Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Machi 2006                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


MALEZI BORA YA WATOTO
 WA KIROHO

Tunakusalimu katika Jina la Yesu Kristo.

Wasomaji wa Biblia ni rahisi kukubaliana nasi tukisema ya kuwa panapotokea uamsho mahali fulani mambo mengi yanatokea – pamoja na matunda hayo ya uamsho kunakuwepo na watu WANAOOKOKA – wanaoamua kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao.

Mara nyingi tumesikia usemi wa namna hii: “kuzaa ni rahisi lakini kulea ni kazi ngumu”. Pia kuna usemi unaosema hivi: “uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi”.

Hata katika mambo ya uzazi wa kiroho maneno hayo ni kweli kabisa. Ni rahisi kuzaa watoto wa kiroho – yaani watu kuokoka, lakini kuwatunza hao waliookoka wakue kiroho wasirudi nyuma ni kazi ngumu. Ni wazi ya kuwa mtu kama hajawahi kumshuhudia au kumwombea mtu mwingine mpaka aokoke mara nyingi anakuwa hana uchungu anapoona mtu aliyeokoka anarudi nyuma kiroho. Ukitaka kuijua sababu yake ni rahisi – maana uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi!

Jumapili moja katika miaka ya nyuma sisi na wenzetu – watumishi wa Mungu tulikwenda kijiji fulani kuhudumia mkutano wa kiroho. Siku hiyo watu wengi waliokoka na kujazwa nguvu za Roho Mtakatifu, pia wagonjwa wengi tuliwaombea walipona magonjwa yaliyokuwa yanawasumbua. Tuliondoka tukiwa tumejaa furaha katika Roho Mtakatifu huku tukimtukuza Mungu kwa matendo makuu aliyoyafanya.

Hiyo sehemu hatukurudi tena kwa muda mrefu kwani tuliamini ya kuwa hao waliookoka watatunzwa vizuri na wenzao. Lakini baada ya mwaka kupita tulisikitika sana kusikia ya kuwa watu waliookoka – ambao walikaribia kufikia mia moja wakati ule – wamerudi nyuma kiroho na wengi wameacha wokovu – na waliosimama katika wokovu walikuwa hawazidi watano kati ya wale mia moja. Tulikuwa tumekosea wapi?

TULIKUWA TUMEKOSEA WAPI?

Tunajua wengine hawapati nafasi ya kujiuliza swali hili wanaposikia ya kuwa watu waliookoka katika huduma zao wamerudi nyuma au wametawanyika kama kandoo wasio na mchungaji. Tunajua hakuna mzazi anayependa mtoto wake aliyemzaa afe. Atajitahidi kwa uwezo wake wote ambao Mungu amempa amlee mtoto wake katika hali ambayo ataishi maisha marefu na mazuri.

Inatakiwa hata katika uzazi wa kiroho tuwe na mawazo ya namna hiyo ya kutaka kuona watoto tunaowazaa kiroho wanaendelea katika wokovu na kumpenda na kumtumikia Yesu Kristo maisha yao yote.

Hilo ndilo tuliloitiwa! Mungu ametuita katika Kristo Yesu tushirikiane naye katika uamsho ambao matunda yake hayapukutiki bali katika uamsho ambao matunda yake yanadumu. Ndiyo maana Yesu Kristo alisema hivi:

“Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi
              niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka

              mwende mkazae matunda; na matunda
              yenu YAPATE KUKAA; ili kwamba lo
              lote mmwombalo Baba kwa jina langu
              awapeni”.
(Yohana 15:16)

Yesu Kristo anasema ametuchagua na kutuweka katika kazi yake ili tuzae matunda, na matunda hayo yapate kukaa maana yake matunda hayo yadumu siku zote. Kati ya matunda hayo anayotaka tuzae ni watoto wa kiroho – kushuhudia na kuwaombea watu hadi waokoke. Nia yake ni kuona ya kuwa watoto hawa tunaowazaa kiroho hawarudi nyuma katika wokovu bali wanadumu katika Yeye siku zote.

