1:20, 21 ‘nyota yake’ ina maana ya ‘malaika wake’.

Kwa hiyo mamajusi walipokuwa wanaongozwa na nyota iliyokuwa inatembea hadi ikasimama juu ya nyumba – tunajua malaika wa Bwana ndiye aliyewaongoza, ila alijifunua kwao kama “nyota”! Hata wewe unajua, nyota ya kawaida haiwezi kusimama juu ya nyumba! Huyo alikuwa malaika wa Bwana, ila alionekana kama “nyota”!

Habari zingine za malaika wakiwa kazini baada ya Yesu kuzaliwa, ni wakati walipomtokea tena Yusufu katika ndoto mara mbili! Mara ya kwanza ni wakati alipoambiwa na malaika wa Bwana katika ndoto ya kuwa akimbilie Misri “ maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize” (Mathayo 2:13)

Mara ya pili ni wakati malaika wa Bwana alipomtokea katika ndoto akiwa Misri akimwambia amchukue mtoto na mama yake waende “ nchi ya Israeli, kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto” (Mathayo 2:20)

Je! Yesu amezaliwa katika
Maisha yako?

Tumeona jinsi malaika wa Bwana walivyohusika kwa namna nyingi wakati wa kuzaliwa kwa Yesu – kabla na baada! Tunaamini ya kwamba hata leo Yesu anapozaliwa katika moyo wa mtu – malaika wanashughulika sana – hata kama hatuwaoni!

Kila mtu anayempa nafasi Bwana Yesu azaliwe ndani ya moyo wake, anakuwa mrithi wa wokovu. Anapata wokovu, na anakuwa ameokoka!

Biblia iko wazi kutuambia ya kuwa kuna malaika wa Bwana walioandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuwahudumia wote wanaorithi wokovu! Hivi ndivyo tunavyosoma katika Waebrania 1:14. Imeandikwa hivi: “Je! hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?”

Hata ikiwa huwaoni – wapo! Jifunze habari zao, ili usije ukakosa kile ambacho Mungu amekusudia ukipate katika maisha yako katika mwaka mpya huu akiwatumia malaika. Soma pia Zaburi 34:7; Zaburi 91:11,12.

Ukiisoma biblia vizuri utaona ya kuwa ukiamua kuurithi wokovu, malaika wapo kwa ajili ya kukuhudumia, lakini pia wapo kwa ajili ya kukulinda. Kinachowafanya wakulinde ni kwa sababu ndani ya moyo wako, au nyumba yako umeamua kumpa nafasi Yesu Kristo. Na kwa kuwa hawawezi kuwa mbali na Yesu, vivyo hivyo hawawezi kuwa mbali na wewe!

Ukiwa karibu na Yesu, na malaika wanakuwa karibu na wewe! Na kwa sababu wanalitii neno analosema Yesu, vivyo hivyo watatii neno la Yesu linalotoka katika kinywa chako!

Malaika wa Bwana ni watumishi katika kulitumikia kusudi la Bwana hapa duniani na huko mbinguni.

Ukiwa katika kulitumikia kusudi la Mungu ukiongozwa na Roho Mtakatifu ni muhimu ujue, na utiwe moyo, na ufarijike kwa habari hizi ya kwamba malaika wa Bwana atakuwa pamoja na wewe – hata kama humwoni kwa macho haya ya kibinadamu. Wewe liamini neno lake!

Ukisoma kitabu cha Matendo ya Mitume utaelewa tunachokuambia katika barua hii. Ukisoma habari za upinzani katika utumishi wa mitume tunasoma ya kuwa: “wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu” (Matendo ya Mitume 5:18 -19)

Hii inaonyesha malaika wa Bwana alikuwa pamoja nao katika huo utumishi wakati wote ila alijifunua katika kipindi hicho, ili watiwe moyo katikati ya upinzani kwa kujua ya kuwa Mungu hajawaacha na amemtuma Malaika wake awasaidie!

Ukisoma habari za utumishi wa Filipo katika Matendo ya Mitume sura ya nane na mstari wa ishirini na sita, utaona jinsi ambavyo malaika wa Bwana alishikana naye bega kwa bega katika kuufanikisha utumishi huo.

Mahali popote wokovu wa Yesu aliyezaliwa kwa bikira Mariamu unapohubiriwa, au unapotafutwa, au unapopokelewa, uwe na uhakika malaika wa Bwana wapo pia!

Yule afande Kornelio wa kikosi cha kirumi (kiitalia) alitokewa na malaika wa Bwana na kumweleza juu ya kuusikia ujumbe wa wokovu aliokuwa nao mtume Petro. Soma habari hii katika Matendo ya Mitume 10:1 – 47.

Malaika wa Bwana wanaweza
Kutumwa kukuletea majibu ya maombi yako!

Kumbuka jambo hili wakati unapoomba kwa Mungu, malaika wa Bwana aliyetumwa kukusaidia, anatiwa nguvu zaidi na Roho Mtakatifu kufanikisha jibu la Mungu kwako! Ukikata tamaa kuomba kabla hujajibiwa ombi lako, na ukaacha kuliombea hilo jambo, unamnyima malaika wa Bwana msaada wa nguvu za Roho Mtakatifu katika kufuatilia upatikanaji wa jibu la ombi lako!

