Yesu Akamwambia "Lisha Kondoo Zangu" (Yohana 21:17)
Home
Maombi
Ratiba
Shuhuda
Mafundisho
Maswali na Majibu
Barua za Mwezi
Kuchangia Huduma

Barua ya Mwezi Januari 2007                                                            Kutoka kwa Christopher na Diana Mwakasege


KWA NINI HUKUFA MWAKA 2006?

          Salamu katika Jina la Yesu.

          Tunamshukuru Mungu kutupa nafasi ya kukuandikia barua hii ya kwanza kwa mwaka huu wa 2007.

Tunaamini hauko hai kwa bahati mbaya au bahati nzuri. Tunaamini uko hai kwa sababu ya huruma na rehema za Mungu.

Tunasoma katika biblia ya kuwa: “Najikumbusha neno hili, kwa hiyo nina matumaini. Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, kwa kuwa rehema zake hazikomi. Ni mpya kila siku asubuhi …….” (Maombolezo 3:21 – 23).

Kuna watu wengi waliokufa mwaka 2006, lakini wewe haukuwemo – la sivyo usingekuwa unasoma ujumbe huu! Sisi tunakuuliza swali hili: je, unajua ni kwa nini hukufa mwaka 2006?

Watu wengi walikufa mwaka 2006 kwa ajali mbalimbali, lakini wewe hukufa! Wengine walikufa kwa magonjwa na kwa sababu zingine mbalimbali, lakini, wewe ulibaki – hukufa, unadhani ni kwa nini?

Mwandishi wa kitabu cha Maombolezo anasema “Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, kwa kuwa rehema zake hazikomi …..”

Ni kweli ya kwamba ni kwa sababu ya huruma na rehema za Mungu “hatukuangamia” mwaka 2006!

Kwa hiyo, ikiwa Mungu amekulinda mwaka wote wa 2006 na hakukuacha uangamie, ina maana ana sababu za msingi za kukuruhusu uingie na uishi mwaka huu wa 2007. Sababu hizo ni zipi?

Sababu
ya
Kwanza

Tunaloamini ni kwamba sababu ya kwanza ya Mungu kumpa kila mtu anayeishi – aendelee kuishi ni hii: Alitimize na alikamilishe kusudi la Mungu katika maisha yake.

Kwa tafsiri iliyo nyepesi au tafsiri nyingine ni kwamba kuna kazi ambayo Mungu anataka uifanye. Na ili uweze kuifanya Mungu anakulinda na kukupa nafasi ya kuendelea kuishi.

Tukisoma Yohana 17:15,16,18 tunaona Yesu Kristo akituombea kwa Mungu juu ya ulinzi kwa kuunganisha na utumishi anaotaka tutumike hapa ulimwenguni.

Yesu Kristo aliomba hivi: “Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu ……..kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni”.

Kwa hiyo kuna uhusiano kati ya ulinzi wa Mungu juu yetu na utumishi wa Mungu tulionao!

Hii ina maana Mungu anakulinda ili usiangamizwe na adui shetani kwa kuunganisha ulinzi huo na kwa wewe kulitekeleza kusudi lake lililomfanya akulete duniani, na akuweke mahali ulipo.

Mtume Paulo aliandika juu kutokufa kwake akiunganisha na utumishi aliopewa.

Mtume Paulo anasema: “ Kwa maana kwangu kuishi ni Kristo, na kufa ni faida. Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui. Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo; maana ni vizuri zaidi sana; bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu” (Wafilipi 1:21-24)

Ni kama vile Mtume Paulo anasema ninaishi au nimebaki duniani “kwa ajili yenu”. Anasema kwake kubaki katika mwili “ni matunda ya kazi”.

Hiyo ina maana ya kuwa kuna kazi aliyopewa na Mungu ili aifanye na izae matunda katikati ya Wafilipi.

Lakini alipotumia maneno haya “ni matunda ya kazi” kuelezea kuendelea kwake kuishi – alitaka tujue ya kuwa kati ya matunda ya kazi yake katikati ya Wafilipi ni yeye kuendelea kuishi au kuendelea kubaki katika mwili.

Yesu Kristo aliwahi kutoa mfano wa mti uliotaka kukatwa na mwenye shamba kwa kuwa ulikuwa hauzai matunda. Lakini mtunzaji wa shamba  akamwomba mwenye shamba asiukate huo mti, bali auache ili aupalilie ili aupe nafasi aone kama unaweza kuzaa matunda.

Lijue jambo hili ya kuwa unatakiwa “uzae matunda” au “utimize kusudi” la Bwana Mungu mahali ulipo – maana ndio sababu mojawapo bado uko hai – na hukufa mwaka 2006.

Ikiwa hulijui kusudi la Bwana unalotakiwa ulifanye mahali ulipo-tenga muda wa kuliombea jambo hili ili Mungu akueleze juu kusudi lake juu yako.

Ukilijua hili itakuwa rahisi sana kuweka malengo yako ya mwaka 2007, na kuwa na mipango ya maisha yako ya kila siku.

Tunapozungumza juu ya wewe kutimiza kusudi la Mungu kwako –  si lazima iwe kuhubiri maana si kila mtu ameitwa kuhubiri. Lakini kila mtu ameitwa na amewekwa kulitumikia shauri fulani la Bwana mahali alipo. Ni lipi hilo? Muulize Mungu atakuambia.

