Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Agosti 2007                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


Jina la Yesu Kristo Libarikiwe milele na milele. Amina!

Tunayo furaha katika Roho Mtakatifu kukuandikia barua ya mwezi huu ambayo ni mwanzo wa mfululuzo wa barua nne zenye ujumbe muhimu sana.

Je, unajua kiwango cha umuhimu wa maombi yako unapoombea toka katika nafasi ya mfalme na kuhani katika Kristo? Swali hili tutalijibu katika barua hizi nne kuanzia na hii unayoisoma sasa.

Neno la Mungu katika biblia linatuambia ya kuwa tunapokuwa katika Kristo Yesu tunafanyika pia kuwa Wafalme na Makuhani kwa Mungu wetu.

            Ufunuo wa Yohana 5:9,10 inasema ya kuwa; “Ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu, nao wanamiliki juu ya nchi”.

            Ufunuo wa Yohana 1:5,6 inasema ya kuwa; “....Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa  ufalme na makuhani kwa Mungu.....”.

            Maneno haya “wafalme na makuhani” katika tafsiri zingine za awali za biblia yanasomeka hivi “wafalme na makuhani”. Ndiyo – katika Kristo Yesu tunafanyika wafalme na makuhani kwa Mungu wetu.

            Kwa kuwa walio ndani ya Kristo wamefanyika “wafalme na makuhani” – biblia inasema kwa sababu hiyo “wanamiliki katika nchi” (Ufunuo wa Yohana 5:10), na tena kufuatana na Warumi 5:17 wanatawala katika maisha haya kwa uzima wa Kristo uliomo ndani yao!

            Kufanyika na kuwa mfalme na kuhani kwa wakati mmoja ni nafasi kubwa na heshima kubwa ambayo Mungu anampa mtu kati ya watu wengine ili wamiliki na kutawala pamoja naye katika eneo alilomkabidhi.

            Tena, kuwa mfalme na kuhani ni wajibu mkubwa sana ambao katika agano la kale walipewa watu wachache sana….wakati katika agano jipya wengi amepewa ila hawajui! Na wale wanaojua juu ya wajibu huu hawautumii ipasavyo.

            Mungu analiheshimu sana Neno linalotoka katika maombi ya mtu ambaye amesimama katika nafasi ya mfalme na kuhani! Hii ni kwa sababu hayo yanakuwa si maombi ya kawaida, kwa kuwa ni maombi yanayotoka kwenye kinywa cha mtu ambaye yuko kwenye nafasi ya mfalme na kuhani.

            Ni muhimu kujua ya kuwa nguvu ya neno asemalo mtu, inatoka kwenye nafasi ya mtu asemaye neno hilo, kulielekeza kwenye eneo linalohusika na nafasi hiyo.

            Kwa mfano; mke wangu ni mwanamke kama wanawake wengine lakini nafasi aliyonayo kwangu inafanya neno lake analolisema kwangu liwe na uzito kwangu kuliko neno atakalolisema mwanamke mwingine. Hii si kwa sababu neno la mwanamke mwingine si la maana bali linakosa nguvu kwa sababu ya nafasi aliyonayo kwangu – ni tofauti na nafasi aliyonayo mke wangu.

            Ukiangalia mfano wa Rais wa nchi, utaona ya kuwa kuna marais wengi duniani, lakini si kila neno la kila Rais lina uzito ule ule kwa kila nchi! Lakini neno la Rais lina uzito zaidi katika nchi ambayo yeye ni Rais!

Neno la Rais, au la mkuu wa mkoa lina nguvu na sauti katika eneo lile tu analiongoza, kufuatana na katiba ya nchi na heshima aliyonayo kwa watu walio katika eneo analoliongoza.

Ndiyo maana nauliza swali hili muhimu - ikiwa unajua kiwango cha umuhimu wa maombi yako unayoomba ukiwa katika nafasi ya mfalme na kuhani katika Kristo Yesu.

Hebu tuangalie na kutafakari kwa undani mifano ifuatayo ya biblia:

Mfano wa maombi
ya nabii Eliya

Katika kitabu cha Yakobo 5:10 – 18 tunasoma ya kuwa “….kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinye; na mvua haikunya juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake”.

Mistari hii inataka tujue ya kuwa pamoja na kwamba nabii Eliya alikuwa kwa jinsi ya nje mtu wa kawaida kama sisi – lakini kuomba au kutokuomba kwa nabii Eliya ndiko kulikokuwa na uamuzi wa mwisho juu ya mvua inyeshe au isinyeshe katika eneo alilokuwepo!