IMEANDIKWA KAZI ZITAPIMWA

Kama ulikuwa umesahau, tunapenda kukukumbusha ya kuwa kila kazi ambayo Mungu anatupa tuifanye katika Kristo Yesu inapimwa – inapimwa kama inaweza kudumu au ni ya muda. Mtume Paulo ameandika katika 1 Wakorintho 3:11-15 anasema hivi:

“Maana msingi mwingine hakuna mtu
  awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule
  uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo.
  Lakini  kama mtu akijenga juu ya msingi
  huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani,
  au miti au majani au manyasi, kazi ya
  kila mtu itakuwa DHAHIRI. Maana
  siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa
  katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu
   kazi ya kila mtu, ni ya namna gani…..”

Hebu na tutafakari pamoja maneno haya: Anaposema “….siku ile itaidhihirisha….” ana maana siku ile ambayo Bwana atakaporudi mara ya pili kuchukua kanisa na kukagua kazi alizowapa watumishi wake (Mathayo 24:42-51). Uzuri au ubaya wa kazi unayomtumikia Bwana sasa – siku ile utakuwa wazi – ingawa hata sasa unaweza ukaona matokeo ya kazi hiyo – lakini thawabu utakayopata itategemea sana kama MATUNDA YA KAZI HIYO YAMEWEZA KUDUMU MPAKA YESU ATAKAPORUDI! Ndiyo maana mtume Paulo anaendelea kusema hivi:

“….kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa,
             atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea;

             atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa;
             lakini ni kama kwa moto”.

Kwa mfano rahisi tunaweza kusema hivi; ikiwa umehubiri na watu 1000 wameokoka lakini katika “siku ile” ya Yesu kurudi anakuta watu 10 wanaoendelea na wokovu kati ya watu 1000 waliookoka katika huduma yako – thawabu utakayopewa na Bwana itakuwa ni kwa ajili ya watu 10 aliowakuta bado wameokoka na siyo wale 990 waliokoka na baadaye kuacha wokovu. Je!unaelewa uzito wa jambo tunalokuambia?

UMECHUKUA HATUA GANI?

Hili ni swali muhimu ambalo tunataka likufuate kila mahali mpaka uchukue hatua za kulijibu katika huduma ambayo Mungu amekupa. Unadhani Mungu anafurahi anapoona watoto wake wa kiroho wanakufa kiroho kwa sababu tu watumishi wake hawafuati utaratibu wa malezi bora ya watoto wake wa kiroho? Ni dhahiri Mungu hapendi.

Basi, umechukua hatua gani? – unapoona watu waliookoka katika huduma yako wakirudi nyuma kiroho na kuacha wokovu? Je! umeawaacha tu na kusema “shauri lao kila mtu atachukua mzigo wake mwenyewe?” Je! una uchungu nao?

MALEZI BORA YA WATOTO WA KIROHO

Kwa kusoma jinsi ambavyo Mtume Paulo alivyoongozwa na Roho Mtakatifu kuwatunza watoto wake wa kiroho – hata sisi tutapata mbinu za kuwatunza watoto wetu wa kiroho – wapate malezi bora – ili matunda hayo yapate kudumu – hata “siku ile” Bwana Yesu Kristo apate kuwakuta wanaendelea na wokovu. Mambo manne yafuatayo yanajitokeza wazi kuwa ndiyo yaliyokuwa msaada kwa Mtume Paulo:

a)    Aliendelea kuwaombea wakue kiroho:

Watumishi wengi wanaomba sana na kwa muda mrefu ili watu waokoke – na hii ni nzuri – na Mungu anajibu watu wanaokoka. Lakini jambo la kusikitisha ni kuona kuwa hawatumii muda wa kutosha kuwaombea hao watu waliookoka ili wakue kiroho na kudumu katika Yesu.