Tunasoma jambo hili katika habari za mfalme Daudi ya kuwa; “kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibufu” (Matendo ya Mitume 13:36).

Sababu
ya
Pili

Baada ya kuitazama sababu ambayo sisi tunaiona ni ya kwanza iliyomfanya Mungu akupe nafasi ya kuishi mwaka huu, - ni vizuri tukuangalize juu ya sababu tunayoiona ni ya pili.

Sababu ya pili ni hii: Upate nafasi ya kutubu dhambi zako.

Biblia inatuambia ya kuwa Mungu “ hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba” ( 2 Petro 3:9).

Tena tunasoma katika 1 Timotheo 2:4 ya kuwa Mungu “hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli”.

Unaona nini katika mistari hii ya biblia? Sisi tunaona rehema za Mungu na uvumilivu wa Mungu kwetu sisi wanadamu. Na Mtume Petro aliliona hili alipoandika ya kuwa, “nanyi hesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu” ( 2 Petro 3:15).

Unaona nini tena katika mistari hiyo ya biblia? Sisi tunaona ulinzi wa Mungu juu ya wanadamu wote ili wapate nafasi ya kutubia dhambi na waokolewe ili wasije wakaangamizwa kwa adhabu iliyowekwa tayari kwa wote wasiomcha Mungu.

Inawezekana hujui ya kuwa dunia hii (- pamoja na wewe) inalindwa na Mungu isiangamie kabla ya siku yake ya hukumu. Sababu mojawapo ya kuilinda dunia hii na wewe pia kulindwa ni kwamba Mungu hataki upotee bali upate nafasi ya kutubu ili usamehewe dhambi, na uokolewe. Soma habari hii vizuri katika 2 Petro 3:1-15.

Ukijua hili kinachofuata ni kila mtu aliyeingia mwaka 2007 kujiuliza juu hali yake ya kiroho ya mwaka 2006 ilikuwaje! Je, ni eneo gani la maisha yako ya kiroho  halikuwa zuri? Je, ni dhambi ipi ilikusumbua mwaka jana?

Fahamu hili - Mungu amekupa nafasi ya kuishi – pamoja na sababu nyingine alizonazo – ni ili upate nafasi ya kutengeneza maisha yako ya kiroho. Upate nafasi ya kutubu, na kumwomba Mungu akupe ushindi kuanzia mwaka huu na kuendelea juu ya dhambi zilizokushinda mwaka jana!

Hata kama sababu ya kwanza ya Mungu kukubakiza duniani ni ili ulitumikie kusudi lake mahali ulipo, lakini pia tumia nafasi hiyo kwa ajili ya kutengeneza maisha yako ya kiroho yapate kumpendeza Mungu.

Maana unaweza ukatumikia kusudi la Mungu halafu kiroho ukakataliwa na Mungu! Mtume Paulo aliliweka wazi hili alipokuwa anaelezea juhudi zake za kutengeneza maisha yake ya kiroho – akasema “isiwe nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa”. (Wakorintho 9:27)

Hata Yesu Kristo alikwishatoa maonyo juu ya hali hii aliposema: “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinginu. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu” (Mathayo 7:21-23).

Nasi tunasisitiza ya kuwa katika nafasi hii uliyonayo ya kuishi jichunguze hali yako ya kiroho ya mwaka jana – je uliridhika nayo? Je, Yesu akirudi leo au ukifa leo una uhakika wa kupokelewa na Mungu? Au utajikuta unakataliwa tofauti na ulivyotarajia?

Mungu alimvumilia Farao, akamlinda na hakumwangamiza mapema – ili tu amalize kulitumikia kusudi ambalo Mungu alitaka alitumikie! Lakini hatuoni katika biblia kama Farao alipata nafasi ya kutubia dhambi zake na kuyatengeneza maisha yake ya kiroho.

Jifunze jambo hili muhimu ya kuwa: Mungu kumkubali mtu kiutumishi haina maana amemkubali pia kiroho!

Jambo hili likutie changamoto ya “kuhubiri na kujenga Safina” kwa wakati huo huo. Maana Nuhu angehubiri bila kujenga Safina wakati huo huo, hata yeye angeangamia katika gharika!

Unaposimamia kusudi la Mungu mahali ulipo – hakikisha wakati huo huo unajenga Safina, au unatengeneza maisha yako ya kiroho.

Usiwe kama Farao, bali uwe kama Nuhu! Farao alitumikia kusudi la Mungu (Soma Kutoka 9:15,16, Warumi 9:17) lakini hakukumbuka kutumia wakati huo huo kutengeneza mambo yake ya kiroho. Lakini Nuhu alifanya yote mawili wakati huo huo, alilitumikia kusudi la Mungu na pia “alijenga Safina” apate kuokoka!

Mwezi ujao katika barua yetu ya Februari 2007 tutakuletea sababu ya tatu ambayo ni miongoni mwa sababu zilizomfanya Mungu akupe nafasi ya kuishi tena mwaka huu.

Tuzidi kuombeana.
 

UNATAKA KUOKOKA?
Kama unataka kumpa YESU maisha yako sasa, bonyeza hapa
©2003 Tanzania Social and Economic Trust.  All Rights Reserved.