Mtume Petro alipofungwa jela, kanisa liliomba kwa juhudi kwa ajili yake (Matendo ya Mitume 12:5). Matokeo ya maombi hayo ni Mungu kumtuma malaika wake kujibu hayo maombi kwa kumfungua Petro na kumtoa gerezani kimuujiza!

Si hivyo tu, kwa kuwa huduma hiyo ya malaika wa Bwana ilikuwa ni matunda ya maombi ya kundi fulani la watakatifu waliokuwa wakiombea “nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana” (Matendo ya Mitume 12:12), ilimbidi Malaika wa Bwana amchukue Petro na kumwongoza mpaka karibu na eneo hilo yalikokuwa yanafanyika maombi!

Mazingira ya kufungwa kwa Petro hayakuwakatisha tamaa, bali waliendelea kuomba, - na kule kuendelea kuomba kulimpa nafasi malaika wa Bwana kuifanya kazi aliyotumwa kuifanya, na kuimaliza kwa mafanikio.

Jambo la jinsi hii tunaliona pia katika kitabu cha Danieli. Malaika wa Bwana walikuwa wakitumwa kumletea majibu ya maombi yake toka kwa Mungu! Kwa mfano, soma sura za 7,8,9,10,11, na 12 za kitabu cha Danieli utaona jinsi malaika wa Bwana walivyotumika kumletea Danieli majibu ya maombi yake kwa Mungu.

Na wakati mwingine ilimbidi aombe kwa kufunga kwa muda mrefu, lakini mwisho wake malaika alitumwa toka kwa Mungu kumletea majibu ya maombi yake.

Kwahiyo ikiwa kuna jambo unaliombea na bado hujajibiwa, usilikatie tamaa wala usikate tamaa. Endelea kuomba, na kusubiri jibu lako kwa imani. Tunaamini utajibiwa tu!

Kumbuka si lazima malaika wa Bwana wajifunue ndipo ujue wapo, lakini amini neno la Mungu linalosema wapo, na ya kwamba Mungu huwa anawatumia kukusaidia kwa njia nyingi hata bila ya wewe kujua!

Ikiwa, basi, Mungu ataamua wajifunue kwako uwaone, utawaona na utawatambua. Lakini ni muhimu uzingatie angalizo lifuatalo:

Angalizo Muhimu!

Biblia inafundisha wazi ya kuwa kuna makundi mbalimbali ya malaika, na kazi zao zinatofautiana. Lakini, kwa kuisoma biblia tunasoma ya kuwa kuna malaika walio chini ya uongozi wa Mungu, na wako walio chini ya uongozi wa shetani. Soma mwenyewe katika 2 Wakorintho 11:14 inaposema; “Wala si ajabu. Maana shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru”.

Kwa hiyo si kila kiumbe kinachojifunua kwako kama malaika – ni malaika toka kwa Mungu! Shetani naye anaweza kujigeuza ili aonekane kama malaika toka kwa Mungu. Kwa mantiki hii basi, jifunze kuwapima malaika, usije ukawapokea ambao hawakutumwa na Mungu.

Njia mojawapo ya kuwapima ni kwa kutumia neno la Mungu. Ikiwa wanachosema au wanachofanya hakifanani na neno la Mungu usilazimike kuwapokea na kufuata wanachosema! Biblia inasema katika Zaburi 103:20: “Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, mkiisikiliza sauti ya neno lake”.

Ikiwa malaika wa Bwana ni watendaji na wasikilizaji wa sauti ya neno la Bwana, basi hawawezi kufanya au kusema chochote nje ya neno la Bwana! Kumbuka hili ikiwa malaika watajifunua kwako!

Lakini pia njia nyingine ya kuwapima malaika ni kuangalia wanakuongoza kumwabudu nani? Ikiwa hawakuongozi kumwabudu Mungu katika Yesu Kristo usiwakubali wala kuwakubalia neno lao!

Ndicho kilichotokea kwa Yohana katika kisiwa cha Patmo – malaika alipomaliza kuongea naye. Yohana anasema hivi: “ Na hapo nilipoyasikia na kuyaona nilianguka, ili nisujudu mbele ya miguu ya malaika yule mwenye kunionyesha hayo. Naye akaniambia, angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako, na wa ndugu zako manabii, na wa wale wayashikao maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu” (Ufunuo wa Yohana 22:8 -9).

Unaona jinsi malaika huyu alivyokataa kuabudiwa? Malaika anayedai umwabudu hakutoka kwa Mungu wa Yesu Kristo! Malaika wa Bwana ni watumishi wenzetu katika kulitimiza kusudi la Mungu.

Hata malaika aliyemtokea Manoa na mke wake akiwapa habari za kuzaliwa kwa Samsoni – alikataa kupokea sadaka walipotaka kumtolea yeye! Akamwambia Manoa “….inakupasa kumsogezea Bwana” (Waamuzi 13:16).

Mwisho

Tunakutakia mwaka mpya wa 2006 baraka za Bwana Yesu na ushindi tele. Usikose kuungana nasi katika barua ya mwezi ujao. Pia angalia ratiba ya semina zetu, ili utuombee, na ikiwezekana uweze kuhudhuria. Mungu akuongoze pia na kukupa uhuru wa kutupa mchango wako wa fedha kama sadaka katika kutusaidia kugharamia kazi za huduma tulizonazo mwaka huu.
 

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.