Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Aprili 2007                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


Salamu katika Jina la Yesu Kristo,

HUWEZI KUONDOA JAMBO LA UCHUMI

NDANI YA DAMU YA YESU

Barua ya mwezi uliopita (Machi 2007) tulizungumza na wewe ya kuwa mtu hawezi kuondoa jambo la uchumi ndani ya damu ya Yesu.

Tulianza kwa kukupa sababu mbili zinazotufanya tuamini ya kuwa hakuna mtu anayeweza kuondoa jambo la uchumi ndani ya damu ya Yesu.

Tulikwambia ya kuwa sababu ya Kwanza ni kwamba: Agano jipya katika damu ya Yesu linahusisha pia jambo la uchumi.

Na sababu ya Pili ni ya kuwa: Kile kinachokumbukwa wakati wa kusherehekea sikukuu ya pasaka – ni pamoja na mtu kukombolewa ki-uchumi.

Leo tunataka tuzungumze na wewe juu ya sababu ya Tatu ambayo ni: Kupokea baraka ya Ibrahimu kupitia katika damu ya Yesu.

Wagalatia 3:13,14 inatuambia hivi:

“Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo…….”

Kwa lugha nyepesi au kwa tafsiri nyepesi tunaambiwa hapa ya kuwa, kule kusulubiwa kwa Kristo msalabani kumefungua mlango kwa kila atakaye kupokea urithi wa baraka ya Ibrahimu – katika Yesu Kristo.

Tafsiri hii inathibitishwa na maneno ya Wagalatia 3:29 yanayosema; “Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi”.

Ikiwa kwa kumwamini Yesu Kristo juu ya kile alichofanya msalabani na damu kumwagika kwa ajili yetu, kunatufanya pia tuwe “uzao wa Ibrahimu na warithi sawasawa na ahadi” – ni muhimu tuifuatilie ahadi hiyo ya urithi ya Ibrahimu, ili tujue tumerithi mambo gani.

Tunasoma katika Warumi 4:13,16 ya kuwa; “kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani …. Kwa hiyo ilitoka kwa imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote, si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote”

Ni ahadi gani ambayo Ibrahimu alipewa na Mungu? Ni hii ya kuwa “mrithi wa ulimwengu”. Kwa hiyo ikiwa na sisi ni uzao wa Ibrahimu kwa imani ndani yake Kristo Yesu, ina maana basi na sisi ni “warithi wa ulimwengu”.

“Ulimwengu” ndio “baraka” aliyopewa Ibrahimu na Mungu kama ahadi ya urithi kwa ajili yake, na uzao wake – pamoja na sisi tulio uzao wake kwa imani katika Kristo Yesu.

“Mrithi wa ulimwengu” maana yake nini? Ni mrithi wa “baraka” ipi hiyo inayojulikana kama “ulimwengu”?

Hii ina maana baraka isemwayo hapa ilikuwa inahusu vitu vya hapa ulimwenguni! Ndiyo maana katika kitabu cha Mwanzo 22:14, Mungu alijifunua kwa Ibrahimu kama “Yehova-yire”.

“Yehova- yire” maana yake ni Mungu au Bwana ambaye anapata katika ulimwengu huu kila anachohitaji kupata kwa ajili ya kuwabariki au kuwafanikisha watu wake hapa ulimwengu.

Ndiyo maana baada ya Mungu kujifunua kwa Ibrahimu kama “Yehova – yire” katika Mwanzo 22:14; tunaona chini yake katika mstari wa 17-18 akimwambia Ibrahimu ya kuwa: “katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia, kwa sababu umetii sauti yangu”

Kilichomfanya Mungu ajifunue kwa Ibrahimu na kuitamka hiyo ya baraka- ni kumwagika kwa damu ya kondoo kama sadaka badala ya mtoto wake Isaka.

Ukiifuatilia habari hii ya Ibrahimu kupokea baraka za “Yehova – yire” juu ya kuishi kwake hapa ulimwenguni, utaona ya kuwa Mungu alimbariki “Ibrahimu katika vitu vyote” (Mwanzo 24:10.)

Mjakazi wa Ibrahimu aliorodhesha baraka za Ibrahimu aliposema; “Bwana amembarikia sana Bwana wangu, amekuwa mtu mkuu; amempa kondoo, na ng’ombe, na fedha, na dhahabu, na watumwa, na wajakazi, na ngamia, na punda”.

Kila unapozisoma baraka za Ibrahimu ni muhimu uwe unajikumbusha ya kuwa hizo baraka ni urithi wako pia ukiwa ndani ya Kristo. Kwa sababu ya damu ya Yesu iliyomwagika kwa ajili yetu!

Umeziangalia vizuri hizo baraka? Utaona zinahusu uchumi wa Ibrahimu na uzao wake, hii ni ikiwa pamoja na wewe kama Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wako.

Kutoka sura ya 13:14-18 na sura ya 15:1-21 inatuonyesha ya kuwa “kumiliki ardhi” ni sehemu ya “urithi wa ulimwengu” aliopewa Ibrahimu na uzao wake.

Kwa sababu ya undugu uliopo kati ya Ibrahimu na Yesu Kristo kwa njia ya damu ya Yesu, ni vigumu mtu kuweza kuondoa jambo la uchumi ndani ya damu ya Yesu. Pamoja na mambo mengine ambayo damu ya Yesu inafanya kwa mwanadamu, tukumbuke ilimwagika pia ili kutusaidia hali zetu za uchumi ziwe nzuri.

Unapokuwa ndani ya Yesu
Unakuwa mrithi mara mbili!

Ndivyo biblia inavyotuambia – ya kwamba mtu anapokuwa ndani ya Yesu, anakuwa mrithi mara mbili!

Kufuatana na Wagalatia 3:29 mtu anapokuwa ndani ya Yesu Kristo anakuwa “mrithi wa Ibrahimu” Imeandikwa;

“Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi”.

Tena kufuatana na Wagalatia 4:6-7 na Warumi 8:16,17 mtu anapokuwa ndani ya Kristo anakuwa “mrithi wa Mungu”.

Imeandikwa juu ya jambo hili ya kwamba: “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba. Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu”.

“Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye”

Hii inatufanya tuwe warithi mara mbili! Warithi wa Ibrahimu na warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo.

Ndani ya urithi wa Ibrahimu, tunarithi baraka za Ibrahimu. Na ndani ya urithi wa Mungu, tunaourithi pamoja na Kristo, tunarithi “baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho ndani yake Kristo” (Waefeso 1:3)

Ikiwa katika baraka za Ibrahimu tunarithi “ulimwengu”, - au tunarithi “mafanikio ya ulimwengu huu”, na ikiwa katika Mungu tunarithi pamoja na Kristo baraka zote za rohoni  basi hakuna sababu kwa nini mtu aliye ndani ya Kristo asifanikiwe katika mambo yake yote – kiroho , kiakili, kimwili na ki-uchumi.

Mungu akubariki sana.
UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.