Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Februari 2007                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


KWA NINI HUKUFA MWAKA 2006?

(Sehemu ya Pili)

            Salamu katika Jina la Yesu Kristo, jina lipitalo kila jina.

          Mwezi uliopita katika barua tuliyokuandikia tulikupa sababu zilizomfanya Mungu akupe tena nafasi ya kuishi mwaka huu wa 2007.

Tulijifunza  sababu mbili muhimu za kile kilichomfanya Mungu akulinde usife mwaka 2006, na badala yake akakupa nafasi ya kuishi mwaka huu wa 2007.

Sababu ya kwanza: ni ili upate nafasi zaidi ya kulitumikia kusudi la Mungu mahali ulipo. Sababu ya pili: ni ili upate nafasi ya kutengeza maisha yako ya kiroho – utubu dhambi zako, usiangamie bali uokolewe!

Sababu ya tatu ni hii: Ili upate nafasi ya kuyafurahia maisha haya uliyopewa kuishi!

Kwa wengine jambo hili linaweza likawa jipya kwao – kwa sababu hawajui ya kuwa si tu kwamba Mungu anataka waishi, bali zaidi sana anataka wayafurahie maisha wanayoishi!

Tafakari pamoja nasi maneno ya Bwana Yesu yafuatayo:

“Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu, mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yohana 10:10). Umewahi kujiuliza uzima ulio “tele” ni uzima kiasi gani? Tunaamini Yesu hapa anazungumzia juu kuwa na wokovu na furaha pia!

Kuna watu wameokoka lakini hawana furaha! Yesu alikuokoa ili uwe na uzima, kisha uwe nao tele! Maana maisha yako yajaye furaha ndani ya wokovu.

Daudi aliandika alisema “siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, tutashangilia na kuifurahia” (Zaburi 118:24). Je, wewe unaufurahia mwaka huu? Je, unafurahia maisha yako siku ya leo?

Unaweza ukasema umesongwa na majaribu kwa hiyo huna furaha. Lakini biblia inatuambia unatakiwa kufurahi katika majaribu pia!

Ndivyo ilivyoandikwa katika Yakobo 1:2 tunaposoma ya kuwa “Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali”.

Mungu amekuacha uishi ili pia uweze kuyafurahia maisha unayoishi sasa!

Angalia tena maneno haya ya Bwana Yesu aliposema: “ Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu” (Yohana 16:24).

Unaona nini katika maneno hayo ya Bwana Yesu? Sisi tunaona ya kuwa ikiwa huna furaha – unaweza ukaomba ili Mungu akupe hicho ulichokikosa ukakosa furaha – Yesu anasema “nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu”.

Mungu anataka si tu kwamba uishi, bali pia uyafurahie maisha!

Watu wengine wanaishi maisha ya kukosa furaha kwa sababu maisha wanayoishi si matamu bali yamekuwa machungu!

Zaburi 91:16 inasema: “Kwa siku nyingi nitamshibisha….”

Anayetoa siku za kuishi ni Mungu na anayekula siku za kuishi ni mwanadamu. Tukiliangalia jambo hili kwa misingi ya chakula utaona ya kuwa aliye na njaa atataka kula zaidi hasa ikiwa chakula ni kitamu!

Na anayesema nimeshiba si yule atoaye chakula, bali yule alaye chakula!

Je! Ukiulizwa leo juu ya kuongezewa siku za kuishi utasemaje – uongezewe au usiongezewe? Kwa yule mwenye maisha matamu hatasita kusema aongezewe siku za kuishi! Ikiwa maisha yako si matamu Yesu amesema omba kwa jina lake upate kitakachofanya uyaone maisha matamu, au kitakachofanya furaha yako iwe timilifu!

Ndio maana alisema katika Mathayo 11:28,29 ya kuwa: “Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu”.

Yesu Kristo anataka uishi bila mahangaiko na kukosa raha. Ishi katika pumziko la Yesu huku akikupa raha nafsini mwako. Inawezekana kabisa!

Tafakari maneno haya ya Mhubiri 3:12,13 yanayosema: “ Mimi najua ya kwamba hakuna jema kwao kupita kufurahi ….maadamu wanaishi. Tena ni karama ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburudisha kwa mema katika kazi yake yote”.

Neno hili karama limeandikwa likiwa na maana ya zawadi. Kwa hiyo ni zawadi ya Mungu kila mtu apate kula na kunywa, na kujiburidisha kwa mema katika kazi yake yote! Soma pia Mhubiri 5:18,19.

Je! wewe umeipokea zawadi hii ya Mungu kwa mwaka huu 2007?

Na neno hili je! umewahi kulisoma? Linalosema: “Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye siku zote za maisha yako ….” (Mhubiri 9:9).

Ikiwa umeoa au kuolewa ni maombi yetu kwa Mungu ya kuwa ndoa yako mwaka 2007 itajaa furaha – tena furaha tele! Hayo pia ni mapenzi ya Mungu kwa ajili ya ndoa yako!

Je! umeokoka lakini huna furaha katika wokovu wako kama mwanzo – usisahau kuomba kama Daudi aliposema “ Unirudishie furaha ya wokovu wako” (Zaburi 51:12), na Mungu atakujibu kwa kukurudishia furaha hiyo – ili furaha yako iwe timilifu!

Mwisho

Tunatarajia ya kuwa umeuanza mwaka huu (2007) kwa jina la Yesu Kristo; na ya kwamba utaendelea nao kwa jina la Yesu Kristo; na ya kwamba utaumaliza kwa jina la Yesu Kristo.

          Usisahau kutuombea.
 

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.