Mtume Paulo aliwaandikia Wagalatia waliookoka na kuwaambia hivi:

“Vitoto vyangu (watoto wangu wa kiroho), ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu” (Wagalatia 4:19)

Mtume Paulo alikuwa anawaambia watoto wake hao wa kiroho ya kuwa ingawa wameokoka – bado anazidi kuwaombea (kuwaonea utungu tena) mpaka Kristo aumbike ndani yao. Nia ya Mtume Paulo ilikuwa ni kuwaombea watoto wake wa kiroho wapate kuukulia wokovu.

Soma pia Waefeso 1:15-23 alipowaandikia watoto wake wa kiroho waliokuwa Efeso akianza kwa kusema: “Kwa sababu hiyo mimi nami, tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na Pendo lenu kwa watakatifu wote, siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika SALA ZANGU….”

Soma pia Wafilipi 1:3-11; Warumi 1:9,10; na Wakolosai 1:9-23. Mifano hii michache ikutie kiu ya kuwaombea watoto wa kiroho siku zote. Usipowaombea wewe mzazi wao – nani unataka achukue mzigo wa kuwaombea? Kumbuka uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi!

b)    Alirudi kuwatembelea tena:

“Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Turejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika KILA MJI tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani” (Matendo ya Mitume 15:36). Kama Paulo na Barnaba walivyofanya – uwe na utaratibu wa kwenda kuwatembelea tena watu uliowahubiri neno la Mungu ili uone wanaendeleaje kiroho. Je!huwa unafanya hivyo? Kama hufanyi hivyo kitu gani kinakuzuia kuanza sasa kuwatembelea?

Ikiwa kwa sababu moja au nyingine wewe binafsi unashindwa kuwatembelea mwombe mtumishi mwingine wa Mungu awatembelee. Hebu soma maneno haya ambayo Mtume Paulo aliwaandikia Wakolosai – alisema hivi: “Tikiko, ndugu mpendwa, mtumishi mwaminifu, mjoli wangu katika Bwana, atawaarifu mambo yangu yote; ambaye nimemtuma kwenu kwa sababu iyo hiyo, ili mjue mambo yetu, naye akawafariji mioyo yenu; pamoja na Onesimo, ndugu mwaminifu, mpendwa, aliye mtu wa kwenu. Hao watawaarifu mambo yote ya hapa kwetu” (Wakolosai 4:7-9).

Ikiwa utashindwa kuona mtumishi mwingine wa Mungu ambaye unaweza kumwomba awatembelee watoto hao wa kiroho mwombe Mungu ainue watenda kazi wake popote walipo ili waende kuwatembelea – soma Mathayo 9:36-38.

c)     Aliwaandikia barua (Nyaraka) mara kwa mara:

Nyaraka za Mtume Paulo tunazozisoma katika Biblia ni barua ambazo Roho Mtakatifu alimwongoza kuziandika kwa ajili ya kuwaonya, kuwatia moyo, kuwafundisha watoto wake wa kiroho – soma 1 Wakorintho 4:14.

Si hivyo tu lakini aliagiza kuwa nyaraka hizo zisomwe hata na wale walio jirani na wale walioandikiwa kwa mfano aliwaambia Wakolosai hivi:

Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu, fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi” (Wakolosai 4:16).

Jambo hili ni muhimu sana, na inasikitisha kuona kuwa Watumishi wengi wa Mungu ni wavivu kuwaandikia hata maneno machache ya kuwatia moyo watoto wa kiroho. Jitahidi kulifanya jambo hili muhimu.

d)    Aliishi kwa ushuhuda mzuri mbele yao:

Mara nyingi mtoto huwa anafuata tabia ya mzazi wake hata kama ni mbaya labda Mungu aingilie kati kumsaidia – la sivyo atafuata tabia ya mzazi wake.

Tuangalie sana tunavyosema na tunavyoenenda mbele ya watoto wetu wa kiroho – tusije tukawa chanzo cha kuanguka kwao kiroho bali tuwe chanzo cha kuimarika kwao kiroho. Tuwe na ujasiri wa kusema kama Mtume Paulo:

“….Mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili….Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo” (1 Wakorintho 4:15 na 11:1).

Je! Kama mtumishi wa Mungu ushuhuda wako ni wa namna gani? Una mfano gani mbele ya watoto wako wa kiroho?

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.