Hujakosea – umesoma sawa sawa ya kuwa; kuomba au kutokuomba kwa nabii Eliya ndiko kulikokuwa na uamuzi wa mwisho juu ya mvua inyeshe au isinyeshe katika eneo alilokuwepo!

Neno lake linakuwa amri ya mwisho juu ya mvua katika taifa lile – na Mungu akalisimamia. Tunasoma katika 1 Wafalme 17:1 ya kuwa nabii Eliya alimwambia Ahabu hivi;  “Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu”.

Nabii Eliya asingekuwa na ujasiri wa kusema neno la jinsi hii kama asingekuwa na uhakika na nafasi aliyokuwa nayo kwa Mungu wake!

Ukisoma Wafalme wa kwanza sura ya 18 utaona ya kuwa katika mstari wa 1 Mungu anamwambia nabii Eliya ya kuwa, “Enenda ukajionyeshe kwa Ahabu; nami nitaleta mvua juu ya nchi”.

Kumbuka kufuatana na Yakobo 5:17 neno la nabii Eliya liliifunga mvua kwa miaka mitatu na nusu, lakini mara baada ya kupita miaka mitatu - Mungu alimwambia nabii Eliya akajionyeshe kwa Ahabu ataleta mvua!

Nabii Eliya na Ahabu walipokutana mvua haikunyesha! Soma mwenyewe katika 1 Wafalme 18:17,18.

Pamoja na kwamba Mungu alimwambia nabii Eliya ataleta mvua atakapojionyesha kwa Ahabu, bado mvua haikunyesha walipokutana hadi nabii Eliya alipochukua hatua ya kuomba ili mvua inyeshe – ndipo Mungu akaleta mvua!

Hivi ndivyo tunavyosoma katika 1 Wafalme 18:41 – 45 na Yakobo 5:18 kwa nini Mungu aheshimu neno na maombi ya nabii Eliya kwa kiwango kikubwa hivi?

Jibu lake ni kwa sababu nabii Eliya alisema neno alilosema akiwa katika nafasi ya mfalme kwa Mungu; na alipoomba alichoomba aliomba akiwa katika nafasi ya kuhani kwa Mungu.

Nafasi hizi mbili zilimpa nabii Eliya uwezo wa kumiliki na kutawala juu ya kunyesha au kutokunyesha kwa mvua katika eneo alilokuwa anaishi wakati huo.

Kumbuka mfalme ni mtu yule anayeongoza katika maamuzi katika eneo ambalo yeye ni mfalme. Neno lake ni la mwisho, na neno lake ni sheria, na linaweka utaratibu anaotaka ufuatwe na wote waliochini ya himaya yake.

Kumbuka kuhani ni mtu yule anayefanya maombi kwa ajili yake au kwa ajili ya mwingine kwa nia ya kumkaribisha Mungu ahusike na hicho anachokiombea.

Pamoja na kwamba wakati wa utawala wa Ahabu, manabii wengi walikuwepo    (1 Wafalme 18:4), lakini si wote walipewa na Mungu kushika nafasi ya mfalme na kuhani katika ulimwengu wa roho – isipokuwa nabii Eliya peke yake!

Nafasi hizi mbili ndizo zilizomfanya nabii Eliya aseme neno na aombe maombi kwa namna ambavyo Mungu alisimama upande wake!

Je itakuwa ni sawa sasa tukijuliza kwa mfano, ikiwa nchi inasumbuliwa na hali mbaya ya hewa kama ukame au mafuriko basi kuna mtu aliyetakiwa asimame kwenye zamu yake ya kuombea hali ya hewa nchini iwe inakuwa nzuri lakini hakuomba, au ikiwa aliomba basi hakuomba ipasavyo? Je, mtu huyo ni wewe?

Mfalme Ahabu alipomwona nabii Eliya, akamwambia “Je!ni wewe, ewe mtaabishaji wa Israeli?” (1 Wafalme 18:17). Ahabu alimwona Eliya ya kuwa ni “mtaabishaji wa Israeli” kwa kuwa alijua ya kuwa kunyesha au kutokunyesha kwa mvua katika nchi yao kulitegemea maombi ya Eliya – lakini Eliya alikaa kimya!

Je! wewe ni mwombaji au mtaabishaji juu ya eneo ambalo Mungu amekuweka ukae hapo, au ufanya kazi hapo, au ufanye huduma hapo, au uishi hapo?

Usikose kuisoma barua yetu ya mwezi ujao ambayo tutaendelea kukuletea mwendelezo wa ujumbe huu muhimu.

Usisahau kutuombea – Mungu azidi kututunza na kututumia sawa na mapenzi yake juu ya maisha yetu.

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.